 |
ZIJUE KARAMA ZA ROHO MTAKATIFU
SIKU YA KWANZA:
I Wakorintho 14:12. Inasema 'vivyo hivyo na ninyi, kwa kuwa mnatamani
sana kuwa watu wenye karama za rohoni, takeni kwamba mzidi sana kuwa
nazo ili kulijenga kanisa. Mungu hafanyi kitu bila kusudi, na kusudi la
semina hii ni:-
-
Kuna jambo Mungu anataka
kufundisha katikati yetu ambalo litahusisha sana utendaji wa karama
za Roho Mtakatifu.
-
Kurahisisha ujenzi
wa kanisa lake na kazi zake. Mfano, kuna urahisi wa kujenga kwa
kutumia mashine za kujengea na kubeba matofali kuliko kutumia mkono,
ni sawa na kufanya kazi ya Mungu kwa kutumia karama za Roho
Mtakatifu.
I Wakorintho 12:4; anasema pana tofauti za karama bali Roho ni yeye
yule. Karama si za mtu ni za Roho Mtakatifu na kazi yake ni
kulijenga kanisa.
Yesu alisema katika kitabu cha Mathayo 16:18; ''nitalijenga kanisa
langu wala milango ya kuzimu haitaliweza''. Karama zinatokea mahali
kama apendavyo Roho. Katika kitabu cha Yohana 14:16, Yesu
alizungumza habari za kutuletea msaidizi mwingine, yaani Roho
atakapokuja atachukua nafasi ya Yesu katika kulijenga kanisa lake.
Roho Mtakatifu sio karama bali anazo karama, pia Roho Mtakatifu sio
nguvu bali anazo nguvu. Tunda la Roho linapofunuliwa ndani ya mtu
tabia ya Mungu hujitokeza kwake.
Katika kutafuta vitu vya Mungu, ili kufahamu karama za Roho
Mtakatifu na kazi zake, kuna gharama. Mfano, kwenye ndege kuna first
class, business class na third class. Ukitaka kupata huduma nzuri
zaidi lazima uongeze pesa (gharama) ili upande business class au
first class. Lakini dereva wa ndege (captain) ni yule yule. Vivyo
hivyo katika maswala ya Mungu wako wanaokaa first, business au third
class, lakini wote tunakwenda mbinguni. Hivyo tunahitaji kuingia
gharama ili tukae first class ndani ya Yesu. Gharama hizo ni kama:-
i) kusoma neno la Mungu kwa bidii kwa kadri inavyowezekana ili neno
hilo likae ndani yako kwa wingi, maan kujua karama za Roho Mtakatifu
bila kuwa an maneno ya Mungu ni vigumu.
ii) Maombi n.k.
I Wakorintho 12:1 inasema 'basi ndugu zangu kwa habari ya karama za
roho, sitaki mkose kufahamu'. Tunahitaji kuwa na hamu ya kuona
kwamba karama za Roho Mtakatifu zinafanya kazi na zinafahamika. Hamu
hiyo imepotea katika kanisa la Mungu na hivyo kufanya kazi ya ujenzi
wa kanisa la Mungu kutofanyika kama Mungu anavyokusudia.
SIKU YA PILI
I Wakorintho 14:12; ''Vivyo hivyo na
ninyi kwa kuwa mnatamani sana kuwa watu wenye karama za roho, takeni
kwamba mzidi sana kuwa nazo ili kulijenga kanisa''.
UTENDAJI KAZI WA KARAMA.
Mambo muhimu (ya msingi) kufahamu ili karama
ziweze kufanya kazi. Mambo hayo ni:-
1.) kubali kuwa karama za Roho zinaweza kufanya kazi kwako pia. I
Wakorintho 12:4.11; ''Basi pana tofauti za karama bali Roho ni yeye
yule, lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule,
akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye''. Roho Mtakatifu
ndani ya mtu anazo karama zote bali anamgawia kila mtu kama
apendavyo yeye. Rumi 12:3-6; inasema ''kwa maana kwa neema
niliyopewa na mwambia kila mtu aliyeko kwenu asinie makuu kupita
ilivyo mpasa kunia ..........., basi kwa kuwa tuna karama zilizo
mbalimbali ..............''.
2.) Uwe na hamu (haja) kubwa ya msaada wa Mungu. I Wakorintho:1,12;
''ufuateni upendo na kutaka sana karama za rohoni, lakini zaidi
kwamba mpate kuhutubu, vivyo hivyo na ninyi kwa kuwa mnatamani sana
kuwa watu wenye karama za roho, takeni kwamba mzidi sana kuwa nazo
ili kulijenga kanisa''.
