Yesu Akamwambia "Lisha Kondoo Zangu" (Yohana 21:17)
Home
Maombi
Ratiba
Shuhuda
Mafundisho
Maswali na Majibu
Barua za Mwezi
Kuchangia Huduma

Barua ya Mwezi Mei 2007                                                            Kutoka kwa Christopher na Diana Mwakasege


Salamu katika Jina la Yesu.

            Tunaamini Mungu anaendelea kukusaidia. Tena tunamshukuru Mungu kwa kukupa nafasi ya kusoma barua yetu ya mwezi huu.

            Barua hii ni mwanzo wa mfululizo wa barua tatu tunazolenga kukushirikisha juu ya uhusiano uliopo kati ya kumtumikia Mungu na taifa la Israeli. Tunaamini utapata mengi ya kukusaidia.

            Maswali mawili ya msingi:

Swali la Kwanza:            Je, unajua uhusiano uliopo kati ya wito wa kumtumikia Mungu katika nyakati hizi za siku za mwisho na Taifa la Israeli?

Swali la Pili:       Je, unajua ya kuwa usipomtumikia Mungu ipasavyo kuna uwezekano wa kuikosa Mbingu?

Swali hili la pili ndilo linalotufanya tutoe angalizo hili kwa wale wanaomtumikia Mungu katika kizazi hiki. Angalizo lenyewe ni hili – ya kwamba – usipomtumikia Mungu ipasavyo kuna uwezekano wa kuikosa Mbingu!

            Ni kitu gani kinatufanya tufikie uamuzi huu wa kutoa angalizo hili kwa wanaomtumikia Mungu?

            Haya ni baadhi ya matokeo ya kuanza kuisoma upya Biblia ili kuona jinsi inavyoioanisha nchi ya Israeli na Kanisa.

Mwanzoni mwa mwezi Mei mwaka 2007 tulipata nafasi ya kuitembelea Nchi ya Israeli kwa mara ya kwanza katika maisha yetu. Safari hiyo tuliyoongozana na wenzetu kadhaa, – jumla tukiwa watu arobaini, – iliweka ndani yetu hamu mpya ya kutaka kujua umuhimu wa uhusiano wa Taifa la Israeli kwa Kanisa, kwa kuisoma Biblia kwa upya; tukitaka kujua inasema nini juu ya jambo hili.

            Jambo mojawapo tuliloliona kwa upya, na tunalotaka kukushirikisha hapa, ni lile la uhusiano uliopo kati ya wito wa kumtumikia Mungu na Taifa la Israeli; na jambo hili la uwezekano wa mtumishi wa Mungu kuikosa Mbingu kwa kutokumtumikia Mungu ipasavyo.

            Je unajua kitu alichosema Yesu Kristo juu ya mtumishi wake atakayemkuta hafanyi mapenzi ya Mungu “kwa wakati wake” katika kuwapa watu wake “Posho au chakula”?

            Hebu kwanza tuangalie Yesu Kristo alisema nini juu ya ujio wake wa kulichukua Kanisa – alisema hivi: “Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu. Lakini fahamuni neno hili; kama mwenye nyumba angalijua ile zamu mwivi atakayokuja, angalikesha, wala asingeliacha nyumba yake kuvunjwa. Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja(Mathayo 24:42 – 44).

Baada ya kusema maneno hayo – ndipo Yesu Kristo alipoweka angalizo hili kwa watumishi wa Mungu.

            “Ni nani basi yule mtumwa mwaminifu mwenye akili, ambaye bwana wake alimweka juu ya nyumba yake, awape watu chakula kwa wakati wake? Heri mtumwa yule, ambaye bwana wake ajapo atamkuta akifanya hivyo. Amini, nawaambieni, atamweka juu ya vitu vyake vyote”.

            “Lakini mtumwa yule mbaya akisema moyoni mwake, Bwana wangu anakawia; akaanza kuwapiga wajoli wake, na kula na kunywa pamoja na walevi; bwana wake mtumwa huyo atakuja siku asivyodhani, na saa asiyojua, atamkata vipande viwili, na kumwekea fungu lake pamoja na wanafiki; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno” (Mathayo 24:45 – 51).

            Ukitaka kutafakari angalizo hili la Yesu Kristo kwa uzito na umuhimu unaostahili – basi ondoa neno “mtumwa” weka badala yake neno “mtumishi”. Hii ni kwa sababu neno mtumwa hapa limetumika likiwa na maana ya mtumishi!

            Ukitafakari maneno haya ya Bwana Yesu Kristo utaona ya kuwa hili ni angalizo linalokwenda moja kwa moja kwa watumishi wa Mungu!

            Kwa Mfano – hebu soma maneno haya kwa upya; “Ni nani basi mtumishi mwaminifu mwenye akili, ambaye bwana wake alimweka juu ya nyumba yake, awape watu chakula kwa wakati wake? Heri mtumishi yule, ambaye bwana wake ajapo atamkuta akifanya hivyo”.

            Ni dhahiri ya kwamba Chanzo cha watumishi wa Mungu kupoa kiroho na kuzembea katika kazi ya Mungu ya kuwapa “watu chakula kwa wakati wake” ni kule kutokujali muda wa ukaribu wa ujio wa Bwana Yesu kuja kulichukua Kanisa!.

            Yesu Kristo alisema; “bwana wake mtumishi huyo atakuja siku asiyodhani, na saa asiyojua, atamkata vipande viwili, na kumwekea fungu lake pamoja na wanafiki; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno”.

