Yesu Akamwambia "Lisha Kondoo Zangu" (Yohana 21:17)
Home
Maombi
Ratiba
Shuhuda
Mafundisho
Maswali na Majibu
Barua za Mwezi
Kuchangia Huduma
RIPOTI YA KIGOMA


Ripoti ya semina ya Kigoma ya tarehe 10 – 13 Julai 2003

 

MGUSO MPYA WA ROHO MTAKATIFU KIGOMA

Utangulizi:

          Hii ni semina ya pili baada ya kuifanya nyingine mwaka jana (2002) katika mfululizo wa semina za neno la Mungu tunazoendelea kuzifanya mkoani Kigoma. Katika semina zote hizi mbili tulikuwa tumeongozana na wenzetu katika timu ya huduma ambao wengine ilikuwa ni mara yao ya kwanza kabisa kufika mkoani Kigoma.

          Kwa mtu ambaye hajawahi kufika Kigoma mara nyingi anasikia habari ambazo si nzuri juu yake. Habari zingine zinazosikika juu ya Kigoma zimewatia hofu watu wengine kiasi cha kusita kwenda kuhudumu mkoani Kigoma.

          Lakini jambo la kushangaza ni kwamba kila tunapokwenda Kigoma tunakuta mazingira katika ulimwengu wa roho ambayo ni mepesi kuliko mikoa mingi tuliyowahi kupita. Kigoma kuna uwepesi wa kufanya maombi; kuna wepesi wa kuhubiri na kufundisha neno! Kuna utulivu fulani ambao mtumishi wa Mungu anaupata rohoni mwake ambao ni vigumu kupata maneno ya kuelezea.

          Unapofika na ukiwa Kigoma inakuwa kama mtu uliyeingia katika eneo lililotekwa tayari na Bwana lakini watu wa Mungu hawajajua! Tunataka kuwatia moyo watumishi wengine ya kuwa Mungu akikutuma kwenda Kigoma kumtumikia – usisite, bali nenda kwa moyo ulio tayari kuyaona matendo makuu ya Mungu na ushindi uliowazi!

Somo

          Bwana Yesu alitupa somo kwa ajili ya semina hii lenye kichwa kinachosema; “ NANYI MTAPOKEA NGUVU ZA ROHO MTAKATIFU – kwa ajili ya nini?” Tunataka tukuambie pia ya kuwa kila semina ina lengo lake. Mungu huwa anatueleza lengo la kila semina anayotuongoza kuifanya ili tuweze kuwepa mkazo wa mafundisho na maombi wa kulifikia hilo lengo. Kwa semina hii ya Kigoma Mungu alitueleza ya kuwa lengo la semina ni kuona watu wanaongezewa hamu au kiu ndani yao ya kupokea nguvu za Roho Mtakatifu na kuzitumia.

          Kati ya jambo linalosumbua kanisa (yaani mwili  wa Kristo) na hata wakati mwingine kuleta kutokuelewana ni juu ya nafasi ya Roho Mtakatifu katika maisha ya kila siku ya mkristo. Si wakristo wengi walio na hamu ya kupokea nguvu za Roho Mtakatifu. Hii inatokea si kwamba hawazitaki nguvu hizi, bali ni kwa sababu hawazijui faida zake!

          Neno lililokuwa ni msingi wa somo katika semina hii lilikuwa ni Matendo ya Mitume 1:8 linalosema: “Nanyi mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.”

          Yesu alisema “ mtapokea ….” Akitaka tujue ya kuwa katika Roho Mtakatifu kuna kupokea. Na jambo mojawapo tunaloweza kupokea toka kwa Roho Mtakatifu ni nguvu za Mungu. Lakini wote tunajua ya kuwa si kawaida mtu kupokea kitu usichokitaka, na hata ukilazimishwa kukipokea unaweza usikitumie. Pia, huwezi kupokea na kukitumia ipasavyo kitu usichojua faida yake au kazi yake.