Angalizo: karama siku zote zina mvuto.
3.) Tembea katika wito (nafasi) yako. Warumi 12:6, ''......... kwa
kadri ya neema tuliyopewa...'', yaani wito (kiwango) ulichopewa.
Ndani ya wito kuwa nafasi ambayo Mungu amekupa. Kuna ngazi, kuna
mahali na muda unaotakiwa kuufanyia huo wito. Galatia 2:6-7 ''......walipokwisha
kujua neema niliyopewa........ walinipa mimi mkono wa kuume wa
shirika''.
Mfano: kuna tofauti ya karama ya unabii na huduma ya unabii, yaani
kila mtu aliyeokoka anaweza kutoa unabii bali si kila mtu ana karama
ya unabii.
4.) karama kutenda kazi vizuri ndani ya mtu inategemea kiwango cha
Imani alichonacho. Rumi 12:6; ''basi kwa kuwa tuna karama zilizo
mbalimbali ........ ikiwa unabii tutoe unabii kwa kadri ya imani''.
Sio zaidi ya hapo. Rumi 10:17; ''imani chanzo chake ni kusikia na
kusikia huja kwa neno la kristo'' yaani kiwango cha imani
ulichonacho hakiwezi kuzidi hapo. Imani huja tu kwa neno la Kristo.
Biblia haituruhusu kutembea kwenye karama zaidi ya imani tuliyo nayo.
Angalizo: kufahamu neno la Kristo kwa wingi ni muhimu. Tembea katika
karama za roho kwa kadri ya imani.
SIKU YA TATU
Jambo
la nne linaendelea:
Karama zitumike kwa kadri ya Imani yaani utendaji kazi wa karama za
Roho Mtakatifu ndani ya mtu utategemea kiwango cha neno la kristo
kilichoko ndani yake. Hii ni kwa sababu Mungu alikusudia kuwa karama
katikati ya kanisa zifanye kazi kwa ufanisi na usalama ili kulijenga
kanisa.
Mfano: Mungu hakuweka unabii ili uongoze kanisa; ila ni kwa ajili ya
kuthibitisha neno ambalo Mungu amekwisha kulisema ndani ya mtu.
Kwa sababu karama si zako ni za Roho Mtakatifu, kama huna neno la
kutosha ndani yako karama inaweza ikaletwa ndani yako ukaikataa.
I Wakorintho 12:8 ''maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la hekima;
na mwingine neno la maarifa apendavyo Roho yeye yule''. I Petro
4:10; ''kila mmoja kwa kadri alivyoipokea karama, itumieni kwa
kuhudumiana....''. Kuna kupewa na kupokea- karama. Unaweza kukataa
kwa kutokuja au hofu n.k.
5.) Jifunze jinsi Roho anavyowasiliana na roho yako, nafsi yako na
mwili wako. I Wakorintho 3:16; ''hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu
la Mungu na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?'' Mtu ni roho
anayo nafsi na anaishi katika mwili. Roho Mtakatifu pia yuko ndani
ya mwili. Hesabu 30:2 ''Mtu atakapo mwekea Bwana nadhiri, .......
Asitangue neno lake; atafanya sawasawa na hayo yote yamtokayo
kinywani mwake''. Unaposema maneno yanafunga nafsi yako. Mwili
unatawaliwa na nafsi, nafsi kazi yake ni kutafsiri kile ambacho
mwili unasema ili roho ielewe na kile ambacho roho inasema ili mwili
uelewe. Kwa hiyo nafsi inasaidiwa pale, unaposoma neno ili iweze
kutafsiri mambo ya rohoni sawasawa na neno. Marko 2:5-8, ''naye Yesu,
alipoiona imani yao, ........ wakifikiri mioyoni mwao ..... Yesu
akafahamu rohoni mwake kwamba wanafikiri hivyo nafsini mwao .....''.
Galatia 6:17; ''tangu sasa mtu asinitaabishe kwa maana ninachukua
mwilini mwangu chapa zake Yesu.
6.) Ujazo wa Roho Mtakatifu. Sio wa siku moja ambao unatosheleza. I
Petro 4:9-11 ''mkaribishane ninyi kwa ninyi, pasipo kunung'unika,
kila mmoja kwa kadri alivyoipokea karama,........... mtu akihudumu
na ahudumu kwa nguvu anazojaliwa na Mungu, .......''. yaani kila
wakati kuna nguvu fresh, mtu asihudumu kwa nguvu alizojaliwa bali
anazojaliwa kila wakati na Mungu. Hivyo tunahitaji kurudi kwa Mungu
kila wakati kujazwa nguvu za Roho Mtakatifu.
