HONGERA KWA KUOKOKA
UTANGULIZI
Karibu
kwenye Ufalme wa Mungu
Kitabu
hiki kimeandikwa kwa ajili yako. Roho Mtakatikfu amekiweka mikononi
mwako kwa kusudi muhimu la Mungu ndani ya Kristo.
Katika
Jina lile lipitalo majina yote jina la Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi
wetu, napenda kukukaribisha katika Ufalme wa Mungu!
Imeandikwa
wazi kabisa katika kitabu cha Waefeso 2:19 ya kuwa; “Basi
tangu sasa ninyi si wageni wala wapitaji, bali ninyi ni wenyeji pamoja
na watakatifu, watu wa nyumbani mwake Mungu”.
Umepata
neema hii ya Mungu, na sasa umeokoka – biblia inakuambia tangu sasa
wewe si mgeni wala mpitaji katika Ufalme wa Mungu -
bali wewe ni mwenyeji pamoja na watakatifu wengi waliomo katika
nyumba ya Mungu!
Nia
ya Roho Mtakatifu kukuwekea kitabu hiki mikononi mwako, ni kukufahamisha
angalau kwa kiasi fulani juu ya uamuzi uliofanya wa kutubu dhambi zako,
na kumpokea Yesu Kristo kama Bwana na Mwokozi wako.
Kitabu
hiki kitakusaidia kujua kitu gani kimetokea ulipookoka na mambo muhimu
ya kufanya katika maisha hayo mapya ya wokovu.
Umefanya
uamuzi wa busara – katika Luka 15:10 biblia inatuambia ya kuwa hata
malaika wa mbinguni wanashangilia na kuufurahia uamuzi huo uliofanya.
Na
mimi kama mtumishi wa Mungu aliye hai napenda kumshukuru Mungu katika
Kristo Yesu kwa kukufunulia siri hii ya wokovu ambayo wengi hawajaiona
na wengine wameiona lakini wanaipuzia. Ni maombi yangu kwa Mungu ya kuwa
atakutia nguvu na kukupa ufahamu wa rohoni unapokisoma kitabu hiki ili
kikusaidie katika maisha yako ya kila siku.
Christopher
na Diana Mwakasege
,
S.L.P. 2166,
ARUSHA
UMEFANYA
UAMUZI WA BUSARA
Umefanya uamuzi wa busara. Ndiyo! – tena ni kweli kabisa.
Umefanya uamuzi wa busara. Umeamua kutubu dhambi zako kwa Mungu, na
kumpokea Yesu Kristo moyoni mwako kama Bwana na Mwokozi wako –
umefanya uamuzi wa busara. Naamini pia ya kuwa uamuzi huu uliofanya ni
uamuzi wa kudumu.
Nimeona nikutie moyo namna hii kwa kuwa mtu anapookoka wakati
mwingine anasumbuka na mawazo na kujiuliza maswali mengi – akijiuliza
ikiwa kwa kuokoka amefanya uamuzi sahihi. Watu wengine kwa kutopata
majibu sahihi ya swali hili wanakata tamaa na kurudi nyuma kiroho – na
hata wapo wengine wanaoamua kuacha wokovu kabisa.
Nakutakia heri kwa Bwana na kumwomba Mungu azidi kujifunua wazi
zaidi kwako ili usiwe kati ya wale wanaokata tamaa na kuacha wokovu.
Umeifanya sala ya toba kwa moyo wako wote na umeokoka – ni uamuzi wa
busara mtu yeyote asikudanganye wala kukukatisha tamaa.
Umechagua
Baraka!
Umechagua kuokoka kwa kumwamini na kumpokea Yesu Kristo kama
mwokozi wako,maana yake umechagua baraka.
Inawezekana hukujua lakini mtu ambaye hajaokoka anaishi chini ya
laana, na mara anapookoka – Yesu Kristo anamtoa kwenye laana
nakumwingiza ndani yake – ambaye ndiye Baraka na chanzo cha baraka
zote za Mungu.
Tangu zamani Mungu alimpa mtu uhuru wa kuchagua kati ya baraka na
laana aliposema
“
Angalieni, nawawekea mbele yenu hivi
leo baraka na laana;
baraka ni
hapo mtakapoyasikiza maagizo ya Bwana
Mungu wenu…. Na laana ni hapo msiposikiza
maagizo ya Bwana….
(Kumbukumbu la Torati 11:26-28)
Umechagua kuokoka – umechagua baraka! Baraka maana yake, furaha, amani,
kufanikiwa, kustawi, kukua,kunawiri na kunona!
Ndiyo maana Mtume Paulo aliandika katika kitabu cha Waefeso 1:3
hivi, “Atukuzwe
Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa baraka zote za
rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo.”
Huu mstari unazungumza juu yako pia kwa kuwa unapookoka unaingia “ndani
yake Kristo”. Kwa kuwa ulipookoka uliingia ndani yake Kristo, kwa
hiyo umebarikiwa kwa baraka zote za rohoni!
Unaweza ukajiuliza kama ni baraka zote za rohoni je za kimwili na
za akili nitazipataje? Fahamu neno hili baraka zote zimeanza rohoni!
Ndiyo maana imeandikwa hivi katika kitabu cha Wagalatia 3:13, 14
kuwa; “Kristo
alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili
yetu, maana imeandikwa amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti, ili
kwamba baraka ya Ibrahimu iwafikilie mataifa katika Yesu Kristo, tupate
kupokea ahadi ya roho kwa njia ya amani”.
Ndani ya baraka ya Ibrahimu tunayoipata katika Kristo Yesu kuna
mafanikio katika maisha ya sasa na ya baadaye – baada ya kufa.
