Yesu Akamwambia "Lisha Kondoo Zangu" (Yohana 21:17)
Home
Maombi
Ratiba
Shuhuda
Mafundisho
Maswali na Majibu
Barua za Mwezi
Kuchangia Huduma
MKRISTO NA UCHUMI


Sura ya Saba

UKITOA TEGEMEA KUPOKEA

            Sehemu nyingi nilizotembelea nimeona na kufahamu ya kuwa watu wengi wanatoa sadaka – fedha taslimu au vitu au wanyama kwa Mungu BILA KUTEGEMEA KUPOKEA KUTOKA KWA MUNGU.

             Furaha ya utoaji inatokana na kufahamu matokeo ya utoaji huu. Ndiyo maana mkristo yuko tayari kuweka shilingi 10,000/= katika mradi utakaompa faida kuliko kutoa kanisani ambako anafikiri sadaka hiyo haina faida kwake binafsi. Kwa hiyo siku zote atatoa sadaka kidogo kanisani au kwenye kazi ya Mungu.

            Bila ya mkristo kujua kwamba anajua na kuwa na uhakika moyoni mwake kuwa akitoa sadaka anastahili kupokea ZAIDI YA KIWANGO ALICHOTOA KUTOKA KWA  MUNGU – utoaji wake utakuwa chini siku zote.

            Wakristo wengi wanafikiri wakimtolea Mungu kitu, watazidi kupungukiwa na kufilisikia. Lakini ukweli wa mambo ni kwamba ukimtolea Mungu ulicho nacho UNAFUNGUA MLANGO WA KUFANIKIWA kwa ulivyo navyo. Unapomtolea Mungu hufilisiki bali unatajirika!

             Tunapokuwa ndani ya Kristo, tunachukua na kubeba tabia ya Mungu ndani yetu. Imeandikwa hivi:

“ Bali wote waliompokea(Kristo) aliwapa UWEZO wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake” (Yohana 1:12) “ Kwa kuwa UWEZA wake wa UUNGU umetukirimia vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe” (1Petro 1:13)

        Ni vizuri ufahamu ya kuwa mojawapo ya tabia ya Uungu tuliyo nayo ndani yetu katika Kristo ni tabia ya kutoa HUKU UKITEGEMEA KUPOKEA. Mungu akitoa kitu anategemea kupokea.

Tabia ya Mungu ya Utoaji

            Mungu alipokuwa anamtoa mwana wake wa pekee, alimtoa huku akitegemea kupata watoto wengi wa kiroho. “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanae pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele” (Yohana 3:16)
            Mungu alipokuwa anamtuma Roho Mtakatifu juu ya wanafunzi wake, alimtoa huku akitegemea kupata mashahidi wengi watakaosimama upande wake na kulitetea jina lake hapa duniani. “Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalem, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi” (Matendo ya Mtume 1:8)
            Mungu anapotoa utajiri kwa watu wake, anautoa huku akitegemea kupata agano lililo imara kati yake na wanadamu. “ Bali utamkumbuka Bwana, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako,kama hivi leo” (Kumbukumbu la Torati 8:18).
            Hii ndiyo tabia tuliyo nayo ndani ya Kristo, kutoa huku tukitegemea kupokea. Hili jambo la kutoa na kupokea wakati mwingine linajulikana kama KUPANDA na KUVUNA.
            Hakuna mkulima anayepanda mbegu shambani bila kutegemea kuvuna. Kama hana tegemeo la kuvuna, basi hata haja na hamu ya kupanda inapotea – inakuwa haina maana kupanda maana hatapata kitu.
            Katika mambo ya kiroho ni vivyo hivyo. Utakachotoa ndicho utakachopata. Utakachopanda ndicho utakachovuna. Ukipanda fedha utavuna fedha. Ukipanda upendo utavuna upendo. Ukipanda ng’ombe utavuna ng’ombe. Ukitoa vitabu utapokea vitabu. Imeandikwa hivi; “ Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna” (Wagalatia 6:7).
            Hivi ndivyo ilivyo, utakachopanda ndicho utakachovuna. Kwa maneno mengine, ni kwamba ukipanda tegemea kuvuna.

