Yesu Akamwambia "Lisha Kondoo Zangu" (Yohana 21:17)
Home
Maombi
Ratiba
Shuhuda
Mafundisho
Maswali na Majibu
Barua za Mwezi
Kuchangia Huduma
RIPOTI YA MOSHI


Ripoti Semina ya Moshi 27 Julai hadi 3 Agosti 2003

KUNA JAMBO ANALOFANYA MUNGU KILIMANJARO!

          Tunasema hivi kwa sababu ya mambo yale tuliyoyaona na kuyasikia wakati tulipofanya semina nyingine ya neno la Mungu pale Moshi Mjini tarehe 27 Julai hadi 3 Agosti 2003. Ni vigumu kuona tuliyoona na kusikia tuliyosikia bila kufikia kutuunga mkono katika kusema, ‘ kuna jambo analolifanya Mungu Mkoani Kilimanjaro’

Maelfu wahudhuria na kuokoka!

          Kila siku kulikuwa na watu waliokuwa wanahudhuria semina wastani wa watu 20,000 (elfu ishirini). Na kwa siku zote nane za semina hii tulishuhudia na kuwaongoza sala ya toba watu wapatao 7000 (elfu saba)! Wakaokoka na kuanza maisha mapya ndani ya Yesu!

          Haya ni mavuno makubwa kuyapata kwa siku nane. Na tunaamini waliokoka wengi zaidi ya hapo kwa kupitia kwenye radio. Maana kila siku jioni tulikuwa tunarusha kwenye radio mafundisho ya semina hiyo kwa siku zote nane mfululuzo. Na radio hii ya ‘Sauti ya Injili’ inasikika sehemu za kusini mwa Kenya, na pia wilaya zote za mikoa ya Kilimanjaro na Arusha; na pia sehemu  fulani fulani za mkoa wa Tanga.

          Semina hii tuliifanya ndani ya hema letu kubwa lenye uwezo wa kukalisha watu 15,000 (elfu kumi na tano). Wakati wa semina hii – hema lilionekana dogo. Tuliweza kuweka viti vya kukalisha watu elfu kumi na tano (15,000) lakini kila siku vilikuwa vinajaa na watu walikuwa wanasimama kwa maelfu. Siku za Jumamosi na Jumapili inawezekana kabisa watu waliohudhuria walifikia kati ya 25,000 hadi 30,000 kwa jinsi walivyokuwa wengi.

          Katika kusanyiko la watu wengi namna hii tuliweza kujua, angalau kwa uchache ya kuwa kuna watu waliohudhura semina hii toka Kenya, Kigoma, Morogoro, Arusha, na Dar es Salaam. Hii ni pamoja na waliotoka wilaya zote za Mkoa wa Kilimanjaro. Tunamshukuru Mungu sana kwa jinsi ambavyo ameamua kujidhihirisha Kilimanjaro kwa namna hii. Na tunaamini ya kuwa mbegu ya neno la Mungu  iliyopandwa ndani yao inaota na kumzalia Mungu matunda, na kumletea Yeye utukufu anaoustahili!

“….. Na tulishuhidia Uponyaji!

Chura atoka ndani ya suruali……”

          Kijana mmoja ambaye alikuwa amesafiri toka Morogoro kwa ajili ya kuhudhuria semina  na kuombewa – alipata kutoka kwa Yesu kile alichokuwa anakitafuta! Ingawa alikuwa ameokoka siku nyingi, kuna mapepo ambayo yalikuwa yanamsumbua kwa muda mrefu bila kutoka. Katika semina hii ya Moshi wakati wa maombi ya wagonjwa yaliyofanyika kila siku alifunguliwa na kupona. Yaliyotokea kila mtu aliyekuwa karibu naye alishangaa. Maana wakati maombi yanaendelea alitoka chura toka ndani ya suruali yake katika mguu wake mmoja na kuanza kukimbia! Chura huyo alipotoka na mapepo yote yaliyomsumbua siku  nyingi yalimwachia na kutoka kabisa, na akawa huru! Jina la Yesu na litukuzwe milele kwa matendo haya ya ajabu!

          Ukituuliza kwa nini chura huyo alitokea kwenye suruali yake – hata sisi hatujui! Ila tunachojua Jina la Yesu Kristo lilimweka huru mbali na mapepo yote yaliyokuwa yanamsumbua.

          Tulisikia shuhuda nyingi sana za uponyaji katika semina hii – na tukabaki tunashangaa na kumtukuza Mungu pamoja na maelfu ya watu waliohudhuria. Baba mmoja wa makamo ambaye na alikuwa na mvi kichwani alishuhudia ya kuwa amepona sikio la kulia lililokuwa halisikii tangu alipozaliwa. Tulijaribisha usikivu wa sikio hilo mbele ya watu wote, na akaweza kusikia vizuri bila shida yo yote.

          Akina baba wengine wawili kwa siku tofuati katika semina hii walishuhudia walivyopona ugonjwa wa mapafu na kukohoa damu. Ingawa walishuhudia katika semina hii, lakini walisema walipona katika maombi tuliyoifanya katika semina ya siku 16 ya Januari 2003. Mzee mmoja kati yao alisema hospitali walikuwa wamejaribu kumtibu bila kupata nafuu yoyote. Na ilifika wakati alikata hata tamaa ya kuishi. Lakini alipokuja kwenye semina hiyo, wakati wa maombi ya wagonjwa Mungu akamponya kabisa! Huku akitokwa machozi huyu mzee akasema “Jamani kweli Mungu yupo na anaponya”! Na wote tukalia machozi ya shukrani pamoja naye!

