|
KAMA SI MUNGU -
KILIMANJARO NA WASEME!
[Siku
16 za Miujiza na semina ya Neno la Mungu – Moshi Tarehe 12 –
27 Januari 2003]
Katika Zaburi 124:1
tunasoma maneno haya, “Kama si Bwana aliyekuwa pamoja nasi,
Israeli na aseme sasa.” Haya ni maneno ambayo mfalme Daudi
aliyasema ili kuweka wazi jinsi mkono wa Mungu
ulivyojidhihirisha katikati ya taifa la Israeli. Na sisi tunaona
tuandike kichwa hiki kwa ajili ya ripoti hii kinachosema; “Kama
si Mungu Kilimanjaro na waseme!” Tumeona na sisi tutumie
maneno haya kama ya mfalme Daudi ili kueleza kile ambacho
kimetokea katika siku zote 16 za semina ya Neno la Mungu
tuliyoifanya Moshi mjini katika viwanja vya mashujaa tarehe
12-27 Januari 2003.
Mahudhurio
Mahudhurio ya watu katika semina yalikuwa makubwa kuliko
tulivyotarajia; kwa hiyo maandalizi yake hayakuweza kukidhi
maelfu ya watu waliohudhuria. Tunasema hili kwa kuwa tulikuwa na
hema lenye uwezo wa kukalisha watu 15,000 na tukaweka viti
vilivyokuwa na uwezo wa kukalisha watu 12,000; bado kuna maelfu
ya watu waliokuwa wanasimama ndani na nje ya hema – hasa siku
za Jumamosi na Jumapili!
Watu walitoka karibu katika wilaya zaote za mkoa wa Kilimanjaro,
na wako waliokuwa wanahudhuria toka Arusha mjini kila siku
– kwa siku zote 16! Tunamshukuru Mungu sana kwa wenye mabasi
ambao walijikuta wakibadili utaratibu wao wa kila siku wa
kusafirisha abiria, na badala yake kujikuta wanaleta watu kwenye
viwanja tulipofanyia semina, na kuwasubiri watu kila siku jioni
hapo hapo uwanjani.
Masomo
Mungu alitupa utaratibu na mpangilio wa vipindi kwa namna
ambavyo siku 16 zilionekana chache! Tunaamini kabisa yakuwa
uwepo wa Roho Mtakatifu ndio uliofanya siku ambazo zilikuwa
zinaonekana nyingi – zionekane chache! Wiki ya kwanza
tulifundisha somo linalosema “USIMZUIE YESU KUKUSAIDIA”.
Wiki ya pili tulifundisha juu ya majaribu, tukilenga juu ya .
“LAKUFANYA UNAPOSONGWA NA MAJARIBU”. Masomo haya
tulifundisha vipindi vya jioni.
Siku ya pili ya semina tuliwafundisha jinsi ambavyo mtu anaweza
kumzuia Yesu asimsaidie kwa kuamua kumchanganya Mungu na miungu
mingine katika maisha yake. Inajulikana wazi ya kuwa sehemu
kubwa ya watu wa Kilimanjaro ni wakristo; lakini pia bado wana
tabia ya kufanya matambiko kwa mizimu ya babu zao. Lakini, pia,
kuna baadhi yao wamekuwa wakienda nje ya Kilimanjaro kununua
uchawi hasa kwa ajili ya ‘kujilinda’ na kusaidiwa kupata ‘mali’.
Tuliwaonyesha jinsi biblia inavyokataza mchanganyo huu na
madhara yake kwao, kwa ardhi, na kwa watoto wao, ikiwa
hawatatubia uovu huu.
Tunamshukuru Mungu kwamba wengi walitubu kwa ajili yao na kwa
ajili ya familia zao; huku wakileta ‘hirizi’ na
‘bangili’ za matambiko, ambavyo vyote vilichomwa moto katika
Jina la Yesu!
Wakati wa asubuhi tulikuwa tunaombea nchi yetu hasa katika
wiki ile ya kwanza. Katika wiki ya pili watu walifundishwa juu
ya “ufuasi na ufuatiliaji” na walimu toka ofisi ya ‘Life
Ministry’ ya Arusha.
Maelfu
Waokoka!
Inakisiwa na kamati ya maandalizi ya kuwa kiasi cha wastani wa
watu 7000 walimpa Yesu maisha yao na kuokoka katika siku hizo 16
za semina. Makisio haya yalifikiwa baada ya kuona ya kuwa kadi
zote 6000 zilizotengenezwa kwa ajili ya kuwaandikisha wanaookoka
zilikwisha!
