Wiki ya Nne
HATUA
TANO MUHIMU KATIKA KUSAMEHE
Biblia inatuambia kwamba Mungu huyu ambaye amesema anafuta na kuyasahau
makosa yetu, kwa ajili yake mwenyewe, anakaa ndani ya watu wote
waliompokea. Hebu soma na kutafakari maneno yafuatayo:
"Hapa mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu,
naye Neno alikuwa Mungu. Naye Neno akafanyika mwili, akakaa kwetu,
nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa
Baba, amejaa neema na kweli. ...... Wote waliompokea aliwapa uwezo wa
kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake,
waliozaliwa,si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi
ya mtu, bali kwa Mungu" (Yohana 1:1, 14, 12, 13).
Yesu
Kristo anapoingia ndani ya moyo wako, baada ya wewe kumwamini na
kumpokea, unapewa uzima wa milele ndani yako, na unaanza maisha
mapya.Imeandikwa kwamba, " Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya
Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita; tazama! Yamekuwa mapya
(2Wakorintho 5:17)
Utu
mpya unazaliwa ndani yako, maisha, mawazo, matendo, maneno, yanatakiwa
kubadilika Yesu Kristo aingiapo ndani yako. Pia, kusamehe kwako
kunabadilika kunakuwa kupya.Lakini utaona kwamba watu wengi waliozaliwa
mara ya pili, na kumkiri Kristo kuwa ni Bwana na Mwokozi wao, bado
wanaendelea kusamehe kama zamani.
Biblia inasema " ya kale yamepita, tazama!yamekuwa mapya"(2Wakorintho
5:17).
Kwa maneno mengine ni kwamba kusamehe kwako ulivyokuwa unafanya zamani,
hakuhitajiki tena, tazama! Kusamehe sasa ni kupya. Tabia ni mpya.Zamani
ulisamehe lakini bado ulikumbuka makosa uliyofanyiwa. Tena ulisamehe si
kwa ajili yako bali kwa ajili yake aliyekukosea na wakati mwingine
ulitaka uthibitisho kwanza kuwa kosa hilo halitarudiwa na ndipo usamehe.
Ni lugha ya kawaida kusikia mtu akisema 'nasamehe lakini sitasahau'.
Katika maisha mapya utatakiwa usamehe na kusahau kwa ajili yako mwenyewe,
ili kuomba kwako kusizuiliwe na baraka zako zisizuiliwe. Kwa kuwa
imeandikwa hivi:
"Yeye asemaye yakuwa anakaa ndani yake, imempasa kuenenda mwenyewe
vile vile kama yeye alivyoenenda" (1Yohana 2:6)
Wewe unayesema kwamba una Kristo ndani yako, basi inakupasa kuenenda
kama Kristo alivyoenenda alipokuwa hapa duniani katika mwili.Kwa kuwa
Kristo alisamehe na kusahau, basi na wewe inakubidi kusamehe na kusahau.
Hatua
tano zifuatazo zitakupa msingi imara wa kuishi siku zote katika upendo
na amani na jirani zako na ndugu zako. Na pia, zitafungua milango mipya
ya uhusiano wako na Mungu utakaoinua huduma yako katika kumtumikia Mungu.
Na zaidi ya yote zitakuweka huru na magonjwa mengi yanayokusumbua:
1. Fahamu kuwa si wewe bali Kristo.
"Nimesulibiwa pamoja na Kristo, lakini ni hai, wala si mimi tena,
bali Kristo yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao sasa katika mwili,
ninao katika imani ya Mwana wa Mungu ambaye alinipenda akajitoa
nafsi yake kwa ajili yangu" (Wagalatia 2:20)
"basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo
juu, Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu, yafikirini
yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi.Kwa maana mlikufa, na uhai wenu
umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu" (Wakolosai 3:1-3)
Mistari hii michache ni baadhi tu ya ile inayotufunulia mambo
yaliyofanyika ndani yetu tulipompokea Kristo kuwa Bwana na Mwokozi
wetu.Si wewe unayeishi, bali ni Kristo aliye ndani yako. Na uhai ulio
nao sasa, baada ya kuzaliwa mara ya pili, unao katika imani ya Mwana wa
Mungu.Soma tena mstari huu:-
"..... Kwa maana mlikufa na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo
katika Mungu."