Ukiokoka unaanza kubarikiwa ukiwa hapahapa duniani!
Hakuna
hasara!
Umefanya uamuzi wa busara ulipoamua kuokoka kwa sababu ndani ya
Yesu Kristo hakuna hasara. Wewe uwe mtendaji wa neno lake, na ndipo
utakapojua na kuthibitisha ya kuwa kweli kwa Yesu Kristo kuna kila kitu
unachokihitaji sasa na cha maisha ya siku zote.
Inawezekana umewahi kusikia watu wakisema mtu anapookoka
anafilisika – na inawezekana umewahi kuona watu wengine waliookoka
wakiwa na maisha duni. Nataka nikueleze ya kwamba haimo katika mpango wa
Mungu kuwafilisi watu wake wanapookoka. Wengi wanakuwa na maisha duni
kwa sababu ya kukosa mafundisho sahihi ya neno la Mungu baada ya kuokoka!
Wanaangamia kwa kukosa maarifa ya neno la Mungu.
Ukichukua biblia yako na kusoma kitabu cha 2Wakorintho 8:9 utaona
wazi wazi ya kuwa kati ya mambo aliyoyafanya Yesu msalabani alipokufa
kwa ajili yetu – ni kuuchukua umaskini wetu ili tupate kupokea utajiri
wake.
Ndiyo sababu Yesu Kristo aliwahi kuwaambia wanafunzi wake (ambao
ni pamoja na wewe sasa kwa kuwa umeokoka) ya kwamba:
“
Hakuna mtu aliyeacha nyumba, au ndugu
waume, au ndugu wake,
au mama, au baba,
au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu,
na kwa ajili ya Injili, ila atapewa mara mia
sasa wakati huu, nyumba, na ndugu waume,
na ndugu wake, na mama, na watoto,
na mashamba, pamoja na udhia; na
katika ulimwengu ujao uzima wa milele”
(Marko 10:29,30).
Haya ni maneno ya Yesu Kristo mwenyewe, na Roho Mtakatifu
anakuletea maneno haya ndani ya moyo wako kukuondoa wasiwasi. Umeamua
kuokoka – umeamua kupokea baraka kuanzia sasa.
Nataka nizidi kukutia moyo ya kuwa umefanya uamuzi wa busara kwa
kuokoka. Maana umechagua baraka umeikataa laana; umechagua Uzima,
umeikataa mauti; Umechagua Nuru, Umeikataa giza; Umemchagua Yesu,
umemkataa shetani;Umechagua kwenda mbinguni, umekataa kwenda jehanamu!
Hata kufahamu ya kuwa ulipookoka umefanya uamuzi wa busara – ni
baraka ya pekee pia! Au wewe unasemaje? – ni kweli au uongo?
Kumbuka unapookoka unampokea Yesu Kristo moyoni mwako ambaye
ndiye KWELI kwa hiyo nakushauri kataa uongo unaotaka kukurudisha nyuma
kiroho. Umeamua kuokoka – umeamua kwa busara na uwe ni uamuzi wa
kudumu!
KITU
GANI KIMETOKEA ULIPOOKOKA?
Mtume Paulo alipokuwa anawaandikia Wakorintho katika waraka wa
kwanza sura ya kumi na tano na mstari wa tatu, juu ya kufa na kufufuka
kwa Bwana Yesu Kristo alisema;
“Kwa
maana naliwatolea ninyi hapo mwanzo
yale niliyoyapokea mimi mwenyewe; ya kuwa
Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu,
kama yanenavyo maandiko; na yakuwa alizikwa;
na ya kuwa alifufuka siku ya tatu,
kama yanenavyo maandiko”.
“Kama yanenavyo maandiko” – ni maneno ambayo Mtume Paulo
ameyatumia mara mbili katika mstari huu wa biblia, - akiwa na nia ya
kuwaonyesha wasomaji kuwa chanzo cha maelezo yake juu ya kufa, na
kuzikwa na kufufuka kwa Kristo ameyasema sawa na MAANDIKO.
Ukitaka kujua kitu gani kimetokea ulipoamua kuokoka, ni muhimu
tusome maandiko – bibilia kuona inasemaje juu ya hali yako sasa.
Katika sura hii ya tatu ya kitabu hiki nataka nikupe baadhi ya
maandiko katika biblia ambayo yatakusaidia kujua kilichotokea ulipookoka:
- Umesamehewa
dhambi zako zote!
“Na
ninyi mlipokuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu…. Aliwafanya hai
pamoja naye, akiisha kutusamehe makosa yote; akiisha kuifuta ile hati
iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu;
akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani …” (Wakolosai
2:13,14).
“Tukiziungama
dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu na
kutusafisha na udhalimu wote” (1Yohana 1:9).
- Jina
lako limeandikwa mbinguni!
“…furahini
kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni” (Luka 10:20).
“Yeye
ashindaye atavikwa hivyo mavazi meupe, wala sitalifuta kamwe jina lake
katika kitabu cha uzima, nami nitalikiri jina lake mbele za Baba yangu,
na mbele ya malaika zake” (Ufunuo 3:5).
- Umekuwa
kiumbe kipya!
“Hata
imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale
yamepita; tazama! Yamekuwa mapya” (2Wakorintho 5:17).
“Lakini
mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu chochote ila msalaba wa Bwana
wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulubiwa kwangu, na mimi
kwa ulimwengu. Kwa sababu kutahiriwa si kitu, wala kutokutahiri, bali
kiumbe kipya” (Wagalatia 6:14,15).