Tumia tabia ya Mungu iliyo ndani yako

            Ikiwa wewe unakaa ndani ya Kristo na Kristo anakaa ndani yako, basi uwe na uhakika ya kuwa tabia ya Uungu ya kutoa na kupokea, kupanda na kuvuna imo ndani yako.
            Inaonekana wazi ya kuwa wakristo wa kanisa la Korintho na Filipi katika nyakati za huduma ya Mtume Paulo – walishiriki sana katika habari hii ya kutoa na kupokea. Siyo kutoa bila kupokea bali kutoa na kupokea. Hii ni tabia iliyoonekana wazi katika ukristo wao. Hebu soma maneno yafuatayo juu ya habari hii katika kitabu cha Wafilipi katika nyakati za huduma ya Mtume Paulo – walishiriki sana katika habari hii ya kutoa na kupokea. Siyo kutoa bila kupokea bali kutoa na kupokea. Hii ni tabia iliyoonekana wazi katika ukristo wao. Hebu soma maneno yafuatayo juu ya habari hii katika kitabu cha Wafilipi 4:10-14;

            “ Nalifurahi sana katika Bwana, kwa kuwa sasa  mwisho mmehuisha tena fikra zenu kwa ajili yangu,    kama vile mlivyokuwa mkinifikiri hali yangu; lakini mkupata nafasi. Si kwamba nasema haya kwa kuwa  nina mahitaji; maana nimejifunza kuwa radhi na hali  yo yote niliyo nayo. Najua kudhiliwa, tena najua kufanikiwa; katika hali yo yote, na katika mambo yo yote, nimefudishwa kushiba na kuona njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa. Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu. LAKINI MLIFANYA VEMA, mliposhiriki nami katika dhiki yangu”.

             Mtume Paulo hapa anawaambia Wafilipi wazi kuwa maisha yake yote na katika mambo yote na katika hali yo yote tumaini lake na ushindi wake ni katika UWEZA WA KRISTO amtiaye nguvu – na wala si katika uweza wake Paulo au huruma za wanadamu. Hata hivyo aliwaambia “MLIFANYA VEMA MLIPOSHIRIKI NAMI KATIKA DHIKI YANGU”. Katika maneno yanayofuata aneleza kwa nini walifanya vema kumhudumia katika dhiki yake.

            “Nanyi pia, ninyi wenyewe mnajua, enyi Wafilipi, ya kuwa   katika mwanzo wa Injili, nilipotoka Makedonia, hakuna   kanisa lingine lililoshirikiana nami katika habari hii ya     KUTOA NA KUPOKEA, ila ninyi peke yenu. Kwa kuwa  hata huko Thesalonike mliniletea msaada kwa mahitaji  yangu, wala si mara moja. Si kwamba nakitamani kile kipawa, bali NAYATAMANI MAZAO YANAYOZIDI KUWA MENGI, katika HESABU YENU” (Wafilipi 4:15 – 17).

            Ni wazi kabisa ya kuwa kwa sababu ya kushiriki katika habari ya KUTOA NA KUPOKEA – Wafilipi hawakufilisika wala kupungukiwa bali MAZAO YALIZIDI KUWA MENGI KATIKA HESABU YAO. Huyu Mungu aliyewafanikisha Wafilipi, ndiye atakayekufanikisha wewe na kuongeza mazao mengi katika habari hii ya KUTOA na KUPOKEA.

            Kumbuka siku zote kuishi kwa kuitumia na kutegemea tabia ya Mungu iliyo ndani yako katika Kristo. Tabia hii itakusaidia kutoa na kutegemea kupokea – kupanda na kutegemea kuvuna. Imeandikwa hivi

            “Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa – sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu” (Luka 6:38)

UNATAKA KUOKOKA?
Kama unataka kumpa YESU maisha yako sasa, bonyeza hapa
©2003 Tanzania Social and Economic Trust.  All Rights Reserved.