Kuna kiwango cha nguvu za Roho Mtakatifu ndani ya mtu ambacho
hakiwezi (kwa kuwa ni kidogo) kusukuma karama fulani ili ziweze
kuhudumu au kufanya kazi; ndio maana tunahitaji kujazwa kila wakati.
SIKU YA NNE
Karama ya neno la
Maarifa
I Wakorintho 12:4,8; ''Basi pana tofauti za karama bali Roho ni yeye
yule. Maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la hekima, na mwingine
neno la maarifa, apendavyo Roho yeye yule''.
Kama tulivyo jifunza huko nyuma kazi ya karama ni kulijenga kanisa.
Kazi ya karama ya neno la maarifa.
-
Kukupa habari ya
mambo yaliyopo na/au yaliyopita ili kukurahisishia kufanya maamuzi
na kutambua hila zilizojificha ili kukwamisha utumishi wako.
-
Wakati mwingine karama
hii itakupa kujua maswali waliyonayo watu kabla hawajauliza au kujua
mahitaji waliyonayo kabla hawajakwambia.
Njia nne ambazo karama ya neno la maarifa inafanya kazi:
i. kwa kutumia mawazo
ii. kwa kutumia ndoto
iii. kwa kutumia maono, maono yamegawanyika katika sehemu zifatazo:
-
maono ya ndani
-
maono ya wazi
-
maono yanayotokea
wakati akili zako hazina matunda.(suspended)
iv. kwa kutumia njia ya kuweka mwilini
mwako maumivu au hali aliyo nayo mtu mwenye kuhitaji.
Karama zinafanya kazi kwa kutegemeana/kushirikiana.
Mfano. Unaweza kupewa swali na jibu. Kulijua swali ni neno la
maarifa na kujua jibu la swali hilo ni neno la hekima.
i. Njia ya kutumia MAWAZO / WAZO
Hii ndio njia kuu ambayo inatumika mara nyingi zaidi. Marko
2:6-8 inasema ''....... Mara (ghafla) Yesu akafahamu rohoni mwake
kwamba wanafikiri hivyo nafsini mwao.....''. Maana yake ghafla wazo
tofauti, na lile alilokuwa akiwaza saa hiyo lililetwa na Roho
Mtakatifu ndani yake.
Ukisoma Luka 3:15-16; inasema ''..........Yohana alijibu akawaambia
wote,............''. Yaani alijibu swali ambalo lililetwa ndani yake
na Roho Mtakatifu; sio kwamba aliulizwa na mtu yeyote yule.
Luka 20:18-26; inasema ''..........wakamvizia-vizia, wakatuma
wapelelezi waliojifanya kuwa watu wa haki, ili wamnase katika maneno
yake, wapate kumtia katika enzi na mamlaka ya liwali. Wakamwuliza
wakisema,................... Lakini yeye alitambua hila yao
akawaambia ................ Wakastaajabia majibu yake, wakanyamaa''.
Mambo ya kukuwezesha kufanya kazi na njia hii
ya mawazo:
a. Jizoeze kukabidhi roho yako, nafsi yako na mwili wako kila siku
upya mbele za Mungu.
b. Omba maombi ya vitu vifuatavyo:
-
Usikivu
(sensitivity)
-
Utulivu
-
Kufundishwa na
Mungu namna ya kutembea katika hiyo karama.
Hii inasaidia kwa mfano, Mungu akisema jenga safina wakati sio msimu
wa mvua. Yaani kutii sauti ya Mungu bila kuangalia dalili za nje.
SIKU YA TANO
Karama ya neno la
hekima
I Wakorintho 12:4,8; inasema '' Basi pana tofauti za karama bali
Roho ni yeye yule. Maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la hekima.......''.
I Wakorintho 14:12 '' ......takeni sana mzidi kuwa nazo ili
kulijenga kanisa''.
Karama ya neno la maarifa na neno la hekima zinafanya kazi kwa karibu
sana.
Kazi ya karama ya neno la hekima na
inavyofanya kazi:
1. kukupa jibu la swali unaloulizwa lakini hasa swali lenye hila,
mtego, ushindani au mashtaka ndani yake.
