Sura ya Pili
MAMBO
MANNE UNAYOPASWA KUYAJUA
Kuna mafundisho ambayo si sahihi yaliyowafanya wakristo wengi hasa wale
waliookoka kutokujua cha kuamini juu ya uhusiano wa ukristo wao na
utajiri. Na tuangalie maeneo manne yafuatayo ambayo wakati mwingine
yamezaa mafundisho yasiyo sahihi:
- TAJIRI
NA UFALME WA MUNGU:
Nadhani utakuwa umewahi kusikia watu wakisema; “Matajiri hawataurithi
ufalme wa Mungu” Na wanasema ndivyo Bwana Yesu alivyosema baada ya
tajiri aliyetaka uzima wa milele kukataa kuuza mali yake.
Hata mimi mwanzoni ilikuwa
karibu sana nikubaliane na usemi huu. Lakini baada ya kuyachunguza
maandiko niliona ya kuwa Yesu Kristo hakusema hivyo bali anasingiziwa tu.
Yesu Kristo alisema hivi;“Kwa
shida gani wenye mali WATAUINGIA
ufalme wa Mungu”
(Luka 18:24)
Kwa
mstari huu tunajua ya kuwa Yesu Kristo hakusema ya kuwa wenye mali
hawatauingia ufalme wa Mungu; bali alisema “kwa
shida gani wenye mali watauingia ufalme wa Mungu!”
Na
akaendelea kusema, “ Kwa maana ni vyepesi
ngamia kupita katika tundu la sindano kuliko tajiri kuingia katika
ufalme wa Mungu.” (Luka 18:25). Na wale waliosikia
wakashtuka na kushangaa, kwa maana waliona itakuwa vigumu sana kwa
tajiri kuokoka, na naona walifikia mawazo kama waliyonayo wengi siku
hizi ya kuwa tajiri hawezi kuingia katika ufalme wa Mungu. Ndiyo maana
wakauliza “Ni nani basi awezaye kuokoka?” (Luka 18:26).
Yesu
Kristo akawajibu akasema;“Yasiyowezekana
kwa wanadamu yawezekana
kwa Mungu” (Luka
18:26).
Kwa
maneno mengine alikuwa anasema tajiri anaweza KUWEZESHWA NA MUNGU
kuingia katika ufalme wa Mungu akiiamini injili inayookoa. Hata hivyo
maskini naye anaokolewa kwa neema ya Mungu.
Na
kwa kuamini kuwa tajiri hawezi kuurithi ufalme wa Mungu, wakristo wengi
kwa kudhamiria kabisa wameamua kuwa maskini ili wasije wakaukosa ufalme
wa Mungu. Lakini hii si sawa na ni kukwepa wajibu wetu tulionao kama
mawakili wa mali zote za Mungu.
Na ni
vizuri ufahamu ya kuwa umaskini wa kukosa chakula, mavazi na nyumba ya
kukaa siyo tiketi ya kuingia katika ufalme wa Mungu. Na wala umaskini
siyo utakatifu – ingawa kuna maskini walio watakatifu! Na pia utajiri
siyo utakatifu ingawa kuna matajiri walio watakatifu.
Kuna
Mkristo mmoja wa dhehebu fulani alikuwa akinieleza hali iliyowasonga
katika dhehebu lao; alisema;
“Katika
kanisa letu Mchungaji akionekana amevaa vizuri,
wakristo wake wanasema amepoa kiroho. Kwao mtu wa kiroho ni
mtu aliye maskini, asiyevaa nguo nzuri wala viatu vizuri.”
Niliposikia
maneno hayo nilisikitika sana, na nikakumbuka maneno ya Mungu aliyosema
kwa kutumia kinywa cha nabii Hosea, yasemayo, “Watu
wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa ….” (Hosea 4:6) na
pia Yesu Kristo aliwahi
kusema ya kuwa watu wanapotea kwa kuwa hawajui maandiko wala uwezo wa
Mungu.
Kwa
hiyo fungua moyo wako uisikie kweli ambayo ndiyo neno la Mungu. Na
utaifahamu kweli na hiyo kweli itakuweka huru (Yohana 8:32)
- MUNGU
NA MALI
Kuna uhusiano gani kati ya Mungu na Mali? Kuna uhusiano gani kati ya
Mkristo na Mali? Kuna uhusiano gani kati ya wokovu na mali?
Je, ni dhambi kwa mkristo kuwa
na mali nyingi? Hebu na tuangalie maneno ya Yesu Kristo juu ya Mungu na
Mali.
