Yesu Akamwambia "Lisha Kondoo Zangu" (Yohana 21:17)
Home
Maombi
Ratiba
Shuhuda
Mafundisho
Maswali na Majibu
Barua za Mwezi
Kuchangia Huduma

Barua ya Mwezi Februari 2009                                                            Kutoka kwa Christopher na Diana Mwakasege


JE UNAJUA KWANINI UMEPEWA NAFASI ULIYONAYO?

Tunakusalimu katika Jina la Yesu Kristo,

 

Umepewa nafasi katika ulimwengu wa roho ili uitumie ikusaidie kufanikiwa katika nafasi uliyonayo katika ulimwengu wa kimwili.

 

Ndiyo! Ndivyo ilivyo wala usishangae!  Ikiwa umeokoka, basi ujue ya kuwa unayo nafasi katika ulimwengu wa roho, unayotakiwa uitumie ikusaidie kufanikiwa katika nafasi uliyonayo katika ulimwengu wa kimwili.  Kwa mantiki hii, maana yake Mungu anapokupa nafasi katika ulimwengu wa kimwili, anataka uitumie kufanikisha makusudi yake yaliyomo katika kuuleta ufalme wake hapa duniani.

 

Aina mojawapo ya hizi nafasi ni hizi za kufanyika wafalme na makuhani kwa Mungu wetu. Imeandikwa hivi:

“Nao waimba wimbo mpya wakisema,

  wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu na

  kuzifungua muhuri zake; kwa kuwa ulichinjwa,

  ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa

  kila kabila na lugha na jamaa na taifa,

  ukawafanya kuwa ufalme na makuhani

  kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu

   ya nchi” (Ufunuo wa Yohana 5:9,10)

 

Haya maneno “ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu…..”, yanasomeka kwa sura tofauti unapoyasoma toka katika tafsiri ya kiingereza ya King James Version. Katika tafsiri hii ya kiingereza yanasomeka hivi: “ And has made us unto our God kings and priests….”

 

Maneno hayo kwa Kiswahili tunayatafsiri hivi “Na ametufanya sisi kwa Mungu wetu tuwe wafalme na makuhani…..”

Ninalotaka ulione hapa ni maneno haya “Wafalme na Makuhani”. Hizi ni nafasi mbili ambazo Yesu Kristo anampa mtu anayemwokoa kwa kumnunua kwa damu yake ya thamani.

 

Nafasi hizi mbili zinauhusiano wa karibu sana na nafasi ambayo mtu anakuwa nayo anapookolewa au baada ya kuokolewa. Nafasi ambayo anakuwa nayo ndani ya kabila, au katika lugha, au katika jamaa, (ukoo) au katika taifa.

 

Ukiusoma mstari huu wa Ufunuo wa Yohana 5:9,10 kuanzia mstari wa 9 na ndipo uende mstari wa 10, si rahisi sana kuliona jambo hili ninalotaka ulione hapa.

Lakini Roho Mtakatifu aliponiongoza kuusoma na kuutafakari kwa kuanzia mstari wa 10 na halafu wa 9 – nikaona waziwazi alichotaka nikione ndani yake.

 

Angalia! Anawafanya wawe wafalme na makuhani wale ambao amewanunua wakiwa ndani ya kabila zao, lugha zao, jamaa zao na taifa lao!

 

Wanazo nafasi zao katika ulimwengu wa kimwili ndani ya kabila zao, na ndani ya lugha zao, na ndani ya jamaa zao, na ndani ya taifa lao. Lakini hapo hapo anaamua kuwapa nafasi za kuwa wafalme na makuhani katika ulimwengu wa roho!

 

Kwa hiyo, mara tu wanapookoka wanajikuta wamepewa nafasi zingine katika ulimwengu wa roho, wakati bado wanazo nafasi pia katika ulimwengu wa kimwili.

Mtu anapookoka anajikuta anaishi maisha ya aina mbili kwa wakati mmoja (2 Wakorintho 5:15,16,17). Pia, anajikuta anaishi katika falme mbili kwa wakati huo huo ( Yohana 14:30).

 

Mtu ni roho, anayo nafsi na anaishi katika mwili (1 Wathesalonike 5:23). Mungu amemuumba mtu kwa namna ambayo anatakiwa awe na uwezo wa kuishi kwa mafanikio katika ulimwengu wa kiroho na katika ulimwengu wa kiroho kwa wakati mmoja!

 

Ukiangalia mistari hii ya Ufunuo wa Yohana 5:9,10 utaona ya kuwa Mungu anamwezesha mtu katika Yesu Kristo ashike nafasi mbili katika ulimwengu wa roho wakati pia katika ulimwengu wa kimwili anazo nafasi au katika kabila; au katika lugha; au katika jamaa (ukoo wake)yake; na au katika taifa lake!

 

Kusudi mojawapo la Bwana Yesu kutoa nafasi hizo zilizoko katika ulimwengu wa roho kwa watu wake, ni ili waweze kufanikiwa katika maeneo yote yanayowahusu ya ulimwengu wa roho na yale yanayowahusu ya ulimwengu wa kimwili.

 

Hivi ndivyo mtu alivyoumbwa – ya kwamba, kwa wakati huo huo aweze kuishi katika ulimwengu wa kiroho na ule ulimwengu wa kimwili, bila kikwazo cho chote.

