|
|
| ||
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
Tunakusalimu
katika jina la Yesu Kristo. Karibu katika kuisoma barua yetu hii ya
mwezi huu ambayo ni mfululuzo wa pili katika kukujulisha na kukufundisha
juu ya uhusiano uliopo kati ya kumtumikia Mungu na taifa la Israeli. Katika
barua ya kwanza katika mfululuzo huu tuliyoitoa mwezi uliopita tuliuliza
maswali mawili muhimu nayo ni haya: Swali
la kwanza: je, unajua uhusiano uliopo kati ya wito wa kumtumikia Mungu
katika nyakati hizi za mwisho na Taifa la Israeli? Swali
la kwanza: je, unajua ya kuwa usipomtumikia Mungu ipasavyo kuna
uwezekano wa kuikosa mbingu? Mwezi
huu tunaendelea kuchambua kwa undani juu ya jambo hili. Wakati ni muhimu katika uhusiano
Katika Mathayo Sura ya 24 Yesu Kristo amezungumza na kusisitiza
juu ya wakati mara kumi na mbili kwa kutumia maneno tofauti – tofauti!
Na ilipofika kuzungumzia juu ya watumishi wake, anataka muda wake au wakati wake wa kurudi utakapofika, anatarajia
awakute watumishi wake wakiendelea “kuwapa
watu chakula kwa wakati wake”.
Kwa “wakati wake”
akiwa ana maana ya kuwa kuwapa watu chakula cha neno la Mungu katika
wakati unaotakiwa! Kila mtu anatakiwa afanye jukumu linalomhusu, na
wajibu unaomhusu, katika wakati unaotakiwa, huku akijua ya kuwa kurudi
kwa Yesu Kristo kumekaribia sana!
Kwa nini? Kwa sababu kujali ukaribu “wakati”
wa kurudi wa Bwana Yesu Kristo ni muhimu sana – unapounganishwa na
kupeleka chakula cha neno la Mungu kwa watu.
Kwa Mfano; kwa kuwa hakuna aijuaye “siku
ile wala saa ile” – neno la Mungu linasaidia kuwapa watu “utayari”
wa kujua ya kuwa “wakati
wa mavuno karibu”, na ya kwamba Yesu Kristo “yu karibu milangoni”.
Lakini pia neno la Mungu linatuambia ya kuwa kurudi kwa Yesu
Kristo kunategemea kuhubiriwa kwa “habari
njema ya Ufalme … katika Ulimwengu wote” (Mathayo
24:14).
Hii ikiwa na maana ya kwamba, ikiwa tunataka Yesu Kristo arudi
haraka, basi ni muhimu kila mtu “kwa
wakati wake”, ashike zamu ya utumishi wake ipasavyo, bila kuzembea
wala kulegea! Kumbuka Biblia inasema; “Na
alaaniwe mtu afanyaye kazi ya Bwana kwa ulegevu ….” (Yeremia
48:10).
Tena ni lazima kila amtumikiaye Mungu katika ngazi yo yote ile,
ajue hana muda wote anaodhani ya kuwa anao wa kumtumikia Mungu. Yesu
Kristo alisema; “Imetupasa
kuzifanya kazi zake yeye aliyenipeleka maadamu ni mchana; usiku waja
asipoweza mtu kufanya kazi” (Yohana
9:4).
Unataka siku ile Yesu Kristo atakaporudi akuambie nini kama
mtumishi wake? Tafakari maneno yafuatayo; “ … mtumwa (mtumishi) mwaminifu na mwenye akili …” (Mathayo 24:45). “ … mtumwa (mtumishi) … mbaya …” (Mathayo 24:48). “vema, mtumwa (mtumishi) mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya
mengi; ingia katika furaha ya bwana wako” (Mathayo
25:21). “Wewe mtumwa (mtumishi) mbaya na mlegevu …” (Mathayo 25:26). “Na mtumwa (mtumishi) yule asiyefaa, mtupeni mbali katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio
na kusaga meno” (Mathayo 25:30).
Unataka maneno gani yawe yako kati ya hayo tuliyosoma hapa juu
Yesu Kristo atakapokuwa “anawalipa” watu kwa utumishi ule
waliomtumikia? Je, itakuwaje kwako ukijikuta unaikosa furaha ya mbingu
kwa ajili ya kutokumtumikia Mungu kwa kujali “wakati
wake”.
Kwa nini uikose mbingu kwa kutokumtumikia Mungu ipasavyo kwa “wakati wake”? Tunaujua “wakati wake” kwa
“Wakati wake” maana yake “wakati wa Mungu” Si wakati wetu-
Hapana! Bali wakati wake!
Mungu anataka tuwape watu chakula cha neno la Mungu kwa wakati
wake na siyo kwa wakati wetu sisi.
Mungu anajua watu wanahitaji chakula kipi cha neno lake, na kwa
wakati wake upi! Na ndilo analotaka watumishi wake wajue, na ndilo
analotaka walifuate – kuwapa watu chakula cha neno la Mungu kwa wakati
wake!
Watumishi wanapojichagulia chakula cha neno lolote la Mungu na
kuwapa watu kwa wakati wao na si wakati wa Mungu – ni kwenda kinyume
na mapenzi ya Mungu!
Kwa kuwa hakuna aijuaye siku ile na saa ile itakuwa lini, Yesu
Kristo alihakikisha anawapa watumishi wake mahali pa kuangalia ili
wapate kujua ukaribu wa wakati wa ujio wake.
Kabla Yesu Kristo
hajatoa angalizo lake kwa watumishi wake katika siku hizi za mwisho juu
ya kujali “wakati wake” katika kuwapa watu neno la Mungu, tunaona
kwanza akitoa angalizo la jambo
la kutokuijua siku ile wala saa ile!
“Walakini habari ya siku
ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio Mbinguni, wala Mwana,
ila Baba peke yake. Kwa maana kama vile ilivyokuwa siku za Nuhu, …
kama vile siku zile zilizokuwa kabla ya Gharika … ndivyo kutakavyokuwa
kuja kwake Mwana wa Adamu, wakati ule … mmoja atwaliwa, mmoja aachwa”
(Mathayo 24: 36 – 41).
Hili lilikuwa angalizo muhimu, ili mtu awaye ye yote asije
akaweka tarehe na saa ya “Siku
ile na saa ile”. Lakini kwa kuwa kujua ukaribu wa siku ile na saa ile ni muhimu kwa kila mtu nasi kwa
watumishi wa Mungu tu – Yesu Kristo alihakikisha anatueleza mahali pa
kuangalia juu ya ukaribu wa wakati wa ujio wake!
Yesu Kristo alisema hivi juu ya jambo hili. “Basi
kwa mtini jifunzeni mfano; tawi lake likiisha kuchipuka na kuchanua
majani, mwatambua ya kuwa wakati wa mavuno ukaribu; nanyi kadhalika,
myaonapo hayo yote, tambueni ya kuwa yu karibu, milangoni” (Mathayo
24: 32 – 33).
Yesu Kristo alitaka na anataka tujue ya kuwa ili kufahamu ya kuwa
“yu karibu milangoni”
akiwa na mama ya “ukaribu
wa kurudi kwake” – basi ni muhimu tujifunze kutoka kwenye
mabadiliko yanayotokea katika mti wa mtini!
Mwezi huu tunaishia hapa. Soma barua yetu ya mwezi ujao ili upate
mambo tuliyoyatayarisha katika kuhitimisha maelezo juu ya uhusiano
uliopo kati ya kumtumikia Mungu na taifa la Israeli.
Tuzidi kuombeana. |
|