Yesu Akamwambia "Lisha Kondoo Zangu" (Yohana 21:17)
Home
Maombi
Ratiba
Shuhuda
Mafundisho
Maswali na Majibu
Barua za Mwezi
Kuchangia Huduma

Barua ya Mwezi Machi 2007                                                            Kutoka kwa Christopher na Diana Mwakasege


Salamu katika Jina la Yesu Kristo,

HUWEZI KUONDOA JAMBO LA UCHUMI

NDANI YA DAMU YA YESU

Ni kweli kabisa! Hata kama ungetaka kutenganisha mambo ya uchumu na damu ya Yesu – usingeweza! Huwezi kuondoa jambo la uchumi ndani ya au kwenye damu ya Yesu!

Hebu tuangalie sababu tatu za msingi zinazofanya mtu asiweze kuondoa jambo la uchumi ndani ya damu ya Yesu.

Sababu ya Kwanza: Agano jipya katika damu ya Yesu linahusisha pia jambo la uchumi.

Yesu Kristo alipokuwa anazungumza na wanafunzi wake juu ya agano jipya – pamoja na mambo kadhaa aliyowaambia – pia alisema maneno haya:

 “Kikombe hiki ni agano jipya katika
damu yangu,inayomwagika kwa ajili
yenu”
(Luka 22:20)

Ukiifuatilia habari hii katika biblia huoni wanafunzi wa Yesu wakiuliza maswali juu ya agano jipya – hii ikiwa ni ishara ya wao kuelewa jambo ambalo Bwana Yesu alikuwa anawaeleza.

Neno hili “agano” maana yake ni mapatano, au makubaliano, au maelewano, baina ya pande zisizopungua mbili,huku yakiwa na masharti au ahadi ndani yake toka pande zinazohusika na agano hilo.

Ile kusema “agano jipya” maana yake hilo si agano la kwanza. Lilikuwepo agano la kwanza linalojulikana zaidi kama agano la kale lililofanyika kati ya Mungu na wanadamu, na hili analolisema Bwana Yesu katika Luka 22:20 ni agano la pili au agano jipya.

Biblia inatuambia ya kuwa agano jipya ni bora kuliko agano la kale, kwa kuwa agano jipya limewekwa “juu ya ahadi zilizo bora” (Waebrania 8:6).

Kufuatana na Waebrania 8:7,13 agano la kwanza lilikuwa na mapungufu ambayo yameshughulikiwa na agano jipya.

La msingi kujua ni kwamba katika maagano hayo mawili, kulitolewa nafasi ya makubaliano ya mabadilishano kwa njia ya kumwagika damu.

Ndiyo maana tunasoma ya kuwa, “kwa hiyo hata lile la kwanza halikuanzwa pasipo damu” ( Waebrania 9:18).

Katika agano la kale, ilitumika damu ya wanyama, na katika agano jipya imetumika damu ya Yesu – kuhalalisha na kuthibitisha mapatano hayo.

Kufuatana na Waebrania 9:16-20 ilikuwa muhimu damu itumike kuhalalisha na kulithibitisha agano kwa kuwa agano “…..lina nguvu palipotukia kufa kwa mtu; kwa kuwa halina nguvu kabisa, akiwa yu hai yeye aliyelifanya”.

Ndiyo maana Yesu ilimbidi si tu amwage damu yake – bali kumwagika kwa damu yake kuambatane na kifo chake – kifo chake msalabani!

Ni pale msalabani ambapo kulitokea nafasi ya mwanadamu ye yote kwenda kubadilishana na Mungu mizigo aliyonayo ili asiendelee kuibeba.

Ukipeleka dhambi zako msalabani Mungu anakupa msamaha na utakatifu wake. Ukipeleka ugonjwa wako msalabani, Mungu anakuponya na kukupa afya yake. Ukipeleka huzuni yako msalabani, Mungu anakufariji na kukupa furaha yake.

