Yesu Akamwambia "Lisha Kondoo Zangu" (Yohana 21:17)
Home
Maombi
Ratiba
Shuhuda
Mafundisho
Maswali na Majibu
Barua za Mwezi
Kuchangia Huduma
RIPOTI YA MOSHI - JANUARI 2004


LITUMIE JINA LA YESU KRISTO LIKUSAIDIE

(Ripoti ya Semina tuliyoifanya Moshi mjini 18-25 Januari 2004)

Utangulizi:

Katika semina hii tumeiona tena kwa upya neema ya Bwana Yesu Kristo ikitusaidia! Na pia tumeuona upendo wa Mungu ukitubidisha kuifanya kazi ya Mungu bila kuchoka! Tena, tumeona ushirika wa Roho Mtakatifu ukiifanye kazi iliyo nzito kuwa nyepesi, ili jina la Yesu Kristo lipate kutukuzwa, kwa utukufu wa Mungu Baba aliye juu mbinguni!

Haya yote tuliyashuhudia katika semina ya neno la Mungu tuliyoifanya Moshi mjini tarehe 18-25 Januari 2004. Tulifundisha somo lililokuwa lina kichwa kinachosema: ‘Litumie Jina la Yesu Kristo Likusaidie’. Hii ilikuwa semina ya kwanza kati ya mfululizo wa semina tutakazokuwa nazo mwaka huu – sehemu mbalimbali – ndani na nje ya nchi yetu. Tunashukuru sana kwa kutuombea na pia kutusaidia kwa fedha zako ili kulipa gharama za semina hiyo. Na pia kama ulishiriki kufika katika semina hiyo ya Moshi Mjini tunasema ahsante kwa kuja. Semina zinazofuata ni Arusha Mjini 15 – 22 Februari 2004 katika kiwanja cha mpira cha shule ya Sekondari ya Arusha – Meru. Pia tarehe 2 -7 Machi 2004 tutakuwa na semina Tanga Mjini; na tarehe 22 – 29 Machi 2004 tutakuwa na semina Dar es Salaam.

Mahudhurio makubwa….
…… na maelfu waokoka!

          Tunaposema mahudhurio yalikuwa makubwa, hatuzungumzii mamia ya watu bali maelfu ya watu. Gazeti la ‘Nyakati’ la Jumapili ya tarehe 25 Januari 2004 liliandika ya kuwa katika siku ya kwanza ya semina ilikisiwa ya kwamba watu waliohudhuria semina yetu walikuwa wastani wa watu 20,000! Tuliona watu waliohudhuria karibu kutoka wilaya zote za Kilimanjaro. Lakini pia tuliona watu waliohudhuria kutoka Dodoma na Tanga. Siku ya mwisho ya semina tulishuhudia watu wasiopungua 30,000 wakihudhuria.

          Tunamrudishia sifa na heshima Mungu wetu katika Jina la Yesu Kristo kwa kuwaleta watu wengi namna hiyo kila siku kwa siku nane mfululuzo kujifunza neno la Mungu na kuhudumiwa mahitaji mbalimbali waliyokuwa nayo.

          Watu waliookoka kwa siku zote nane walikuwa wengi sana. Walioweza kuandikwa majina yao walikuwa 6800! Lakini kuna wengi sana pia waliookoka wakati huo huo ambao hawakuweza kuandikwa kwa sababu ya uchache wa wahudumu, kuishiwa na fomu za kujaza, na muda kutokuwa wa kutosha kuwafikia wote na kuwaandika.

          Hebu shirikiana nasi kumshukuru Mungu kwa ajili ya maelfu ya watu hawa waliookoka wakati wa semina, na tuwaombee wasimame na kudumu katika wokovu siku zote za maisha yao. Pia tuwakumbuke wote waliokutana na Yesu wakati wakiisikiliza semina hiyo hiyo kwa njia ya vipindi vya Radio Sauti ya Injili tulivyokuwa tukivirusha kila siku usiku.

Ishara mbili za kukumbuka ….

