Wiki ya Tatu
HASARA
ZA KULIPIZA KISASI
Usilipize Kisasi! Unasikia? Hata ikiwa umefanyiwa ubaya wa namna gani,
Biblia inafundisha na inakusihi usilipize kisasi kwa huyo aliyekufanyia
ubaya. Biblia inasema hivi:
"Wapenzi, msijilipizie kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu;
maana imeandikwa, kisasi ni juu yangu Mimi, Mimi nitalipa, anena
Bwana" (Warumi 12:19)
Kuna
hasara zinazoweza kukupata ukiamua kulipa kisasi kwa mambo uliyofanyiwa
ambayo hayakupendezi. Ikiwa ni masuala ya kikabila, usilipe kisasi.
Ikiwa ni masuala ya kidini, usilipe kisasi. Ikiwa ni masuala ya
kifamilia, usilipe kisasi. Ikiwa ni masuala ya kikazi, usilipe kisasi.
Ikiwa ni masuala ya uhusiano wako na majirani zako, usilipe kisasi.Ndiyo!
Usilipe kisasi! Kwa nini? Kwa sababu "imeandikwa kisasi ni juu
yangu Mimi; Mimi nitalipa, anena Bwana".
Lakini ikiwa utaona ya kuwa Mungu hawezi kukusaidia na ukaamua
kujichukulia madaraka ya kujilipiza kisasi hasara zifuatazo hakika
zitakupata!
Hasara ya Kwanza:
UTASHINDWA!
Katika jambo lolote lile lililokukasirisha - liwe la kidini, au kikabila,
au kifamilia, au kikazi, na kadhalika ukiamua kulipa kisasi utashindwa
wewe kwa sababu vita hivyo si vya mwili na wala silaha ambazo Mungu
amekupa si za mwili! Tunasema hivi kwa sababu katika 2 Wakorintho
10:3- 5 imeandikwa hivi:"Maana ingawa tunaenenda katika mwili,
hatufanyi vita kwa jinsi yamwili; maana silaha za vita vyetu si za mwili,
bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome, tukiangusha mawazo na
kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka
nyara kila fikra ipate kumtii Kristo".
Tena
katika kitabu cha Waefeso 6:12 imeandikwa hivi: "Kushindana
kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu
ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa
roho".
Uwanja wa mapambano uliyonayo ni "katika ulimwengu wa roho"
na mapambano uliyo nayo "si juu ya damu na nyama" - ingawa
unaona ya kuwa ni watu na ni binadamu kama wewe wanaokusonga - lakini
fahamu hili ya kuwa wanatumiwa tu na ibilisi!
Mbinu
mojawapo ya shetani anayotumia akitaka kukuangamiza ni kukufanyia kitu
kitakachokukasirisha ili uamue kujibu au kushindana kimwili kwa sababu
anajua ukishindana "kimwili" au katika mwili utashindwa hakika,
maana vita hivyo si vya mwili wala silaha ambazo Mungu amekupa si za
mwili!
Hasara ya Pili:
MATATIZO HAYATAKWISHA!
Kumbuka imeandikwa hivi katika kitabu cha Wagalatia 6:7; "Msidanganyike,
Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa chochote ampandacho mtu. Ndicho atakachovuna".
Ikiwa
umeamua kulipa kisasi kwa kumfanyia ubaya yule aliyekufanyia - ubaya
hautakwisha, kwa sababu utavuna ulichopanda.Ndiyo maana imeandikwa hivi:"Yeye
arudishaye mabaya badala ya mema, mabaya
hayataondoka nyumbani mwake" (Mithali 17:13)
Ukiamua kulipiza kisasi kwa kumfanyia ubaya yule wa nyumbani mwako -
Biblia inasema "mabaya hayataondoka nyumbani mwako" Hii ndiyo
maana matatizo mengi katika ndoa na katika jamii hayaishi - kwa sababu
mtu akifanyiwa ubaya naye analipa kisasi.
Ukiamua kulipa kisasi kwa kumfanyia ubaya yule wa nchini mwako ujue
hakika mabaya hayataondoka nchini mwako. Hili ndilo lililowapata wenzetu
wa nchi za Burundi na Rwanda - kulipizana kisasi - matokeo ni uhasama
usiotaka kupotea - pamoja na juhudi zote za kimataifa kutafuta suluhisho.
Ukiamua kulipa kisasi kwa kumfanyia ubaya yule wa kazini kwako - fahamu
mabaya hayataondoka kazini kwako. Ikiwa ni shuleni - mabaya hayataondoka
hapo shuleni.
Tena
hali ya mwisho inakuwa mbaya zaidi,kila wakati kisasi kinapoendelea
kupandwa. Kwa sababu ukiwapa watu ubaya - nawe utapewa ubaya kwa; "kipimo
cha kujaa na kushidiliwa, na kusukwa - sukwa - hata kumwagika, ndicho
watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile upimacho
ndicho mtakachopimiwa (Luka 6:38)
Kumbuka ubaya haushindwi na ubaya mwingine, bali unashindwa na wema -
kama vile dawa ya chuki si chuki bali upendo! Ndiyo maana Warumi
12:21 inasema; "Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema".
Hasara ya Tatu:
UNAMZUIA MUNGU KUKUPIGANIA
Unaweza ukashangaa, lakini ndivyo ilivyo! Ukiamua kulipa kisasi juu ya
tatizo ulilonalo - unamzuia Mungu asikusaidie kulitatua.Mungu hawezi
kukusaidia kwa sababu imeandikwa "msijilipize kisasi, bali
ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana, imeandikwa, kisasi ni juu yangu mimi;
mimi nitalipa, anena Bwana".
Neno "ipisheni" limeandikwa kwa sababu kulipa kisasi "kunazuia"
ghadhabu ya Mungu isipigane upande wako! Tena si hivyo tu lakini ukilipa
kisasi unaingilia kazi ambayo si yako! Ni kazi ya Mungu maana anasema
"Kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena Bwana" Ikiwa
kisasi ni juu ya Mungu kulipa, basi huhitaji wewe kulipa. Je, tunakwenda
pamoja katika hili?
Hatua
yako ya kulipa kisasi inazuia mkono wa Mungu kukupigania - kwa hiyo
ipishe ghadhabu ya Mungu kwa kutokujilipizia kisasi!
Hasara na Nne:
UNAJICHUMIA DHAMBI!
Unapoamua kulipa kisasi, unajichumia dhambi! Hii ni kwa sababu kulipa
kisasi huja kwa njia ya chuki iliyojengeka ndani yako kwa ajili ya mambo
mabaya uliyofanyiwa. Huwezi kulipa kisasi bila ya kumchukia huyo
unayejilipizia kisasi kwake. Na Biblia inasema hivi:
"Kila amchukiaye ndugu yake ni mwuaji: nanyi mnajuaya kuwa kila
mwuaji hana uzima wa milele ukikaa ndani yake" (1 Yohana 3:15).
Umeona hilo! Chuki huzaa kisasi, na huzaa dhambi ya kuua! Na
Isaya 59:2b inasema; "dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone,
hata hataki kusikia".
Kwa
hiyo kama umekwisha lipa kisasi au umekusudia moyoni mwako kulipa kisasi
ni muhimu utubu ili Mungu akusamehe na mawasiliano yako na Yeye
yawe mazuri.
Usikose kusoma wiki ya
nne ya mfululizo huu tutakapojifunza juu ya:
Hatua tano Muhimu katika kusamehe na kusahau
Jifunze
kusamehe na kusahau / Utang /
1 / 2 / 3 / 4 /
5 / 6 /