Wiki ya kwanza
KUTOKUSAMEHE
NI KIKWAZO
" Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni mkiwa na neno juu ya mtu;
ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu.
Lakini kama ninyi hamsamehi, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe
ninyi makosa yenu" (Marko 11:25,26).
Kutokusamehe ni kikwazo na kizuizi kikubwa ambacho kinasimama kati ya
mtu na majibu ya maombi yake. Watu wengi wanapenda imani zao zikue,
lakini kwa sababu ya kutokusamehe imani zao zinakuwa hazina matunda.
Tatizo si kwamba watu hawapendi kusamehe. Ingawa watu wanapenda
kusameheana, lililo wazi ni kuwa walio wengi hawajui namna ya kusamehe
kule kunakokubalika na Bwana. Watu wengi wanajifunza katika biblia juu
ya imani, maombi, utakatifu na mambo mengine ya kiroho. Lakini ni watu
wachache wanaojifunza kutoka katika biblia namna ya kusamehe.Kati ya
vizuizi vya mtu kupokea jibu la maombi yake kutoka kwa Mungu, ni tatizo
la kutokujua jinsi ya kusamehe.
Bwana
Yesu alipowambia wanafunzi wake juu ya kusamehe alitaka waone uhusiano
ulipo kati ya sala na kusamehe. Kwa maneno mengine alitaka wafahamu kuwa
kujibiwa kwa maombi na sala na dua kunategemea sana uhusiano walionao na
watu wengine.Kabla Yesu hajasema juu ya kusamehe alizungumza maneno
muhimu sana juu ya maombi. Yesu alisema hivi:
" Mwamini Mungu. Amini, nawaambia, yeyote
atakayeuambia mlima huu, ng'oka ukatupwe baharini, wala asione shaka
moyoni mwake, ila aamini kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake.
Kwa sababu hiyo nawaambia, Yoyote myaombayo mkisali, aminini ya
kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu." (Marko11:22 - 24)
Haya
ni maagizo muhimu sana kwa kila mkristo, kwa ajili ya maisha ya ushindi
kila siku. Na watu wengi wamekuwa wakiitumia mistari hii, ili kupata
mahitaji yao ya kiroho na ya kimwili.
Mafanikio yako katika kutumia mistari hiyo na ahadi hizo za Bwana Yesu,
yatategemea sana jinsi wewe unavyofuata maagizo ya Yesu juu ya matumizi
ya mistari hiyo.
Kuna
mtindo uliozuka katikati ya watu wa Mungu, wa kuifanya biblia kuwa kama
duka. Wanafungua biblia, wanachagua mistari wanayotaka na ahadi
wanazotaka, wanaondoka nazo, huku wakiiacha mistari mingine kwenye
biblia.
Lakini wanapoitumia hiyo mistari ya ahadi wanazotaka, na kuona hakuna
matokeo yoyote, wanaona kama kwamba neno la Mungu limepungua nguvu.Hiyo
si kweli. Neno la Mungu halijapungua nguvu zake wala halitakujapungua
nguvu zake. Neno la Mungu hudumu milele.Kwa hiyo ni vizuri kusoma na
kutafakari ahadi za Mungu juu ya maombi, lakini pia ni muhimu sana
kuhakikisha kuwa unafuata maagizo yote ya utumiaji wa ahadi hizo.Kwa
hiyo walio wengi. Maombi yao juu ya magonjwa, ndoa zao, wokovu wa ndugu
zao na kadhalika, yamefungwa kwa kutotimiza maagizo haya ya Bwana Yesu.
"NINYI KILA MSIMAMAPO NA KUSALI, SAMEHENI, mkiwa
na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe
na ninyi makosa yenu. Lakini kama ninyi hamsamehi, wala Baba yenu
aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu" (Marko 11;25,
26).
Maombi yako hayajibiwi mara nyingi kwa sababu ya wewe kutosamehe wengine.
Kwa maneno mengine Yesu alitaka tufahamu kuwa, tusipojifunza kusamehe
wengine waliotukosea, tutabaki na dhambi mbele za Mungu.
Maana yake nini basi?
Maana
yake, kutokusamehe kunahesabiwa kuwa ni kosa mbele za Mungu, na ni
dhambi inayotutenga na uso wa Mungu, ili tusijibiwe maombi yetu toka kwa
Mungu.
Kutokusamehe ni uasi Dhambi ni uasi (1 Yohana 3:4) Dhambi ni
kuasi maagizo ya Mungu.
Kama
Mungu ameagiza kwa kinywa cha Kristo kuwa kabla hatujaomba lo lote, ni
lazima tusamehe kwanza; inakuwaje basi, wewe unataka ujibiwe maombi yako
kabla hujamsamehe mwenzako?
Na
kwa kutokusamehe umeasi agizo la Mungu, na kufuatana na waraka wa kwanza
wa Yohana 3:4 umehesabiwa kuwa
umetenda dhambi.Kwa hiyo unahitajiwa utubu juu ya kutokusamehe!
Tuna
uhakika kuwa wewe unayesoma hayo umewahi kuisema 'Sala ya Bwana'
iliyoandikwa katika kitabu cha Mathayo, Sura ya
6:9-15.
Hatujui kama unaelewa uzito wa maneno yaliyomo katika sala hiyo. Walio
wengi wanaisema kwa sababu wameikariri, lakini si kwamba wameielewa
maana yake.