          Tunataka tukuambie juu ya ishara mbili kubwa zilizotokea wakati wa semina, ambazo ni muhimu sana kuzikumbuka, kuzitakari na kujifunza ndani yake. Ishara ya kwanza ilitokea siku ya tatu ya semina tulipojikuta tunashindwa kufundisha baada ya uwepo wa Mungu kujifunua katika semina na kuufunika mkutano kwa muda wa masaa karibu mawili mazima! Na wakati wote huo tuliona Roho Mtakatifu akiwahudumia watu kwa njia mbalimbali huku wakifunguliwa matatizo waliyokuwa nayo. Tulichojifunza katika ishara hii ni kwamba Mungu anataka muda wa kutosha kuliko tunaompa ili awahudumie watu wake moja kwa moja kwa njia ya Roho Mtakatifu! Kila mtu aliyeokoka ana uwepo wa Mungu katika maisha yake – lakini je huu uwepo wa Mungu tunaupa muda kiasi gani ili utuhudumie mahitaji tuliyonayo?

          Ishara ya Pili ilitokea siku ya mwisho wa semina baada ya mvua iliyokuwa imeanza kunyesha - kuacha kunyesha  mara moja baada ya maelfu ya watu kusimama na kumwomba Mungu mvua hiyo iache kunyesha, ili semina iendelee vizuri. Ingawa tunafanyia semina zetu ndani ya hema lenye uwezo wa kukalisha watu 15,000 – lakini lilikuwa dogo sana kuweza kuwafunika watu wasiopungua 30,000! Kwa hiyo unaweza ukaelewa mioyo yetu ilivyokuwa baada ya kuona mvua imeanza kunyesha wakati ndio mara tu tunaanza kipindi. Lakini tunamshukuru Mungu aliyeinyamazisha mvua hiyo baada ya maombi!

          Katika ishara hii ya pili tulijifunza ya kuwa Mungu yuko tayari kuingilia kati na kubadilisha mazingira na hali zinazotuzunguka zinazoweka pingamizi tusisikie neno la Mungu! Je! Kuna jambo lolote linalokuzuia usiweze kujifunza neno la Mungu vizuri? Usikate tamaa wala usiishie kulalamika tu – bali muombe Mungu abadilishe hayo mazingira yanayosababisha iwe tatizo kwako kusikia na kujifunza neno la Mungu. Tunataka tukutie moyo ya kuwa Mungu atajibu na kukusaidia!

Somo tulilojifunza lilikuwa tamu …..!

          Kila somo ambalo Mungu anawapa watu wake linakuwa tamu ‘kama asali’ mdomoni hasa likiwa limetolewa kwa wakati ule Mungu alioutaka na kwa namna alivyotaka. Roho Mtakatifu huwa anakuwepo na upako wake ili kulifanya hilo somo liwe na utamu wa Ki-Mungu!

          Katika somo tulilojifunza kwenye semina ya Moshi Mjini wakati huu tulikuwa na lengo la kuona watu wanapata uelewa na ufahamu zaidi juu ya kulitumia Jina la Yesu ili liwe la msaada kwao.

          Tulikuwa tunataka semina inapoisha wawe wamepata majibu ya maswali yafuatavyo – ambayo inawezekana hata wewe umewahi kujiuliza wakati mwingine. Kwa mfano:

          Kwa nini wakati mwingine unalitumia Jina la Yesu unafanikiwa, na wakati mwingine ukilitumia hufanikiwi?

          Kwa nini mtu mmoja anaweza akalitumia Jina la Yesu akafanikiwa, lakini mtu mwingine akashindwa kufanikiwa?

          Kwa nini mahali pengine unalitumia Jina la Yesu na unafanikiwa, na mahali pengine hufanikiwi? Kwa nini kuna wakati Jina la Yesu linaambatana na nguvu au upako mwingi, na wakati mwingine nguvu zinazoambatana na Jina hili zinaonekana kuwa kidogo?

          Kwa nini wakati mwingine unalitumia Jina la Yesu kwa jambo fulani na unapata unachotaka ukilitumia Jina hili kwa kutaka kupata jambo jingine?

