Sura ya Tatu
NANI
ANAUPENDA WOKOVU WA KIMASIKINI?
“Nani anaupenda wokovu wa Ukristo wa
kimaskini?” Ukiona mtu amefika hali ya kujiuliza swali la jinsi
hii, ujue ana hali ngumu sana kiuchumi.
Hili
swali nilijikuta najiuliza mwenyewe baada ya kuwa na hali ngumu sana
kimaisha baada kuokoka. Kuna wakati fulani baada ya kuokoka mimi na mke
wangu tulijikuta tumefika mahali pa kukosa hata dawa ya mswaki, nguo,
viatu, na chakula kizuri. Licha ya shida hizi zote bado zilifuata
zingine baada ya ndugu zetu wawili tuliokuwa tunawalipia masomo yao
kufukuzwa na kurudi nyumbani kwa kukosa ada. Na waliambiwa wasirudi
shuleni bila nusu ya ada!
Unadhani tulikuwa na furaha tena? Ingawa tulikuwa tunasema tumeokoka, na
mtu akituambia ‘Bwana asifiwe’ tuliitika ‘Amina’ ndani ya mioyo
yetu tulikuwa na vita vikali na maswali mengi.
Ni
vigumu kuieleza hali hiyo tuliyoipitia ilivyokuwa ngumu kwa maneno.
Lakini utaelewa mtu mwenye familia anavyojisikia anapoona anakosa hata
fedha za kuwanunulia mke na watoto wake chakula licha ya mavazi. Wakati
huo tulikuwa na mtoto mmoja.
Hali
ilivyozidi kuwa ngumu, ndivyo nilivyozidi kusongwa na mawazo. Ilifika
wakati ambapo nilikuwa naona aibu hata kukaa sebuleni, maana niliogopa
hata kuwaangalia wale vijana waliofukuzwa shule, nikijua kuwa
wataniangalia kwa macho ya huruma ili niwape ada warudi shule. Lakini si
kwamba nilikuwa siwahurumii, bali sikuwa na fedha za kuwapa.
Ningeanzaje kuwaambia kuwa sina fedha, wakati wanajua nafanya kazi, na
pia waliona nilikuwa na fedha nyingi kabla sijaokoka? Jambo hili
lilinifanya niwaze sana. Inakuwaje kabla sijaokoka nilikuwa na fedha
nyingi na baada ya kuokoka najikuta nimefilisika? Ingawa ni kweli kwamba
kabla ya kuokoka fedha zingine nilizipata kwa njia zilizo kinyume cha
ukristo lakini nilikuwa nazo. Na baada ya kuokoka ilibidi niziache njia
hizo – na matokeo yake nilijikuta nimefilisika.
Lakini nilikuwa nimesoma katika Hagai 2:8 kuwa fedha na dhahabu ni mali
ya Mungu. Na pia nilijua kuwa vyote vya Mungu ni vyangu nikiwa ndani ya
Kristo. Kwa hiyo ilikuwa vigumu kuelewa kwa nini Mungu aseme fedha ni
mali yake, halafu mimi niliye mtoto wake nisiwe nazo.
Ningewezaje kusema wokovu ni mzuri wakati baada ya kuokoka nimejikuta
sina fedha za kutosha kununua chakula, nguo, dawa ya mswaki na hata
kukosa ada za watoto! Je ndivyo Mungu anavyotaka tuwe baada ya kuokoka?
Wakati huo ndipo nilipoelewa kwa nini wana wa Israeli waliyakumbuka
masufuria ya nyama ya Misri, ingawa walikula nyama hizo wakiwa utumwani.
Ni rahisi sana mtu aliyeokoka kurudia njia au maisha mabaya ya kutafuta
fedha kwa njia zilizo kinyume cha ukristo anapokuta anabanwa na matatizo
ya kiuchumi maishani mwake. Na hata wakati mwingine unakesha katika
maombi ili kumlilia Mungu akupe chakula na mavazi unaona kama vile
hasikii.
Nilipokuwa nasumbuliwa na hali hii ndipo nilipojikuta najiuliza mwenyewe;
“ Nani anaupenda wokovu wa kimaskini?” Nilijikuta siupendi kabisa.