          Vivyo hivyo na Roho Mtakatifu. Huwezi kuwa na kiu ya kupokea nguvu zake kama hujui faida zake na kazi zake. Katika semina hii tuliangalia faida tatu za kupokea nguvu za Roho Mtakatifu. Tuliziangalia tatu tu kwa sababu ndizo tulizoweza kujifunza kwa muda tuliokuwa nao wa siku nne – lakini biblia inaelezea faida zaidi ya tatu za kupokea nguvu za Roho Mtakatifu.

          Tulijifunza ya kuwa unapopokea nguvu za Roho Mtakatifu zinakusaidia:

  1. Uwe shahidi wa Yesu kusimama upande wake na kuthibitisha ya kuwa aliyoyasema ndiyo kweli inayotakiwa kuaminiwa na kila mtu. Soma Matendo ya Mitume 1:8.
  2. Uwe tajiri (yaani upate kila unachokihitaji) kwa ajili ya kuliimarisha agano lake kwa wanadamu. Soma Kumbukumbu ya Torati 8:18.
  3. Uwe jasiri – usiwe mwoga katika kumtumikia Mungu! Soma 2Timotheo 1:7. Woga unaweza kukufanya usitumie kipawa alichokupa Mungu ipasavyo; na unakufanya usiitumie nafasi Mungu anayokupa ipasavyo.

Shuhuda za Uponyaji

Tulishuhudia Mungu akifanya mambo makuu katikati ya watu wake – kama ilivyo kawaida yake. Haitakuwa rahisi kukushirikisha yote yaliyofanyika katika ripoti hii fupi – lakini tutajitahidi kukupa shuhuda chache.

          Kuna mama mmoja ambaye alikuwa amesumbuliwa na uti wa mgongo kwa muda wa miaka mitano kiasi cha kushindwa kuinama vizuri. Hospitali alipokwenda kupimwa aliambiwa kuna baadhi ya mifupa katika uti wa mgongo iliyoikuwa imepishana. Wakati wa maombi tulimwambia anyooshe mikono yake yote mbele ili tuone kama inapishana – na kweli ilikuwa imepishana. Mkono mmoja ulikuwa mfupi kidogo. Tulimwombea na kila aliyekuwa karibu aliona mkono mfupi ukikua na kufanana urefu na mkono mwingine na mara hiyo maumivu ya mgongo yakatoweka! Na aliweza kuinama na kuinuka bila shida – jambo ambalo alikuwa hajawahi kulifanya kwa muda wa miaka mitano iliyopita. Ni kweli rehema za Mungu ni kubwa!

          Mama mwingine alikuwa na uvimbe upande wa chini wa tumbo kwa muda mrefu, na ambao ulikuwa unaongezeka. Baada ya maombi uvimbe huo ulitoweka na akashuhudia jambo hilo mbele ya kusanyiko lililokuwepo hapo. Ndiyo! Jina la Yesu linaponya!

          Baada ya neno la maarifa tulilosema juu ya kuwa kuna watu wanaosumbuliwa na ugonjwa wa tumbo unaoletwa na mdudu aitwaye ‘amoeba’ – akina mama wawili walijitokeza. Tuliwaombea na Mungu akawaponya hapohapo – maumivu ya tumbo yaliyowasumbua muda mrefu yalinyamaza!

          Dada mwingine alisimama kushuhudia juu ya muujiza alioupata wakati wa maombezi ya wagonjwa. Alisema alikuwa anasumbuliwa na matatizo ya meno yaliyokuwa yanauma na yalikuwa yametoboka. Aliendelea kusema ya kuwa baada ya maombi maumivu yalinyamaza na aliporudi nyumbani aliweza kula kwa kutumia upande wa mdomo ambao alikuwa hautumii kwa kuwa meno yalikuwa yametoboka. Na aliweza kula bila kupata shida wala maumivu. Jina la Yesu libarikiwe kwa jinsi anavyoponya magonjwa mbalimbali ya watu wake!

          Na mtu mwingine ambaye alikuwa anapata maumivu akilalia upande wake wa kushoto alipokea uponyaji katika maombezi ya wagonjwa katika semina hiyo. Akasema kwa mara ya kwanza katika muda wa miaka mingi ameweza kulalia upande wa kushoto usiku bila kupata maumivu.

