|
|
| ||
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
(Ripoti ya Semina ya Arusha 15 – 22 Februari 2004) - Christopher na Diana Mwakasege - Utangulizi Tunapoikumbuka semina hii, tunabaki kumtukuza Mungu kwa namna ambayo si rahisi kujieleza vizuri kwa maneno tuliyonayo. Kila semina tunayoifanya mahali po pote ina upekee wake; na kwa sababu hiyo ndani ya mioyo yetu tunajawa na shauku kila wakati kutaka kujua kile ambacho Mungu anakifanya. Semina ya Arusha tuliifanya tarehe 15 – 22 Februari 2004 ndani ya hema tuliyoisimika katika kiwanja cha mpira cha shule ya sekondari ya Arusha – Meru. Mahudhurio yalikuwa makubwa sana. Tulikuwa na watu kati ya 15,000 hadi 20,000 waliokuwa wanahudhuria kila siku. Ila siku za mwisho za Jumamosi na Jumapili watu waliongezeka sana hadi kufikia wastani wa watu 30,000! Somo lililofundishwa! Somo tulilofundisha lilikuwa na kichwa kinachosema; “ Mbinu za Kulitumia Jina la Yesu”. Somo hili lilikuwa na mambo mengi mazuri sana, na haitakuwa rahisi kukueleza kila jambo katika makala hii fupi. Ila tunawiwa ndani yetu kukushirikisha angalau mambo kadhaa ambayo tunaamini yatakupa picha ya ‘utamu’ wa somo ulivyokuwa. Mstari wa biblia tuliopewa ili kutuongoza katika somo hili ni huu wa Wakolosai 3:17 unaosema:
“ Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote Mambo ya msingi tuliyojifunza yaliangukia katika haya yafuatayo: La Kwanza: Tulijiuliza maswali yafuatayo: Unawezaje kufanya yote katika Jina la yesu bila kuzijua mbinu mbalimbali za kulitumia? Je, Jina la Yesu linahusika kwa kiasi gani katika yote unayofanya? Je, Jina la Yesu lina sehemu gani katika maisha yako ya kila siku? Je, unaona matokeo ambayo biblia inasema yatatokea unapolitumia jina la Yesu Kristo? Labda umetumia majina mengine mengi ili upate msaada na bado hujapata – je, umejaribu kulitumia jina la Yesu Kristo? Na baada ya kulitumia hili jina la Yesu Kristo, umepata matokeo gani? La Pili: Unahitaji angalau kwa uchache mambo yasiyopungua matano ili uweze kulitumia Jina la Yesu kwa mafanikio makubwa– kwa ajili yako na kwa ajili ya wengine. Mambo haya matano ni 1. Uhalali wa kulitumia Jina la Yesu; 2. Imani katika Jina la Yesu unapolitumia; 3. Mamlaka uliyonayo katika kulitumia Jina la Yesu; 4. Upako wa Roho Mtakatifu katika kulitumia Jina la Yesu; na 5. Mbinu za kulitumia Jina la Yesu Kristo. La Tatu: Unaweza ukapata msaada wa Jina la Yesu bila ya wewe kujua mbinu ya kulitumia. Lakini ni vizuri upate mtu anayejua mbinu za kulitumia Jina la Yesu ili akusaidie. Kwa mfano, tuliona ya kuwa si lazima uwe daktari ili kupata msaada wa kidaktari; au, si lazima uwe dereva ili upate msaada wa gari; au, si lazima ujue kupika ili upate chakula! La Nne: Kwamba somo hili halikulenga kumsaidia kila mtu, ila ni kwa wale ambao walikuwa wanataka kulitumia Jina la Yesu kwa mafanikio – kwa ajili yao wao wenyewe, na kwa ajili ya wengine. Mbinu za kulitumia Jina la Yesu Kwa muda wa siku saba mfululizo tuliweza kujifunza mbinu tano za kulitumia Jina la Yesu. Mbinu hizo ni (1) Kulitumia jina la Yesu kama funguo; (2)Kulitumia jina la Yesu kama sadaka; (3) Kulitumia jina la Yesu kwa kuamuru kutokee kitu unachotaka kitokee; (4) Kulitumia jina la Yesu kama silaha, na (5) Kulitumia jina la Yesu kama kiungo kwa ajili yako na malaika wa Mungu. Siku ile ya mwisho wa semina – siku ya nane tulijifunza jambo hili ya kwamba: Ili kutatua tatizo moja unaweza ukahitaji mbinu za kulitumia jina la Yesu zaidi ya moja. Hii ilikuwa muhimu tujifunze kwa sababu, kwa mfano, funguo peke yake haiwezi kufungua mlango uliofungwa kwa funguo pamoja na kubanwa kwa komeo. Lazima utahitaji mbinu zaidi ya moja ili kuufungua huo mlango! Katika Jina la Yesu maana yake nini? Kama tulivyotangulia kukwambia ya kuwa mstari wa biblia uliokuwa unatuongoza katika semina hii ni ule wa Wakolosai 3:17 unaosema: “Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu baba kwa yeye” Kwa sababu ya mstari huu ulivyo ilibidi tujifunze maana yake nini neno hili “fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu….” Tuliona ya kuwa neno hili linaweza kuwa na maana ya fanyeni yote katika