|
|
| ||
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
Tunaamini Mungu anaendelea kukutunza katika Kristo Yesu, na
ndiyo maana amekupa nafasi ya kuisoma barua yetu hii. Mwezi uliopita katika barua yetu tuliyokuandikia tulianza
kujibu swali linalokutazamisha juu ya umuhimu wa maombi yako, hasa
unapoombea toka kwenye nafasi ya mfalme
na kuhani katika Kristo. Ndani ya barua hii tunataka kumalizia juu ya mfano wa maombi
ya nabii Eliya. Badala
ya kulumbana Malumbano ya kidini hapa duniani katika nchi na jamaa na
dini mbalimbali si mambo mapya. Kila dini inataka Mungu wao ndiye awe
Mungu anayeheshimiwa na kila mwanadamu – jambo ambalo toka zamani hadi
leo limekuwa gumu kutekelezeka. Vita kadhaa hapa duniani vimeanza kwa sababu ya malumbano ya
kidini. Tena machafuko mbalimbali katika nchi nyingi duniani yameazishwa
na malumbano ya kidini katika nchi hizo. Pendekezo ninalotaka kuweka mbele yako ni kwamba; badala ya
kulumbana kidini ni bora kufanya maombi – ili
Mungu wako ajitetee na kujijulisha mwenyewe ya kuwa hakuna Mungu
mwingine kama Yeye! Nabii Eliya aliwahi kufanya kosa la kutaka kuanzisha
malumbano ya kidini na manabii wa Baali, lakini manabii hao wa Baali
walikataa kuingia kwenye mtego huo. Biblia inasema; “
Naye Eliya akawakaribia watu wote akanena, mtasita-sita katikati ya
mawazo mawili hata lini? Bwana akiwa ndiye Mungu, mfuateni, bali ikiwa
Baali ni Mungu, haya! mfuateni yeye. Wale watu hawakumjibu neno” (1
Wafalme 18:21). Biblia inasema “Wale
watu hawakumjibu neno”. Hii ikiwa ina maana ya kuwa hao watu
walikataa kuingia katika malumbano ya kidini, au malumbano juu ya nani
anafaa kati ya Mungu wa Eliya na yule mungu wao. Mara naye nabii Eliya alitambua ya kuwa aliokuwa anatofautia
nao kiimani walikuwa hawako tayari kuingia katika malumbano ya kidini
juu ya Mungu yupi ndiye anayefaa kufuatwa na watu. Ndipo nabii Eliya akaja na pendekezo la pili ili kutafuta
kumaliza ushindani huo. Pendekezo hili lilikuwa ni kuhusu pande zote
mbili kutoa sadaka na kuomba kwa Mungu wake, halafu akasema: “Nanyi
ombeni kwa jina la Mungu wenu, Biblia inasema baada ya watu kusikia pendekezo hilo wakasema,
“…..maneno haya ni mazuri”
(1 Wafalme 18:24). Watu walionyesha wazi ya kuwa badala ya kulumbana na
kubishana juu ya nani na ni yupi Mungu anayefaa, ni bora zaidi kutafuta
ufumbuzi wa jambo hili kwa njia ya maombi! Jambo la msingi la kuona katika hili ni umuhimu wa maombi
katika kumaliza ubishi wa kidini! Ukiona malumbano ya kidini yameibuka na kupamba moto katika
eneo fulani – ujue hiyo ni ishara ya maombi kutokuwepo katika eneo
hilo, na hata kama maombi yapo basi ni maombi hafifu – kiasi ambacho
hayana uwezo wa kutoa maamuzi katika ulimwengu wa roho ili Mungu wa
Eliya atawale! Manabii wa Baali waliomba kuanzia asubuhi hadi jioni –
lakini mungu wao hakujibu cho chote! Nabii Eliya aliomba kwa Mungu wake,
naye akajibu kwa moto machoni pa kila mtu! Na ubishi wa kidini ukakoma!