Hayo ni baadhi tu ya mabadilishano yanayofanyika msalabani kwa sababu ya agano jipya katika damu ya Yesu, iliyomwagika kwa ajili yetu.

Jambo ambalo si wengi wanalijua na wengi wa wale wanaolijua si wote wanaolikubali ni kwamba: Ukipeleka umaskini wako msalabani, Mungu anakupa utajiri wake!

Haya mabadilishano kati ya umaskini wa mtu na utajiri wa Mungu yanafanyika msalabani kwa umwagiko wa damu ya Yesu.

Tunasoma katika kitabu cha 2 Wakorintho 8:9 ya kuwa: “maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri,ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake”

Hii inaonyesha wazi ya kuwa ndani ya agano jipya katika damu ya Yesu Kristo kuna fursa ya mtu kupata msaada wa kuondokana na uchumi mbaya au uchumi usioridhisha.

Kwa sababu ya 2 Wakorintho 8:9 mtu ye yote hawezi akaondoa jambo la uchumi ndani ya damu ya Yesu!

Tupo pamoja mpaka hapo! Msalabani usiende kutafuta msaada wa matatizo machache tu, bali matatizo yote uliyonayo unaweza ukapata msaada wake hapo, hata kama ni tatizo la ki-uchumi.

Sababu ya Pili:

Kwa sababu ya kile kinachokumbukwa wakati wa kusheherekea sikukuu ya pasaka – ni pamoja na mtu kukombolewa ki-uchumi.

Kusulubiwa kwa Bwana Yesu kulitokea wakati wa sikukuu ya pasaka. Tunasoma katika kitabu cha Luka 22:15 Bwana Yesu akiwaambia wanafunzi wake ya kuwa: “Nimetamani sana kuila pasaka hii pamoja nanyi kabla ya kuteswa kwangu”.

Wakati wakiendelea na sherehe hiyo ya pasaka ndipo aliposema maneno haya: “….kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu, inayomwagika kwa ajili yenu” (Luka 22:20).

Kulikuwa na sababu kubwa sana kwa tukio hilo la Yesu Kristo kuangikwa msalabani kufanyika wakati wa sherehe za pasaka.

Habari ya chimbuko za sherehe za pasaka unazipata katika kitabu cha Kutoka 12:1-51.

Katika habari hii tunaona ya kuwa “damu ya mwana-kondoo” iliyowekwa juu ya miimo ya kila mlango wa nyumba ya wana wa Israeli – iliwafanya wasipate pigo lililowapata wamisri la kufiwa na wazaliwa wa kwanza wote wa wanadamu na wa wanyama.

Hili ndilo pigo la mwisho lililomfanya Farao awaachie wana wa Israeli waweze kutoka katika utumwa wa Misri na kuanza safari ya kwenda Kaanani.

Huu ulikuwa ni ukombozi toka katika utumwa wa kiuchumi na wakapata uhuru wa kiuchumi. Uhuru huu wa kiuchumi waliupata kwa msaada wa damu ya mwana-kondoo iliyomwagwa kwa ajili ya kila nyumba!

Hilo lilikuwa ni pigo ambalo Farao alishindwa kulivumilia. Damu ya wana-kondoo ilifanya mambo kadhaa hapo: (i) Ilifungulia adhabu kwa Farao na watu wake, (ii) Iliweka ulinzi juu ya nyumba za wana wa Israeli, na (iii) Ilifungulia fursa ya wana wa Israeli kupata uhuru wa kujitawala kiuchumi chini ya Mungu wao.

Ukitaka kuhakikisha ya kuwa huo ulikuwa ni uhuru wa kiuchumi, soma na tafakari maneno ambayo Mungu alizungumza na Musa alipokuwa anamtuma kuwatoa wana wa Israeli utumwani.

Mungu alimwambia Musa ya kuwa: “nimeshuka ili niwaokoe na mikono ya Wamisri, niwapandishe kutoka nchi ile, hata nchi njema, kisha pana; nchi ijaayo maziwa na asali……. (Kutoka 3:8).

