|
|
| ||
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
Salamu katika Jina la Yesu Kristo, Ndani ya barua yetu hii ya kwanza
kabisa katika mwaka 2009, tunataka tukushirikishe – angalau kwa maneno
machache umuhimu wa mtu kuijua tofauti iliyopo kati ya kusudi la Mungu na mpango
wa Mungu, ili uweze kuyaona mafanikio ambayo Mungu ameyapanga katika
maisha yako. Hili ni jambo la muhimu sana
ulijue…..maana si kila mtu anajua kutofautisha kati ya kusudi la Mungu
na mpango wa Mungu juu ya maisha yake. Unapousoma mstari wa Yeremia
29:11 utaona unasomeka hivi: “
Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya
amani, wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho”. Tafsiri mojawapo ya kiingereza
juu ya mstari huu inasomeka na kutafsiriwa kwa Kiswahili kama ifuatavyo:
“ Maana nayajua mipango
niliyowapangia ninyi, asema Bwana, ni mipango ya kuwapa mafanikio, wala
si ya kuwafanya msifanikiwe, ili niwape tumaini juu ya maisha mazuri ya baadaye…..” Kwa hiyo kwa tafsiri hii tunaona
ya kuwa neno “mawazo”
lina maana ya “mipango”;
na neno “amani” lina maana ya “mafanikio”. Mungu anaposema “nayajua
mawazo ninayowawazia ninyi….” Ina maana anayo tayari mipango
aliyotupangia – si ya kuitafuta – bali ipo kwake kwa ajili yetu! Lakini pia tunasoma katika Isaya
55:8 Mungu anapotuambia ya kuwa; “mawazo
yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu”. Kwa kusema
hivi, Mungu anataka tujue ya kuwa, kuna mawazo
yake juu yetu, na pia mawazo yetu
juu yetu – na mawazo haya ya aina mbili yanatofautiana! Pia, kwa hili
tunapata kujua ya kuwa kuna mipango
yake aliyonayo juu yetu ambayo ni tofauti na mpango
yetu tuliyonayo juu yetu! Tena ukisoma Isaya 55:9 utaona ya
kuwa mawazo au mipango ya Mungu juu yetu ni ya kiwango cha juu sana
katika ubora wake….. na ndiyo maana katika Yeremia 29:11 Mungu anasema
mipango yake hiyo juu yetu ni ya kutufanikisha! Wasomaji wengi wa biblia
wanapoisoma mistari hii wanaona wazi umuhimu wa si tu umuhimu wa kujua
mipango ya Mungu juu yao, bali pia kuijua njia (Isaya 55:8,9) ya
kuitekelezea hiyo mipango ili wafanikiwe katika maisha yao! Pamoja na hamu kubwa wanayokuwa
nayo ya kuijua mipango ya Mungu juu yao, wanajikuta hata wakiomba
hawajibiwi juu hili, au hata wakijibiwa hawaelewi ipasavyo tafsiri ya
majibu hayo. Hii ni kwa sababu ukitaka kujua mpango wa Mungu kwako,
inakubidi pia ulijue kusudi la Mungu kwako. Ukimwomba Mungu akueleze mpango
wake juu yake – mara nyingi katika jibu analokupa atahakikisha
anakueleza pia kusudi lake juu yako ni nini. Na kwa kuwa si wengi wanaojua
tofauti ya kusudi la Mungu na mpango wa Mungu - wanajikuta wanapata
ugumu sana kuelewa Mungu amewapangia mipango gani katika maisha yao! Badala ya kuwa na maisha ya
uhakika wa kile unachokifanya ya kuwa ndicho mpango wa Mungu juu yako;
unakuwa na maisha ya kubahatisha au maisha yasiyo na uhakika! Tunachokushauri katika barua hii
ni kwamba tafuta kulijua kwanza
kusudi la Mungu juu ya maisha yako, kabla
ya kuujua mpango wa Mungu juu yako! Au, ikiwa unataka Mungu akueleze
mpango wake juu yako basi usiache kuomba akueleze pia na kusudi lake juu
yako ni nini! Hili ni muhimu sana kwa sababu mpango
upo tu kwa ajili ya kutekeleza kazi zilizowekwa katika hatua mbalimbali
na kwa muda maalum, katika kuhakikisha ya kuwa kilichokusudiwa
kimefikiwa; au katika kuhakikisha kusudi
linafikiwa. Bila kulijua kusudi,
mpango wa utekelezaji unakosa msukumo, na pia unakosa mwelekeo! Ndiyo
maana basi, bila kulijua kusudi la Mungu la kukuweka hapa duniani wakati
huu, mpango wo wote unaoutekeleza ili kufanikisha maisha yako, unakosa
msukumo mzuri, na unakosa mwelekeo thabiti. Matokeo yake ni mipango yako
kutofanikiwa, na ikifanikiwa, basi mafanikio hayo yanakuwa ni ya muda
mfupi tu; au mafanikio hayo yanafanya hali yako ya kiroho isiwe ile ya
kumpendeza Mungu. Biblia inasema “Kufanikiwa
kwao wapumbavu kutawaangamiza”. (Mithali 1:32). Kwa hiyo si kila
kufanikiwa ni kuzuri! Kutekeleza mpango bila kujua ni kwa ajili ya
kutimiza kusudi gani – kunaweza kukakupa mafanikio yasiyo mazuri! Kusudi la Mungu maana yake nini? Neno hili “kusudi la Mungu” linatafsiriwa kwa kiingereza kama “the
Purpose of God”. Neno hili “the
purpose of God” au “kusudi
la Mungu” lina maana ya:
Kiswahili kinachotumika zaidi
katika mazungumzo ya kawaida badala ya neno “kusudi” ni hili neno “lengo”.
