Sura ya Nane
SADAKA
NA WOKOVU
“Palikuwa na mtu Kaisaria jina
lake Kornelio, akida wa kikosi kilichoitwa Kiitalia, mtu mtauwa,
mchaji wa Mungu, yeye na nyumba yake yote, naye alikuwa akiwapa watu
SADAKA NYINGI, na kumwomba Mungu daima. Akaona katika maono waziwazi,
kama saa tisa ya mchana, malaika wa Mungu, akimjia na kumwambia,
Kornelio! Akamtazama sana, akaogopa akasema, kuna nini, Bwana?
Akamwambia, Sala zako na SADAKA ZAKO zimefika juu na kuwa ukumbusho
mbele za Mungu. Sasa basi, peleka watu Yafa, ukamwite Simoni, aitwaye
Petro. Yeye ni mgeni wa mtu mmoja, jina lake Simoni, mtengenezaji wa
ngozi, ambaye nyumba yake iko pwani; ATAKUAMBIA YAKUPASAYO KUTENDA” (Matendo
ya Mitume 10:1 – 6).
Tabia hii ya Kornelio ya kuwa mtu mtauwa, mchaji wa Mungu, yeye na
nyumba yake yote, na pia tabia ya utoaji wa sadaka na kumwomba Mungu
daima, inaonyesha wazi kuwa Kornelio alimpenda Mungu sana na alikuwa
anatafuta namna yakukubalika mbele zake na namna ya kumpendeza Yeye.
Tungezungumza kwa lugha nyepesi zaidi, ni kwamba alitaka kwa MATENDO
YAKE aende mbinguni na kuurithi Uzima wa Milele baada ya kufa kwake .
Kwa kifupi alimtafuta Mungu kwa njia ya Matendo.
Hii ina maana ya kuwa Kornelio alitaka kuvuna
baraka za Agano Jipya katika damu Yesu, wa kutumia njia za
kupendeza Mungu zilizomo katika Agano la Kale.
Tena ingawa yeye hakuwa Myahudi kwa kuzaliwa, alitaka sana kuvuna
baraka ambazo Mungu aliahidi juu ya Wayahudi.
Mpaka hivi leo kuna watu wengi wanataka kuvuna baraka toka kwa Mungu
bila kutumia utaratibu aliouweka Mungu wa kuzipokea. Ni vigumu sana
kupokea ahadi za Mungu nje ya mpango wake.
Huwezi kupokea ahadi za agano la kale kwa kutumia mbini za agano la
kale na huku sasa hivi tumo katika kipindi cha agano jipya.
Baraka zote zilizomo katika agano la kale aliahidiwa Ibrahimu na uzao
wake MILELE. Soma mwenyewe Mwanzo sura ya 17 na 22. Kwa hiyo ukitaka
kupokea baraka za agano la kale lililofungwa kati ya Mungu na Ibrahimu,
inabidi uwe mzao au mtoto wa Ibrahim.
-
Kornelio hakufahamu hili; hata leo hii wengi hawafahamu.
Baraka zote zilizomo katika agano jipya zimeahidiwa wale walio ndani
ya Kristo – waliotoa maisha yao kwa Yesu kama vile Yesu Kristo
alivyotoa maisha yake kwa ajili yao.
Ni vigumu kupokea baraka za ahadi za agano la kale na zile za agano
jipya NJE YA YESU KRISTO. Imeandikwa hivi katika Wagalatia
3:13,14,29;
“Kristo
alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa
alifanywa
laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa,
baraka
ya Ibrahimu IWAFIKILIE MATAIFA KATIKA
YESU KRISTO, tupate kupokea ahadi ya Roho kwa
njia
ya imani…… Na kama ninyi ni wa Kristo, basi,
mmekuwa
uzao wa
Ibrahimu, na warithi sawasawa na ahadi.
"
Ndiyo maana Mungu alimtuma Malaika wake ili amwambie Kornelio kuwa
amwite Simon Petro ili awaeleze habari za Yesu Kristo – ili baraka
ya Ibrahimu iwafikie na wapate kupokea ahadi ya Roho kwa njia ya imani
– SIYO KWA MATENDO PEKE YAKE.
Jambo ambalo Mungu alitaka Kornelio ajue na sisi pia tujue ni kuwa
matendo mema, maombi na SADAKA bila “kupokea
ahadi ya Roho kwa njia ya imani” yaani kuzaliwa mara ya
pili kwa Roho au kuokoka – haitoshi kumpendeza Mungu, wala
kukubalika mbele zake au kuhesabiwa haki.
Ndiyo maana Yesu Kristo alimwambia Nikodemo, yule Farisayo kuwa “Mtu
asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu …..