“Hakuna
mtu awezaye kutumikia mabwana wawili, Kwa
maana atamchukia huyu, na
kumpenda huyu; ama
atashikamana na huyu, na kumdharau huyu. Hamwezi
kumtumikia
Mungu na Mali” (Mathayo
6:24)
Neno
la kiingereza lililotafsiriwa na kuandikwa ‘mali’ ni ‘mammon’
Na neno hili ‘mommon’ ni jina la roho ya ibilisi inayotawala mali.
Kwa maneno mengine naweza kusema kuwa ‘mammon’ ni jina la pepo.
Kwa
hiyo, neno ‘mali’ lilivyotumika hapa linamaanisha ‘pepo linaloitwa
Mali’ Ndiyo maana Yesu Kristo alisema; “Hakuna
mtu awezaye kutumikia MABWANA wawili ….” Yesu Kristo
asingeliita mali kuwa ni mojawapo ya MABWANA kama hakuwa anasema juu ya
roho inayoitwa mali. Roho hii ya shetani iitwayo Mali imewafanya watu
wengi, hata wakristo waache kumtumikia Mungu aliye hai, na badala yake
waitumikie roho inayowasukuma na kuwatamanisha juu ya mali, ili waitumie
kwa uchoyo na ubinafsi.
Wakristo wengine wanadhani wanaweza kumtumikia Mungu na vile vile
wamtumikie Mali. Yesu Kristo alisema; “HAKUNA
mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana ATAMCHUKIA HUYU, NA
KUMPENDA HUYU: AMA ATASHIKAMANA NA HUYU, NA KUMDHARAU HUYU. Hamwezi
kumtumikia Mungu na Mali.”
Kwa
kusema hivi hakuwa anamaanisha kuwa na vitu vinavyoitwa mali ni vibaya.
Kitu anachosema ni kibaya ni KUITUMIKIA MALI! Biblia inasema katika
Zaburi 24:1 kuwa, “Nchi
na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana; Dunia na wate wakaao ndani yake.”
Mtu
hakuumbwa ili kuitumikia mali. Mtu aliumbwa kwa ajili ya utukufu wa
Mungu na amtumikie Yeye peke yake. Mali ya dunia iliwekwa kwa ajili ya
kumtumikia mtu, na siyo mtu kuitumikia mali! Mtu aliwekwa juu ya mali
yote na aliagizwa kuitawala (Mwanzo 1:28 – 30).
Kuwa
na mali siyo vibaya, wala siyo dhambi. Mali inakuwa kikwazo katika
maisha ya ukristo inapoanza kumfanya mtu amsahau Mungu na mapenzi yake.
Ndiyo maana Yesu Kristo alisema; “Kwa shida
gani wenye mali watauingia ufalme wa Mungu” (Luka 18:24)
siyo kwamba hawezi kuuingia ufalme wa Mungu, bali kwa shida wenye mali
watauingia ufalme wa Mungu. Kwa maneno mengine ni kwamba wakimtanguliza
na kumtumikia Mungu, mali haitakuwa kwazo katika maisha yao ya ukristo.
Sasa
tuishije katika ushauri wa namna hii?
“Kwa sababu hiyo nawaambieni,
msisumbukie maisha yenu,
mle nini au mnywe nini; wala miili yenu, mvae nini. Maisha je! Si zaidi
ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi? Waangalieni ndege wa angani, ya
kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani; na Baba yenu
wa mbinguni huwalisha hao. Ninyi je! Si bora kupita hao? NI YUPI KWENU
AMBAYE AKIJISUMBUA AWEZA KUJIONGEZA KIMO CHAKE HATA MKONO MMOJA? Na
mavazi, ya nini kuyasumbukia? Fikirini
maua ya mashamba, jinsi yameavyo; hayafanyi kazi, wala hayasokoti;
nami nawaambia ya kwamba hata Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa
vizuri kama mojawapo la hayo. Basi, ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya
kondeni, yaliyopo leo, na kesho hutupwa kalibuni, JE! HATAZIDI SANA
KUWAVIKA NINYI, ENYI WA IMANI HABA? Msisumbuke basi, mkisema, Tule nini?
au Tunywe nini? au Tuvae nini? Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta;
kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote”
(Mathayo 6:25 – 32)
Kuna
wakristo wengine wameyaelewa vibaya maneno haya ya Bwana Yesu Kristo
hata kufikia kutokufanya kazi kwa kisingizio cha kwamba Yesu Kristo
alisema tusiyasumbukie maisha. Kwao kufanya kazi ina maana kusumbukia
maisha. Lakini napenda kukuambia ya kuwa Yesu Kristo hakuwa ana maana ya
kutuambia tusifanye kazi aliposema tusiyasumbukie maisha.
