Yesu Akamwambia "Lisha Kondoo Zangu" (Yohana 21:17)
Home
Maombi
Ratiba
Shuhuda
Mafundisho
Maswali na Majibu
Barua za Mwezi
Kuchangia Huduma
RIPOTI YA WIKI TANO ZA SEMINA MFULULIZO - JULAI NA AGOSTI 2006


WIKI 5 ZA SEMINA MFULULIZO….

….watu 4248 waokoka!

Tulianza na semina ya Dodoma mjini ( 5 – 9 Julai 2006), halafu tukaenda Mwanza mjini ( 13 – 16 Julai 2006). Tulipotoka Mwanza mjini wiki iliyofuata tulifanya semina ya tatu Shinyanga mjini ( 21-23 Julai 2006). Wiki iliyofuata ya nne tulifanya semina Tabora mjini ( 28 – 30 Julai 2006), na tukamalizia Kigoma mjini ( 4- 6 Agosti 2006) ikiwa ni semina ya wiki ya tano.

Tunamshukuru Mungu sana kwa kutuwezesha kuzifanya semina zote hizo kwa mafanikio makubwa! Sifa na utukufu tunamrudishia Bwana Yesu ambaye kufuatana na kitabu cha Wafilipi 4:19 ametutia nguvu na kutuwezesha katika kila hatua ya wiki hizo tano.

Wiki hizo tano zilikuwa na baraka mpya katika kila wiki. Kuna rafiki yetu mmoja ambaye ni mkazi wa Mwanza na alikuwepo na kuhusika vilivyo katika semina ya Mwanza, na akaamua wiki iliyofuata aje Shinyanga ahudhurie semina siku za Jumamosi na Jumapili.

Tulipomaliza semina ya siku ya Jumamosi pale Shinyanga akatufuata akasema “Mungu amewapendelea watu wa Shinyanga, mbona Mwanza hatukuona Mungu akifanya mambo kama alivyofanya Shinyanga leo?”

Tulichomjibu ni kwamba: “Huu ndio uzuri wa semina mbalimbali tunazofanya! Maana hazifanani – ingawa Mungu ni Yeye yule atendaye katika semina zote kwa uwezo wa Roho Mtakatifu”.

Uzuri wa Semina ni
Utofauti wake!

Kila semina tunayoifanya iko tofauti! Na utofauti huu ndio unaofanya semina ziwe nzuri na kukufanya mtu usichoke kuzifanya na kuzihudhuria!

Fikiria semina zote tano tulizozifanya kwa wiki tano mfululizo katika miji na mikoa mitano tofauti zingekuwa zote zimefanana – ingekuwaje!

Jibu ni rahisi tu ya kwamba semina hizo zingekuwa zimefanana zingemchosha kila mtu! Lakini Mungu wetu ni mzuri sana ambaye kwa uwezo wa Roho Mtakatifu amezifanya zitofautiane!

Huo ndio uzuri wa semina hizi! Kwa mfano: Katika semina hizo tano tumejifunza masomo matano tofauti – na kila somo lilikuwa na utamu wake ambao haufanani na wa somo jingine!

Semina ya Dodoma mjini tulifundisha somo linalosema: “Ukipata ushindi katika mawazo yako utapata ushindi katika maisha yako pia”.

Lengo lilikuwa ni wasikilizaji wajue ya kuwa mawazo yao ni uwanja wa mapambano kati ya Mungu na shetani. Atakayeongoza maisha ya mtu – iwapo ni Mungu au shetani – inategemea matokeo ya mapambano yao katika mawazo ya mtu.

Mistari ya msingi kwa somo hili kutoka katika biblia ilikuwa ni hii:

“Maana ingawa tunaenenda katika mwili,
  hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; (maana
  silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina
  uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome)
 tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka,
 kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu;
 tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo”

               (2 Wakorintho 10:3-5)

Tulipokwenda kufanya semina mjini Mwanza tulifundisha somo lililokuwa na kichwa kilichosema: “Uhusiano wa fedha na hali yako ya kiroho”

Neno la kutuongoza katika semina hiyo tulilitoa toka kitabu cha Mathayo 6:21 linalosema: “Kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako”.