Usistaajabu kwa kuwa nilikuambia, HAMNA BUDI kuzaliwa mara ya
pili”(Yohana 3:3,7).
Haya maneno “Hamna Budi” maana
yake ni “lazima” kwa hiyo Yesu
Kristo alikuwa anasema “…… LAZIMA
kuzaliwa mara ya pili”.
Yesu Kristo alikuwa anasisitiza kwa Nikodemo, na hata kwetu sote
tunaotaka kuurithi ufalme wa Mungu, kuwa hakuna njia nyingine
isipokuwa LAZIMA kuzaliwa mara ya pili kwa Roho (au kwa maneno mengine)
LAZIMA Kuokoka!
IMANI
NA MATENDO
Matendo peke yake hayatoshi kukupa ufalme wa Mungu. Kuna watu wengi
sana ambao ni waaminifu sana katika kusali na kumtolea Mungu sadaka,
lakini hawakubaliani na jambo kuokoka. Wanaona kuwa wao tayari
wameokoka kwa sababu tu wanasali, wanatoa sadaka na kujitahidi kuishi
katika matendo mema. Hebu soma maneno ya mistari hii uone
yanavyopingana na msimamo huu;
“Kwa
maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya
imani;
ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; WALA SI
KWA MATENDO,
mtu
awaye yote asije akajisifu” (Waefeso 2:8,9)
Tunaokoka kwa njia ya imani itendayo kazi katika Yesu Kristo, “Wala
si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu”. Matendo
yana faida zaidi kwa mtu baada ya kuokoka. Na pia imani bila matendo,
imani hiyo imekufa nafsini mwake. Biblia inasema hivi:
“Ndugu zangu, yafaa nini, mtu akisema ya kwamba anayo imani, lakini
hana matendo? Je! ile imani yaweza kumwokoa?…. Vivyo hivyo na imani,
isipokuwa ina matendo, imekufa nafsini mwake. Lakini mtu atasema, wewe
unayo imani, nami ninayo matendo. Nionyeshe imani yako pasipo matendo,
nami nitakuonyesha IMANI YANGU KWA NJIA YA MATENDO YANGU ……..
Maana kama vile mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo na imani pasipo
matendo imekufa” (Yakobo 2:14,17,18,26).
Jambo ambalo Yakobo alikuwa anasisitiza hapa ni kutaka kuwaonya watu
kuwa kusema wewe ni mkristo na huku matendo yako hayalingani na
ushuhuda wa mdomo wako ni bure. Wokovu uonekane katika maisha yetu
kila siku – la sivyo imani tuliyo nayo inakosa kuzaa matunda ya
uzima wa milele. Ndiyo maana Yesu Kristo aliwahi kuzungumza juu ya
kukatwa kwa tawi (Mkristo) lisilo zaa, soma Yohana 15:1-8 ili upate
picha zaidi juu ya jambo hili.
CHUKUA
HATUA LEO
Malaika
alimwambia Kornelio atume watu wakamwite Simoni aitwaye Petro ili
AMWAMBIE YAMPASAYO KUTENDA. Mungu kwa uweza wa Roho wake Mtakatifu
amekuletea maneno haya mkononi mwako ili UFAHAMU YAKUPASAYO KUTENDA.
Kama
hujaokoka na unadhani unaweza kuokoka kwa kutoa sadaka nyingi
NAKUSHAURI KWA JINA LA YESU KRISTO WA NAZARETI uombe sala hii kwa
sauti, ili utubu na kumpa Yesu Kristo maisha yako leo. HALAFU endelea
kutoa sadaka nyingi ukiwa ndani ya Yesu Kristo.
Omba
sala hii kwa sauti; “Mungu
Baba, unisamehe dhambi zangu zote nilizokukosea katika maisha yangu.
Ninatubu kwako. Nitakase kwa damu ya Yesu Kristo. Bwana Yesu Kristo
nimefungua moyo wangu nakukaribisha uingie ndani yangu, kwa uwezo wa
Roho wako. Uwe Bwana na Mwokozi wa maisha yangu – sasa na hata
milele. Asante kwa kunisamehe dhambi na kuniokoa. Amina”.
Ikiwa
umeisema sala hii kwa uaminifu, basi umefanyika kiumbe kipya –
umezaliwa mara ya pili na Mungu hakumbuki dhambi zako tena. Soma
2Wakorintho 5:17, Waebrania 8:12. Karibu sana katika ufalme wa Mungu
kwa jina la Yesu Kristo!
Hili
ndilo lililotokea kwa Kornelio na jamaa yake, Simoni Petro alipofika
kwao aliwaambia habari za Yesu Kristo – walisikia maneno hayo
wakamwamini Yesu na kujazwa na nguvu za Roho Mtakatifu wakati huo huo.