Nadhani
unaamini ya kuwa ni Roho wa Kristo aliyemwongoza Mtume Paulo kuwaandikia
Wathesalonike juu ya mashauri mbali mbali ya kikristo. Katika
1Wathesalonike 3:10b anasema, “Ikiwa mtu
hataki kufanya kazi, basi, asile chakula.” Ni muhimu
kufanya kazi. Kufanya kazi siyo kusumbuka na maisha. Kusumbuka na maisha
siyo kufanya kazi.
Jambo
ambalo Bwana Yesu Kristo alitaka tufahamu wakati alipokuwa akisema
tusisumbukie maisha, ni kwamba katika kila jambo tumshirikishe Mungu na
kumtanguliza Yeye. Wakristo wengine wanadhani wanaweza kula, kunywa na
kuvaa bila msaada wa Mungu. Yesu Kristo alisema katika Yohana 15:5b kuwa;
“…… maana pasipo mimi ninyi hamwezi
kufanya NENO LO LOTE” (Hili ni pamoja na kula, kunywa na
kuvaa) Ndiyo maana katika Wafilipi 4:13 imeandikwa kuwa “Nayaweza
mambo yote katika YEYE anitiaye nguvu” Yesu Kristo ndiye
atutuaye nguvu.
Yesu
Kristo alitoa mwongozo mzuri sana wa jinsi ya kuishi hapa ulimwenguni
aliposema;
“Bali
utafuteni KWANZA ufalme wake, na haki yake; na hayo
yote mtazidishiwa”
(Mathayo 6:33)
Ukiyaangalia
maisha ya watu wengi waliookoka utadhani Yesu Kristo alisema, “Bali
utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote MTAONDOLEWA.”
Inahuzunisha kuona ya kuwa watu wengi wakiokoka maisha yao yanageuka
kuwa duni, wanashindwa kula vizuri, wala kuvaa vizuri.
Ngoja nirudie kusema kuwa SI MAPENZI YA MUNGU TUWE MASKINI. SI MAPENZI
YA MUNGU TUKOSE CHAKULA WALA MAVAZI. Ni Mungu yupi ambaye atawapenda
ndege akawavika na kuwalisha, na akawaacha watoto wake aliowaumba kwa
mfano wake wakose chakula na mavazi?
Mungu wetu tunayemwabudu na kumtumikia katika Kristo Yesu, anapenda
tuishi maisha mazuri, tule, tunywe na kuvaa vizuri. Tunachotakiwa
kufanya ni kuutafuta KWANZA ufalme wake, na haki yake, na hayo yote (chakula
na mavazi) TUTAZIDISHIWA na siyo TUTAONDOLEWA.
Ukiona mtu anasema ameokoka na halafu anajikuta anakosa chakula na
mavazi huku anafanya kazi, basi ujue anafanya kazi na kukusanya vitu
hivyo pasipo Bwana; kwa kuwa asiyekusanya pamoja na Bwana hutapanya.
- FEDHA
NA KUPENDA FEDHA
Nimewahi kumsikia mhubiri mmoja akisema; “Fedha
ni shina la maovu, kwa hiyo wakristo wajihadhari nazo.” Na
wakristo wengi wamekuwa wakisikika wakisema hivyo, kwa hiyo wanaogopa
kuwa na fedha za kutosha.
Lakini
ninaposikia watu wakisema hivi, huwa najiuliza wanaupata wapi usemi huu?
Biblia haisemi; “Fedha ni shina la maovu.”
Badala
yake Biblia inasema hivi;“
Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha;ambayo wengine
hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu
mengi”(1Timotheo 6:10)
Kupenda
fedha ni kuwa na tamaa ya fedha; ni kuzitamani fedha. Na kupenda fedha
huku ndiko shina moja la mabaya ya kila namna.
Kuwa
na fedha nyingi au kidogo siyo dhambi, kwa kuwa fedha ni mali ya Mungu (Hagai
2:8) Lakini kupenda fedha nyingi au kidogo ni shina moja la maovu.
Tamaa
ya fedha ndiyo inayoleta wizi, ujambazi, mauaji, dhuluma, kutokutosheka,
uchoyo, wivu, uasherati; nakadhalika. Lakini unaweza kuwa na fedha bila
ya kufungwa na roho ya kupenda fedha.