“Mvue
kwa habari ya mwenendo wa kwanza utu wa zamani, unaoharibika kwa
kuzifuata tamaa zenye kudanganya; na mfanywe wapya katika roho ya nia
zenu, mkavae utu mpya ulioumbwa kwa namna ya Mungu katika haki na
utakatifu wa kweli” (Waefeso 4:22-24).
- Umekuwa
mtoto wa Mungu!
“Bali
wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale
waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya
mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu (Yohana 1:12,13).
“Tazameni,
ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na
ndivyo tulivyo… Wapenzi, sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika
bado tutakavyokuwa; lakini twajua ya kuwa atakapodhihirishwa, tutafanana
naye; kwa maana tutamwona kama alivyo” (1Yohana 1:1,2).
- Malaika
wamekuzunguka hata kama huwaoni!
“Je!
hao wote (malaika) si roho watumikao, waliotumwa kuwahudumia wale
watakaorithi wokovu? (Waebrania 1:14).
“Kwa
kuwa atakuagizia malaika zake wakulinde katika njia zako zote. Mikononi
mwao watakuchukua, usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe” (Zaburi
91:11,12)
- Umekuwa
makao ya Kristo na Mungu!
“Yesu
akajibu, akamwambia, mtu akinipenda atalishika neno langu; na Baba yangu
atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake” (Yohana 14:23)
“Nimesulibiwa
pamoja na Kristo; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai
ndani yangu; na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya
Mwana wa Mungu, ambaye alinipenda akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu”
(Wagalatia 2:20).
“Katika
yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika Roho” (Waefeso
2:22).
- Roho
Mtakatifu yumo ndani yako sasa!
“Lakini,
ikiwa Roho wake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu,
yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo
katika hali ya kufa, kwa roho wake anayekaa ndani yenu” (Warumi 8:11).
“Au
hamjui ya kuwa miili yenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu,
mliyepewa na Mungu? (1Wakorintho 6:19).
- Una
mamlaka juu ya shetani na kazi zake tangu sasa!
“Tazama,
nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui,
wala hakuna kitu kitakachowadhuru” (Luka 10:19)
“Na
ishara hii zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo ….
Wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya” (Marko
16:17,18).
“Basi
mtiini Mungu. Mpingeni shetani, naye atawakimbia” (Yakobo 4:7).
- Utafufuliwa
au kunyakuliwa Yesu akija kulichukua kanisa maana unao uzima wa
milele!
“Yeye
aliye naye Mwana, anao huo uzima; asiye naye Mwana wa Mungu hana huo
uzima” (1Yohana 5:12).
“Kwa
sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na
sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika
Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai tuliosalia,
tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na
hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele” (1Wathesalonike 4:16,17).
“Huo
ndio ufufuo wa kwanza. Heri na mtakatifu, ni yeye aliye na sehemu katika
ufufuo wa kwanza; juu ya hao mauti ya pili haina nguvu …. (Ufunuo 20:6
Haya
ni baadhi tu ya maneno mengi mazuri ambayo yamo katika biblia
yanayoeleza kilichotokea ulipookoka. Nakupa ushauri ya kuwa uyasome mara
kwa mara pamoja na mengine yaliyomo katika biblia ili upate kujijua wewe
sasa ni nani mbele za Mungu na
za shetani baada ya kuokoka.
USIOGOPE
KUSEMA JUU YA UAMUZI WAKO
“Msiogope
kutisha kwao, wala msifadhaike…. Mwe tayari siku zote kumjibu kila mtu
awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa
hofu” (1Petro 3:14-15)
Je!
unaogopa kuwaambia ndugu zako, majirani zako au rafiki zako ya kuwa sasa
umeokoka, na Yesu Kristo ni Bwana na Mwokozi wa maisha yako?
Je!
unaogopa kuwaeleza watu waziwazi ukiulizwa juu ya mabadiliko ya tabia
yako ya kuwa sasa wewe ni “kiumbe kipya”?
Je!
unababaika na kushindwa kujibu ukiulizwa ikiwa umeokoka? Maana
inawezekana hata wewe ingawa umeokoka kweli, lakini ukiulizwa kama
umeokoka unababaika na kusita kusema uhusiano wako mpya na Yesu Kristo.
Kuna
wengine hata wanadiriki kuishi maisha ya kinyonga. Akiwa katikati ya
kundi la watu waliookoka, kwake inakuwa rahisi kusema ya kuwa ameokoka.
Na akiwa katikati ya kundi la watu wasiokoka, anashindwa kuonyesha
msimamo wake hata kama akitakiwa kufanya hivyo.
Je!
unayafahamu madhara ya maisha ya namna hii? – yapo madhara yake kwako.
Ndiyo maana biblia inasema.” Msiogope kutisha kwao, wala msifadhaike…
mwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini
lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa hofu.”
Kuna
madhara yake ukiogopa kumkiri Yesu mbele ya watu ya kuwa ni mwokozi wako
– yapo madhara.
Yesu Kristo mwenyewe alisema hivi juu ya jambo hili, maana alijua
litatokea jambo kama hili;
“Basi,
kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu
aliye mbinguni. Bali mtu yeyote atakayenikana mbele ya watu, nami
nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni” (Mathayo 10:32,33).
Yesu
Kristo hapa anazungumza juu ya maisha ya sasa. Kumbuka Yesu ameketi
mkono wa kuume wa Mungu Baba, na huko anatuombea na ndiye mtetezi wetu.
Hakuna
namna ambavyo utasikilizwa maombi yako na Baba Mungu na kupata msaada
unaouhitaji bila msaada wa Yesu Kristo. Kwa hiyo mojawapo ya madhara ya
kumkana Yesu mbele za watu ni kwamba na wewe ukihitaji akutaje mbele za
Baba ili ujibiwe maombi yako na yeye atakaa kimya.
