Yesu Akamwambia "Lisha Kondoo Zangu" (Yohana 21:17)
Home
Maombi
Ratiba
Shuhuda
Mafundisho
Maswali na Majibu
Barua za Mwezi
Kuchangia Huduma

Barua ya Mwezi Julai 2007                                                            Kutoka kwa Christopher na Diana Mwakasege


Salamu katika Jina la Yesu Kristo, jina lipitalo majina yote!

Mwezi huu tunamalizia maelezo ya kimafundisho juu ya uhusiano uliopo kati ya kumtumikia Mungu na taifa la Israeli. Sasa endelea…

Mtini ni Taifa
la
Israeli.

            Ukisoma katika Kitabu cha Yoeli 1:6, 7 utaona ya kuwa Mungu ameulinganisha mti wa mtini na Taifa la Israeli – anaposema hivi; “maana Taifa limepanda juu ya nchi yangu, lenye nguvu, tena halina hesabu; meno yake ni kama meno ya simba, yana ana magego ya simba mkubwa. Ameuharibu mzabibu wangu; ameuvunja mtini wangu …”

            Mungu anaposema; “Nchi yangu” na kuifananisha na “mzabibu wangu” na “mtini wangu” – tunajua ya kuwa anazungumzia juu ya Taifa la Israeli au nchi ya Israeli.

            Tunaliona wazo hili likijitokeza tunaposoma Hosea 9:10 hivi; “Mimi nilimkuta Israeli kama zabibu nyikani; nami naliwaona baba zenu kama matunda ya mtini yaliyoiva kwanza …”

            Ikiwa mti wa mtini wakati mwingine katika Biblia unatumika kuelezea juu ya nchi ya Israeli – basi tujue ya kuwa Yesu Kristo alipokuwa anasema “kwa mtini tujifunzeni mfano” alitaka na anataka tujifunze kutoka kwa taifa la Israeli!

            Tujifunze jambo gani kutoka kwa taifa la Israeli? Ni muhimu kwanza tujue kwa mtini alitaka tujifunze nini! Yesu Kristo alisema juu ya mtini hivi; “tawi lake likiisha kuchipuka na kuchanua majani, mwatambua ya kuwa wakati wa mavuno u karibu”.

            Kufuatana na ukuaji wa mtini, tawi lake huwa linapukutisha majani yake wakati wa msimu wa baridi kali (winter), na huwa linachipuka na kuchanua majani wakati wa kipindi cha joto kinapoanza. Mabadiliko haya ya tawi la mtini ni matokeo ya mabadiliko ya majira na nyakati ambazo Mungu aliziamuru ziwepo juu ya eneo ambalo mtini unaota!

            Yesu Kristo baada ya kuelezea mabadiliko ya tawi la mtini akasema; “nanyi kadhalika, myaonapo hayo yote, tambueni ya kuwa yu karibu milangoni” (Mathayo 24:33).

            Lakini tukumbuke ya kuwa “tawi” la mtini haliwezi likawa na mabadiliko au haliwezi kuwepo kama tawi ikiwa mtini “haujapandwa na kuota”.

            Kwa hiyo, ikiwa Yesu Kristo alipotoa mfano wa mtini alikuwa anaulinganisha na Taifa la Israeli, basi, ni muhimu tujue alitaka tufahamu ya kuwa Israeli itakapokuwa Taifa na kujitawala katika nchi yake yenyewe, ndipo tunapotakiwa kuangalia mabadiliko yaliyotabiriwa kutokea juu yake! Kwa kuwa mabadiliko hayo yanaonyesha na kuashiria ukaribu wa kurudi kwa Yesu Kristo kulichukua Kanisa.

Tawi linapochipua halileti mabadiliko, bali linatoa taarifa juu ya mabadiliko, yaliyokwisha kutokea katika eneo mtini ulipo! Umepata tunachotaka ukione hapa? Ngoja turudie! Tawi linapochipuka huwa halileti mabadiliko ya msimu kwa kuchipia kwake, bali kwa kuchipua kwake, tawi hilo huwa linatoa taarifa kwa walitazamao ya kuwa kuna mabadiliko ya msimu au nyakati katika eneo ambalo mti huo umepandwa!