"Kwa
maana mlikufa." Utu wako wa kale, na mtu wa kale ndani yako alikufa
siku ulipompokea Kristo maishani mwako. Kilichofuata ni uzima wa Kristo,
katika utu mpya ukidhihirishwa katika maisha yako.Sasa unaweza kuelewa
kwa nini Yesu Kristo alisema awachukiae ninyi, amenichukia mimi. (
Yohana 15 :18)
Mtu
akikufanyia ubaya, usione kuwa anakufanyia wewe, ona kama vile Mungu
aonavyo kuwa, ubaya huo anafanyiwa Kristo aliye ndani yako.Mtu
akikutukana, akikusemea mabaya, akikupiga, fahamu kuwa si wewe
anayekufanyia hayo, bali Kristo aliye ndani yako!Kuthibitisha haya
Biblia inasema:
"Vita hivyo si vyako ni vya Bwana" (2 Mambo ya Nyakati
20:15). Ukiwa na wazo hilo katika roho yako, chukua hatua ya pili
ifuatayo:
2. Mpende adui yako Umuombee
"Mmesikia
kwamba imenenwa, Umpende jirani yako na umchukie adui yako; lakini
mimi nawaambia, wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi
...." (Mathayo 5:43, 44)
Jambo
ambalo liko wazi ni kwamba hakuna msamaha wa kweli pasipo upendo,
"Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda
ulimwengu hata akamtuma Mwanae ..." (Yohana 3:16)
Kilichomfanya Baba Mungu kumtuma Yesu Kristo duniani ni Upendo.
Alitupenda sisi mno, alitupenda upeo wakati bado tulipokuwa tungali
wenye dhambi. Na kuudhihirisha upendo huo, Yesu Kristo alizaliwa duniani
na kufa masalabani ili sisi tupone.
Msamaha wa kweli unadhihirisha upendo ulio ndani ya mtu. Pasipokuwa na
upendo, kusameheana hakupo. Palipo na upendo wa kinafiki, pia pana
kusameheana kinafiki.
Kusameheana hakuonekani siku hizi, katika ndoa, kati ya ndugu, kati ya
majirani, kati ya watu wa Mungu, KWA SABABU UPENDO WA WENGI UMEKWISHA
POA!
Watu
siku hizi wanafanya kile ambacho Yesu Kristo aliwaambia wasifanye. Yesu
alisema, " Wapendeni adui zenu." Lakini, unaona katika watu wa
Mungu, chuki imejaa, ndoa zinaharibika kwa sababu ya chuki, undugu
unakufa kwa sababu ya chuki. Na ni hao wanaosema kuwa wameokoka na Yesu
Kristo yumo ndani yao. Usiwachukie wanaokuudhi, wapende.
Yesu
Kristo anakuambia watu wa dunia wanawapenda wanaowapenda na kuwachukia
wanaowachukia, lakini wewe si wa dunia hii, wapende hata wale
wanaokuchukia na ili kuonyesha kuwa unawapenda kweli, uwaombee!
Kwa
nini Yesu Kristo, alisema "Wapendeni adui
zenu, waombeeni wanaowaudhi?"
Ni,
"Ili
mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua
lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki Maana
mkiwapenda wanaowapenda ninyi, mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru,
je! Nao hawafanyi yayo hayo? Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda
tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je? Nao hawafanyi kama hayo?"
(Mathayo 5:45- 47).
Ulipompokea Kristo, ulipokea upendo mpya ndani yako, unaokuwezesha
kufanya mambo ambayo mtu wa kale aliyekuwa ndani yako asingeweza kufanya.
Mtu mpya ndani yako ana upendo mpya.
Upendo huu mpya, una tabia mpya, na mambo mapya.
"Upendo huvumilia, hufadhili, upendo hauhusudu; upendo hautakabari;
hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii
udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli huvumilia yote; huamini yote;
hustahimili yote. Upendo haupungui neno wakati wo wote"(1Wakorintho
13:4 - 8).
Upendo huu umo ndani yako, na ndio unaokufanya uwe kiumbe kipya. Ni
upendo ulio hai (Warumi 5:5)
Ni
upendo unamuondolea mtu chuki, uchoyo na ubinafsi.
Kwa upendo huu, Bwana Yesu anataka uwapende adui zako, na kuwaombea pia
ili wasamehewe na Mungu juu ya makosa waliyoyafanya.