Ingawa
ni kweli unapookoka, Mungu anakutumia malaika wa kukuhudumia na
kukulinda, lakini ukiona aibu kumkiri Yesu mbele za watu unapotakiwa
kuonyesha msimamo wako kiroho – malaika nao hawakusaidii – kwa
sababu malaika wanakusaidia kwa sababu ya neno la Kristo juu yako kwao.
Yesu akikaa kimya, na malaika wanakaa kimya! Ndiyo maana Yesu Kristo
alisema;
“Nami
nawaambia, kila atakayenikiri mbele ya watu, Mwana wa Adamu naye
atamkiri yeye mbele ya malaika wa Mungu; na mwenye kunikana mbele ya
watu, huyo atakanwa mbele ya malaika wa Mungu” (Luka 12:8,9).
Fikiria
upo katikati ya majaribu, na unahitaji msaada wa Mungu; halafu malaika
wanaokuzunguka wanamuuliza Yesu Kristo kama wakusaidie au la – Yesu
Kristo atakaa kimya asiseme kitu au anaweza kukukana mbele ya hao
malaika ikiwa utakuwa na tabia ya kumwonea aibu na kumkana mbele za watu.
Na
majaribu yatakusonga na kukuangusha, utadhani ya kuwa Mungu hasikii
maombi yako. Lakini ni vizuri ufahamu utaratibu huu wa kusaidiwa na
Mungu ya kuwa ukiogopa kumkiri Yesu Kristo mbele ya watu (ndugu zako au
rafiki zako) ya kuwa ni Bwana na Mwokozi wako, siku ukihitaji msaada wa
Mungu Yesu atakaa kimya, Baba Mungu atakaa kimya na malaika watakaa
kimya.
Ukitaka
msaada wa haraka katika majaribu hasa ya kuanguka dhambini usione haya
kumkiri Yesu mbele za watu ya kuwa ni Bwana na Mwokozi wako. Mungu
atakupa haraka njia na hekima ya kutoka katika hayo majaribu.
Nimeona
watu wengi waliookoka wakirudi kuvuta sigara kwa sababu hawakuwaeleza
rafiki zao ya kuwa wameokoka, walipokaribishwa kuvuta sigara walishindwa
kukataa na walishindwa kuwaambia rafiki zao ya kuwa Yesu ni Mwokozi wao
kwa hiyo hawavuti sigara tena.
Vivyo
hivyo nimeona watu wengine waliookoka wakirudi kunywa pombe kwa sababu
waliona aibu kuwaeleza ndugu zao na rafiki zao ya kuwa wameokoka na Yesu
ni Bwana na Mwokozi wao, kwa hiyo hawatakunywa pombe tena. Lakini kwa
kuona aibu kumkiri Yesu mbele ya watu wanaowakaribisha pombe –
wanaanguka kwenye ulevi tena.
Nimeona
pia watu wengi waliookoka – hasa wasichana na wanawake wakianguka
katika uasherati kwa sababu ya kutowaambia wanaume wanaowasumbua ya kuwa
wameokoka na hawataki utani wala kuharibu maisha yao ya kiroho kwa
uzinzi. Wengi wa wale nilioweza kuzungumza nao kama wangekuwa wamefuata
misingi ya neno la Mungu ya kutomwonea haya mwana wa Adamu –
wasingeanguka katika zinaa.
Tatizo
lilipo
Kinachowafanya
wengi waogope kumkiri Yesu Kristo mbele za watu ni kwa sababu wanaogopa
kuchekwa au kuzomewa au kutengwa na jamii au rafiki au ndugu; wengine
wanaogopa kupigwa na wazazi wao au waume zao; wengine wanaogopa
kufukuzwa kazi; na kadhalika, ili mradi kila mtu anayo sababu ya
kujitetea kwa nini anashindwa kusema ameokoka.
Lakini
hawajui baada ya muda wanapoa kiroho na kurudi nyuma kabisa; hata
wengine kuacha wokovu kwa sababu hawana msaada wowote wa kuyashinda
majaribu.
Biblia
inasemaje juu ya jambo hili? Biblia imezungumza mengi juu ya jambo hili
na baadhi ya mistari hiyo ni hii:
“Msiogope
kutisha kwao, wala msifadhaike…. Mwe tayari siku zote kumjibu kila mtu
awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa
hofu” (Petro 3:14,15)
Yesu
Kristo alisema hivi;
“Heri
wenye kuudhiwa kwa sababu ya haki; maana ufalme wa mbinguni ni wao. Heri
ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa
uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu
ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa
kabla yenu” (Mathayo 5:10-12)
Unaweza
kuikosa mbingu
Usifanye
mzaha kwenye wokovu. Uamuzi ulioufanya wa kuokoka ni uamuzi wa busara
– lakini pia ni uamuzi wa ‘kufa na kupona’. Maana shetani
amekukasirikia lakini usiogope kwa sababu yeye aliye ndani yako ni mkuu
kuliko yeye aliye katika dunia (1Yohana 4:4)
Kwa
kuwa umeamua kuokoka bila kulazimishwa, basi usione aibu kumkiri Yesu
Kristo mbele za watu ya kuwa ni Bwana na Mwokozi wako.