Luka 21:12-15 inasema ''lakini, kabla hayo yote hayajatokea
watawakamata na kuwaudhi; watawapeleka mbele ya masinagogi........
basi kusudieni mioyoni mwenu, kutofikiri-fikiri kwanza, mtakavyojibu,
kwa sababu mimi nitawapa kinywa na hekima ambayo watesi wenu wote
hawataweza kushindana nayo wala kuipinga''.
Luka 20:19-26; ''...lakini yeye alitambua hila yao .....''
Marko 3:1-6; inasema ''..........akamwambia yule mtu mwenye mkono
uliopooza simama katikati ..........nyosha mkono wako. Naye
akaunyosha mkono wake ukawa mzima tena''.
Hapa tunaona neno la maarifa (kutambua hila ya wale waliotaka
kumkamata) ilianza kufanya kazi, neno la hekima pia likafanya kazi
baadaye pale Yesu alipomwambia yule mwenye kupooza ''simama katikati''
na tunasoma akaanza kuzungumza na wale watu.
2. inakupa uwezo wa kutatua tatizo lililoko
mbele yako.
Mathayo sura ya 1 na ya 2: Habari ya Yusufu na Mariamu. Katika sura
hizi karama ya neno la maarifa na la hekima ilifanya kazi kwa kutumia
ndoto. Si ndoto zote zinatoka kwa Mungu lakini kama ukiwa na neno la
Mungu utatambua ndoto ya Mungu na isiyo ya Mungu.
3. kukupa uhuru wa kushirikiana na watu
usiowajua kwa kazi ya Mungu.
Matendo ya mitume 10:1-20; Habari za Petro na Kornelio. Habari hii
inaeleza jinsi Petro alivyoona maono wakati amezimia roho (akili
zake zilikuwa hazina matunda).
Maono ya aina nyingine, kama tulivyokwishaona hapo nyuma ni ya wazi,
ambapo akili zako zinaona na zinaelewa na bado unaweza kuona katika
ulimwengu wa roho.
Aina nyingine ni maono ya ndani kwa mfano: unapoomba halafu ghafla
ndani yako inakuja picha.
Sasa karama ya neno la maarifa na la hekima itakusaidia kukuwezesha
kushirikiana na watu usiowajua.
4. inakurahisishia kuamua kwa haki katika
nafasi ya uongozi Mungu aliyokupa au mahali unapohitajika kutoa
maamuzi
I Wafalme 3:4-28; habari za mfalme Sulemani, jinsi alivyoomba hekima
kwa Mungu na akapewa. Vilevile tunaona jinsi ambavyo aliweza kutoa
uamuzi wa haki juu ya kesi ya wanawake wawili waliokuwa wakigombea
mtoto.
Uamuzi wa haki unahitaji msaada wa Mungu.
SIKU YA SITA
Karama ya
unabii
I Wakorintho 12:4,10 ''Basi pana tofauti za karama bali Roho ni yeye
yule. na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii, na
mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine
tafsiri za lugha.
I Wakorintho 14:12; inasema ''.......takeni kwamba mzidi sana kuwa
nazo ili kulijenga kanisa''.
Mambo ya msingi kuhusu huduma ya Nabii na karama ya unabii:-
1. kuna tofauti kati ya huduma ya nabii na karama ya unabii.
Efeso 4:11 ''Naye alitoa wengine kuwa Mitume; na wengine kuwa
manabii....''. Hapa anazungumza habari ya nabii (ofisi) ya nabii.
Huduma ni ofisi na karama ni vitendea kazi katika ofisi.
Kazi za nabii (kama huduma)
-
kufundisha mafundisho ya
msingi / ya kuweka msingi wa kiroho ndani yako. Efeso 2:19-20
inasema, ''Basi tangu sasa ninyi si wageni wala wapitaji, ........mmejengwa
juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni
jiwe kuu la pembeni''. Hii haimaanishi kwamba kila nabii amepewa
kufundisha.
-
Nabii pia anaweza
kupewa kufanya kazi ya kubomoa na kuharibu kazi za shetani na
kupanda pando la Mungu ndani ya mioyo ya watu, kama kuna mahali
panahitajika kufanya hivyo. Tunaweza kusoma haya katika kitabu cha
Yeremia 1:4,5,10; inasema '' .....kabla sijakuumba katika tumbo
nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa
nabii wa mataifa ............. Ili kung'oa na kubomoa na kuharibu na
kuangamiza; ili kujenga na kupanda''.
-
Kazi nyingine ni kuonya.