uwepo wa Yesu kwa mantiki ya Mathayo 18:20. Lakini pia linaweza kuwa na maana ya kufanya yote kwa lengo la kuona jina la Bwana Yesu linatukuzwa au kwa lengo la Mungu ajulikane. Hii ni kwa mantiki ya Wafilipi 2:11 au, neno hilo linaweza pia kuwa na maana ya fanyeni yote kama vile unamfanyia Bwana, hii ni kwa mantiki ya Wakolosai 3:23-24. Au, neno hilo linaweza pia kuwa na maana ya fanyeni yote kwa kibali/mamlaka ya Bwana Yesu. Hii ni kwa mantiki ya Matendo ya Mitume 4:5-7. Au, pia linaweza kuwa na maana ya fanyeni yote kwa heshima ya Bwana Yesu. Hii ni kwa mantiki ya Wafilipi 2:9,10. Mungu alishuhudia pamoja nasi! Mwandishi wa Waebrania 2:3,4 anasema: “Sisi je! tutapataje kupona, tusipojali wokovu mkuu namna hii? Ambao kwanza ulinenwa na Bwana, kisha ukathibitika kwetu na wale waliosikia; Mungu naye akishuhudu pamoja nao kwa ishara na ajabu na nguvu za namna nyingi, na kwa magawanyo ya Roho Mtakatifu, kama alivyopenda mwenyewe” Mungu alishuhudia pamoja nao wale waliokuwa wanatangaza habari za wokovu. Mungu alishuhudia pamoja nao au alitenda kazi “pamoja nao kwa ishara na ajabu na nguvu za namna nyingi, na kwa magawanyo ya Roho Mtakatifu….” Hii ndio neema ambayo na sisi tuliiona katika semina hii ya Arusha. Tulimwona Mungu akishuhudu pamoja nasi kwa ishara na ajabu na nguvu za namna nyingi, na kwa magawanyo ya Roho Mtakatifu, kama alivyopenda mwenyewe! Hali hii ya uwepo wa Mungu ilijenga mazingira yaliyofanya maelfu na maelfu ya watu wamiminike kiwanjani kwenye semina kila siku kwa siku zote nane. Ilikuwa ni kiu ya ajabu! Kwa mfano katika siku ile ya nane ya semina ambayo ilikuwa ni Jumapili – kiwanja kizima cha mpira kilikuwa kimejaa watu kuanzia mapema ya saa sita na nusu mchana! Unaelezaje kuwepo kwa maelfu ya watu ambao wamejaa uwanjani kuanzia mapema namna hiyo – wanamsubiri nani? Haiwezekani ya kwamba walikuwa wanamsubiri mwanadamu! Tunaamini walikuwa wana hamu kubwa ya kukutana na Yesu ambaye jina lake tulikuwa tunalifundisha katika semina hiyo. Hakika tunaweza kusema kama ilivyoandikwa katika Yohana 2:23 ya kuwa “watu wengi waliamini jina lake, walipoziona ishara zake alizozifanya”. Na ndivyo ilivyokuwa, maana mwisho wa semina tulijikuta tumeandikisha majina 7100 ya watu waliomwamini Bwana Yesu na kuokoka! Watu wengi waliokuwa wagonjwa walisimama na kushuhudia jinsi ambavyo Mungu amewaponya. Ilikuwa furaha ya ajabu! Kuna waliopona wakati wa semina, na kuna waliopona wakisikiliza kipindi cha semina kulichokuwa kikitangazwa na radio sauti ya injili. Mvua iliyonyesha hakuogopesha watu! Kipindi hicho cha semina kiliambatana na mvua ambazo kwa jinsi zilivyokuwa zinanyesha ungetegemea watu waogope kuhudhuria semina hiyo. Lakini tuliona jinsi kiu waliyokuwa nayo ilivyozidi hofu ya kunyeshewa kiasi kwamba watu waliendelea kuja tu kwenye semina kwa maelfu. Siku ya mwisho wa semina (Jumapili) mvua ilianza kunyesha kwa nguvu sana na kwa wingi tulipokuwa tumemaliza maombi ya wagonjwa na kuanza kushuhudia kwa wale waliopona. Wakati huo tulikuwa hatujasikia neno bado. Mvua hiyo ilianza kunyesha saa 10 na dakika tano na iliendelea kunyesha kwa saa nzima bila kupungua. Wako baadhi ya watu wachache walioondoka, lakini maelfu ya watu waliokuwa bado wamejaa kiwanja kizima walibaki na kukaa hapo wakati wote wa mvua hiyo. Watu hao walikaa makundi makundi chini ya mahema huku wakiimba na kumsifu Mungu kwa nguvu na kwa furaha. Wakati watu wengine walipokuwa wanaimba – wengine walikuwa wakiendelea kuomba. Nguvu za Mungu zilikuwa nyingi kiasi ambacho mapepo yalikuwa yanajidhihirisha na kuwatoka watu wakati huo huo! Mama mmoja aliyekuwa ana maumivu ya miguu aliamua kuondoka uwanjani kwa haraka kwa hofu ya kuloa. Lakini alipofika nyumbani alijikuta Mungu amemponya na maumivu katika miguu yake yameondoka! Akawa na furaha kuu na akatuma ujumbe kwa simu uwanjani juu ya uponyaji huo. Mvua ilipokwisha tukaendelea na shuhuda na tukafundisha neno – na watu wengi wakaokoka tulipowahimiza kufanya hivyo.
Sisi tunamshukuru Mungu sana kwa yale aliyoyafanya katika
semina hiyo ya ajabu. Sifa na heshima ni zake maana ndiye anayestahili
kusifiwa. |
|