Kwa
sababu ukimwonea aibu sasa, siku atakapokuja kuchukua wateule wake –
wewe utaachwa! Hutanyakuliwa! Ndivyo Yesu Kristo mwenyewe alivyosema:
“Akawaambia
wote, mtu yeyote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike
msalaba wake kila siku, anifuate ….kwa sababu kila atakayenionea haya
mimi na maneno yangu, Mwana wa Adamu atamwonea haya mtu huyo, na
atakapokuja katika utukufu wake na wa Baba na wa malaika watakatifu” (Luka
9:23,26).
Kwa nini ukubali kuupoteza ufalme wa mbinguni kwa kuwaogopa
wanadamu? Ndiyo maana Mtume Petro aliongozwa na Roho wa Mungu
kutuandikia maneno haya ya kututia moyo aliposema; “Wapenzi, msione
kuwa ni ajabu ule msiba ulio kati yenu, unaowapata kama moto ili
kuwajaribu, kana kwamba ni kitu kigeni kiwapatacho. Lakini kama
mnavyoshiriki mateso ya Kristo, furahini; ili na katika ufunuo wa
utukufu wake mfurahi kwa shangwe.
“Mkilaumiwa
kwa ajili ya Jina la Kristo ni heri yenu; kwa kuwa Roho wa Utukufu na wa
Mungu anawakalia. Maana mtu wa kwenu asiteswe kama mwuaji, au mwivi, au
mtenda mabaya, au kama mtu ajishughulishaye na mambo ya watu wengine.
Lakini ikiwa kwa sababu ni mkristo asione haya, bali amtukuze Mungu
katika jina hilo” (1Petro 4:12-16)
Kumbuka
ya kuwa hata kama ndugu zako au rafiki zako au wanaokuzunguka
hawafurahii kuokoka kwako – mbinguni wanafurahi – malaika pia
wanafurahia – soma mwenyewe katika kitabu cha Luka 15:7,10.
Kama
ulikuwa na aibu ya kumkiri Yesu mbele za watu, nakushauri sasa hivi
utubu na Mungu atakusamehe, halafu mwombe Mungu akupe ujasiri na hekima
ya namna ya kumkiri mbele za watu bila kuona haya kila nafasi inapotokea.
Sema hivi unaposali (ikiwa unapata shida juu ya namna ya kutubu).
“Mungu
Baba nisamehe kwa kumwonea haya mbele za watu Mwana wako Yesu Kristo
aliye Mwokozi wangu. Nitakase kwa upya kwa Damu yake na Neno lake.
Naomba unipe ujasiri na hekima ili nijue kumjibu kila mtu juu ya wokovu
ulionipa. Kwa jina la Yesu Kristo nimeomba na kuamini ya kuwa umenisikia
– Amina”.
UHAKIKA
WA WOKOVU WAKO
Ni
rahisi sana kufika wakati mwingine ukajihukumu mwenyewe, na hata
kufikiri labda hujaokoka sawasawa.
Pia,
unaweza ukahukumiwa na watu wengine wakikuambia hujaokoka sawasawa
wakitoa sababu nyingi wanazojua wao – na usipokuwa na maandiko ya
kutosha unaweza kubabaika sana – na msimamo wako wa kiroho kuyumba.
Utapataje
uhakika wa wokovu wako? Utajuaje ya kuwa kweli umeokoka – hata wakati
wengine wanakwambia hujaokoka sawasawa – tena wengine wameokoka siku
nyingi kabla yako?
Yesu
Kristo alisema; “ Tena mtaifahamu kweli, nayo kweli itawaweka huru”
(Yohana 8:32). Alikuwa ana maana gani alipokuwa anasema tutaifahamu
kweli? ‘Kweli’ maana yake nini? Yesu alipokuwa akifanya sala katika
Yohana 17:17 alisema; “Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli”.
Naamini
kweli utakayoifahamu katika sura hii, itakuweka huru – tena utakuwa
huru kweli kweli!
Mambo
mawili makubwa yafuatayo yatakusaidia kupata uhakika wa wokovu wako;
1.
Kujua ya kuwa umesamehewa dhambi zako na Mungu hazikumbuki tena;
- Kujua
ya kuwa Roho Mtakatifu aliye ndani yako ni muhuri wa Mungu wa
kuonyesha ya kuwa wewe tayari ni wake milele!
Sasa
na tuangalie kwa kifupi jambo moja moja.
1.
Juu ya Msamaha wa dhambi
Unahitaji
kujua na kuwa na uhakika siku ile uliyotubu kumpokea Yesu Kristo kama
Bwana na Mwokozi wako, dhambi zako ZILISAMEHEWA, ZILIFUTWA, WALA MUNGU
HAZIKUMBUKI TENA.
Ndiyo
Mungu hazikumbuki tena! Ndivyo neno lake linavyosema. Hebu tafakari
mistari ifuatayo:
“Haya,
njooni, tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana,
zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa
kama sufu” (Isaya 1:18).
Tena
Mungu alisema hivi katika Isaya 43:25;
“Mimi,
naam, mimi, ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe; wala
sitazikumbuka dhambi zako”.
Mungu
anasema hatazikumbuka tena dhambi zako! Sasa wewe kwa nini dhambi
ulizokwisha kuzitubu bado zinakusumbua rohoni? – Inakuwa kama vile
Mungu hajakusamehe!
Lakini
nakwambia ya kuwa ikiwa ulitubu katika roho na kweli – umesamehewa
dhambi zako – wala Mungu hazikumbuki tena! Kwa hiyo na wewe
usizikumbuke tena! Hata kama mawazo yako yanakuzomea – hata kama
wenzio wanakuzomea – Mungu amekusamehe, wala hazikumbuki dhambi zako
tena.
Unaweza
ukasema, lakini ndugu Mwakasege, hiyo mistari iko katika agano la kale,
Je! tuna mistari kama hiyo katika Agano Jipya?