          Mafundisho tuliyoyatoa wakati wa semina tukijifunza juu ya Jina la Yesu yalisaidia sana kupata majibu ya maswali tuliyoyaorodhesha hapa.

          Kwa muhtasari tu tulijifunza ya kuwa ili uweze kulitumia Jina la Yesu na uone likikusaidie unahitaji angalau (au kwa uchache) mambo matano yafuatayo:

1.      UHALALI wa kulitumia hili Jina la Yesu au unatakiwa uwe na uhalali wa kulitumia hili Jina wakati unapolitumia. Tulisoma Matendo ya Mitume 19:11-16.

2.      IMANI ya kulitumia hili Jina la Yesu au unatakiwa uweke imani yako katika Jina la Yesu ili Jina la Yesu lifanye kazi badala yako. Tulisoma Matendo ya Mitume 3:1-9,13-16

3.      MAMLAKA ya kulitumia hili Jina la Yesu. Tulisoma Matendo 4:1-12. Au uwe na mamlaka ya kulitumia Jina la Yesu.

4.      NGUVU ya kulitumia Jina la Yesu; au uwe na nguvu (upako) unapolitumia hili Jina la Yesu. Tulisoma Wafilipi 2:9-10

5.      MBINU za kulitumia hili Jina la Yesu; au uwe na mbinu mbalimbali za kulitumia hili Jina la Yesu. Tulisoma Wakolosai 3:17 na Marko 16:17,18.

Shuhuda motomoto za matendo makuu ya
Mungu zilikuwepo ….

          Tukisema tuandike shuhuda zote tulizoziona na kusikia kutokana na matendo makuu Yesu aliyofanya, hii ripoti itakuwa ndefu sana. Lakini ni muhimu tukuandikie chache! Tunachotamani sana ni siku nyingine ukipata nafasi ufike katika semina hizi ushuhudie mwenyewe kama hujawahi kuhudhuria. Wale waliowahi kuhudhuria semina hizi tunazozifanya wanajua ya kuwa Mungu huwa anatenda mambo mengi makubwa wakati huo.

          Kuna mama mmoja alishuhudia jinsi Mungu alivyomsaidia akapata mtoto wa kiume kwa njia ya maombi ya kipindi cha radio tunachorusha katika Radio Sauti ya Injili. Akasema ya kwamba alikuwa amejaliwa kuzaa mtoto wa kwanza wa kike na baada ya hapo ikapita miaka 14 bila kupata mtoto mwingine. Akiwa anasikiliza kipindi chetu kwa njia ya radio – wakati wa maombi aliweka mikono yake juu ya tumbo lake, huku akishiriki maombi yale. Baada ya wiki kadhaa kutokea siku hiyo akapata uja uzito. Wakati akishuhudia katika semina alikuwa amekuja na huyo mtoto! Sote tukamshukuru Mungu sana pamoja naye.

          Mama mwingine alikuja na mtoto ambaye ana umri wa miaka mitano na alikuwa hajawahi kutembea wala kukaa tangu kuzaliwa!  Lakini katika maombi wakati wa semina tuliyoifanya mwaka jana mjini Moshi – Bwana Yesu alimponya. Huyo mtoto sasa anaweza kukaa na kutembea bila shida.

          Mtoto mwingine aliyepona semina za mwaka jana aliletwa na mama yake ili maelfu ya watu yashuhudie jinsi anavyoweza kuongea bila matatizo yoyote. Mtoto huyo aliyekuwa na miaka kama mine hivi ulimi wake ulikuwa mzito kiasi cha kinywa chake kushindwa kutamka maneno vizuri. Aliwahi kupelekwa hospitalini na kufanyiwa upasuaji wa kurekebisha ulimi wake – lakini pia hakupona. Mwaka jana mama yake alimleta huyo mtoto katika semina tuliyoifanya mjini Moshi – na Bwana Yesu akamponya. Na sasa anaongea na kutamka maneno vizuri tu bila matatizo.