Tunaweza kuona haya katika kitabu cha Ezekieli 2:3-5; ''akaniambia
mwanadamu, nakutuma kwa wana wa Israel, kwa mataifa wanaoasi,
walioniasi mimi wao na baba zao wamekosa juu yangu.....''
-
Kazi nyingine ni mwonaji.
I Samweli 9:9 ''(Hapo zamani katika Israel, mtu alipokwenda kuuliza
neno kwa Mungu, husema hivi, Haya! Twende kwa mwonaji; maana mtu
aitwaye sasa Nabii hapo zamani aliitwa mwonaji)''.
-
Kutabiri (kusema
mambo yajayo). Yeremia 23:21; inasema ''mimi sikuwatuma manabii hao,
lakini walikwenda mbio; sikusema nao, lakini walitabiri.
Kazi ya karama ya unabii. (kama kitendea kazi):
Ni kujenga, kufariji, kutia moyo na kujirunza, pia huthibitisha kile
ambacho Mungu amekwisha kusema na wewe. Katika kitabu cha I
Wakorintho 14:3,4,24,25,31; tunasoma ''Bali yeye ahutubuye, asema na
watu maneno ya kuwajenga, na kuwafariji, na kuwatia moyo. Yeye
anenaye kwa lugha hujijenga nafsi yake; bali ahutubuye hulijenga
kanisa. Lakini wote wakihutubu, kisha akaingia mtu asiyeamini, au
mjinga, abainishwa na wote, ahukumiwa na wote; siri za moyo wake
huwa wazi, na hivyo atamwabudu Mungu, akianguka kifudi-fudi, na
kukiri ya kuwa Mungu yu kati yenu bila shaka. Kwa maana ninyi nyote
mwaweza kuhutubu mmoja mmoja, ili wote wapate kujifunza, na wote
wafarijiwe''.
2. manabii wapo hata leo ila nafasi zao ni
tofauti na za wale wa agano la kale.
Efeso 4:11,14; ''naye alitoa wengine kuwa mitume na wengine kuwa
manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na
waalimu; kwa kusudi la kuwakamisisha watakatifu; hata kazi ya huduma
itendeke hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote
tutakapoufikia umoja wa Imani na kumfahamu sana mwana wa Mungu, hata
kuwa mtu mkamilifu............. Ili tusiwe tena watoto wachanga,
tukitupwa huku na huku na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa
hila ya watu, kwa ujanja tukizifuata njia za udanganyifu''.
Pia katika kitabu cha Matendo ya Mitume 13:1; tunasoma ''.......
Palikuwako manabii na waalimu .....''. hii inaonyesha kuwa manabii
wapo hata leo.
Tofauti iko hivi: kwamba manabii hapo zamani (katika agano la kale)
walikuwa viongozi wakiongoza watu, yaani walipewa kuongoza watu,
lakini katika agano jipya huduma ya nabii ipo ndani ya Kanisa na
nabii hakupewa kuongoza kanisa- kila mmoja wakati huu amepewa Roho
Mtakatifu ambaye anamwongoza. Hivyo nabii anayesema kwa mausia ya
Mungu ni yule anayesema sawasawa na neno la Mungu.
Kanisa linajengwa juu ya misingi miwili ambayo
ni:
a. Yesu Kristo
b. Mafundisho ya mitume na manabii ambao wanafundisha mafundisho ya
msingi ambayo yanamfanya mtu awe mkristo. (foundation series).
Ukisoma kitabu cha Waebrania 6:1; inasema ''kwa sababu hiyo,
tukiacha kuyanena mafundishao ya kwanza ya Kristo; tukaze mwendo ili
tuufikilie utimilifu; tusiweke msingi tena wa kuzitubia kazi zisizo
na uhai, na wa kuwa na Imani kwa Mungu na wa mafundisho ya mabatizo,
na kuwekea mikono, na kufufuliwa wafu na hukumu ya milele''.
Manabii wa sasa wanatofauti na akina Paulo na akina Petro ambapo hao
wa zamani walipewa mafundisho ya msingi na hawa wa sasa wanapewa
wito (hekima au special revelation) wanaposoma Biblia wanafungua
siri za mafundisho ya msingi, ambayo akina Paulo walifundisha, na
kutufunulia sisi.
SIKU YA SABA
Mambo ya msingi
kuhusu huduma ya Nabii na karama ya Unabii, inaendelea........'
I Wakorintho 12:4,10
3. Karama ya Unabii (kinachosemwa na Nabii) lazima kipimwe.
Kwa nini kupima?
-
Si wote wametumwa
na Mungu.