Hiyo
mistari ipo mingi tu – lakini fahamu pia ya kuwa hiyo mistari ingawa
iliandikwa wakati wa agano la kale ilikuwa inazungumza na watu walio
katika agano jipya. Hii ni kwa sababu katika agano la Kale – pamoja na
sadaka zilizokuwa zinatolewa, Mungu alikuwa anazikumbuka dhambi zao.
Soma Waebrania sura ya 8,9, na ya 10.
Katika
agano jipya, yaana wakati huu, mtu anapookoka, damu ya Yesu Kristo iliyo
mbele ya kiti cha enzi kwa ajili yetu – inafuta hati zote
zilizopelekwa na kuandikwa mbele za Mungu ambazo zilikuwa zimejaa dhambi
zetu.
Ndiyo
maana imeandikwa;
“Na
ninyi mlipokuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kutokutahiriwa kwa
mwili wenu, aliwafanya hai pamoja naye; akiisha kutusamehe makosa yote;
akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake,
iliyokuwa na uadui kwetu, akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani”
(Wakolosai 2:13,14).
Tafsiri
ya Kiswahili cha kisasa inasema hivi katika mistari hii ya Wakolosai
2:13,14;
“Wakati
mmoja nanyi mlikuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kwa sababu
ninyi mlikuwa watu wa mataifa mengine. Lakini Mungu amewapa ninyi uzima
pamoja na Kristo. Mungu ametusamehe dhambi zetu zote; alifutilia mbali
ile hati ya deni iliyokuwa inatukabili na masharti yake, na kuifuta
kabisa kwa kupigilia Msalabani.
Soma
pia Waebrania 9:23 – hati iliyotumwa mbinguni na shetani kukushitaki
imefutwa! Shetani anapojaribu kukukumbusha juu ya dhambi za zamani
ulizozifanya kabla ya kuokoka, ujue ameshika nakala tu ya hati, lakini
hati yenyewe ilikwishafutwa kwa damu ya Yesu.
Mbele
ya Mungu unaonekana huna kosa, kwa sababu hujasimama mwenyewe mbele zake
– lakini Yesu aliyekuokoa yuko pamoja na wewe – kwa kuwa uhai wetu,
“umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu” (Wakolosai 3:3)
Hebu
zidi kutiwa moyo na maneno yafuatayo yaliyomo katika Warumi 8:31-39
yanayosema: “Basi, tuseme nini juu ya hayo? Mungu akiwapo upande wetu,
ni nani aliye juu yetu?Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali
alimtoa kwa ajili yetu sisi sote atakosaje kutukirimia na mambo yote
pamoja naye? Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye
mwenye kuwahesabia haki. Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu
ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye
yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea.
“Ni
nani atakayetutenga na upendo wa Kristo?…. lakini
katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi
ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua
hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye
mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala
yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza
kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.”
2.
Juu ya Roho Mtakatifu aliye ndani yako.
Katika
sura zilizotangulia za kitabu hiki nilikwambia ya kuwa kati ya mambo
yaliyotokea wakati ulipookoka ni kwamba Roho Mtakatifu aliingia ndani
yako – maana ndiye aliyekuzaa mara ya pili, umekuwa kiumbe kipya, na
uzima wa milele umo ndani yako.
Biblia
inasema hivi;
“Lakini
msingi wa Mungu ulio imara umesimama, wenye mihuri hii, Bwana awajua
walio wake” (2Timotheo 2:19).
Kinachomfanya
Mungu awajue walio wake ni kwa kuangalia muhuri aliouweka katika mioyo
yao. Ndiyo maana itakuwa rahisi kutubagua siku ya kutubagua kama kondoo
na mbuzi.
Mfugaji
yoyote anajua ya kuwa akitaka mifugo yake iwe rahisi kuitambua hata kama
itajichanganya na ya wengine ni kwamba lazima aipige muhuri usiofutika
kirahisi mifugo yake. Kwa sababu ya muhuri huo – inakuwa rahisi kuijua
mifugo iliyo yake.
Biblia
inatuambia ya kuwa Yesu Kristo ni mchungaji mkuu wa kondoo wake, ambao
ni sisi – na pia ametupiga mihuri mioyoni mwetu ili iwe rahisi kwetu
kutambulikana kwake, na kwa shetani pia.
Imeandikwa
hivi;
“Na
kwa kuwa ninyi mmekuwa wana,
Mungu alimtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, aliaye, Aba, yaani,
‘Baba’ (Wagalatia 4:6)
Tena
imeandikwa hivi;
“Nanyi
pia katika huyo mmekwisha kumwamini yeye, na kutiwa muhuri na Roho yule
wa ahadi aliye Mtakatifu. Ndiye aliye arabuni ya urithi wetu, ili kuleta
ukombozi wa milki yake kuwa sifa ya utukufu wake” (Waefeso 1:13,14).
Je!
umejionea mwenyewe maneno haya?…. “mmekwisha kumwamini yeye, na
kutiwa MUHURI na roho yule wa ahadi aliye mtakatifu.” Ikiwa umepigwa
au umetiwa muhuri na Mungu kwa njia ya Roho Mtakatifu aliye ndani yako,
ni nani atakayethubutu kusema hujaokoka sawasawa na
ubabaike? Jibu ni hakuna!
Pia,
fahamu ya kuwa si tu kwamba Roho Mtakatifu ametutia muhuri wa Mungu
ambao kwa huo uzima wa milele uliomo ndani yetu anatutambua tu wake, -
lakini pia Roho Mtakatifu “ndiye aliye ARABUNI ya urithi wetu….”