            Israeli “imepandwa” lini na kuwa Taifa? Ilipandwa mwaka 1948 kwa tamko rasmi la Umoja wa Mataifa ulio na makao makuu yake nchini Marekani katika jiji la New York. Kwa hiyo tunaweza kusema 1948 ni mwaka ambao mtini (Israeli) ulipandwa!

            Yesu Kristo anatuambia tuagalie mabadiliko yanayotokea juu ya tawi la mtini kutokana na majira yaliyowekwa juu yake. Halafu akasema “nanyi kadhalika, myaonapo hayo yote …” tuyaonapo yote – yapi? … ni yale yaliyatabiriwa kutokea juu ya Taifa la Israeli kuanzia mwaka 1948!.

            Ni mambo gani yaliyotabiriwa kutokea juu ya Taifa la Israeli baada ya mwaka 1948? Pamoja na kwamba yako mambo kadhaa yaliyotabiriwa juu ya Israeli juu ya siku za mwisho, kabla na baada ya mwaka 1948, itakusaidia ukifuatilia kwa karibu maeneo yafuatayo:-

1.                   Mipaka ya ardhi ya nchi ya Israeli.

2.                   Umiliki wa mji wa Yerusalemu.

3.                   Ujenzi wa hekalu la tatu.

4.                   Mabadiliko ya uongozi wa juu wa Taifa la Israeli.

            Kumbuka jambo hili unapofuatilia mambo haya: Tawi la mtini linapochipuka na kuchanua huwa – halileti mabadiliko ya msimu – bali linatoa taarifa ya mabadiliko ya msimu yaliyokwisha kutokea tayari!

            Kwa hiyo basi unapofuatilia mambo hayo manne makubwa fahamu ya kuwa kutokea kwa mabadiliko yaliyotabiriwa kutokea juu ya taifa la Israeli- ni njia ya Mungu kuliarifu Kanisa, watumishi wake, na ulimwengu wote ya kuwa kurudi kwa Yesu Kristo kuja kilichukua Kanisa kumekaribia sana!

            Kwa maneno mengine, Mungu anataka tuiangalie Israeli kama “saa ya nyakati za” au “Kipima muda cha” siku za mwisho; na mabadiliko yaliyotabiriwa kutokea baada ya Israeli kuwa Taifa mwaka 1948 yatakuwa yanatuonyesha ukaribu wa ‘siku ile na saa ile” ambayo “hakuna aijuaye – hata malaika walio mbinguni wala Mwana, ila Baba peke yake” (Mathayo 24: 36).

            Vita vilivyodumu siku sita ambavyo Israeli ilipigana na majeshi ya nchi za Kiarabu Juni 1967 vilikuwa ni vita vilivyotoa taarifa kwa Kanisa, kwa watumishi wa Mungu, na kwa ulimwengu wote ya kuwa msimu mpya katika siku za mwisho umeujilia ulimwengu, na kurudi kwa Yesu Kristo kunazidi kukaribia sana!

            Hivi vita viligusa mambo yote manne tuliyoyaorodhesha hapo juu, kwa hiyo ni muhimu uyafuatilie unapojifunza juu ya Taifa la Israeli.

            Vita hivyo vya siku sita vya Juni 1967 vilipokoma, na Israeli ikiwa imeshinda vita hivyo, mambo ya kinabii yaliyotabiriwa yalitokea ni kama ifuatavyo:-

1.                  Mipaka ya Nchi ya Israeli.

            Israeli ilipopewa utaifa na Umoja wa Mataifa – mipaka ya Nchi yake haikuwa sawa na ile ambayo Mungu alikuwa ameiweka ya kuwa itakuwa mipaka ya nchi ya Israeli katika siku hizi za mwisho.