Tulilitafsiri neno “hazina” ya kuwa ni “fedha”, na neno “moyo” tulilitafsiri ya kuwa ni “nafsi”. Mstari huo wa Mathayo 6:21 tuliusoma hivi; “kwa kuwa fedha yako ilipo,ndipo itakapokuwapo na nafsi yako”.

Kwa hiyo tulitaka wasikilizaji wajue ya kuwa kufuatana na maneno hayo ya Yesu Kristo, fedha ina nguvu kuliko nafsi ya mtu. Na kwa sababu hiyo fedha ina sauti kubwa juu ya mwelekeo wa hali ya mtu ya kiroho.

Tulijifunza na kuzichambua aina nne za nguvu zilizomo ndani ya fedha, na namna ya kuithibiti hiyo nguvu kibiblia, ili mtu awe na fedha na zisiharibu hali yake ya kiroho.

Semina ya Shinyanga mjini tulijifunza somo linalosema: “ Usikate Tamaa – Liko Tumaini”.

Huu ulikuwa ni ujumbe wa kuwatia moyo na wa kuwajulisha cha kufanya watu waliokata tamaa; na watu wanaolekea kukata tamaa; na kwa ajili ya wale watu waliozungukwa na mazingira ya kukatisha tamaa.

Neno lililotungoza katika somo hilo ni maneno ya Yesu Kristo ya kitabu cha Yohana 16:33 aliyosema hivi: “….. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu”.

Tulitaka watu wajue ya kuwa Mungu anajua dhiki tulizonazo hapa ulimwenguni.Na anataka tujipe moyo katika mazingira ya dhiki hizo, kwa kuwa Yesu ameushinda ulimwengu, na kwa sababu hiyo anaweza kutusaidia kuzishinda dhiki zetu!

Zaidi ya kujua hayo, tulitaka kila mtu afahamu ya kuwa; Yesu halazimishi kumpa mtu msaada! Katika Ufunuo wa Yohana 3:20 anasema: “Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami”.

Lengo la kuwapa mstari huu ni kutaka waelewe ya kuwa, Yesu anasubiri apewe ‘fursa’ au ‘nafasi’ au ‘mwanya’ na mtu anayehitaji msaada kwake ili amsaidie! Na kwa ajili hiyo tukafundisha mambo kadhaa ambayo mtu akiyafanya – yanaweza kumpa nafasi Yesu amsaidie mtu huyo atoke na ashinde dhiki alizonazo!

Tabora mjini tulipokuwa na semina hapo baada ya kutoka Shinyanga mjini tulikuwa na somo lenye kichwa kilichosema: “ Mjue sana Mungu ili ufanikiwe katika maisha”.

Mistari miwili ilituongoza katika kufundisha somo hili: Ayubu 22:21 unaosema: “Mjue sana Mungu ili uwe na amani; ndivyo mema yatakavyokujia”. Na ule wa Danieli 11:32b unaosema: “……lakini watu wamjuao Mungu wao watakuwa hodari,na kutenda mambo makuu”.

Mambo matatu ya msingi tulitaka watu wayajue katika somo hili:

Jambo la Kwanza: Kwamba kuna viwango mbalimbali vya kumjua Mungu na vinasababisha viwango tofauti-tofauti vya mafanikio katika maisha ya watu.

Jambo la Pili: Kwamba unapomjua Mungu kwa kiwango kipya,kuna jambo linaloongezeka katika maisha yako ambalo hukuwa nalo kabla hujamjua Mungu kwa kiwango hicho kipya, - na maisha yako yanakuwa bora zaidi kuliko mwanzo.

Jambo la Tatu: Kwamba kuna mambo kadhaa ambayo biblia inafundisha ya kuwa mtu anaweza kuongeza kiu ya -, na kiwango cha-, kumjua Mungu katika maisha yake.

Semina iliyofuata tuliyoifanya Kigoma mjini tulifundisha somo lililosema: “Kuishi kwa imani maana yake nini?”

Lengo la somo hilo lilikuwa si tu kwamba mtu ajue maana ya kuishi kwa imani, bali pia apate kujifunza namna ya kuishi kwa imani.

Tunasoma katika biblia ya kuwa “Mwenye haki ataishi kwa imani yake,” (Habakuki 2:4 na Warumi 1:17).