Ni wokovu gani huu ambao haunisaidii hata kutunza familia yangu?
Siku
moja nilimuuliza mke wangu; nikasema; “Je! wewe unaupenda wokovu wa
kimaskini?”
Akajibu; “Hapa, siupendi!”
Nikasema; “Naona tuna mawazo yanayofanana. Kwa hiyo naona ni muhimu
tumuulize Mungu katika maombi kwa nini tulipokuwa kwa shetani tulikuwa
na fedha za kutosha, lakini baada ya kuokoka na kuja kwake tunajikuta
hatuna fedha hata za kununulia vitu muhimu?”
Baada
ya kukubaliana hayo, mimi na mke wangu tulianza kumwomba Mungu kwa
mfululizo wa siku tatu juu ya jambo moja hilo hilo. Namshukuru Mungu kwa
kunipa mke ambaye aliweza kusimama pamoja nami katika maombi juu ya
jambo hili. Sijui ningekuwa na hali gani kama angelalamika. Namshukuru
Mungu mke wangu hakulalamika bali ALIOMBA PAMOJA NAMI.
Mungu
alitujibu maombi na akaanza kutufundisha mambo mengi ambayo mengine
nawashirikisha katika ujumbe huu.
Tulijua hakika kuwa hayakuwa MAPENZI YA MUNGU tuwe na hali ngumu ya
kimaisha namna hiyo – kukosa fedha za kutosha kununulia nguo, chakula
na vitu vingine muhimu. Na baada ya kuyaweka katika matendo yale
tuliyoambiwa na Bwana yaliyo katika neno lake, hali yetu ilibadilika. Na
matatizo tuliyokuwa nayo wakati ule yakaisha. Tukaanza kuona furaha tena
katika maisha haya ya wokovu.
Ni
vizuri kujua kuwa Mungu wetu hapendi tuwe maskini. Wala hapendi wokovu
wa kimaskini! Ndiyo maana alimtuma Mwana wake wa Pekee, Yesu Kristo
kutukomboa.
Kwa kukumbusha tu, Yesu Kristo aliyafanya yafuatayo kwa kufa na kufufuka
kwake:
"Yesu
Kristo alifanyika dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tuhesabiwe haki bure
ndani yake ya kusimama tena mbele ya Mungu"
(2Wakorintho 5:21)
"Yesu
Kristo aliuchukua udhaifu wetu, ili katika mambo yote tuzitegemee nguvu
zake" (Mathayo 8:17; Wafilipi 4:13)
Yesu
Kristo aliyachukua magonjwa yetu, ili tusitawaliwe na magonjwa tena na
kwa kupigwa kwake tumepona (Isaya 53:4,5; Mathayo 8:17; 1 Petro 2:24)
Yesu Kristo aliyachukua masikitiko na huzuni zetu, ili tukae katika
amani yake ipitayo fahamu zote (Isaya 53:34; Wafilipi 4:6,7)
Yesu
Kristo alikuwa maskini kwa ajili yetu ingawa alikuwa tajiri, ili sisi
tupate kuwa matajiri katika Yeye (2 Wakorintho 8:9)
Ndiyo maana matunga Zaburi 23 aliandika hivi:
“Bwana ndiye mchungaji wangu, SITAPUNGUKIWA NA
KITU.Katika malisho ya majani mabichi hunilaza, kando ya maji ya utulivu
huniongoza. Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza katika njia za
haki kwa ajili ya jina lake …. Hakika WEMA
NA FADHILI zitanifuata siku zote za maisha yangu; nami nitakaa
nyumbani mwa Bwana milele”.
Ni
rahisi sana kusema. “Bwana ndiye mchungaji wangu, SITAPUNGUKIWA NA
KITU, lakini je! Ni kweli hujapungukiwa na kitu? Je! Zaburi hii ni ya
kweli, au ni maneno mazuri tu ya kutungia nyimbo?