Ukisoma kitabu cha Yeremia 23:21,22; anasema ''mimi sikuwatuma
manabii hao, lakini walikwenda mbio; sikusema nao lakini walitabiri.
Lakini kama wangalisimama katika baraza yangu, ndipo
wangaliwasikizisha watu wangu maneno yangu, na kuwageuza waziache
njia zao mbaya,.....''. Maana yake ni manabii wa kweli ila tatizo ni
kwamba walienda pasipo kutumwa, hawakukaa barazani pa Mungu na
kusikiliza kile ambacho Mungu alitaka kisemwe.
-
Kuna manabii wa
uongo waliojiingiza katika makundi ya Mungu.
Ukisoma Mathayo 7:15; anasema ''Jihadharini na manabii wa uongo,
watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni
mbwa-mwitu wakali.
-
Kuna manabii wa uongo
ambao wanafanya kazi kwa kutumia Ishara na miujiza, ili kuwavuta
watu wawafuate lakini Mungu hakuwatuma. Ukisoma Mathayo 24:24,25 ''kwa
maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa
Ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini hata
waliowateule. Tazama nimekwisha kuwaonya mbele''.
-
Kwa sababu ya
matumizi yasiyo na utaratibu wa ki-Mungu juu ya huduma ya Nabii na
karama ya unabii.
I Wakorintho 14:29,33,39,40; ''Na manabii wanene wawili, au watatu,
na wengine wapambanue. Kwa maana Mungu si Mungu wa machafuko, bali
wa amani, vile-vile kama ilivyo katika makanisa yote ya watakatifu.
Kwa ajili ya hayo ndugu, takeni sana kuhutubu wala msizuie kunena
kwa lugha. Lakini mambo yote na yatendeke kwa uzuri na utaratibu''.
-
Ni agizo.
Ukisoma I Yohana 4:1; anasema '' Wapenzi, msiiamini kila roho, bali
zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii
wa uongo wengi wametokea duniani''. Pia katika kitabu cha 2 Petro
1:20,21; ''mkijua neno hili kwanza, ya kwamba hakuna unabii katika
maandiko upatao kufasiriwa kama apendavyo mtu fulani tu. Maana
unabii haukutolewa popote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu
walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu''.
Unapimaje?
Katika kupima kwa ajili yako wewe kutoa karama ya Unabii au kwa
kusikia kutoka mtu mwingine, jiulize maswali yafuatayo:-
a. Je roho inayokutumia kutoa unabii inakutawala au unaitawala?
Ukisoma kitabu cha I Wakorintho 14:32,33 anasema ''Na roho za
manabii huwatii manabii....'' Roho Mtakatifu hakuleta karama zake
zikufanye mtumwa. Ukiona hali hii kaa kwenye maombi tena.
b. Je hayo yaliyosemwa kwa njia ya unabii ni sawasawa na neno?
Ukisoma Warumi 12:6 inasema; ''......tutoe unabii kwa kadri ya imani''.
Maana yake kwa kadri ya kiwango cha neno ulichonacho ndani yako. Pia
kitabu cha Hesabu 22:18; inasema ''.....siwezi kupita mpaka wa neno
la Bwana, alilosema ndani yangu Mungu wangu, kulipunguza au
kuliongeza.
c. Je unapotumika katika unabii au kama nabii unajionaje ndani yako?
Unaona kama hiyo karama ni kipimo cha kiroho kwamba uko mbali sana?
Kitabu cha I Wakorintho 13:9 '' kwa maana tunafahamu kwa sehemu na
tunafanya unabii kwa sehemu''. Maana yake hakuna mtu ambaye anajua
kila kitu hivyo ni muhimu kuwa mnyenyekevu na kuwa tayari kujifunza
kwa wengine.
Pia katika kitabu cha I Petro 4:9-10; inasema ''........ kila mmoja
kwa kadri alivyoipokea karama, itumieni kwa kuhudumiana; kama
mawakili wema wa neema mbalimbali za Mungu''. Maana yake uwe tayari
kupokea karama ambayo inatenda kazi ndani ya mtu mwingine. Vile-vile
kitabu cha I Wakorintho 13:2; anasema '' tena nijapokuwa na unabii,
na kujua siri zote na maarifa yote, ..... kama sina upendo si kitu
mimi''.
d. Je Kristo anainuliwa au la? Kitabu cha Kumbukumbu la torati
13:1-4. ''kukizuka katikati yako nabii au mwotaji wa ndoto...
akisema, na tuifuate miungu mingine ya nabii yule ............