Neno
“arabuni’ maana yake dhamana. Ngoja nikupe mfano utakaokusaidia
kuelewa vizuri uzito na maana ya neno hili
Ikiwa
una ndugu au rafiki aliyeshikwa na polisi na kuwekwa ndani, kufuatana na
sheria ya nchi, unaweza kumwekea mdhamana mahakamani kwa kuweka ahadi ya
kuwa wewe ndiye utakayefuatilia maisha yake akiwa nje kwa dhamana, na
kwamba akitakiwa mahakamani atakuwepo, na asipokuwepo wewe ndiye
utakayewajibika.
Kumbuka na sisi kabla ya kuokoka tulikuwa tumefungwa katika minyororo ya
dhambi – na Yesu Kristo alikufa na kufufuka ili kututoa katika
minyororo hiyo – na ametutumia ahadi ya Roho mioyoni mwetu kututia
MUHURI ili tusipotee bali tuwe na uzima wa milele na tabia mpya na
mwenendo mpya ili ijulikane ya kuwa sisi ni wake pia, Roho Mtakatifu
ndiye arabuni – mdhamini wa urithi wetu (- tuko nje ya mnyororo wa
dhambi kwa sababu Yesu ametudhamini kwa Roho huyo aliyetupa) – “ ili
kuleta ukombozi wa milki yake” siku ya hukumu ikifika tutakaposimama
mbele ya mahakama ya mbinguni.
Sasa
unaweza ukaelewa vizuri mistari ifuatayo:
“Basi
yeye atufanyae imara pamoja nanyi katika Kristo, na kututia mafuta, ni
Mungu, naye ndiye aliyetutia muhuri akatupa arabuni ya Roho mioyoni
mwetu”
(2 Wakorintho 1:21,22).
Tafsiri
nyingine inasema hivi hasa mstari huu wa 22 ya kuwa “naye ndiye
aliyetutia muhuri akatupa uhakika wa udhamini wake kwa kutupa roho wake
mioyoni mwetu”
Je!
sasa unaelewa? Ukisoma pia 2 Wakorintho 5:5 utaona wazo hili
likijitokeza tena; “Basi yeye aliyetufanya kwa ajili ya neno lilo hilo
ni Mungu, aliyetupa arabuni ya Roho”.
Suala
la wewe kuwa na uhakika ya kuwa umeokoka si suala la kuona jinsi
unavyojisikia bali ni suala la wewe kuamini neno la Mungu ya kuwa
kimetokea moyoni mwako kile ambacho neno linasema kimetokea.
Suala
la wewe kuwa na uhakika wa wokovu wako si suala la kupata maoni kutoka
kwa wanadamu, bali ni suala la wewe kujua neno la Mungu (Biblia)
linasema nini juu ya mtu aliyeokoka na kuliamini.
Kwa
hiyo ikiwa umeifanya sala ya toba na kumpokea Yesu Kristo moyoni mwako
kama Bwana na Mwokozi wako, biblia inasema; 1. Umesamehewa dhambi zako
zote na Mungu, na wala hazikumbuki tena; 2. Roho Mtakatifu yumo ndani
yako na amekutia muhuri kuthibitisha ya kuwa wewe ni mtoto wake na
amekudhamini maisha yako.
Ikiwa
Yesu Kristo katudhamini kwa roho wake (Waefeso 1:13,14), tena ndiye
wakili wetu anayetutetea (1Yohana 2:1,2) wa kutuombea (Waebrania 7:18)
mbele za Baba Mungu …. na ikiwa Mungu Baba amekubaliana na upande wa
utetezi (Warumi 8:31-34) – shetani aliye mshitaki wetu atatubabaisha
nini?
Ndiyo
maana imeandikwa hivi; “Yesu amekuwa mdhamini wa agano lililo bora
zaidi … kwa sababu hii, aweza kuwaokoa kabisa wao
wamjiao Mungu kwa yeye, maana yu hai siku zote ili awaombee” (Waebrania
7:22,25)
Kwa
hiyo usisumbuke kwa mawazo wala maneno yanayosema hujaokoka sawasawa –
kwa sababu Bwana Yesu Kristo amekuokoa “KABISA”!
ATAKAYEVUMILIA
MPAKA MWISHO
Kuna
usemi unaosema ‘kuzaa ni rahisi kuliko kulea”. Wale wakina mama
wenye watoto wanaelewa wazi ya kuwa kumlea mtoto ni kazi ngumu kuliko
kumzaa.
Tukizungumza
kwa jinsi ya rohoni tunaweza kusema kuokoka si kazi ngumu, bali kudumu
katika wokovu ndipo penye mtihani mzito.
Katika
maisha ya wokovu unaweza kukutana na vipingamizi vya kila namna ili
mradi tu shetani apate namna ya kukukatisha tamaa uache wokovu. Ndiyo
maana Yesu Kristo alisema hivi;
“Lakini
mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka” (Mathayo 24:13)
Yesu
hakuwa anatuambia ya kuwa huwezi kuokoka mpaka ufikie mwisho wa maisha
yako, au ufike mwisho wa dunia, bali alikuwa anatutahadharisha juu ya
majaribu tunayoweza kukutana nayo katika maisha ya wokovu.
Ndiyo
maana mistari mingi katika biblia imeandikwa kutukumbusha juu ya jambo
hili. Kwa mfano hebu soma mistari ifuatayo:
“Naja
upesi. Shika sana ulicho nacho asije mtu akaitwaa taji yako” (Ufunuo
3:11).