Lakini zaidi ya hayo siku ya 15 ya semina ambayo ilikuwa na
mahudhurio makubwa kuliko siku nyingine (kati ya watu 16,000
hada 20,000 inakisiwa walikuwepo uwanjani) – watu waliokoka
awamu mbili. Roho Mtakatifu alituongoza kuita watu mbele waokoke
kabla ya neno (awamu ya kwanza) na baada ya neno (awamu ya pili).
Siku hiyo maelfu ya watu waliokoka kiasi ambacho wahudumu
walizidiwa na wingi huo na hawakuweza kuwaandika wote waliookoka
siku hiyo. Sifa zote ni kwa Yesu Kristo! Tunaamini utaungana
nasi kumshukuru Mungu kwa hili, na kuwaombea wote waliookoka
katika semina hii wasimame katika wokovu na kuendelea kwa
ushindi ndani ya Yesu!
Miujiza!
Katika semina hii wagonjwa wengi sana walipona kwa nguvu za Jina
la Yesu! Kwa sababu ya muda tuliokuwa nao kutokutosha, si wote
waliopona waliopata nafasi ya kushuhudia wakati semina
ikiendelea. Lakini kwa wale walioshuhudia tuliona na kusikia
mambo ya ajabu sana na yenye kumtukuza Mungu sana.
Wakati huu baada ya kumaliza semina tunapokumbuka yaliyotokea
tunaona ya kuwa kuna siku wagonjwa wa aina Fulani walikuwa
wanapona wengi kuliko wengine! Kwa mfano, kuna siku walijitokeza
watu watatu mfululizo wote wakishuhudia kupona na kufunguliwa
sikio la kushoto na kuweza kusikia tena. Siku nyingine
walijitokeza watu mfululizo waliokuwa na shida za macho na
kutoona, na wengine kutosoma vizuri. Hao nao wakashuhudia jinsi
Bwana Yesu alivyowaponya.
Siku nyingine tena tukaona watoto na vijana kadhaa, walishuhudia
wakiongozana na ndugu zao jinsi walivyopona magonjwa ya akili.
Kijana mmoja alikuwa amechanganyikiwa akili toka mwaka 1997, na
aliletwa kwenye semina na kijana mwenzake. Wote walikuwa
hawajaokoka. Lakini wakati wa semina yule kijana aliyekuwa na
tatizo la kuchanganyikiwa akili alipona, kisha wote wawili
wakaokoka na kujazwa Roho Mtakatifu! Jina la Yesu libarikiwe
sana!
Tulishuhudia pia ‘wingu’ au ‘upako’ wa Roho Mtakatifu
ukiwaponya watu kadhaa waliokuwa wamepata shida ya mifupa
kuvunjika katika ajali mbalimbali. Kwa mfano mtu mmoja alisema
alipopata ajali alipelekwa hospitali kwa matibabu lakini hata
baada ya kupona mguu haukuunga vizuri, na ukawa mfupi kidogo.
Kwa hiyo akawa hatembei vizuri kwa kunyooka. Wakati wa maombi
katika semina, Bwana Yesu alimponya na kurefusha mguu wake
uliokuwa mfupi – na akaweza kutembea vizuri kama vile mtu
ambaye hakuwahi kupata ajali!
Tunaweza kuendelea kuandika juu ya miujiza hii – lakini nafasi
haitatosha. Lakini pia itakuwa siyo vizuri kutokukwambia jinsi
Mungu alivyowatembelea watoto waliokuwa na shida mbalimbali.
Kuna waliokuwa wamepagawa mapepo kishirikina waliyofunguliwa!
Kuna mama aliyeshuhudia jinsi mtoto wake alivyoweza kuanza
kutembea baada ya kutotembea tangu kuzaliwa! Mtoto mmoja wa
miaka 10 alijitokeza kushuhudia jinsi ambavyo Mungu amemponya na
tatizo la kukojoa kitandani lililokuwa limemsumbua miaka mingi.
Tunaona tukushirikishe pia ya kuwa katika siku za wiki ya kwanza
ya semina hii dada mmoja alishuhudia jinsi Mungu
alivyomponya ukimwi katika semina tuliyoifanya hapo hapo Moshi
mjini mwezi wa nane mwaka 2002. Alisema baada ya semina alirudi
hospitali kupima tena ambako walimkuta hana ukimwi tena!
Radio!
Ili kuwafikia watu wengi wakati wa semina, kila siku usiku
tulikuwa tunarusha radioni mafundisho tuliyofundisha mchana
uwanjani. Radio iliyotumika ni ya ‘Sauti ya Injili Moshi’.