          Vijana wawili – mmoja wa kike na mwingine wa kiume, na kwa siku tofauti walipanda jukwaani kushuhudia ya kuwa Mungu amejibu maombi yao waliyokuwa wameweka katika ‘box’ la maombi tuliloliombea wakati wa semina za Moshi za miaka ya nyuma. Hawa vijana tangu kuzaliwa walikuwa hawajawahi kuonana na baba zao waliowazaa, na pia walikuwa hawajui wako wapi. Lakini walipoweka maombi kwenye ‘box’ ili Mungu awakutanishe na baba zao – Mungu akasikia maombi hayo. Kwa muda tofauti – vijana hao kila mmoja aliwezeshwa na Mungu kukutana na baba yake!

          Mama mmoja ambaye alikuwa amepata shida ya macho na kusababisha kushindwa kuona kwa muda wa miaka miwili – alipona wakati wa semina kwa jina la Yesu Kristo na akaweza kuona tena bila shida.

          Mama mwingine alipona kansa ya tumbo na uvimbe uliokuwa tumboni mwake zaidi ya miaka miwili ulitoweka hapohapo wakati wa maombi katika semina. Huyo mama akasema na maumivu yote aliyokuwa nayo yalikuwa yameondoka katika Jina la Yesu Kristo.

          Kijana mwingine alieleza jinsi alivyokuwa na kiu ya kujazwa Roho Mtakatifu na kunena kwa lugha – lakini alikuwa hajafanikiwa licha ya kuombewa mara nyingi sehemu mbalimbali. Lakini akisikiliza kipindi chetu katika radio na kushiriki maombi – akajwa Roho Mtakatifu na akajaliwa kunena kwa lugha mpya kuanzia wakati huo huo!

          Akina baba wawili – katika siku tofauti wakati wa semina hii ya Moshi mjini walishuhudia jinsi ambavyo Mungu aliwaponya ugonjwa wa ukimwi. Wote wakaeleza jinsi walivyokuja kwenye semina tulizofanya mjini Arusha kuombewa baada ya kuambiwa hospitalini ya kuwa walikuwa wameathirika na ukimwi. Baada ya maombi hayo kila mmoja alirudi kivyake – vyake mahali alipokuwa amepimwa mwanzoni.Lakini baada ya matokeo ya vipimo kutoka ikajulikana ya kuwa hawana tena virusi vya ukimwi! Wakati wa shuhuda mmoja wao alikuja na vyeti vya hospitali. Cheti cha kwanza kikionyesha ya kuwa  anao ukimwi na cheti kingine kikionyesha ya kuwa hana ukimwi baada ya kupimwa mara tu baada ya semina tuliyomwombea kumalizika.

          Mama mwingine alikuja na mtoto wake ambaye alipozaliwa iligundulika na madaktari ya kuwa moyo wake ulikuwa na tundu. Kwa hiyo alikuwa anasubiri muda na mahali pa kufanyiwa upasuaji. Lakini kwenye semina ya mwaka jana alikuja naye ili aombewe – na tukamwombea. Aliporudi hospitalini kwa ajili ya kliniki wakagundua pia ya kuwa lile tundu katika moyo halipo tena! Madaktari walishangaa sana. Lakini kwetu, sisi tunamrudishia Yesu sifa zote kwa uponyaji wake huo.

Mwisho

          Haya mambo machache ndiyo tuliyoweza kukuwekea katika ripoti hii. Lakini yaliyotendeka kwa Jina la Yesu Kristo ni mengi sana! Sifa na utukufu tunamrudishia Bwana Yesu Kristo – peke yake! Tuzidi kuombeana. Usisahau ya kuwa semina zetu zingine zinazofuata ni Arusha Mjini tarehe 15 – 22 Februari 2004; Tanga Mjini tarehe 2 – 7 Machi 2004 na Dar es Salaam tarehe 22 – 29 Machi 2004. Tuombee ili Jina la Yesu likatukuzwe zaidi tena katika semina hizi. Tutashukuru sana ikiwa utaweza kufika na kuhudhuria katika mojawapo ya semina zetu hizi.
 

UNATAKA KUOKOKA?
Kama unataka kumpa YESU maisha yako sasa, bonyeza hapa
©2003 Tanzania Social and Economic Trust.  All Rights Reserved.