          Wako na wengine waliopokea uponyaji katika miili yao – lakini shuhuda hizi chache zitoshe kukuonyesha ya kuwa Mungu alikuwa pamoja nasi akilithibitisha neno lake alilotupa kwa ishara na miujiza iliyofuatana nalo.

Mguso mpya!

          Ndicho tunachoweza kusema juu ya yale ambayo tuliona Mungu akifanya katika semina hii ya Kigoma, Roho Mtakatifu alipowashukia watu waliokuwepo pale. Hakika ni mguso mpya!

          Tuliona watu waliokuwa na kiu kubwa ya kuona Mungu anawagusa upya kwa uwezo wa Roho Mtakatifu katika maisha yao. Na Mungu wetu alivyo mwaminifu hakusita kuwasaidia  – bali aliwajaza nguvu za Roho Mtakatifu kwa uwingi sana. Baada ya semina kumalizika Mchungaji mmoja aliyehudhuria semina hiyo alisema; “ Mungu ameamua kutupa watu wa Kigoma siku ya Pentekoste ya kwetu”!

          Tuna uhakika aliyasema haya akilinganisha yale yaliyotokea Kigoma wakati wa semina na yale yaliyotokea siku ya Pentekoste ambapo biblia inaelezea yaliyowafika wale watu 120 waliokuwa wamekusanyika. Maana Biblia inasema: “ Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka” (Matendo ya Mitume 2:4)

          Ndivyo ilivyotokea Kigoma wakati wa semina hii – watu wengi walijazwa Roho Mtakatifu na kunena kwa lugha mpya kwa mara ya kwanza. Lakini hata wale waliotaka mguso mpya ili kuhuisha maisha yao ya wokovu – hasa katika kupata nguvu mpya za maombi – pia Mungu aliwahudumia.

 

Kigoma mpya inakuja

          Ndivyo Mungu alivyotuonyesha na ndivyo tunaamini itakavyokuwa. Ingawa kwa jinsi ya nje si rahisi kuona tofauti yo yote inayoweza kutokea kwa Kigoma hivi karibuni. Lakini tunamwamini Mungu aliye hai! Kuna mabadiliko mazuri yanakuja kwa ajili ya Kigoma. Wakati wa semina ulishuka upako wa kinabii ambao ndani yake Mungu alitupa kuona na kusema juu mabadiliko mazuri ambayo ameyakusudia kwa ajili ya Kigoma na watu wake.

          Alituonyesha huduma na makanisa wakifanya kazi kwa umoja zaidi kuliko zamani. Alituonyesha idadi ya watu wakiongezeka makanisani na makanisa yakipanuliwa ili kukalisha watu wanaoongezeka kwa Bwana. Mungu alituonyesha pia huduma za watu zilizokuwa zimekufa na zingine kupoa – zikifufuliwa na kuhuishwa kwa upya na kwa nguvu. Mungu alituonyesha uchumi wa Kigoma ukibadilika na kuwa mzuri na mji wa Kigoma kupendeza na kushamiri zaidi kibiashara.

          Haya ni baadhi tu ya yale tuliyoonyeshwa na yapo mengi ambayo hatusikii uhuru ndani yetu kuyaandika lakini tuliwaeleza waliokuwepo pale Kigoma. Lakini zaidi ya yote muujiza ulio mkubwa ni watu wapatao 300 waliokoka katika semina hii na kumpa Yesu maisha yao

Shukrani

          Tunamshukuru kila mtu aliyetuombea na anayetuombea katika semina hizi ambazo Mungu ametupa kuzifanya. Pia, tunamshukuru kila mtu aliyetoa fedha zake na muda wake kuifanikisha semina ya Kigoma. Tunaamini baraka za Bwana zitazidi kuwafanikisha katika kila watendalo katika Kristo Yesu.

          Tuzidi kuombeana. Semina inayofuata ni Moshi tarehe 26 Julai had 3 Agosti 2003 ndani ya hema katika viwanja vya mashujaa. Karibu uhudhurie ukiweza. Usipoweza tuombee.

UNATAKA KUOKOKA?
Kama unataka kumpa YESU maisha yako sasa, bonyeza hapa
©2003 Tanzania Social and Economic Trust.  All Rights Reserved.