Kwa
upendo huu fanya yale ambayo ulikuwa huyafanyi zamani.
Kama ulikuwa husalimiani na adui yako, chukua hatua ya upendo, msalimie
na ikibidi mtembelee nyumbani mwake. Kula pamoja naye, furahi pamoja
naye, na omba pamoja naye.
Kuna
watu wengine hawasalimiani wala kutembeleana na wazazi wao, au baba au
mama, kwa sababu ya mambo yaliyofanyika zamani ambayo hawakuyapenda.
Sasa,
chukua hatua waandikie barua, na uwatembelee kwa maana upendo wa Kristo
umekuweka huru, na chuki na kinyongo.
Kumbuka unayafanya hayo kwa ajili yako mwenyewe ili maombi yako
yakubaliwe mbele za Mungu.
Nafahamu kwa jinsi ya mwili, na kwa kutumia akili ya kibinadamu hatua
hizo ni ngumu kuchukua.
Ni
kweli, lakini kumbuka si wewe unayeishi, bali Kristo ndani yako. Na
unayaweza yote (pamoja na kuwapenda adui zako) katika yeye akutiaye
nguvu (Wafilipi 4:13)
Upendo unavunja nguvu za uadui. Usimuone jirani au ndugu ni adui tena.
Kama vile wewe ulivyo kiumbe kipya ndani ya Kristo, kwa jicho la upya
huo waone adui zako kuwa ni rafiki. Anza uhusiano mpya nao.
" Lakini nawaambia ninyi mnaosikia wapendeni adui zenu, watendeeni
mema wale ambao wawachukia ninyi wabarikieni wale ambao wawalaani ninyi,
waombeeni wale ambao wawaonea ninyi" (Luka 6:27,28)
3. Samehe na Kusahau:
Wakati fulani nilikuwa mahali nikifanya semina ya neno la Mungu. Mtu
mmoja akanifuata na akaniambia anataka nimuombee.
Nikamuuliza; "Nikuombee nini?"
Akasema; "Mimi shida yangu ni kwamba naona imani yangu ni ndogo na
haikui, na maombi yangu hayajibiwi. Kwa hiyo naona nina shida katika
maisha yangu ya kiroho, uniombee".
Inawezekana hata wewe una shida ya namna hiyo, kwa hiyo tafakari kwa
makini maneno haya.
Niliahidi kumuombea baadaye kwa maana muda ulikuwa umekwisha.
Siku moja nilipokuwa ninaomba kwa Mungu juu ya shida yake, Bwana
akanijibu katika roho yangu kuwa:
"Mtu huyo ana matatizo ya ndoa na kuna jambo lililomuudhi. Yeye
anafikiri amesamehe, lakini bado ana uchungu moyoni mwake. Mwambie
asamehe na kusahau na shida yake itakwisha".
Nilipowasiliana naye juu ya jambo hili, alikubali kuwa, ni kweli mwenzie
amekuwa akimkosea mara kwa mara katika ndoa yao. Lakini alisema
amekwisha msamehe.
Nikamuuliza; "Je! mbona basi kila mkikosana unakumbusha makosa ya
nyuma?"
Akajibu; "Ni kweli, sasa nifanyeje wakati naona kila wakati makosa
aliyonifanyia nyuma yakinijia kichwani?"
Hili
ni tatizo la wengi. Na hujikuta wanasema wamesamehe kumbe bado. Msamaha
si jambo la akili ni hatua ya rohoni. Ni uamuzi unaotoka ndani ya moyo
wako.
"Kisha Petro akamwendea akamwambia, Bwana, ndugu yangu anikose
mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara saba? Yesu akamwambia, sikuambiii
hata mara saba, bali hata saba mara sabini" (Mathayo
18:21, 22)
"Na
kama akikukosea mara saba katika siku moja, na kurudi kwako mara
saba , akisema, nimetubu msamehe. Mitume wakamwambia Bwana
tuongezee imani" (Luka 17:4,5).
Mistari hii inatuonyesha jinsi kukua kwa imani, kunavyohusiana sana na
kusamehe.
Wanafunzi walimwambia Bwana Yesu, awaongezee imani. Kwa kuwa walifahamu
kwamba, kwa uwezo wao wasingeweza kusamehe kama Kristo anavyotaka.