Ni muhimu mtu ajue tofauti kati ya kusudi au lengo la Mungu
ukilinganisha na mpango wa Mungu. Hebu soma na kuitafakari
Kumbukumbu la Torati 8:18 – inasema hivi: “Bali
utamkumbuka Bwana, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata
utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi
leo”. Watu wengi sana hata wale
waliookoka wamefanya “utajiri” kuwa lengo/kusudi la shughuli
wanazofanya. Lakini kufuatana na Kumbukumbu 8:18 – utajiri si lengo au
kusudi la Mungu; bali ni mpango wa Mungu. Na lengo au kusudi la Mungu au
sababu ya Mungu kutajirisha watu wake ni “ili
alifanye imara agano lake”. Ndani ya biblia neno hili “kusudi”
limetafsiriwa kama neno “shauri”.
Ndiyo maana tunasoma katika Mithali 19:21 ya kuwa “Mna
hila nyingi (au mipango mingi)
moyoni mwa mtu; lakini shauri (au
kusudi) la Bwana ndilo litakalosimama (au
litajulikana na kufanikiwa)”. Pia, ukisoma katika kitabu cha
Isaya 46:10 Mungu anasema: “Nitangazaye
mwisho tangu mwanzo, na tangu zamani za kale mambo yasiyotendeka bado;
nikisema, shauri (au kusudi)
langu litasimama (au litajulikana
na kufanikiwa), nami nitatenda mapenzi yangu yote”. Kwa kutafakari maneno ya mistari
hii utajua ya kuwa: (i)
Kusudi la Mungu halibadiliki na limewekwa ili kufanikiwa; na
kumfanikisha kila mtu anayelitekeleza; na (ii)
Mipango ya kutekeleza kusudi inaweza kubadilika, lakini kusudi lenyewe
la Mungu huwezi kulibadilisha. Kwa mfano; kusudi la Mungu la
kumuumba mtu ni ili aweze kuwa na familia ya wanadamu wenye sura yake
wapate kumwabudu daima. Mpango ambao Mungu aliuweka kwa ajili ya kuipata
familia hiyo ilikuwa ni kwa kutumia ndoa za wanadamu. Lakini dhambi ilipoingia, Mungu
akabadilisha mpango, na badala ya kuitumia ndoa kati ya mtu mume na mtu
mke, sasa anatumia uhusiano wa Kristo na kanisa, ili kusudi lake la kuwa
na wanadamu wenye sura yake lipate kutimia, kwa kutumia njia ya mtu
kuzaliwa mara ya pili kwa uwezo wa Roho Mtakatifu! Mfano mwingine, ni ule wa kusudi
la Mungu la kuwafikisha nchi ya Kaanani, wana wa Israeli baada ya
kuwatoa Misri. Mpango wa Mungu ulikuwa ni kumtumia nabii Musa kulifanya
hilo; lakini Musa hakuweza, na badala yake Mungu akamwinua Yoshua ili
kumalizia utekelezaji wa mpango huo! Fahamu hili; mtu ni sehemu ya mpango wa Mungu katika
kulitekeleza kusudi lake alilonalo. Mtu akivuruga maisha yake, na
asipotaka kutubu; na hata akitubu lakini asifuate mpango wa Mungu, kuna
uwezekano mkubwa wa Mungu kuinua mtu mwingine ili atekeleze hilo Mungu
analotaka! Kwa kumalizia barua hii, tunataka
tukwambie ya kuwa, kwa kusoma Matendo ya Mitume 13:36 na 2 Timotheo 4:7
utajua ya kuwa Mfalme Daudi na Mtume Paulo walilitumikia kusudi la Mungu
katika nyakati zao. Je, wewe umeona sasa umuhimu wa
kujua tofauti kati ya kusudi la Mungu na mpango wa Mungu ili uone
mafanikio katika maisha yako? Tuzidi kuombeana. |
|