Lakini napenda kukutia moyo kuwa maneno haya ni ya kweli, ukikaa ndani
ya Kristo hutapungukiwa na kitu. Ndiyo maana Mungu alimwambia Yoshua ya
kuwa atii maagizo yake yote na kuyafanya HATAMPUNGUKIA WALA KUMUACHA (Yoshua
1:5)
Kwa
kuwa maneno haya ni ya kweli, mbona basi wakristo wengi WAMEPUNGUKIWA NA
VITU? Tatizo haliko kwa Mungu, bali kwetu sisi. Na tuwe watendaji wa
neno na tutaona mafanikio.
WAJIBU WA WAKRISTO:
Ni
wajibu wa wakristo (a) kusaidiana sisi wenyewe kiuchumi; na (b)
Kuwasaidia kiuchumi watu wengine wasio wakristo. Kuna wakati fulani mtu
mmoja alikuja kwangu kuomba ushauri.
Nikamuuliza. “Una tatizo gani linalokukabili?”
Akasema; “ Baada ya kuokoka ilibidi niache njia fulani fulani ambazo
zilikuwa zinanisaidia kupata fedha kwa kuwa zilikuwa ni kinyume cha
maadili ya kikristo. Lakini sasa naona napata shida, sina fedha za
chakula, wala sijui kodi ya nyumba mwezi huu nitapata wapi. Licha ya
hayo, wale niliowakopa fedha kufanyia biashara hizo nilizoziacha
wananidai fedha zao. Hata naogopa kukutana nao. Hebu nisaidie mawazo,
najua nimeokoka kweli, lakini NITAISHIJE KATIKA HALI HII?”
Unadhani swali lilikuwa jepesi kujibu? Si swala la kumwambia tuombe
halafu umwache aende zake! Yeye anachotaka baada ya kuomba aone msaada
unamjia. La sivyo maombi hayo yanakosa maana kwake.
Swali
hili “Nitaishije katika hali hii?” Linawasumbua walio wakristo wengi
siku hizi. Na umefika wakati wa kulijibu.
Ngoja
nikuulize swali jingine. Unadhani mwanamke ambaye anafanya uasherati ili
kupata fedha za kuwalishia watoto wake hajui kuwa uasherati ni dhambi?
Nina uhakika anajua kwa kuwa kuna mwingine hata kama anafanya hayo
hakosi kila jumapili kanisani, na wakati mwingine hutoa sadaka kwa fedha
hiyo hiyo. Unadhani hajui kuwa uasherati ni dhambi? Unadhani hamwelewi
mchungaji anaposema acheni dhambi? Unadhani haogopi magonjwa ya zinaa?
Unadhani anapenda kufanya hivyo? Nina hakika walio wengi hawapendi
kufanya hivyo. Lakini jambo linalomsumbua, akiacha uasherati atapata
wapi fedha za kuwatunza watoto wake? Nina uhakika akijibiwa swali hili
ni rahisi kuacha tabia hiyo chafu.
Wasichana wengi mashuleni wamejikuta wamebeba mimba na kuharibu usichana
wao kwa kudanganywa na fedha wanazozihitaji kwa ajili ya kununulia
mafuta ya kupaka, nguo, na kutengeneza mitindo ya nywele.
Vijana wengi wa kiume wamejikuta wamejiingiza katika biashara haramu kwa
sababu ya kutaka utajiri wa haraka haraka.
Kwa
sababu ya kutokujua la kufanya wakristo wengi wamepoteza ushuhuda wao
kwa sababu ya matatizo ya kiuchumi.
Wakristo wenzetu walifanyaje? Tusome kitabu cha Matendo ya Mitume
4:32,34,35.
“Na jamii ya watu waliamini (Wakristo) walikuwa na MOYO MMOJA NA
ROHO MOJA; wala hapana mmoja aliyesema ya kuwa kitu cho chote
alicho nacho ni mali yake mwenyewe; bali walikuwa na VITU VYOTE
SHIRIKA. WALA HAPAKUWA NA MTU MMOJA MIONGONI MWAO MWENYE MAHITAJI; kwa
sababu watu wote waliokuwa na viwanja au nyumba waliviuza,
wakaileta thamani ya vitu vile vilivyouzwa; wakaiweka miguuni pa
mitume, kila mtu akagawiwa KWA KADRI YA ALIVYOHITAJI”
Utaona katika habari hii ya kuwa kwa sababu ya Ukarimu na kutokuwa na
ubinafsi wakristo hao waliweza kupambana na tatizo la umaskini katikati
yao. Ndiyo maana ikandikwa kuwa; “WALA HAPAKUWA NA MTU MMOJA MIONGONI
MWAO MWENYE MAHITAJI”. Jina la Bwana libarikiwe!
