Sura ya Tisa
NATOA
LAKINI SIPOKEI – NIFANYEJE?
Kuna
wakati fulani, mtu mmoja alinifuata baada ya kipindi nilichokuwa
nafundisha Neno la Mungu juu ya utoaji, na akaniuliza hivi; “Kwa
nini mimi nimekuwa natoa zaka na sadaka nyingi lakini sipokei? Hata
miradi niliyo nayo haifanikiwi nilivyokusudia – ni kwa nini iwe
hivyo.
Inawezekana na wewe unayesoma ujumbe huu sasa una maswali kama haya.
Hayo ni maswali ya msingi na ni muhimu tupate ufumbuzi wake. Hata
mkulima ambaye alipanda mbegu katika shamba, na asipate kitu au apate
mavuno machache, atajiuliza maswali kumetokea kitu gani.
Tukumbuke ya kuwa si mapenzi ya Mungu tuwe maskini – tuwe na hali
ngumu kimavazi, chakula na kiafya. Pia, tukumbuke ya kuwa ni tabia ya
kiuungu mtu kutoa na kutegemea kupokea. Ingawa si lazima upate toka
kwa mtu huyo huyo uliyempa, - maana Mungu anaweza kumgusa mtu mwingine
akupe – lakini utaratibu wa Mungu unabaki pale pale, ukitoa tegemea
kupokea.
Ni kitu gani kinasababisha mtu asipokee na huku amekuwa akijitahidi
kutoa? Biblia inatuambia ya kuwa tukiwa waaminifu katika utoaji, Mungu
atatumwagia baraka, “hata isiwepo nafasi ya kutosha ya kuziweka”
– Je! umewahi kumsikia mkristo yo yote akisema amepata baraka nyingi
mno hata amekosa mahali pa kuziweka?
Sababu
zifuatazo zitatusaidia kujua ni kwa nini hatufanikiwi katika utoaji
wetu – na hata hatupokei kama tulivyotegemea na kutarajia;
1. KUVUNJA
MIIKO AU UTARATIBU WA UTOAJI
Kila jambo lina utaratibu wake – usipoufuata usitegemee mavuno
mazuri. Kilimo cha mahindi kina utaratibu wake wa upandaji na palizi
tofauti na kilimo cha ngano au cha kabichi. Ndiyo maana wataalamu wa
kilimo, walianzisha kampeni za kuwafundisha wakulima juu ya “kilimo
cha kisasa” ili kiwasaidie wakulima kupata “mavuno” zaidi toka
katika mashamba yao.
Hata katika “kupanda na kuvuna” au “kutoa na kupokea” katika
mambo ya Mungu kuna utaratibu wake. Ukienda kinyume na utaratibu huo,
usitegemee mavuno ya kuridhisha toka katika utoaji wako
“Lakini nasema neno hili, Apandaye haba
atavuna
haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu.
Kila mtu na atende kama ilivyokusudia moyoni
mwake, si
kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana
Mungu humpenda
yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu” (2Wakorintho 9:6,7).
“….wala
si kama kitu kitolewacho kwa unyimivu”
(2Wakorintho 9:5).
Utaona
katika mistari hiyo Mungu ametueleza kwa kiasi fulani utaratibu ambao
anataka ufuatwe mtu akitaka kuvuna katika utoaji wake. Je! unafuata
utaratibu huu katika utoaji wako?
Utaratibu huo ni huu; utoaji wako uwe si haba (au kidogo) bali uwe kwa
ukarimu. Ukitoa kidogo utapata kidogo – bali ukitoa vingi utapata
vingi. Ndiyo maana imeandikwa;
“Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo
cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho
watu watakachowapa vifuani mwenu. KWA KUWA KIPIMO KILE KILE MPIMACHO
NDICHO MTAKACHOPIMIWA” (Luka 6:38)
Kama
unataka kutoa sadaka tu “ kama ulivyokusudia moyoni mwako”. Kama
ulikusudia kutoa shilingi 100/= toa shilingi 100/=. Fanya hivi siku
zote na utafanikiwa.
Tena, utoaji unatakiwa ufanyike “si kwa huzuni; wala si kwa lazima;
maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu
“… na wala si kwa unyimivu”.
Michango mingi iliyomo makanisani siku hizi
wakati mwingine inafanyika kwa kulazimishana. Mtu anatakiwa
atoe kwa kupenda kwake toka moyoni mwake – SI KWA LAZIMA.