Kumbukumbu ya Torati 8:7-9, Musa anawaambia wana wa Israeli ya kuwa Mungu amewakomboa toka katika utumwa wa Misri, na anawaingiza, “……katika nchi nzuri, nchi yenye vijito vya maji, na chemchem, na visima, vibubujikavyo katika mabonde na vilima, nchi ya ngano na shayiri, na mizabibu, na mitini, na mikomamanga; nchi ya mizeituni yenye mafuta, na asali ……

……nchi utakayokula mikate humo, pasina shida, hutapungukiwa na kitu ndani yake; nchi ambayo mawe yake ni chuma, na milima yake yafukuka shaba”.

Hali hii nzuri ya uchumi wao (wana wa Israeli) waliipata kwa msaada wa damu ya wana-kondoo iliyomwagika wakati wanajiandaa kuondoka utumwani Misri.

Kufuatana na Kutoka 12:11 neno “pasaka ya Bwana” lilianza kutumika siku hiyo. Na wakaambiwa “Nanyi mtalitunza jambo hili kuwa amri kwako na kwa wanao milele” (Kutoka 12:24).

Ndipo tunamsikia Yesu Kristo akiwaambia wanafunzi wake juu ya “pasaka” ya wakati wao ilivyoangukia wakati wa kumwagika kwa damu yake!

Na tangu wakati huo sherehe ya pasaka inafanyika kwa “ukumbusho” au kwa kumbukumbu ya kumwagika kwa damu ya Yesu Kristo.

Damu ya Yesu ni bora kuliko damu ya kondoo. Ikiwa damu ya kondoo Mungu aliitumia wakati ule kuwakomboa wana wa Israeli toka utumwa wa kiuchumi, si zaidi sana Mungu akaitumia Damu ya Yesu Kristo katika kututoa toka kwenye utumwa wa kiuchumi?

Ndio maana katika 2 Wakorintho 8:9 tunaona mabadilishano kati ya umaskini wa mtu na utajiri wa Mungu katika damu ya Yesu.

Ni vigumu kuelewa umuhimu wa mstari huu wa 2 Wakorintho 8:9 – ikiwa mtu hajui ya kuwa umaskini au utajiri chanzo chake ni katika ulimwengu wa roho.

Kati ya matokeo ya dhambi iliyofanyika katika bustani ya Edeni ni kuharibika kwa mahusiano ya kiuchumi kati ya mtu na dunia.

Ukisoma maneno ya Mwanzo 3:17-19 utaona ya kuwa dhambi ilimfanya mtu apoteze uwezo wake wa kumiliki uchumi ki-Mungu.

Tangu wakati huo shetani alichukua nafasi ya kuumiliki uchumi katika ulimwengu wa roho, na anataka kumsaidia mwanadamu awe na uchumi mzuri bila kumtii Mungu. Hii inathibitishwa na habari tunazozisoma katika Luka 4:5-7 na Ufunuo wa Yohana 13:16,17.

Mwanadamu anapomkubali Yesu Kristo kama Bwana na Mwokozi wake, si tu kwamba anasamehewa dhambi zake tu, bali pamoja na kusamehewa dhambi – damu ya Yesu inamkomboa pia toka kwenye madhara yaliyoletwa na dhambi – hii ikiwa ni pamoja na madhara ya kuharibika kwa uchumi.

Kwa sababu ya yale yaliyosababisha kumbukumbu ya pasaka ya Bwana kuwepo, mtu hawezi akaliondoa jambo la uchumi ndani ya damu ya Yesu.

Usikose kusoma barua yetu ya mwezi ujao ili tukumalizie sehemu ya ujumbe huu muhimu.

Tuzidi kuombeana
UNATAKA KUOKOKA?
Kama unataka kumpa YESU maisha yako sasa, bonyeza hapa
©2003 Tanzania Social and Economic Trust.  All Rights Reserved.