Tunaamini Mungu aliwafikia maelflu ya watu pia kwa njia hii.
Maana radio hii inasikika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Tanga.
Kwa mfano kuna mama aliyejitokeza kushuhudia wakati wa wiki ya
mwisho ya semina akisema Mungu amemponya ugonjwa wa ‘High
blood pressure’ wakati akisikiliza kipindi chetu cha radio.
Mwingine akaeleza jinsi alivyojikuta amejazwa Roho Mtakatifu na
kunena kwa lugha mpya aliposhiriki maombi kupitia kipindi chetu
cha radioni!
Hospitali
Yatembelewa!
Kwa sababu ya mambo ambayo watu walikuwa wakisimulia ya kuwa
Yesu anayafanya uwanjani, habari hizi ziliwafikia wagonjwa
waliokuwa wamelazwa katika hospitali ya rufaa ya KCMC iliyopo
mjini Moshi. Kwa hiyo wengi wakataka kuja, wengine walituma nguo
zao ili ziombewe halafu warudishiwe, na hata wengine waliwatuma
ndugu zao waje wasimame katika maombi kwa niaba yao. Kuna mama
mmoja ambaye alikuwa na mume wake amelazwa katika chumba cha
wagonjwa mahututi kwa tatizo la kubanwa kifua, kiasi cha
kushindwa kupumua vizuri na kushindwa kuongea vizuri. Huyu mama
alisema alifika katika semina na kila siku wakati wa maombi ya
wagonjwa alisimama kwa niaba ya mume wake aliyekuwa amelazwa
KCMC. Baada ya kusimama kwa ajili ya maombi kwa siku tatu
mfululizo mume wake ‘ghafla’ akafunguka ‘ICU’ na kupona
– na kutolewa arudi nyumbani!
Lakini pia kulikuwa na wagonjwa waliotaka kuja wenyewe kwenye
semina ili waombewe. Kwa sababu ya hali walizokuwa nazo
madaktari walishauri tuombwe tukawaombee huko huko hospitalini.
Tulipoletewa habari hii tukaamua kwenda kuwaombea wagonjwa hao
siku ya Jumapili asubuhi tarehe 26 Januari 2003. Viongozi wa
hospitali walitupokea vizuri na kutuonyesha orodha ya wagonjwa
waliohitaji maombi iliyokuwa na majina zaidi ya mia moja
ishirini. Tulipokuwa tunaongozwa na viongozi hao kuwaombea
wagonjwa hao; ghorofa kwa ghorofa; na chumba kwa chumba,
tuliwaombea hata wale ambao walikuwa hawajaandikisha majina yao
lakini walitaka maombi hayo pia. Siku hiyo hospitali ilikuwa na
wagonjwa 560 waliokuwa wamelazwa – na tulitumia masaa matatu
kuwaombea wote waliotaka maombi katika vyumba mbalimbali vya
wagonjwa vilivyopo hapo hospitalini.
Tulianza kuzungukia na kuwaombea wagonjwa saa 4 asubuhi na
tukamaliza saa 7 mchana ambapo tulipelekwa ‘Chapel’ ya
hospitali ili kuwaombea wagonjwa wengine waliokuwa wamekusanyika
humo. Moja kwa moja tulianza ibada ya kuwaombea wagonjwa na
kuimaliza saa 8.30 mchana. Wagonjwa wengi walipona na wengine
walipata nafasi ya kushuhudia hapo hapo. Pia, waliookoka watu 62
hapo hospitalini wakiwemo wagonjwa na wauguzi wao vile vile.
Mwisho
Kristo ni Yote katika Yote na sifa zote ni zake! Maana yote hayo
na hata yale ambayo hatukuweza kuandika aliyoyafanya yamefanyika
kwa neema na rehema zake. Tunaomba ushirikiane nasi kumshukuru
Mungu kwa ajili ya hayo.
Pia, tunapenda kumshukuru kila mtu aliyetuombea na kuomba kwa
ajili ya semina hii. Na shukrani kwa kila aliyetoa fedha yake,
mali yake na muda wake ili semina hii ifanikiwe. Mungu awabariki
kila mmoja sawasawa na neno lake.
Tunahitaji maombi kwa ajili ya semina zifuatazo: 16
– 23 Februari 2003 (Arusha mjini), 1 – 9 Machi 2003 (Dar es
Salaam) na Tanga mjini tarehe 18 – 23 Machi 2003.
|