            Lakini vita vya Juni 1967 vilimalizika kwa namna ambayo nchi ya Israeli ilipanua au “ilichanua kama mtini” mipaka yake na kujikuta imepanua ukubwa wa nchi yake hadi kufikiwa kwa sehemu kubwa kwa mipaka ambayo Mungu aliwapa kama tusomavyo katika Kitabu cha Hesabu 34: 1-12.

2.                  Umiliki wa mji wa Yerusalemu.

            Umoja wa Mataifa ulipokuwa unaipa Israeli utaifa katika nchi ya kaanani, mwaka 1948 pia uliugawa mji wa Yerusalemu katika umiliki wa mataifa mawili. Upande wa Magharibi wa mji wa Yerusalemu ndio uliokabidhiwa kwa Taifa la Israeli, na upande wa Mashariki mji wa Yerusalemu lilikabidhiwa Taifa la Jordani.

            Upande wa mashariki mwa mji wa Yerusalemu ndiko kulikokuwa na maeneo muhimu sana yaliyohusu historia ya Taifa la Israeli. Huko ndiko uliko mlima mtakatifu – ambako hekalu za Mfalme Sulemani na Herode zilijengwa. Pia, ndiko kuliko na mlima wa Mzeituni, bustani ya Getsemani, na chuo kikuu cha Kiebrania (Hebrew University).

            Kwa ajili hiyo, Umoja wa Mataifa ukatengeneza mkataba mwaka huo wa 1948 ulioitaka Serikali ya Jordani kuwaruhusu Wayahudi wanaotaka kwenda kuabudu kwenye Mlima mtakatifu wawe na uhuru wa kufanya hivyo. Lakini serikali ya Jordani ya wakati huo, licha ya kuridhia na kutia sahihi mapatano hayo, ilikataa kuwaruhusu Wayahudi kwenda kuabudu katika mlima mtakatifu uliokuwa mashariki mwa mji wa Yerusalemu. Kukataa huku kulifanya Wayahudi washindwe kwenda kuabudu kwenye mlima mtakatifu kwa muda wa miaka 19.

            Wakati wa vita vya Juni 1967, Jeshi la Israeli liliteka upande wa mashariki wa mji wa Yerusalemu, na kwa kufanya hivyo kutimiza unabii wa Yesu juu ya mji wa Yesuralemu aliosema; “na Yerusalemu utakanyagwa na Mataifa, hata majira ya Mataifa yatakapotimia” (Luka 21: 24).

            “Majira ya Mataifa” yalitimia Juni 1967! Mji wa Yerusalemu ukaanza kuhesabu siku za majira mapya juu yake kama mji mmoja ulio “kiti” cha utawala cha mfalme Daudi, na cha Taifa la Israeli!

3.                  Mabadiliko ya Uongozi wa juu wa Taifa la Israeli.

            Kama tulivyokwisha kukueleza juu ya mji wa Yerusalemu, fahamu ya kuwa Juni 1967 kuliingia kipindi kipya cha kinabii juu ya uongozi wa Taifa la Israeli.

            Hii ni kwa sababu mji wa Yerusalemu ndipo panapotakiwa pawe “kiti” cha utawala wa taifa la Israeli katika siku hizi za mwisho. Kabla ya Juni 1967 ilikuwa vigumu kuzungumzia jambo hili, maana mji wa Yerusalemu ulikuwa umegawanywa kwa mataifa mawili – Israeli na Jordani.

            Vita hivyo vilipomalizika vilirudisha sehemu ya mashariki ya mji wa Yerusalemu mikononi mwa taifa la Israeli, na kutimiza andiko la Luka 21:24 linalosema “na Yerusalemu utakanyagwa na Mataifa, hata majira ya Mataifa yatakapotimia”.

            Kwa matiki hii miaka ya kinabii ya Uongozi juu ya Taifa la Israeli yaliingia ukurasa mpya Juni 1967.