Ni
kweli kabisa.
Kama
vile unavyohitaji imani katika kuomba, vile vile katika kusamehe na
kusahau unahitaji imani.
Ulipompokea Kristo ulipokea kiasi cha imani (Warumi 12:3)
Na
ili iongezeke unahitaji kusoma neno la Mungu na kulitenda. Imani huja
kwa kusikia Neno la Mungu. (Warumi 10:17).
Imani
ni ya rohoni na kusamehe ni kwa rohoni.
Unawezaje kusamehe na usiyakumbuke uliyofanyiwa?
Hilo
ndilo tatizo kubwa alilokuwa nalo yule mtu aliyeniambia niomuombee. Na
wengi pia wana tatizo la namna hii, na limekwamisha uponyaji na majibu
mengine ya maombi yao, wameombewa mara nyingi, lakini bila mafanikio.
Kusamehe na kusahau ni kitendo cha imani ambacho ni budi kionekane kwa
njia ya matendo ya mtu.
Kusamehe ni uamuzi wa mara moja na kusahau ni vita vya imani.
Sasa, utaniuliza, Ndugu Mwakasege, utawezaje namna hiyo?
Kabla
sijakujibu, na mimi nakuuliza swali.
Siku
ulipotubu dhambi zako, ulikuwa na uhakika gani ya kuwa Mungu amekusamehe
wala hazikumbuki dhambi zako tena?
Utasema kwa kuwa ukitubu Mungu anasamehe.
Ni
sawa kabisa. Hata mimi nakubaliana na hilo.
Lakini, je! Unaona kuwa Mungu anaweza kukuambia ufanye kitu ambacho
anajua huwezi kukifanya?
Hapana hata kidogo. Bwana wetu si dhalimu!
Anafahamu kuwa WEWE MWENYEWE HUWEZI, LAKINI YEYE KWA KUWA YUMO NDANI
YAKO ATAKUWEZESHA KUSAMEHE NA KUSAHAU.
Unayaweza yote katika yeye akutiaye nguvu (Wafilipi 4:13)
Ukiisha amua kumsamehe mtu hakikisha kwamba hulisemi tena jambo hilo
katika kinywa chako.
Kumbuka kinywa kinanena yaujazayo moyo (Mathayo 12:34)
Na
hayo maneno ndiyo yamtiayo mtu unajisi (Mathayo 15:18 - 20)
Usitafakari wakati wo wote ule, kosa ulilofanyiwa; mawazo mabaya
yanapokujia juu ya kosa ulilofanyiwa, fahamu kuwa ni shetani na nafsi
yako tu.
Biblia inasema mpingeni shetani naye atawakimbia (Yakobo 4:7)
Na wala msimpe nafasi (Waefeso 4:27)
Mwambie shetani aondoke na mawazo yake, kwa kuwa hilo kosa umelisamehe
na kulisahau.
Na wakati huo utafakari nini?
"Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote
yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo
yote ya kupendeza, yo yote yenye sifa njema, ukiwapo wema wo wote,
ikiwapo sifa nzuri yo yote, YATAFAKARINI YAYO" (Wafilipi
4:8)
"Maana
ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili;
(maana silaha za vita vyetu si za mwili; bali zina uwezo katika
Mungu hata kuangusha ngome;) tukiangusha MAWAZO na kila kitu
kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na TUKITEKA NYARA
KILA FIKRA ipate kumtii Kristo" (2 Wakorintho 10:3 - 5)
Kusahau ni vita vikali vya imani vinavyopiganwa katika mawazo yako.
Unaposhinda vita hivi, unajikuta umepiga hatua kubwa ya imani!
KWA HIYO KUMBUKA:Unasamehe kwa ajili yako Mwenyewe.
Na unasahau makosa uliyokosewa kwa ajili yako mwenyewe.
Kumbuka hili kila wakati, unamsamehe aliyekukosea na kuyasahau
aliyokukosea kwa ajili yako mwenyewe.
Na
kila wakati wazo likija kukukumbusha kosa hilo likatae kwa Jina la Yesu.
Na USIKUBALI KULISEMA TENA MAISHANI MWAKO.