Matokeo ya usharika namna hii ni haya; “Na mitume wakatoa ushuhuda wa
kufufuka kwake Yesu kwa nguvu nyingi, na neema nyingi ikawa juu yao wote”
(Matendo ya Mitume 4:33)
Je!
Siku hizi hakuna wakristo wenye mahitaji kati yetu? Na tunafanya nini
ili kuwasaidia? Je! Kuwaombea tu kunatosha? Je! Unashangaa kwa nini
ushuhuda wa kufufuka kwake Yesu hautangazwi kwa nguvu na wakristo?
Nadhani wakristo wengi wanatumia muda wao mwingi sana kujitafutia
mahitaji yao kiasi ambacho muda unaobaki hautoshi kufanya kazi ya
kushuhudia.
Wenzetu walisaidiana, na sisi tusaidiane. Wazazi mara nyingi huwa
wanawasaidia vijana wao waliowaoza kuanza maisha mapya. Na fahamu kuwa
wokovu ni maisha mapya. Tunawajibika sana kuwasaidia wale wanaookoka
kiroho na kimwili kuanza maisha mapya ndani ya Kristo. Kwa kukosa msaada
wa kiuchumi, wengi wamepoa na kurudi nyuma.
Niliwahi kushirikishwa ushuhuda mmoja ambao naamini utakusaidia
kukuelewesha jambo hili ninalokuambia.
Kuna
mtu mmoja aliokoka baada ya muda mrefu kuwa mganga wa kienyeji na mchawi.
Baada ya kuokoka ilibidi aache uchawi na uganga wa kienyeji, shughuli
hizi ndizo zilizokuwa zinamsaidia kupata fedha ya matumizi.
Baada
ya kukaa miezi michache katika wokovu, bila ya kuwa na njia nyingine ya
kupata fedha, ilibidi atumie akiba yote aliyokuwa nayo. Baada ya hiyo
akiba kuisha akaanza kupata shida namna ya kuishi.
Akiwa
katika mahangaiko hayo, wakaja watu nyumbani kwake wakiomba msaada wa
kutibiwa magonjwa yao. Hao watu walisikia kuwa yeye ni mganga wa
kienyeji, wala hawakujua kuwa alikuwa ameokoka na kuacha uganga huo.
Kwa
sababu ya kukosa fedha, huyo mtu aliyeokoka akawaza moyoni mwake;
“Hawa watu hawajui kuwa nimeokoka, kwa hiyo hakuna haja ya kuwaambia,
kwani kuna ubaya gani nikienda kuwachimbia dawa ninazozifahamu halafu
wanipe fedha inisaidie?”
Kwa
hiyo akaenda akawachimbia hizo dawa akawapa. Na hao watu wakaondoka
baada ya kumlipa fedha. Lakini usiku, huyo aliyeokoka alipokuwa amelala
aliona katika maono. Katika maono hayo akayaona majini mawili yaliyokuwa
yanamsaidia katika uchawi zamani kabla ya hajaokoka. Hayo majini
yakasema; “Tulikwaambia hutafanikiwa katika wokovu, sisi ndiyo
tumekufilisi mali yako. Na pia sisi ndiyo tuliowatuma wale wagonjwa waje
kwako. Ulipochima zile dawa ukatuita tulikokuwa. Sasa tumekuja, mwache
Yesu njoo kwetu nasi tutakutajirisha”.
Huyo
mtu aliyeokoka aliposikia hayo, akatambua kosa lake, na mara hiyo
akalikumbuka jina la Yesu Kristo. Kwa hiyo akayakemea yale majini nayo
yakatoweka. Akamka akiwa anatetemeka.