Malumbano ya kidini yakaisha! Unaliona hili? Angalia na kutafakari maneno haya ya maombi
ya nabii Eliya ili uone uzito wa maombi hayo – na ya kwamba nabii
Eliya aliomba maombi hayo katika nafasi ya mfalme
na kuhani katika ulimwengu wa roho wa eneo la utawala wa Ahabu. Nabii Eliya aliomba akasema. “Ee, Bwana, Mungu wa Ibrahimu, na wa Isaka, na wa Israeli, na
ijulikane leo ya kuwa wewe ndiwe Mungu katika Israeli, na ya kuwa mimi
ni mtumishi wako, na ya kuwa nimefanya mambo haya yote kwa neno lako.
Unisikie, Ee Bwana, unisikie, ili watu hawa wajue ya kuwa wewe, Bwana,
ndiwe Mungu, na ya kuwa wewe umewageuza moyo wakurudie.” ( 1
Wafalme 18:36,37). Mungu akasikia maombi hayo na akajibu kwa moto, “
Na watu wote walipoona, wakaanguka kifudifudi; wakasema, Bwana ndiye
Mungu, Bwana ndiye Mungu”
( 1 Wafalme 18:39). Fahamu na ushangae kujua ya kuwa ingawa Bwana alikuwa ndiye
Mungu hata kabla ya maombi,
lakini alikaa kimya na hakujifunua kwa jamii ile na uongozi uliokuwepo
hadi au mpaka mtu wa Mungu aliposhika nafasi yake na
kufanya maombi ili Bwana ajijulishe ya kuwa ndiye Mungu! Kwa hiyo, ikiwa eneo ulilopo, au unalofanyia kazi, au
unalofanyia biashara, au unaloishi – halimtambui wala kumfuata Bwana
– basi ni kwa sababu kumekosekana mtu wa Mungu wa kuomba ili Bwana
ajijulishe ya kuwa ndiye Mungu na watu wamfuate. Je, mtu huyo
anayetakiwa kuomba lakini hakuomba ni wewe? Palipo na maombi ya namna hii ubishi wa kidini unakoma!
Kumbuka hili siku zote! Mungu aliye Bwana anaweza asijibu kwa moto kama wakati wa
nabii Eliya,lakini uwe na uhakika ukiomba maombi ya kifalme na kikuhani
hawezi kunyamaza – bali atajijulisha kwa jamii ya eneo unaloliombea
kwa namna ambayo kila mtu atajua Bwana ndiye Mungu! Je, umewahi kuwaza kungetokea nini katika jamii ile, kama
nabii Eliya asingepata wazo la kufanya maombi badala ya kuendelea na
ubishi wa maneno? Ni wazi kungetokea chuki na ugomvi! Na nabii Eliya angeumia,
maana alikuwa peke yake wakati huo.Lakini alipoamua kuomba – maombi
hayo yalimpa Mungu nafasi ya kuingilia kati na kumaliza ubishi huo! Unajifunza nini katika hili – kwa nchi hii ya Tanzania?
Kinachofanya malumbano ya kidini yapambe moto nchini ni ishara ya kuwa
watu wa Bwana ambaye ndiye Mungu hawafanyi maombi yanayotakiwa (yaani ya
kifalme na ya kikuhani). Malumbano ya dini ni matokeo ya watu wa Mungu
kutokuomba toka nafasi zao za kifalme na kikuhani walizopewa katika
Kristo Yesu! Kuomba au kutokuomba kwa nabii Eliya ndiko kulikokuwa na
uamuzi wa mwisho juu ya kuendelea au kutokuendelea kwa malumbano ya
kidini katika kizazi chake! Heshima ya Mungu katika eneo hilo
yalitegemea maombi ya nabii Eliya. Kwa hiyo basi, kuomba kwako au
kutokuomba kwako ndiko kuliko na uamuzi wa mwisho juu ya kuendelea au
kutokuendelea kwa malumbano ya kidini katika kizazi chako kwenye eneo
ulilopo! Heshima ya Mungu wako katika eneo lako yanategemea maombi
yako! Mwezi ujao tutakuelezea juu ya mfano wa maombi ya Musa
katika kumiliki na kutawala. Tuzidi kuombeana. |
|