4. Hasira ipeleke kwenye maombi
"Mwe na hasira, ila msitende dhambi jua
lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka; wala msimpe Ibilisi
nafasi" (Waefeso 4:26, 27)
Mwe
na hasira, ila msitende dhambi, ni mstari ambao watu wengi wameutumia
vibaya. Kutokana na maneno hayo wamefanya vitendo vingi viovu kwa mawazo,
maneno na kwa matendo.
Biblia haiwezi kujipinga yenyewe. Roho Mtakatifu ndiye aliyewaongoza
watu kuandika maandiko hayo Matakatifu.
Lakini, soma mistari ifuatayo:
"Uchungu wote na ghadhabu na HASIRA na kelele na matukano YAONDOKE
KWENU" (Waefeso 4:31)
"..... HASIRA ya mwanadamu haitendi haki ya Mungu" (Yakobo
1:20)
"Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya HASIRA watu watendao
mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu" (Wagalatia
5:19 -21)
Hapa
unaona jinsi hasira ilivyofananishwa na uchawi, uasherati, uadui, ibada
ya sanamu, na mambo mengine kama hayo ambayo yanamzuia mtu asiurithi
ufalme wa Mungu.
Na Yesu Kristo akikaza ubaya wa hasira alisema:
"Mmesikia
watu wa kale walivyoambiwa, Usiue; na mtu akiua, itampasa hukumu. Bali
mimi nawaambieni, kila amwoneaye ndugu yake HASIRA itampasa HUKUMU"
(Mathayo 5:21, 22)
Yesu
anasema ukiwa na hasira unastahili hukumu, lakini Roho aliyesema ndani
ya Kristo, ni huyo huyo aliyesema ndani ya Paulo kuwa, "Mwe na
hasira, ila msitende dhambi".
Je!
Unafikiri biblia inagongana yenyewe? Hapana! Paulo alikuwa ana maana
gani aliposema tuwe na hasira lakini tusitende dhambi? Unawezaje mtu
ukawa na hasira lakini usitende dhambi?
Kuna
uhusiano mkubwa sana kati ya magonjwa na hasira.
Ngoja nikueleze jinsi mimi yalivyonitokea.
Mara tu mimi nilipompokea Kristo katika roho yangu, kulikuwa na kitu
kimoja kilichokuwa kikinisumbua. Ilikuwa mtu akiniudhi nilikuwa
nakasirika haraka sana. Na wakati wote nitakuwa nalifikiria jambo hilo
moyoni mwangu.
Mwisho wake nilikuwa naona uchungu unaingia moyoni mwangu.
Sasa kila mara nilipokasirika nilikuwa nashindwa kuomba na mara ninaanza
kuumwa homa.
Jambo
hili lilinisumbua muda mrefu. Kila nikitubu na kumsamehe aliyenikosea,
na kuliacha hilo mikononi mwa Mungu; ugonjwa niliokuwa nao ulikuwa
unapona.
Nilifahamu kitu kimoja kuwa nikiweza kulitatua tatizo la hasira, ugonjwa
huo hautaniruida tena. Kwa kuwa ulikuwa unakuja mara tu nikikasirika.
Nikawa na tatizo la hasira mikononi mwangu.
Kwa
hiyo, nikamlilia Mungu katika maombi juu ya shida hii.
Watu wengi wanatatizo la namna hii, kila wanapokasirika juu ya jambo
fulani, wanaugua. Utakuta wengi wakikasirika wanaumwa vichwa, vidonda
vya tumbo, kifua, moyo, damu kwenda mbio, homa, na magonjwa mengine.
Tatizo si ugonjwa hapo.Tatizo ni hasira!
Nilipokuwa nikiomba, Roho wa Bwana alinipa jibu na naamini kuwa kama
nilivyosaidiwa mimi na wewe utapata msaada. Na ndiyo maana
nimekushirikisha hili.
Unapoona kuwa kuna jambo limekuudhi, usiwe mwepesi kujibu au kufanya
kitu. Tulia kimya na tafuta nafasi uanze kuomba.
Kwanza tubu kwa Baba juu ya kukasirika kwako, na pili, mwambie Baba
jinsi unavyojisikia moyoni mwako, bila kumficha kitu, na tatu, mwombe
kitu ambacho unataka akufanyie katika jambo hilo.
Utajikuta unapoomba na kuumimina moyo wako kwa Bwana, Yeye ataichukua
hiyo hasira uliyokuwa nayo na uchungu wote. Na badala yake anahuisha
upya upendo mpya ndani ya moyo wako utakaokuwezesha kupita juu ya tatizo
ulilo nalo.