Je!
Unafahamu ni kwa nini shetani hapendi wakristo safi wawe na fedha? Maana
ni kazi ya shetani kuwapiga vita wakristo wanaotaka kujipatia fedha kwa
njia ya halali. Akishindwa kuwazuia kupata fedha; atahakikisha zile
fedha walizonazo wanazimaliza haraka hata kwa matumizi ambayo
hawakupanga.
Je!
Unafahamu ni kwa nini?
Kwa
sababu anafahamu mkristo safi akiwa na fedha za kutosha, atazitumia hizo
kumpiga nazo vita kwa kuihubiri injili! Na shetani anafahamu kuwa Yesu
alisema mwisho hautakuja mpaka injili ihubiriwe katika mataifa yote. Kwa
hiyo anajua akiweza kuwakosesha wakristo fedha za kutosha ili injili
ihubiriwe, yeye anapata muda wa kupumua na kupumzika.
Wengi
wameshindwa kujenga makanisa kwa sababu ya ukosefu wa fedha. Watumishi
wa kanisa wanalipwa mishahara kidogo, kwa sababu ya ukosefu wa fedha.
Mikutano ya injili na semina za neno la Mungu hazifanyiki mara kwa mara
kwa kukosa fedha. Wainjilisti wanatafuta fedha za kununulia vipaza sauti
wanakosa. Na matokeo yake ni kazi ya Mungu kupoa.
Je!
Unadhani ni nani ambaye anaweza kutoa fedha yake ili ikahubiri injili
kama siyo wakristo wenyewe? Na wakristo watatoaje fedha kama hawana
fedha? Na watakuwaje na fedha, kama wanadhani kuwa na fedha nyingi ni
dhambi?
Na
shetani ameutumia mwanya huu kuzitumia fedha ambazo wanazo watu
wasiopenda haki kueneza dhambi na uovu. Je, ni haki kwa nchi nyingine
kutumia ma-billioni ya fedha kutengeza silaha ambazo baadaye
wanaziharibu tena, huku mamillioni ya watu wanakufa kwa njaa na maafa
mengine?
Kwa hiyo usikubali unaposikia mtu akisema kuwa na fedha ni vibaya;
lakini uwe mtu wa kutokupenda fedha. Kwa kuwa ukizitamani fedha
utajikuta unaanza kuzitafuta hata kwa njia ambazo ni kinyume cha maadili
yetu ya Kikristo; na pia kinyume cha utu wa mwanadamu.
- MASKINI
NA TAJIRI
Nafahamu ya kuwa si mpango wa Mungu kwa mtu aliye tajiri kumtawala
maskini kwa sababu ya umaskini wake. Na pia nafahamu si mpango wa Mungu
kwa nchi zilizo tajiri kuzitawala nchi maskini kwa sababu ya umaskini
wake.
Lakini ni vizuri tufahamu uhusiano uliopo kati ya matabaka haya mawili:-
Biblia inasema;“Tajiri
humtawala maskini, Naye akopaye ni mtumwa
wake
akopeshaye.” (Mithali 22:7)
Maneno
haya ni kweli kabisa, na mtu ye yote ambaye ni msomaji wa historia na
magazeti, anafahamu majadiliano ya muda mrefu yaliyopo kati ya nchi
tajiri na nchi maskini duniani.
Ukoloni
mbaya uliopo sasa hivi kati ya nchi na nchi, ni ukoloni wa kiuchumi.
Katika ukoloni huu wa kiuchumi nchi tajiri zinatumia utajiri wake katika
kuzikandamiza nchi maskini. Na kwa njia hii mamillioni ya watu wamo
katika hali mbaya sana kimaisha.
Na
njia kuu ambayo nchi hizi tajiri zinatumia kuzitawala nchi maskini ni
kwa njia ya kuzipa mikopo. Na nchi maskini zote zimejikuta zimeingia
katika utummwa mbaya kwa sababu ya mikopo ambayo haijajulikana kama
inaweza kulipwa yote.
Inakisiwa
ya kuwa jumla ya madeni yote ya nchi zinazoendelea ni mabilioni ya dola
za Kimarekani na yanazidi kuongezeka.
Ni
kweli kabisa kwamba utajiri huu wa nchi hizo si wote uliopatikana kwa
njia ya halali. Na wafuatiliaji wa mambo ya uchumi duniani, wanafahamu
jinsi nchi hizi zilizoendelea zinavyobuni mbinu mbalimbali kuzinyonya
nchi zinazoendelea.