Kumlazimisha mtu kutoa ni kwenda kinyume cha utaratibu wa utoaji.
Wakristo wengi wamekosa baraka au mafanikio katika utoaji kwa sababu
wanatoa huku WANAHUZUNIKA AU WANALALAMIKA! Wengi wanawanung’unikia
viongozi wa makanisa yao kuwa wanatumia fedha au vitu vibaya. Kama una
wasiwasi na matumizi ya matoleo yako – yaombee kwa Mungu ayalinde
yatumike kwa utukufu wake kuliko kulalamika.
Wengine
wanahuzunika na kulalamika kuwa michango imezidi. Je! umewahi kumsikia
mkulima akihuzunika au kulalamika kwa kuwa ameongezewa shamba la
kulima na kupanda? Hakuna. Mkulima halalamiki bali anafurahi kwa kuwa
amepata eneo kubwa zaidi la kupanda umeongezewa eneo la KUPANDA ili
AVUNE ZAIDI. Ni eneo la kukusaidia kutoa zaidi ili UPOKEE ZAIDI!
2. IBILISI
AMEZUIA BARAKA ZAKO;
Kati ya baraka ambazo zinapatikana kutokana na mtu kuwa mwaminifu
katika utoaji wa zaka (fungu la kumi) na dhabihu (matoleo mbalimbali)
na kuzidiwa wakati wa matatizo, Mungu alisema hivi;
“Nami
kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala
hataharibu
mazao ya ardhi yenu; wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake
kabla ya wakati wake
katika
mashamba ….” (Malaki 3:11).
Ni
wazi kuwa aliye nyuma ya kuharibika kwa mazao shambani au biashara ni
yule ‘alaye’ ambaye ni Ibilisi. (Hii ni kama mkulima au mfanya
biashara amefanya anachotakiwa kukifanya kilicho ndani ya uwezo wake).
Kinyume cha jambo hili ni kwamba usipokuwa mwaminifu kutoa fungu la
kumi toka katika mazao ya shamba lako, usitegemee Mungu akupiganie
wakati mharibu anapoingilia mimea yako na kuiharibu. Vile vile
usipokuwa mwaminifu kutoa fungu la kumi toka katika mapato ya biashara
yako, usitegemee Mungu akusaidie wakati mharibu anapoingilia biashara
yako na kuiharibu.
Inawezekana unatoa sadaka, na huoni baraka zozote zinazotokana na
kutoa kwako – hebu angalia na jichunguze kama umekuwa mwaminifu
katika kutoa ZAKA KAMILI. Kwa mfano kama fungu la kumi la pato
lako ni shilingi 2,000 – toa zaka kamili yaani shilingi 200/=.
Usitoe pungufu ya hiyo maana haitakuwa zaka KAMILI.
Ikiwa umekuwa mwaminifu katika kutoa Zaka kamili na dhabihu
halafu huoni matokeo yake basi, tumia mamlaka ya Jina la Yesu Kristo
– mfunge na kumkemea ibilisi ambaye ndiye mharibu wa mali yako
aondoe mikono yake juu ya mali yako.
Kumbuka Yesu Kristo alisema;
“Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote
utakalofunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote
utakalolifunga duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni” (Mathayo
16:19).
Kuna mtumishi mmoja wa Mungu ambaye anasimulia jinsi ambavyo mkulima
mmoja wa pamba alivyosaidika na uwezo wa jina la Yesu Kristo.
Huyo Mkulima alikuwa mwaminifu katika kumtolea Mungu fungu la kumi la
mapato ya shamba lake kila mwaka, na alikuwa haelewi kwa nini pamba
yake ilikuwa haifunguki ingawa muda wa kufunguka na kuchanua ulikuwa
umefika. Wataalamu wa kilimo cha pamba walikuja kuliangalia shamba
hilo lakini hawakuweza kumsaidia mkulima huyo kutatua tatizo hilo.
Mtumishi wa Mungu huyo alifika hapo, na alisikia habari ya mahangaiko
ya mkulima huyo. Baada ya kufahamu ya kuwa mkulima huyo alikuwa
mwaminifu katika kutoa fungu la kumi – alimwambia waende shambani
ili waombe.
Huyo mtumishi wa Mungu wakiwa shambani na mkulima huyo; - akimkumbusha
Mungu juu ya ahadi yake ya Malaki 3:7-11. Na mwishoni akamwamuru
ibilisi aondoke kwenye pamba hiyo. Mara tu baada ya kumaliza sala hiyo
– pamba ilianza kufunguka na kuchanua! Bwana
asifiwe sana kwa uwezo huu ulivyo wa ajabu.