Ukiona bado hasira inatokea, ikemee kwa jina la Yesu, na itatoweka.
Paulo aliposema, Mwe na hasira, ila msitende dhambi hakuhalalisha ya
kuwa hasira ni nzuri.
Kwa
maneno mengine alikuwa akisema kuwa unapopata uchungu kwa kuudhiwa
angalia usifanye vitendo vitakavyomuaibisha Kristo.
Kwa
kuwa kuudhiwa kupo maadamu upo duniani, na kwa mtu wa Mungu maudhi
yanazidi. Lakini Paulo anasema watu wajue namna ya kuishughulikia hasira
inapokuja kutokana na maudhi.
Ndiyo maana aliendelea kusema:
"Jua lisichwe na uchungu wenu bado
haujawatoka, wala msimpe ibilisi nafasi" (Waefeso 4:26,28)
Usimpe ibilisi nafasi kwa kuiacha hasira ikazaa ugomvi, matusi na fitina.
Uchungu huo utautoaje?
Usiupeleke kwa aliyekuudhi, wala usikae nao. Upeleke kwenye maombi na
upendo utavuma baada ya Mungu kuondoa uchungu uliokuwa nao.
Kuna
wengine wanasema hasira aliyonayo ni ya ukoo kwa kuwa ndugu zake
waliomtangulia wana hasira.
Kuna
wengine huwa wakikasirika kuna kitu kinapanda na kikifika shingoni
kinamfunga asiseme, na anaanza kupumua kwa nguvu na wakati mwingine
huanza kulia.
Ukiona namna hiyo, chukua silaha mkononi ya Jina la Yesu na ukemee.
Maana hiyo ni roho ya shetani iliyojifunika katika hasira.
Hakuna hasira ya ukoo kwa watu wa Mungu, ambao ni uzao mpya katika uzao
wa Mungu. Ukoo wako ni ukoo wa Mungu. Ni ukoo wa Upendo si wahasira.
Baada
ya mimi kuchukua hatua hizo, ule ugonjwa sijauona tena, na hasira
sikuiona kunifuatafuata kwa kuwa niliacha kuwatizama watu kwa jinsi ya
mwili, bali nilianza kuwatambua kwa jinsi ya rohoni (2Wakorintho 5:16)
5. Furahi siku zote.
Siri
ya ushindi katika matatizo yoyote, inatokana na furaha ya Kristo iliyo
ndani ya mtu.
Neno
la Mungu linasema, "Furahini katika Bwana
siku zote, tena nasema, Furahini" (Wafilipi 4:4)
" Heri ninyi watakpowashutumu na kuwaudhi na
kuwanenea kila neno baya kwa uongo kwa ajili yangu. Furahini, na
kushangilia;kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo
walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu" (Mathayo 4:11,
12)
Huu
ni ujumbe mzuri sana wa Bwana Yesu, kwa mtu wake aliyesongwa na maudhi
pamoja na makwazo mbali mbali.
Inawezekana kuwa ndani ya nyumba yako una makwazo ya kila siku, kutokana
na mume wako au mke wako ambaye hatembei katika nuru ya Kristo.
Na
pia, inawezekana unapata maudhi sana juu ya tabia za watoto wako, ambao
hawaenendi katika kweli ya neno la Mungu. Inawezekana unapata maudhi
shuleni au kazini.
Hata
kama umesongwa na makwazo na maudhi namna hiyo, Yesu Kristo , aliye
bwana na Mwokozi wako, anakuambia. "FURAHI NA KUSHANGILIA".
Furahi na kushangilia katika Bwana siku zote na katika yote. Hii ndiyo
siri ya ushindi.
Kwa nini ufurahi na kushangilia?:
Kwa
kuwa unafahamu kuwa mgomvi wako si mtu bali ni shetani. (Waefeso 2:1 -
3).
Kwa
kuwa unafahamu kuwa anayekuudhi si mume wako, wala mke wako, wala watoto
wako, bali ni shetani anayewatumia kutaka kukukasirisha wewe, ili
umkosee Mungu wako.
Kwa
kuwa unafahamu kuwa shetani ameshindwa; na wewe una mamlaka juu yake na
maudhi yake yote (Luka 10:19)
Kwa hiyo ufanyeje?