Ingawa
si mapenzi ya Mungu tuwe maskini, lakini pia si mapenzi ya Mungu tuwe
matajiri ili kuwatawala wengine kwa sababu ya umaskini wao. Ole ni kwa
matajiri wanaoutumia utajiri wao kuonea na kuwafanya wenzao kuwa watumwa.
Mungu
anapotupa nguvu za kupata utajiri ndani ya Kristo ni kwa kusudi muhimu
la kuimarisha agano lake la kumhudumia mtu mzima – kiroho na kimwili.
Ni
kweli maskini ana shida, maana hata biblia inasema maneno yake
hayasikilizwi (Mhubiri 9:16). Na hii imejionyesha wazi sana katika maoni
na malalamiko ya nchi maskini ambayo yanapuuzwa na kutosikilizwa na nchi
tajiri.
Lakini
hali hii si kwa nchi tu, bali hata katikati yetu humu humu makanisani.
Sehemu nyingi kuna wakristo ambao ni matajiri, na mara kwa mara huwa
wanatumia utajiri wao katika kuwatawala viongozi wa kanisa; na hata
wakati mwingine kudiriki hata kutaka kubadilisha maamuzi ya vikao vya
kanisa.
Na
kwa upande mwingine viongozi wa sharika wanajikuta wameingiwa na hofu na
kushindwa kuwakemea matajiri hao wakati wanapokwenda kinyume na maadili
ya kikristo. Kama siyo ukoloni wa namna yake ulioingia katika kanisa ni
nini basi?
Naamini
ya kuwa wachungaji na viongozi, wengi wao wangekuwa na hali nzuri
kiuchumi, baadhi ya matajiri wanaotaka kutawala viongozi wengine
wangeshindwa katika mbinu zao. Au wewe unasemaje?
Shetani
amekuwa akijitahidi sana kuwakandamiza wakristo wasiwe matajiri kwa
kutumia njia mbali mbali kwa kutegemea mazingira yalivyo. Mahali pengine
ametumia mifumo na vyombo vya fedha kama mabenki; pengine ametumia
serikali, pengine ametumia mafundisho mabaya kwa wakristo, nakadhalika.
Na
shabaha yake ya kufanya hivyo ni:-
(a)
Maneno ya wakristo
yasisikilizwe wanapohubiri, kwa kuwa imeaandikwa; “….Walakini
hekima ya maskini hudharauliwa wala maneno yake hayasikilizwi” (Mhubiri
9:19b). Kwa lugha nyingine maana yake “hayatiliwi maanani.”
(b)
Wakristo waendelee
kuwa watumwa ingawa wanadai ya kuwa wamewekwa huru. Kumbuka imeandikwa
hivi; “Tajiri
humtawala maskini. Naye akopaye ni mtumwa wake akopeshaye” (Mithali
22;7)
Na maneno haya ni kweli kabisa. Hebu nieleze ni nani atakayesikiliza na
kuyaamini maneno ya mchungaji au mwinjilisti au mtumishi yoyote wa Mungu
anayesema mtegemee Yesu katika kila kitu wakati yeye mwenyewe ana nguo
yenye viraka! Jambo la kwanza ambalo msikilizaji atajiuliza ni kwamba
kama huyu Yesu ameshindwa kumpa mtumishi wake nguo nzuri, atawezaje
kunisaidia mimi mkristo wa kawaida?
Kwa
hiyo lazima tuwe waangalifu ili tunayosema yawe sawa na tunavyoishi. Na
tuishi sawa sawa na ahadi za Mungu tunazozisimamia.
Siku
moja nilimsikia mchungaji mmoja mwanafunzi wa chuo kimoja cha biblia
akisema hivi; “Kuna mtu mmoja alikuja kutufundisha kuwa sisi kama
wachungaji tusisikitike tunapoona hatuna nguo nzuri, wala chakula kizuri,
wala sabuni nzuri za kuogea kwa sababu IKO SIKU MOJA VITU HIVI
TUTAVITAWALA NA BWANA MBINGUNI”.
Mara moja nikamkatisha na nikasema; “
Hayo mafundisho si sawa. Unadhani Mungu aliweka hivi vitu duniani (chakula,
mavazi, sabuni) kwa ajili ya shetani na watu wake? Unadhani mbinguni
tukifika tutahitaji tena chakula, mavazi na sabuni? Hivi vitu Mungu
aliviweka kwa ajili yetu tuvitumie wakati huu.”