Usibaki unalalamika na kuhangaika kama vile mtu asiyejua ahadi za
Mungu. Simamia haki zako ndani ya Kristo kwa kuwa mtendaji wa neno na
utafanikiwa.
3. KUTOKUPANDA
KATIKA UDONGO MZURI
Utoaji ni
sawasawa na upandaji. Mtu akipanda anategemea kuvuna pia. Kwa hiyo mtu
akitoa anategemea kupokea.
Mkulima yo yote akitaka mavuno mazuri toka shambani mwake kati ya vitu
anavyoviangalia ni aina ya mbegu na aina ya udongo. Siku zote atapanda
kwenye udongo mzuri wenye rutuba.
Mfanya biashara siku zote anataka aweke mtaji wake katika vitu
vitakavyomletea faida kibiashara na siyo hasara.
Lakini, inasikitisha kuona kuwa inapofika wakati wa utoaji –
wakristo wanatoa tu bila kuangalia kwanza “udongo mzuri” ni upi
ili utoaji wao uwaletee matokeo mazuri.
Biblia inatuambia katika mfano wa mpanzi ya kuwa mbegu zingine“….
Zikaanguka penye udongo ulio mzuri, zikazaa matunda, zikimea na kukua,
na kuzaa, moja thelathini, moja sitini, na moja mia” (Mathayo
4:8).
Je, “udongo mzuri” unaoleta faida
nzuri ni upi? Sehemu za kutoa zenye matokeo au mavuno mazuri ni hizi
zifuatazo;
(a)
Katika nyumba ya Mungu
– kanisani ili kuendeleza kazi ya Mungu – soma Malaki 3:10-11; na
Kumbukumbu ya Torati 8:18.
(b)
Kuwasaidia watumishi
wa Mungu na watakatifu wake kwa vitu/mali ulizo nazo. Soma 1Wafalme
17:10-24 na 2Wakorintho 9:10-13.
(c)
Kuwasaidia maskini kwa
vitu/mali ulizo nazo. Soma 2Wakorintho 9:8-9.
4.
KUKATA TAMAA
Wagalatia
6:9 inasema hivi; “Tena tusichoke katika
kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho”.
Tafsiri iliyo nyepesi inasema,
“maana tutavuna kwa wakati wake tusipokata
tamaa”.
Wakristo wengi wanatoa lakini hawana uvumilivu. Mkulima asipokuwa
mvumilivu kusubiri mazao ya shamba lake yanayokuja kwa wakati wake –
hawezi kuvuna alichopanda.
Vile vile mtoaji asiyejifunza kumvumilia Mungu ili amletee matokeo ya
utoaji huo kwa WAKATI WAKE – hawezi kuvuna alichopanda.
Mungu si mwongo! Wala ahadi zake hazijui kusema uongo. Alichoahidi
atatenda. Ukitoa utapokea KWA WAKATI WAKE USIPOKATA TAMAA.
Usianze kutafuta njia za mkato ili ufanikiwe – uwe mvumilivu
ulichopanda kwenye udongo mzuri utavuna.
Mkumbuke Ibrahimu alivyovumilia. Biblia inasema hivi;
“Lakini akiiona ahadi ya Mungu hakusita kwa kutokuamini,
bali alitiwa nguvu kwa imani, akimtukuza Mungu; huku
akijua hakika ya kuwa Mungu aweza kufanya yale
aliyoahidi” (Warumi 4:20-21).
5.KUTOA
KWA MAJIVUNO NA KUTAFUTA KUSIFIWA NA WATU
“Angalieni msifanye wema wenu
machoni pa watu, kusudi mtazamwe na wao; kwa maana mkifanya kama hayo,
hampati thawabu kwa Baba yenu aliye mbinguni. Basi wewe utoapo sadaka,
usipige panda mbele yako, kama wanafiki wafanyavyo katika masinagogi
na njiani, ili WATUKUZWE NA WATU. Amin, nawaambieni,wamekwisha kupata
thawabu yao. Bali wewe utoapo sadaka, hata mkono wako wa kushoto
usijue ufanyalo mkono wako wa kuume; sadaka yako iwe kwa siri; na BABA
YAKO AONAYE SIRINI ATAKUJAZI” (Mathayo 6:1- 4)