Pia
katika Kitabu cha Ufunuo 3:7,11,17, 26-28 na Ufunuo 3:5,12 na 21 utaona
jinsi Yesu Kristo anavyoeleza na kututia moyo akieleza kitu gani
kitatokea watu wake wakishinda mitego na mitihani ya maisha iliyoko
mbele yao. Katika Ufunuo 2:10 anasema:
“Usiogope
mambo yatakayokupata; tazama huyo ibilisi atawatupa baadhi yenu gerezani
ili mjaribiewe, … uwe mwaminifu hata kufa nitakupa taji ya uzima”.
Sikuandikii
mambo haya kukuogopesha na kukutisha na pia nitakuwa sikuambii ukweli
kama nitakuambia ya kuwa maisha ya wokovu ni mtelemko tu. Maisha ya
wokovu si mtelemko wala lele mama – yana gharama yake. Lakini
kilicho muhimu ni kujua ya kuwa unapookoka Yesu Kristo aliye ndani yako
anakuwezesha kuishi maisha ya ushindi kila siku na kila mahali.
Nakushauri
udumu katika mambo yafuatayo ili maisha yako ya wokovu yazidi kushamiri
na kuimarika sasa na siku zote:
1.
Dumu katika kusoma na kutafakari Neno la Mungu lililomo katika
Biblia. Roho Mtakatifu uliye naye sasa atakusaidia na kukuhekimisha
namna ya kuisoma Biblia – akikufunulia maana ya mistari hiyo
unayoisoma.
2.
Dumu katika maombi – kuzungumza na Mungu wako katika sala.
Biblia ina mistari mingi sana inayoeleza faida ya kudumu katika maombi.
Uwe mtu wa maombi, na utaona mabadiliko makubwa yakitokea hasa katika
kuwa karibu zaidi ya uongozi wa Mungu na msaada wake.
3.
Usiache kukutanika na watu wengine waliookoka katika kushirikiana
neno la Mungu, kuonyana na
kutiana moyo katika safari hii ya wokovu. Mungu atakuongoza katika jambo
hili pia.
4.
Kila mara unapoona nafasi ikitokea, kusudia kabisa, na tamani
watu wengine waokoke kama vile wewe ulivyookoka. Kwa hiyo uwe tayari
kuwashuhudia watu wengine habari za Bwana Yesu ili yamkini neema ya
Mungu iliyo juu yao ikawasaidie wapate kutubu, na kumrudia Mungu wao na
kuokoka.
Katika
mambo yote hayo, ni maombi yangu kwa Mungu ya kuwa yeye mwenyewe
atakutunza na kukusaidia ili maisha yako yawe ya ushuhuda, kila siku na
kila mahali.
Kumbuka
umekuwa kiumbe kipya ndani ya Kristo na unaposema umeokoka – shetani
anategemea tabia yako ibadilike na wanadamu waokuzunguka wanategemea
tabia yako ibadilike. Isipobadilika wanaanza kuwa na wasiwasi na wokovu
wako. Watafikiri unatania. Mimi naamini umeokoka kweli na wala hutanii
– ndiyo maana umekisoma kitabu hiki bila kuchoka mpaka umefikia hapa
– kwa hiyo maisha yako yabadilike na tabia zako zibadilike.
Neno
la Mungu katika Yakobo 2:17,26 linasema; “ Vivyo hivyo na imani,
isipokuwa ina matendo, imekufa nafsini mwake …. Maana kama vile mwili
pasipo roho umekufa, vivyo hivyo na imani pasipo matendo imekufa”.
Maana
yake unatakiwa uwe mtendaji wa neno na usiwe msikiaji tu ukitaka maisha
yako ya kiroho yajengwe juu ya msingi imara na usiotikisika.
MWISHO
TUNAKUTAKIA
BARAKA NA USHINDI
Mimi na mke wangu, Diana, pamoja na watoto wetu Esta, Ana, Sara
na Joshua tukishirikiana na wenzetu wa timu ya maombi tunaodumu nao
katika kazi ya Mungu – tunapenda kukutia moyo na kukutakia baraka za
Bwana na ushindi tele katika maisha haya mpya ya wokovu uliyoanza.
Jipe moyo mkuu kwa kuwa, Mungu amekusudia mambo mazuri juu yako.
Piga vita vile vizuri vya imani; shika uzima ule wa milele ulioitiwa,
uweze kumjibu kila mtu akuulizaye juu ya uhusiano wako na Mungu katika
Kristo Yesu.
Na sisi hatutaacha kutoa shukrani zetu kwa Mungu kwa kukuokoa,
tukikukumbuka katika sala ya kuwa Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba
wa utukufu, akupe wewe, roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye;
macho ya moyo wako yatiwe nuru ujue tumaini la mwito wa wokovu wake juu
yako jinsi ulivyo; na ubora wa ukuu wa uweza wake ndani yako jinsi
ulivyo; kwa kadri ya utendaji wa nguvu za uweza wake; aliotenda katika
Kristo alipomfufua katika wafu, akamweka mkono wake wa kuume katika
ulimwengu wa Roho.
Basi, Mungu huyu wa amani aliyemleta tena kutoka kwa wafu
Mchungaji Mkuu wa Kondoo kwa damu ya agano la milele, yeye Bwana wetu
Yesu, akufanye wewe kuwa mkamilifu katika kila tendo jema, upate
kuyafanya mapenzi yake; naye Mungu akifanya ndani yako lipendezalo mbele
zake; kwa Yesu Kristo; Utukufu una yeye milele na milele Amina.
Ikiwa utapenda kutushirikisha mahitaji yako ya maombi ili
tushirikiane nawe katika maombi basi niandikie:
Christopher
na Diana Mwakasege,
S.L.P. 2166,
ARUSHA.