            Mtu anayefuatilia kwa karibu juu ya miaka ya uongozi juu ya Taifa la Israeli, atakuwa anajua ya kuwa miaka arobaini – arobaini imejitokeza katika historia ya taifa la Israeli kuwa ni kipindi muhimu.

            Kwa Mfano: Wana wa Israeli walikuwa chini ya Utawala wa uongozi wa Mwamuzi Othinieli kwa miaka arobaini (Waamuzi 3: 9 – 11). Pia wana wa Israeli walikaa chini ya uongozi wa Mwamuzi Baraka kwa miaka arobaini (Waamuzi 5: 31). Tena wakawa chini ya uongozi wa Gedioni kwa muda wa miaka aroabaini (Waamuzi 8: 28). Halafu wakawa chini ya uongozi wa Wafilisti kwa jumla ya miaka arobaini (Waamuzi 13:1).

            Umewahi kujiuliza kwa nini miaka arobaini – arobaini ijurudie – rudie, kwa jinsi hii, – tena katika taifa moja?

            Ukiendelea kufuatilia historia ya wana wa Israeli utaona ya kuwa waliwahi kuwa chini ya uongozi wa kuhani Mkuu Eli kwa muda wa miaka arobaini (1 Samweli 4: 18). Tena wakawa chini ya Mfalme Sauli kwa muda wa miaka arobaini (Matendo ya Mitume 13: 21). Mfalme Daudi alitawala juu ya wana wa Israeli kwa miaka arobaini (2 Samweli 5:4). Mfalme Sulemani aliyechukuwa utawala baada ya Mfalme Daudi – naye alitawala juu ya wana wa Israeli kwa miaka arobaini (1 Wafalme 11:42). Halafu wana wa Israeli waliwahi kuwa chini ya Mfalme Yoashi kwa miaka arobaini pia (2 Mambo ya Nyakati 24:1).

            Kipindi hicho cha miaka arobaini  katika mara zote tulizozinukuu, kilikuwa kinaashiria mwisho wa kipindi kimojawapo cha utawala na kuanza kwa kipindi kingine cha utawala.

            Na ikiwa tutaamua kujifunza kutoka kwa mtini kama Yesu alivyosema – tutaelewa ya kuwa mabadiliko ya tawi la mtini yanatoa taarifa ya mabadiliko ya msimu.

            Kwa hiyo “miaka arobaini” juu ya “kiti” cha “Daudi” yaani mji wa Yerusalemu ni kipindi muhimu sana.

            Ukichukua Juni 1967, kipindi ambacho mji wa Yerusalemu ulipokuwa unamaliza “msimu wa kukanyagwa na Wamataifa”, hii ilikuwa taarifa ya kinabii ya mwisho wa msimu wa utawala mmoja na mwanzo wa msimu wa utawala mwingine! Na ukijumlisha miaka arobaini tokea Juni 1967 utajikuta unafika Juni 2007!

            Kwa hiyo basi, Juni 2007 imeashiria na kutangaza msimu mpya katika majira na nyakati za Kiroho na za Kisiasa juu taifa la Israeli.

            Je, kuna uhusiano wo wote kati ya mabadiliko ya nafasi ya Urais wa Israeli uliotokea Juni 2007 na msimu mpya wa uongozi katika ratiba ya Mungu juu ya taifa la Israeli?

            Kama watumishi wa Mungu wanaomtumikia Mungu katika kizazi hiki, tukikazana kwa nia zote, na juhudi zote kuwapa watu chakula cha neno la Mungu kwa wakati wa Mungu, hatuwezi kukwepa kuangalia kwa makini matukio ya yale yaliyotabiriwa yanapotokea juu ya taifa la Israeli!

            Kwetu sisi ni ishara muhimu ya ukaribu wa ujio wa Bwana Yesu Kristo kulichukua Kanisa. Kwa hiyo huu si wakati wa “kulala” au “kuzembea” au “kulegea” au “kusuasua” au “kuzubaa” au “kuchelewa” au “kusita” – katika kumtumikia Mungu!.