 

Dhambi ilipoingia kwa mwanadamu wa kwanza, alipoteza nafasi aliyokuwa nayo katika ulimwengu wa roho. Ndio maana katika kitabu cha Mwanzo 2:9 tunaona Mungu akimwita Adamu, akisema, “Uko wapi”.

 

Mungu hakumuuliza Adamu “unafanya nini”, bali alimuuliza “uko wapi”!

Hii ni kwa sababu, anachofanya mtu na anavyoishi na anavyozungumza – vinategemea nafasi aliyonayo! Hii inahusu pia uhusiano wa mtu na Mungu – unagusa nafasi kwanza kabla ya matendo yake!

 

Kwa hiyo Mungu anapomtembelea mtu, au anapotembelea nchi, - anaangalia kwanza nafasi ambayo mtu wake, au watu wake, wameishika katika ulimwengu wa roho na ulimwengu wa kimwili kabla ya kuangalia matendo yao.

 

Kwa mantiki hiyo ni rahisi kuelewa umuhimu wa nafasi ambayo mtu anapewa katika ulimwengu wa roho wakati anapookoka!

 

Waefeso 2:6 inasema hivi juu ya kinachotokea mtu anapookoka: “ Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu”.

Maana yake nini kuketi “pamoja naye katika ulimwengu wa roho katika Kristo Yesu?”

Waefeso 1:19, 20 inatuelezea juu ya nguvu za Mungu zilizomfufua Yesu Kristo kutoka kwa wafu, ndizo pia zilizomo ndani yetu baada ya kuzipokea wakati tulipokuwa tunaokoka!

 

Maneno hayo yanasema hivi: “na ubora wa ukuu wa uweza wake ndani yetu tuaminio jinsi ulivyo; kwa kadri ya utendaji wa nguvu za uweza wake; aliotenda katika Kristo alipomfufua katika wafu, akamweka mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho”.

 

Warumi 8:11 inaeleza wazo hili hili inaposema “Lakini, ikiwa Roho wake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu….

Huyo Roho wa ufufuo anayekaa ndani yetu – anafanya ndani yetu jambo lile lile alilofanya kwa Yesu alipomfufua kwa wafu! …. Alifanya jambo gani? Waefeso 2:6 inasema; “akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho katika Kristo Yesu”.

 

Waefeso 1:21 inatueleza zaidi kuhusu nafasi hiyo tuliyoketi pamoja na Kristo katika ulimwengu wa roho inaposema: “juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwengu humu tu, bali katika ule ujao pia”.

 

Unaposoma yaliyoandikwa katika Wakolosai 1:13, na kuyaunganisha na yaliyoandikwa katika Waefeso 2:6, na yale ya Waefeso 1:19 – 21; utaona ya kuwa mtu anapookoka, si tu kwamba anakuwa mtoto wa Mungu, bali pia anaingizwa katika uongozi wa juu wa serikali ya ufalme wa Mungu! Umelipata hili? Unapookoka unaingizwa katika uongozi wa juu wa Serikali ya Ufalme wa mbinguni.

Wakolosai 1:13 inasema hivi juu ya kile kinachotokea tunapookoka ya kwamba: “Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake”.

 

Kwa hiyo basi, ni muhimu tujue na tuamini na kuupokea ukweli huu ya kuwa – Tunapookoka si tu kwamba tunazaliwa mara ya pili na kuingizwa katika familia ya Mungu, na kuwa ndugu moja tulio warithi pamoja na Kristo; lakini pia tunapookoka tunaingizwa katika serikali ya ufalme wa Mungu, na kuwa wamiliki na watawala pamoja na Kristo!

 

Ndiyo! Tunapookoka tunafanyika “Wafalme na Makuhani” kufuatana na Ufunuo wa Yohana 5:10. Hii ikiwa na maana ya kuwa tunapewa nafasi za utawala katika ulimwengu wa roho katika “nafasi” ambazo Yesu ametupa “kuketi” pamoja naye.

 

Hizi nafasi zinatupa kuwa wamiliki na watawala juu ya “ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwengu humu tu, bali katika ulimwengu ujao pia” ….tena….. “juu ya vitu vyote …..” (Waefeso 1:21,22).

 

Unaliona jambo hili? Ina maana wakati una nafasi yako katika jamii katika ulimwengu wa kimwili; Mungu anakupa pia nafasi zingine za kiutawala katika ulimwengu wa roho juu ya eneo hilo!

Yesu  anataka uzitumie nafasi hizi alizokupa katika ulimwengu wa roho kwa kiwango ambacho zitakufanikisha katika nafasi uliyonayo katika ulimwengu wa kimwili – katika kabila lako, katika lugha yako, katika ukoo wako na katika taifa lako!

 

Fahamu hili na ukumbuke daima ya kwamba: Mungu anaitaka nafasi uliyonayo katika ulimwengu wa kimwili ili aitumie katika kulitimiza kusudi lake alilokupa katika nafasi zake alizokuweka katika ulimwengu wa roho.

  

Tuzidi Kuombeana.

 

 Christopher na Diana Mwakasege

UNATAKA KUOKOKA?
Kama unataka kumpa YESU maisha yako sasa, bonyeza hapa
©2003 Tanzania Social and Economic Trust.  All Rights Reserved.