tembeeni kwa kumfuata Bwana, Mungu wenu, ........''. Kuna hatari
pale ambapo karama zinafanya kazi halafu utukufu wanapewa watu
badala ya kumwinua Yesu.
e. Je unabii / kilichosemwa na nabii au unabii ulioletwa kwako
unakuweka huru au la? Maana palipo Roho wa Bwana hapo ndipo penye
uhuru.
f. Je unabii huo unatimia au la? Ukisoma Kumbukumbu la Torati
18:20-22 anasema ''Lakini nabii atakayenena neno kwa kujikinai kwa
jina langu, ambalo sikumwagiza kulinena, au takayenena katika jina
la miungu mingine, nabii yule atakufa...... atakaponena nabii kwa
jina la Bwana, lisifuate jambo lile wala kutimia, hilo ndilo neno
asilolinena Bwana;.........''.
g. Je tabia za hao manabii zikoje? Ukisoma Mathayo 7:15-23; anasema
'' ........mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu
kuzaa matunda mazuri.......... Ndiposa kwa matunda yao mtawatambua..............''
Mara nyingi tunda huwa linachukua muda kutokea lakini baada ya muda
huo litatokea tu.
h. Je huo ujumbe aliotoa nabii unajenga au unabomoa? Ukisoma I
Wakorintho 14:3-5,31 '' Bali yeye ahutubuye, asema na watu maneno ya
kuwajenga, na kuwafariji, na kuwatia moyo........... bali ahutubuye
hulijenga kanisa ............ kwa maana ninyi nyote mwaweza kuhutubu
mmoja mmoja, ili wote wapate kujifunza, na wote wafarijiwe''.
Karama ya unabii inavyofanya kazi
-
Kusema chini ya
upako. 2 Petro 1:20-22 anasema '' ..........., wakongozwa na Roho
Mtakatifu
-
Ujumbe unaoambatana
na Matendo. Matendo ya mitume 21:9-14; inasema ''..... alipotufikia
akautwaa mshipi wa Paulo, akajifunga miguu na mikono, akasema, Roho
Mtakatifu asema hivi, hivyo ndivyo wayahudi wa Yerusalemu
watakavyomfunga mtu mwenye mshipi huu nao watamtia katika mikono...........''.
-
Unabii mwingine
unatimia kwa maombi. Yakobo 5:17-18; anasema '' Eliya alikuwa
mwanadamu mwenye tabia pamoja na sisi, akaomba kwa bidii mvua isinye
na mvua haikunya juu ya nchi muda wa miaka mitatu na miezi sita.
Akaomba tena, mbingu zikatoa mvua nayo nchi ikazaa matunda yake''.
SIKU YA NANE
Karama ya
masaidiano.
I Wakorintho 12:28; inasema '' Na Mungu ameweka wengine
katika kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, na tatu waalimu,
kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa, na masaidiano na
maongozi na aina za lugha''.
Kuna huduma ya masaidiano na karama ya masaidiano. Karama ya
masaidiano inafanya kazi kwa karibu sana na karama ya neno la
maarifa ili upate kujua kuna mahali panahitaji msaada. Pia inafanya
kazi kwa karibu sana na karama ya neno la hekima kujua ni msaada
gani unatakiwa, vilevile inafanya kazi kwa karibu sana na karama ya
Imani kwa sababu mahali pengine unahitaji kufanya vitu kwa imani
pasipo kuona ishara ya nje.
Tumekwisha kujifunza kwamba kazi ya karama za Roho Mtakatifu ni
kulijenga kanisa kwa hiyo kazi ya karama ya masaidiano pia ni
kulijenga kanisa.
Maeneo manne ya kukusaidia kuifahamu zaidi
karama ya masaidiano.
1. Inasaidia viungo vingine vifanye kazi yake katika kulijenga
kanisa. Efeso 4:15-16; '' lakini tuishike kweli katika upendo na
kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo.
Katika yeye mwili wote ukiungamanishwa na kushikanishwa kwa msaada
wa kila kiungo, kwa kadri ya utendaji wa kila sehemu moja moja,
huukuza mwili upate kujijenga wenyewe katika upendo''. Maana yake
kila kiungo katika kanisa kina kazi yake. Karama ya masaidiano huwa
haionekani kwa nje lakini ni karama ya muhimu sana.