Tulilitazama jambo hili kutoka maeneo mbalimbali. Kwa mfano, tulijifunza juu ya kuishi kwa imani:

·         Kama kuishi maisha yako ya sasa kwa kutegemea neno la Mungu linasema nini juu ya hali yako ya baadaye;

·         Kama kuishi kwa matarajio ya kuwa alichosema Mungu katika neno lake juu ya maisha yako ndivyo kilivyo na ndivyo kitakavyokuwa;

·         Kama kuishi kwa kuunganisha maisha yako ya sasa na ya baadaye kwa kutumia neno la Mungu;

·         Kama kuishi kwa kuunganisha kitendo unachofanya sasa na matokeo unayotaka yatokee katika maisha yako ya baadaye.

Mistari ya biblia iliyotuongoza kutafakari kuishi kwa imani kwa jinsi hiyo ni Waebrania 11:1 unaotupa maana ya imani; na Warumi 10:17 unaotupa chanzo cha imani, na Yakobo 2:26 unaotueleza umuhimu wa kuonyesha imani yako kwa njia ya kitendo unachofanya; na Waebrania 11:6 unaotueleza ya kwamba haiwezekani kumpendeza Mungu pasipo imani.

Kila Semina ilimzalia
Mungu matunda

Umeona jinsi ambavyo masomo yalivyokuwa tofauti kwa kila semina? Pamoja na utofauti huo ambao uliweka uzuri wa aina yake ndani ya kila semina, bado tuliona Mungu akiokoa, akiponya na akijaza watu Roho wake Mtakatifu!

Jumla ya watu 4248 waliokoka katika semina zote tano. Na waliokoka kwa staili na mfumo tofauti-tofauti. Wengine waliokoka kabla ya neno, wengine waliokoka wakati wa shuhuda za uponyaji, wengine waliokoka baada ya neno, wengine waliokoka wakati wanaombewa ujazo wa Roho Mtakatifu, na wengine waliokoka wakati hema linabomolewa baada ya semina!

Tunamshukuru Mungu kwa matunda hayo na tunaamini utaungana nasi katika kuwaombea ili waukulie wokovu bila kurudi nyuma.

Tena kila semina tuliwaombea watu ujazo wa Roho Mtakatifu.; na Mungu akatusikia na akawajaza Roho Mtakatifu na kuwawezesha kunena kwa lugha mpya!

Jina la Yesu
Lilitukuzwe saana!

Jina la Yesu lina nguvu sana! Tunamshukuru Mungu kwa kutupa nafasi ya kulitumia, kulitangaza na kuona matokeo yake!

Katika semina hizo watu  walifunguliwa toka katika vifungo vya shetani, na wengi pia waliponywa magonjwa kwa jina la Yesu.

Tukiwa Mwanza kijana mmoja alishuhudia jinsi ambavyo alikuwa bubu kwa miezi mitatu na wakati wa semina tuliyoifanya hapo alipona na akaanza kuongea vizuri tu kama kawaida!

Shinyanga mjini tulifuatwa na mzee mmoja siku ya Jumatatu baada ya semina kuisha; na akatuambia ya kuwa ametokea kijijini na ametembea kwa miguu kilomita saba kuja kuhitaji maombi – kwa sababu mke wake alipona kwenye semina jana yake tatizo la kibofu cha mkojo! Ushuhuda wa uponyaji wa mke wake ulimfanya naye amtafute Yesu ili amponye!

Tukamwombea na yeye apone magonjwa aliyokuwa nayo na Mungu akamponya.

Hizi ni shuhuda chache tu – lakini kila semina tuliombea wagonjwa na wengi walipona na kushuhudia uponyaji katika miili yao.

Siku moja katika semina ya Shinyanga walifunguliwa watu wasiopungua 54 kutoka kwenye nguvu za giza!

Semina zinazofuata ni Arusha mjini tarehe 13 – 20 Agosti 2006 katika Kiwanja cha Reli, halafu tarehe 24 – 27 Agosti 2006 tutakuwa Marangu TTC katika kiwanja chao cha mpira, na Tukuyu mjini tarehe 6 – 10 katika kiwanja cha mpira.

UNATAKA KUOKOKA?
Kama unataka kumpa YESU maisha yako sasa, bonyeza hapa
©2003 Tanzania Social and Economic Trust.  All Rights Reserved.