Kama
asingelikumbuka uwezo wa jina la Yesu Kristo, angefanya nini? Naamini
kama angepata msaada wa mahitaji yake toka kwa wakristo wenzake,
asingebanwa na mtego huo. Wakristo naomba kuwakumbusha kusaidiana. Ni
muhimu sana kwa maisha yetu ya kila siku.
Ndiyo
maana Mtume Paulo aliongozwa na Roho Mtakatifu kuandika hivi:
“Kwa
habari za kuwahudumia watakatifu (Wakristo) sina haja ya
kuwaandikia. Maana najua utayari wenu, ninaojisifia kwa ajili yenu
kwa Wamakedonia, kwamba Akaya ilikuwa tayari tangu mwaka mzima; na bidii yenu
imewatia moyo wengi wao ……. Maana utumishi wa huduma hii
hauwatimizii watakatifu (Wakristo) riziki walizopungukiwa tu, bali
huzidi sana kuwa na faida kwa shukrani nyingi apewazo Mungu, kwa kuwa
mkijaribiwa kwa utumishi huo, wanamtukuza Mungu kwa ajili ya utii
wenu katika kuikiri Injili ya Kristo, na kwa ajili ya ukarimu wenu
mliowashirikisha wao na watu wote” (2Wakorintho 9:1,2,12 –
15)
Ndiyo
maana pia katika makanisa kuna mgawanyiko wa huduma. Kuna wengine kazi
yao ni kuhubiri na kuwaambia watu waache dhambi kama, uasherati na wizi.
Ni wajibu wa wale wanaoshughulika na mambo ya miradi ya maendeleo katika
kanisa ni kusaidiana na wahubiri hao kuwaongoza watu waishije baada ya
kuacha uasherati na wizi.
Napenda kukuhimiza hata wewe unayeyasoma haya kuwa, ukiona mwenzako ni
mhitaji wa kitu fulani ambacho unacho, usisite kumsaidia. Kumbuka huduma
hii ina thawabu yake kama Mtume Paulo anavyosema.
Hebu
jibu swali hili; “Lakini mtu akiwa na riziki ya
dunia, kisha akamwona ndugu yake ni mhitaji, akamzuilia huruma zake, je!
Upendo wa Mungu wakaaje ndani yake huyo?" (1Yohana 3:17)
Mzee
Yohana anatushauri anasema, “Watoto wadogo,
tusipende kwa neno, wala kwa ulimi, bali kwa tendo na kweli”
(1Yohana 3:18).
Ni
kweli Bwana Yesu Kristo alipokuwa hapa duniani alikuwa maskini, lakini
baada ya kufufuka alirudishiwa utajiri wake. Ndiyo maana Mtume Paulo
anazungumzia juu ya “……… utajiri wake
Kristo usiopimika” (Waefeso 3:8). Na katika Wafilipi 4:19
tunasoma hivi; “Na Mungu wangu atawajazeni kila
mnachokihitaji kwa kadri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya
Kristo Yesu”.
Kumbuka ya kuwa; Yesu Kristo alichukua madhaifu yetu na magonjwa yetu
yote, na kwa kupigwa kwake sisi tumepona (Isaya 53:5; Mathayo 8:16, 17;
1Petro 2:24). Na kwa kujua hili kanisa linajihusisha na kuombea wagonjwa
na kutoa huduma za afya kwa wagonjwa.
Kumbuka ya kuwa; Yesu Kristo alichukua dhambi zetu na akafanyika dhambi
kwa ajili yetu, “Ili sisi tupate kuwa haki ya
Mungu katika Yeye” (2 Wakorintho 5:21). Na kwa kujua hili
kanisa linahubiri habari za ondoleo la dhambi kwa ye yote atakayemwamini
Kristo.
Kumbuka ya kuwa; Yesu Kristo alikuwa maskini,
ingawa alikuwa tajiri, ili kwa umaskini wake sisi tupate kuwa matajiri
(2Wakorintho 5:21). Na kwa kujua hili kanisa linajihusisha na miradi
mbalimbali ya kimaendeleo ili mtu aondokane na umaskini. Wakristo
binafsi pia wanashauriwa kuwa na miradi isiyovunja maadili ya kikristo,
ili waondokane na umaskini.