Utangulizi
SI MAPENZI YA MUNGU TUWE
MASIKINI!
(Namna
ya mkristo kuishi katika hali ngumu ya uchumi bila kumkosea Mungu)
Kati
ya mambo yaliyotabiriwa kutokea katika siku hizi za mwisho ni dhiki
katika mataifa, pamoja na hali ngumu ya uchumi. Soma mwenyewe katika
Luka 21:25-26 na Ufunuo wa Yohana 6:5-6.
Pia,
tunasoma kutoka katika biblia ya kuwa biashara na uweza wa kuuza na
kununua utafuata mfumo fulani uliojaa dhuluma, ambao utatawaliwa na
kundi fulani ulimwenguni. Watu hawatauza wala kununua bila ya kupatana
na watu wa kundi hilo, na hasa kiongozi wao. Na asomaye na afahamu. Soma
kitabu cha Ufunuo wa Yohana sura yote ya 13.
Si
hivyo tu, bali biblia inaeleza wazi kabisa kuwa katika siku hizi za
mwisho kutakuwa na uhusiano mkubwa sana kati ya utajiri na uasherati na
pia kati ya biashara na uasherati. Soma kitabu cha Ufunuo wa Yohana sura
za 17 na 18. Lakini pia unaweza kuwa na utajiri na ukafanya biashara
bila kujihusisha na uasherati na mambo mengine yaliyo kinyume na maadili
ya Mungu.
Tutawezaje kupona katika hali ya namna hii tusimkosee Mungu wetu
aliyetuita katika utakatifu ndani ya Mwana wake mpendwa Yesu Kristo? Kwa
nini wakristo wengi wanaishi katika hali ngumu kiuchumi kama vile kuna
mtu aliyewawekea vikwazo vya uchumi wasifanikiwe?
Watu
wengi wanapenda kuishi maisha matakatifu na wengi pia wanapenda kuokoka
na kudumu ndani ya kristo, lakini swali linalowasumbua ni wafanyeje
katika hali ngumu hii ya uchumi wapate chakula, malazi na mavazi
kihalali bila kumkosea Mungu?
Ni
watu wachache wanaofahamu uwezo wa mawazo katika kuongoza maneno na
matendo yao ya kila siku. Ni budi ufahamu ya kuwa maneno yako na matendo
yako ni matokeo ya jinsi unavyowaza. Kwa maneno mengine naweza kusema ya
kuwa maisha ya mtu yanategemea mtazamo wa mawazo yake.
Kwa ufafanuzi zaidi ni kwamba jinsi ulivyo ni matokeo ya jinsi
unavyowaza; kwa kuwa unayowaza ndiyo unayoyasema na kuyafanya.
Watu
wengi wamekuwa wakifikiri ya kuwa Mungu ndiye aliyewapangia kuwa maskini.
Na hata wakristo wengine kudiriki hata kuuona umaskini kama sehemu ya
utakatifu na unyenyekevu.
Lakini
Biblia haisemi hivyo, wala haifundishi mawazo hayo. Ni lengo langu
kukueleza katika ujumbe huu ya kwamba SI MAPENZI YA MUNGU TUWE MASKINI.
Nataka
ufahamu pia ya kuwa nitakapokuwa natumia neno wakristo katika ujumbe huu,
ujue namaanisha wakristo wale wanaomkiri Yesu Kristo ya kuwa Bwana na
Mwokozi wao; ambao pia humwabudu Mungu katika Roho na Kweli.
Ni
maombi yangu kwa Mungu katika Jina la Yesu Kristo kuwa atakuwezesha
kusoma na kuelewa somo hili, ili wote tulio wakristo tusimame katika
haki zetu zote zilizopatikana pale msalabani. Nia hasa ni kukupa
mafundisho ya msingi ya kukusaidia uweze kuishi hata katika hali ngumu
ya uchumi bila kumkosea Mungu. Kila wiki nitakuwa nakuwekea sura
mojawapo ya mafundisho haya.
Mafundisho
ninayotarajia kukufundisha yatakuwa na mfululizo wa masomo kama
yafuatayo:
- Kwa
nini si mapenzi ya Mungu tuwe maskini?
- Mafundisho
manne yasiyo sahihi unayopaswa kuyatambua
- Nani
anaupenda wokovu wa kimaskini?
- Utajiri
wake Kristo usiopimika
- Uchumi
wa ufalme wa mbinguni
- Tofauti
ya zaka na dhabihu
- Ukitoa
tegemea kupokea
- Sadaka
na wokovu
- Natoa
lakini sipokei – nifanyeje?
- Ufanyeje
katika hali ngumu ya uchumi?
Haya ni mafundisho ambayo nitayaweka kwa namna ambayo yatakupa
changamoto ya kuyasoma zaidi wewe binafsi na kuyaweka katika matendo.
Kwa hiyo usitegemee kupata majibu ya maswali yote uliyonayo juu ya mambo
niliyoorodhesha hapa juu, bali tegemea mwongozo wa changamoto
itakayokusaidia katika kujifunza zaidi juu ya utajiri
na mkristo.