            Ukiyasoma maneno hayo kwa jinsi yalivyoandikwa na Luka Mtakatifu utaona yanasomeka hivi; “bwana wake mtumwa huyo atakuja siku asiyodhani na saa asiyojua, atamkata vipande viwili, na kumwekea fungu lake pamoja na wasioamini” (Luka 12:46).

            Wasomaji wa Biblia wanajua ya kuwa fungu la wasioamini baada ya kufa au Yesu Kristo atakaporudi – ni Motoni, au Jehanam, au Ziwa la Moto!

            Kwa hiyo mtumishi wa Mungu asipojali muda wa ukaribu wa Ujio wa kurudi kwa Yesu Kristo kuja kulichukua kanisa, na akaacha kuwapa watu chakula kwa  wakati wake; - Yesu Kristo akirudi atamwekea fungu lake pamoja na wasioamini – ikiwa na maana ya kuwa mtumishi huyo  atahukumiwa sawasawa na wasioamini!

Hii maana yake mtumishi wa Mungu anaweza kuikosa Mbingu kwa sababu hakuwa makini kujali uhusiano uliopo kati ya ukaribu wa muda wa ujio wa Yesu Kristo kulichukua Kanisa na wito alionao wa kumtumikia Mungu katika nyakati hizi.

Una Sehemu gani katika kuwapa
Watu “Chakula” kwa “Wakati wake”.

             Ikiwa utumishi wa kutumikia Mungu katika nyakati hizi za sasa una uhusiano mkubwa na ujio wa kurudi kwa Yesu – basi vile vile lazima utumishi huu una uhusiano mkubwa na matukio yaliyotabiliwa kutokea juu ya Taifa la Israeli katika siku hizi za mwisho.

            Lakini kabla – hatujaangalia uhusiano  huu kwa undani – hebu tuchambue kwanza sehemu ulinayo katika kuwapa “watu chakula” kwa “wakati wake”. Kujua – huku kutaweka ndani yako umuhimu mpya ndani yako wa kujali ukaribu wa muda wa ujio wa kurudi kwa Yesu Kristo, katika jambo unalolifanya kwa sasa.

            Tukiuangalia mfano wa kula chakula hotelini au nyumbani, utakuwa unaelewa ya kuwa wale waliohusika na kuhakikisha umepata “chakula” kwa “wakati wake” ni wengi sana! Si kazi ya mtu mmoja, bali ni mahusiano ya kikazi yanayohusisha watu wengi sana.

            Kwa mfano; kuna anayekupa chakula mezani, kuna waliohusika na kupika, kuna walionunua chakula hicho, kuna waliohusika na kulima mazao ya chakula hicho, kuna madreva waliohusika, kuna watoa fedha, kuna waliokinunua toka kwa wakulima na kukiuza kwa walaji, kuna waliohusika na stoo, nakadhalika.

            Kwa hiyo unapoona umewekewa chakula mezani na unakula kwa “wakati wake” ujue ni watu wengi sana sana wamehusika!

            Na inapokuja kwenye “Chakula” cha “Neno la Mungu” ni hivyo hivyo. Watu wanapojikuta wanakula chakula cha neno la Mungu “kwa wakati wake” – basi wajue ni watu wengi sana sana wanahusika.

            Inasikitisha kuona ya kuwa kuna watu wanahusika na kuwapa watu chakula cha neno la Mungu katika ngazi mojawapo ya mlolongo wa Utumishi huu – lakini – hawajui ya kuwa wao pia ni watumishi wa Mungu. Na kwa sababu hiyo wanajiondoa kwenye orodha ya watumishi wa Mungu, kwa kuwa wanajiona si wahubiri basi wao si watumishi wa Mungu! Hawajui ya kuwa kwa kufanya wanachofanya kuwasaidia wahubiri, na kwa ajili hiyo wao pia wanamtumikia Mungu kwa njia hiyo!

            Ukiutazama utumishi huu kwa njia hii ni dhahiri ya kwamba mtumishi aliyepewa kufikisha chakula cha neno la Mungu kwa walaji “kwa wakati wake” – haifanyi kazi hii peke yake! Ni watu wengi sana sana wanahusika katika mlolongo wa utumishi huu hadi neno la Mungu lifike kwa anayetakiwa kulipata.

            Je, wewe unahusika katika nafasi ipi ndani ya mtiririko huu wa kufikisha chakula cha neno la Mungu kwa walaji kwa wakati wake? Je, wewe ni mtoa sadak? ni mwombaji? ni mwanakamati? ni mhudumu? ni mlinzi? ni fundi umeme? ni fundi mitambo? ni mwimbaji? ni mfanya usafi? mali yako yoyote imetumika? ni mtoa kibali? ni mjenzi? ni mtunza watumishi?, nakadhalika.

            Kwa vyo vyote vile unavyohusika kwa sasa, au unavyojisikia moyoni mwako kuhusika katika kupeleka neno la Mungu kwa watu kwa wakati wake; - ujue unahusika na angalizo – hili la Bwana Yesu Kristo!

            Usije ukajikuta umeikosa mbingu kwa sababu ya kuzembea katika zamu yako, kwa kuwa tu umeshindwa kuihusisha zamu yako katika wajibu wa utumishi wako, pamoja na ukaribu wa ujio wa kurudi kwa Yesu Kristo kulichukua Kanisa lake!

            Kwa mwezi huu tunaishia hapa. Usikose kusoma barua yetu ya mwezi ujao ili uweze kujifunza zaidi juu ya jambo hili.

            Mungu akubariki sana.

UNATAKA KUOKOKA?
Kama unataka kumpa YESU maisha yako sasa, bonyeza hapa
©2003 Tanzania Social and Economic Trust.  All Rights Reserved.