Furahi na kushangilia moyoni mwako.
Kumbuka kuwa Kristo aliye ndani yako ni mkuu kuliko shetani na makwazo
yake na maudhi yake (1Yohana 4:4).
Furahi na kushangilia unapoudhiwa, na mtolee Mungu shukrani kwa nyimbo
za sifa.
Fanya
hivyo na hasira haitapata nafasi moyoni mwako, wala uchungu wo wote.
Tumia
tabia ya Kristo iliyo ndani yako ya kuwaombea wanaokuudhi, kama vile
yeye alivyosema pale msalabani, "Baba
uwasemehe kwa maana hawajui walitendalo".
Baada ya kufurahi na kushangilia na kusifu, kitu gani kinafuata?
"Upole wako ujulikane na watu wote" (Wafilipi
4:5)
Na upole ni tunda la Roho. Na kazi ya roho ya upole ni kutuliza maudhi. (Mhubiri
10:4)
Wakati wa maudhi ndiyo wakati mzuri wa kumdhihirisha Kristo aliye ndani
yako katika upole wote na utulivu.
Usijisumbue na kuhangaika katika neno lo lote, bali katika kila jambo,
kwa kusali na kuomba na kushukuru, haja yako na ijulikane na Mungu (Wafilipi
4:6).
Usiwe mwepesi kumwambia mtu maudhi ya nyumbani mwako, au ofisini mwako.
Utajikuta umeingia katika kusengenya na hutafaulu kamwe kujifunza
kusamehe.
Maudhi na makwazo yapeleke kwa Bwana. Yeye anatosha kukushindia.
Fanya
hivyo, na amani ipitayo akili na fahamu zote na maudhi na makwazo
itakuhifadhi na kukufariji moyo wako siku zote katika Bwana (Wafilipi
4:7)
Nilikuwa mahali fulani nikifundisha neno la Mungu, na kila siku
niliombea wagonjwa. Basi, siku moja mama mmoja alisimama kushuhudia
alivyopona.
Na haya ndiyo aliyosema:
"Nina uhakika kuwa ugonjwa huu niliokuwa nao ulikuja kwa sababu ya
dhambi nilizokuwa nazo. Mimi sikushikwa na dhambi zingine kama wengine
wanavyoshikwa. Mimi nilishikwa na dhambi hii.
Mume
wangu huwa hanipi fedha ya kununulia chumvi nyumbani. Basi nilichukia
sana; na mimi nikipata fedha na kununua chumvi, naificha nje ya nyumba.
Mimi na watoto tunakula chakula chenye chumvi. Mume wangu namtengea
chakula kisichokuwa na chumvi.
Na
niliwambia watoto ye yote atakayesema hayo kwa baba yake
atachapwa.Lakini nilipoanza kufanya hivyo nilianza kuugua mara kwa mara,
na hapa kwenye mkutano huu nimekuja na mguu umevimba na kunisababisha
nisitembee vizuri.
Baada
ya kusikia neno la Mungu nilifahamu kuwa ugonjwa huu nimeupata kwa
sababu ya kosa hilo la kumkasirikia mume wangu.
Nikamsamehe mume wangu. Nikatubu kwa Mungu. Na maombezi ya wagonjwa
yalipofanywa nilijikuta nimeanguka chini. Nilipoamka nilikuta uvimbe
mguuni umetoweka. Na sasa nimepona na natembea vizuri.
Nikirudi nyumbani nitamwambia mume wangu yote, na nitamwomba anisamehe".
Hii
ndiyo nguvu ya uponyaji ya neno la Mungu inayoshuka baada ya kusamehe.
Roho zinapona, miili inapona na ndoa zinapona! Yule mama alisamehe
kwanza ndipo akapokea uponyaji.
Na
wewe sasa, samehe na kusahau upokee uponyaji wako au upokee majibu ya
maombi yako.
Kumbuka kabla ya kusimama na kusali samehe kwanza. Hii ni kwa ajili yako
mwenyewe, ili usamehewe na Mungu na upokee unaloomba siku zote
Usikose kusoma wiki ya
Tano ya mfululizo huu tutakapojifunza juu ya:
Je aliyekukosea asipokuomba msamaha ufanyaje?
Jifunze
kusamehe na kusahau / Utang /
1 / 2 / 3 /
4 / 5 / 6 /