Katika sala hiyo, kuna maneno yanayohusu mambo ya kusamehe:
"Utusamehe deni zetu (makosa yetu) kama
sisi nasi tuwasamehevyo wadeni wetu (walio tukosea). (Mathayo6:12)
Tafakari hili neno 'kama'
Utusamehe makosa yetu, kama sisi
nasi tunavyowasamehe waliotukosea.Hii ina maana ya kwamba kipimo kile
unachokipimia katika kuwasamehe wengine ndivyo na Mungu atakavyotumia
kipimo hicho hicho kukusamehe wewe mambo uliyomkosea.Sasa elewa kwamba
hakuna kusamehe kukubwa, wala kusamehe kudogo. Kutokusamehe ni
kutokusamehe. Na kusamehe ni kusamehe. Mizani yake inapima kitu kizima,
haipimi msamaha kidogo kidogo.
Yesu alilifafanua jambo hili aliposema:-
"Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa
mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msiposamehe watu makosa yao, wala Baba
yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu." (Mathayo 6:14,15).
Je, unaweza kusamehe bila kusahau?
Tulipokuwa tunaongea na mama
mmoja juu ya kumsamehe mume wake, ili ugonjwa wake upone, alituambia;
"Mimi nilikwishamsamehe siku nyingi."
Tukamuuliza; "Una
uhakika?"
Akasema, "Ndiyo, la
sivyo ningekuwa nimekwishatengana naye"
Tukamuuliza tena: "Kuna
wakati wo wote huwa unawaza kuwa isingekuwa ni watoto mliozaa naye,
ungeomba talaka au ungeondoka tu?
Akasema; Ndiyo, tena mara
nyingi."
Tukamwambia: "Kusamehe
kwako kuko wapi wakati bado unayahesabu makosa ya mume wako, kiasi
ambacho ndoa imeshikiliwa na watoto badala ya kushikiliwa na makusudi ya
Mungu?"
Yule mama akashangaa.
Kuna watu wengine wanasema
wamesamehe wakati, bado kuna fundo na shina la uchungu katika mioyo yao.
Kwa kinywa wanasema, wamesamehe, lakini moyoni bado hawajasamehe.
Na kuwatambua watu wa namna
hiyo ni rahisi sana.
Mtu huyo huyo akimkosea tena, utamsikia akilalamika akisema;
"Mtu
huyu nilimsamehe lile kosa la kwanza, tena amerudia. Kumbe mambo
yalikuwa hayajaisha, ndiyo maana hata siku fulani alisema maneno fulani,
ndiyo maana hata juzi alimgombeza mtoto wangu ......"
Utaona mtu huyo akiyakumbuka yote mabaya ya nyuma ambayo mwenzake
alimtendea. Wengine hata hudiriki kusema kuwa: "Nitamsamehe
lakini sitasahau"
Sasa, hiyo siyo lugha ya watu wa Mungu, waliookolewa na kununuliwa kwa
damu ya thamani ya Yesu Kristo.
Hiyo
ni lugha ya watu wasiomjua Mungu, watu wa ulimwengu huu. Na Biblia
inatuambia kwamba sisi siyo wa ulimwengu huu. (Yohana
17:16).
Weka hilo katika roho yako. Wewe si wa ulimwengu huu, kwa hiyo lugha na
maneno ya ulimwengu huu hayakuhusu. Zungumza lugha ya watu watakatifu wa
ufalme wa Mungu ambao ndiyo wa uzao wako.
Utawezaje kusema kuwa umemsamehe mwenzako wakati bado una uchungu naye
moyoni mwako? Utasemaje umemsamehe wakati kila wakati unalikumbuka na
kulisema kwa watu kosa alilokufanyia?
Utasema huko ni kusamehe ambako Mungu anataka ufanye, ili na yeye
akusamehe.
La hasha!
Kusamehe bila kusahau kosa ulilokosewa ni kusamehe kusikokamilika wala
kukubaliwa mbele za Mungu. Kusema umesamehe huku bado una uchungu moyoni
mwako, ni unafiki ulio wazi mbele ya Mungu.
Je! hujawahi kusoma mistari ifuatayo:
"Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa,
Usiue; na mtu akiua, itampasa hukumu. Bali mimi nawaambieni, kila
amwoneaye ndugu yake hasira itampasa hukumu, na mtu akimfyolea
ndugu yake itampasa baraza; na mtu akimwapiza itampasa jehanamu ya
moto."(Mathayo 5:21, 22)
Unaweza kuona jinsi Yesu Kristo alivyofananisha hasira hiyo iliyojaa
moyoni mwako juu ya ndugu yako na uuaji. Na adhabu zake zinafanana.Sasa,
utakuwa unajiuliza, inawezekana kwa vipi mtu kusahau mabaya
aliyotendewa?Basi nakuhakikishia kuwa inawezekana kabisa! Kwa kuwa yote
yanawezekana kwake aaminiye. Na imani huja kwa kusikia neno la Mungu (Warumi
10:17) Tatizo lako ni kwamba unaona kusamehe na kusahau ni
vitu viwili tofauti, kwa hiyo unavitenganisha. Huwezi ukatenganisha
kusamehe na kusahau. Kwa kuwa huwezi kusamehe bila kusahau; na huwezi
kusahau bila kusamehe.
Ufanyeje basi, uweze kusamehe na kusahau ili na Mungu naye akusamehe na
kusahau makosa yako?
Ili tuweze kufahamu namna ya kusamehe na kusahau, ni muhimu tuielewe
tabia ya Mungu juu ya jambo hili.
Usiache
kusoma somo la Wiki ya Pili ili kuendelea na somo hili la Jifunze
kusamehe na kusahau katika kipengele kinachosema: Tabia
ya Mungu ya kusamehe ndani yako
Jifunze
kusamehe
na kusahau / Utang / 1 / 2
/ 3 / 4 / 5
/ 6 /