4.                  Ujenzi wa Hekalu la Tatu.

            Yesu Kristo alisema hivi; “Basi hapo mtakapoliona chukizo la Uharibifu, lile lililonenwa na nabii Daniel limesimama katika patakatifu (asomaye na afahamu) …” (Mathayo 24:15).

            Maneno haya yalikuwa yanaashiria kuwepo kwa hekalu jingine katika mlima mtakafitu. Jambo la ujenzi wa hekalu la tatu katika milma mtakatifu lilikuwa ni ndoto ambayo ilikuwa haitekelezeki kabla ya kumalizika kwa vita vya Juni 1967. Kwanza, kwa sababu eneo hilo la mlima mtakatifu lilikuwa linamilikiwa na Serikali ya Jordani kihalali kwa amri ya Umoja wa Mataifa; na pili kwa sababu eneo la juu ya mlima mtakatifu pamejengwa Msikiti wa Kiislamu!

            Lakini ushindi uliotokea kwa Israeli katika vita hiyo ya Juni 1967 kulifungua mlango wa kutimia kwa andiko hili la Biblia la Ufunuo wa Yohana 11: 1, 2 linalosema:

            “Nikapewa mwanzi kama fimbo; na mmoja akaniambia, Inuka, ukalipime hekalu la Mungu, na madhabahu, na hao wasujuduo humo. Na behewa iliyo nje ya hekalu uiache nje wala usipime, kwa maana Mataifa wamepewa hiyo …”

            Viongozi wa Israeli wa wakati huo wa Juni 1967 waliamua kuwapa Waislamu “Kihalali” eneo hilo la mlima mtakatifu, ili waendelee kulitumia kama sehemu ya ibada zao katika msikiti wao. Na kibali hicho kilitimiza andiko linalosema; “Na behewa iliyo nje ya hekalu uiache nje wala usiipime, kwa maana Mataifa wamepewa hiyo, nao wataukanyaga mji mtakatifu miezi arobaini na miwili”.

“… miezi arobaini na miwili” ni miaka mitatu na nusu ambayo inahusu sehemu ya kipindi cha miaka saba cha utawala wa  Mpinga Kristo hapa duniani, ambacho bado kiko mbele yetu – hakijatokea bado!

            Kwa hiyo, ikiwa katika kipindi hicho kutakuwa na “hekalu na Msikiti” kwa wakati mmoja, basi ina maana hekalu la tatu ambalo halipo kwa sasa litajengwa!

            Hii ina maana kwa mara ya kwanza tangu Israeli iwe Taifa mwaka 1948, vita vya Juni 1967 vilifungua mlango wa uwezekano mkubwa sana wa ujenzi wa hekalu la tatu katika mlima mtakatifu, bila kuubomoa msikiti uliopo!

Ni jambo gani linalokupunguzia
“Utayari wako” ndani yako wa 
kumtumikia Mungu “kwa wakati
wake”?

            Tazama ndani ya moyo wako, utayari wako ulionao wa kumtumikia Mungu katika zamu yako, na katika eneo lako, je umepungua au umeongezeka?

            Ikiwa utayari wako umepungua basi unahitaji kujipanga upya ndani ya Bwana Yesu Kristo!

 Je, umewahi kujiuliza Yesu Kristo akirudi sasa hivi – atakukuta katika zamu yako ukifanya sehemu yako katika kuwapa watu chakula “kwa wakati wake” ikiwa ina maana “kwa wakati wa Mungu”?

            Je una cha kujitetea? Una kisingizio gani au sababu gani ya kupunguza utayari wako ndani yako wa kumtumikia Mungu?

            Mungu azidi kukuandaa juu ya ujio wa Yesu Kristo. Maranatha!

UNATAKA KUOKOKA?
Kama unataka kumpa YESU maisha yako sasa, bonyeza hapa
©2003 Tanzania Social and Economic Trust.  All Rights Reserved.