2. Inamsaidia mtu avuke kipindi chake cha mahangaiko asije akaacha
kazi ya kulijenga kanisa. Matendo ya Mitume 9:1-19; anaeleza habari
za Sauli (Paulo) akielekea Dameski. Katika mstari wa 8-9 anasema ''
Sauli akainuka katika nchi, na macho yake yalipofumbuka hakuona kitu;
wakamshika mkono wakamleta mpaka Dameski. Akawa siku tatu haoni;
hali wala hanywi. Basi palikuwapo Dameski mwanafunzi ........''
Hapa tunaona Paulo (Sauli) alikuwa katika mahangaiko ndio
maanahakula wala kunywa kwa siku tatu.
Anania aliwekewa mzingo wa kwenda kumsaidia Paulo katika mahangaiko
hayo na tunasoma kwamba baada ya kumsaidi aliondoka. Hii inatokea
mara nyingi sana pale ambapo watu wanapata mahangaiko ya wito na
hapa ndipo karama ya masaidiano inahitajika.
3. Inamsaidia mtu mwingine afanikiwe katika wito alioitiwa na Mungu.
Yohana 19:38-42; ''Hata baada ya hayo Yusufu wa Arimathaya, naye ni
mwanafunzi wa Yesu (lakini kwa siri kwa hofu ya wayahudi) alimwomba
pilato fuhusa ili auondoe mwili wa Bwana Yesu. Na pilato akampa
ruhusa...........''.
Hapa tunaona wanafunzi wa Yesu, baada ya Yesu kufa, hawakuonekana
kumsaidia Yesu kwenda kuuhifadhi mwili wake. Lakini msaada wa aina
ya pekee ulitolewa na watu wengine ambao hawakuwa wanafunzi wa
karibu sana na Bwana Yesu wakati wa maisha yake. Hii ni karama ya
masaidiano ilishuka ndani yao kwa ajili ya kukamilisha wito wa Bwana
Yesu.
Mfano: katika eneo kama hili ndipo watu wengine wanapewa mzigo kwa
ajili ya utoaji (very specific giving) ili kusaidia kazi ya Mungu
isilale, na hii inafanyika bila kujadiliana na yule anayesaidiwa.
Hii inatokea hata kwa waombaji ambao wakati mwingine Roho Mtakatifu
anaweka mzigo ndani yao ili kuombea tukio (event) fulani tu.
4. Inamsaidia mtu mwingine
akubalike katika wito wake. Ukisoma Matendo ya Mitume 9:26-29;
anazungumza habari za Sauli alipofika Yerusalemu, tunasoma kwamba
alijaribu kujiunga na wanafunzi lakini walimwogopa. Lakini Barnaba,
ambaye aliinuliwa na Mungu ili kusaidia, alimtwaa akampeleka kwa
mitume na kumtambulisha.
SIKU YA TISA
Karama ya
aina za lugha
Ili karama zifanye kazi kwa haraka weka ndani yako kiu ya kuona
Yesu anatukuzwa. Mambo muhimu kuhusu karama ya aina za lugha:-
a. Hizi lugha zinazosemwa ni za aina gani? Ukisoma I Wakorintho 13:1;
anasema '' nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina
upendo nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao''. Maana yake Roho
Mtakatifu anaweza akakuletea lugha ya wanadamu lakini siyo ile ambayo
umejifunza. Na pia anaweza akakuletea lugha za Malaika.
b. kuna tofauti ya kunena kwa lugha kwa kila aaminiye na kunena kwa
lugha kama karama. I Wakorintho 12:29,30 anasema ''Je wote ni Mitume?
Wote ni manabii? Wote ni waalimu? Wote wanatenda miujiza? Wote wana
karama za kuponya wagonjwa? Wote wanena kwa lugha? Wote wafasiri?''
Maana yake si kila mtu anapewa kufanya haya yote yaliyotajwa, si kila
mtu hii karama ya kunena kwa lugha, inatokea kwake kila wakati, ila ni
pale ambapo Mungu anaona panahitajika karama hiyo.
Mfano: karama hii inaweza kukusaidia pale ambapo hufahamu lugha fulani
na unahitajika kupeleka ujumbe kwa lugha hiyo.
Kwa upande mwingine kuna kuna kunena kwa lugha kama ishara. Marko
16:17; '' na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu
watatoa pepo; watesema kwa lugha mpya''. Hapa anazungumza kunena kwa
lugha kwa kila aaminiye na sio karama.
I Wakorintho 14:5; anasema ''nami nataka ninyi nyote mnene kwa lugha
.......''. Maana yake kunena kwa lugha kama ishara kwa kila aaminiye
na siyo karama kwa sababu anenaye kwa lugha anahuisha nafsi yake.
|