          Huyo mwingine aliyepona mapafu alikuwa ni daktari, na akaeleza jinsi alivyokuwa anakohoa damu muda mrefu bila kupona – pamoja na kutibiwa hospitalini. Lakini Mungu ni mwenye rehema; akamhurumiwa na kumponya katika semina ile ya Januari 2003.

          Mtu mwingine kutoka maeneo ya Taveta, Kenya alishuhudia jinsi alivyopona kwa njia ya radio mguu wake uliomsumbua tangu akiwa mtoto. Alisema mwezi wa Januari 2003 alikuwa anasikiliza mafundisho ya semina tuliyokuwa tunafundisha kwa njia ya radio tukiwa Moshi, yeye wakati huo akiwa Taveta. Ilipofika wakati wa maombi ya wagonjwa, anasema aliweka mkono wake juu ya mguu uliokuwa unaumwa kama tulivyoelekeza kwenye radio. Mara akaanguka chini huko nyumbani kwake, na aliposimama baadaye akakuta mguu umepona na akaweza kutembea vizuri kitu ambacho alikuwa hawajawahi kukifanya tangu zamani. Kwa hiyo akasema aliposikia kuna semina yetu nyingine Moshi akaamua kufunga safari toka Taveta na kuja Moshi kwenye semina ili ashuhudie na watu wasikie matendo makuu ambayo Mungu amemfanyia.

          Mzee mwingine alisimama kushuhudia jinsi ambavyo ameitupa fimbo aliyokuwa anaitumia kumsaidia kutembea baada ya kupona wakati wa maombi. Ilikuwa furaha kwa kila mtu aliyemwona huyo mzee akipiga ‘maki-taimu’ kama askari jukwaani ili kuudhihirishia umati wa maelfu uliokuwepo ya kuwa Bwana Yesu amemponya kweli kweli!

“….. kuna ishara za uponyaji zilizokuwa

na ujumbe pia ……!”

            Je! unajua ya kuwa kuna ishara ambazo Mungu anazifanya katikati ya watu na zina ujumbe ndani yake? Mungu aliwahi kumwambia Musa alipokuwa anamtuma kwa Farao na kwa Wana wa Israeli ya kuwa: “ Basi itakuwa, wasipokusadiki, wala kuisikiliza sauti ya ishara ya kwanza, wataisikiliza sauti ya ishara ya pili” (Kutoka 4:8). Kufuatana na mstari huu ishara hizo zilikuwa na sauti ndani yake. Na ikiwa ishara zilikuwa na sauti, basi ina maana ya kuwa zilikuwa na ujumbe kutoka kwa Mungu kwa ajili ya hao ambao ishara zitafanyika kwao.

          Ndicho tulichoshuhudia kikitokea Moshi wakati wa semina. Kuna miujiza ya uponyaji ambayo hao watu waliopona waliposhuhudia tulidaka pia na ujumbe uliokuwemo ndani yake, na tukawaeleza maelfu ya watu waliokuwapo wakati huo. Muujiza mmoja wapo wenye ujumbe ndani yake ulikuwa ni wa mama mmoja aliyeponywa na Yesu tatizo la ugonjwa wa kutokwa usaha sehemu za siri. Ugonjwa huu ulikuwa umemsumbua kama miaka miwili mfululizo iliyopita bila kupona. Tulipoletewa habari za ushuhuda huu tukashauriana  wenyewe ikiwa tumruhusu auseme mbele za watu au anyamaze! Lakini Roho Mtakatifu akatuhimiza  tumruhusu auseme. Na baada ya kumsikiliza mpaka mwisho tukaelewa ni kwa nini ilikuwa muhimu ashuhudie.

          Alisema mama huyo ya kuwa, alikuja kwenye semina tuliyofanya Januari 2002 pale Moshi akiwa mgonjwa, lakini hata baada ya maombi hakupona. Akarudi tena kwenye semina tuliyoifanya mwezi Agosti 2002 pale Moshi, lakini pia hakupona pamoja na maombi yaliyokuwepo. Tulipofanya semina ya siku 16 pale Moshi mwezi Januari 2003, alikuwa bado anaumwa na akatamani kuja lakini  alikosa nauli. Yule mama akasema, alipokosa nauli akaamua ya kuwa saa ya maombi ya wagonjwa yanapoanza uwanjani saa kumi jioni, atakuwa anaingia katika maombi chumbani mwake  ili apate muujiza wake. Kwa hiyo kila siku alikuwa anafanya hivyo hadi mwisho wa semina, na akajikuta amepona kabisa na usaha umekoma kumtoka! Kwa hiyo aliposikia kuna semina nyingine Moshi mwezi wa Julai 2003, aliamua akope fedha za nauli ili aje tu ashuhudie matendo makuu ambayo Mungu amemtendea.

          Mwingine ni mwanamke pia ambaye jino lake moja lilikuwa limeoza na nyama kuota na kuning’inia ndani ya mdomo wake. Alisema alikwenda hospitali mara ya kwanza na wakamkata hiyo nyama iliyojitokeza. Baada ya miezi kadhaa nyama ikaota tena pale pale. Akaenda tena hospitali na ikakatwa. Baada ya miezi kadhaa ikaota tena pale pale, na alipokwenda hospitali wakamwambia ni kansa. Akaueleza umati wa maelfu ya watu uliokuwepo ya kuwa alikuja kwenye maombi ya wagonjwa katika semina zetu mbili tulizofanya Moshi mwaka jana (2002) mwezi wa Januari na ule wa Agosti, - lakini hakupona.

          Tulipokuwa na semina nyingi mwaka huu (2003) mwezi wa Januari pale Moshi, aliamua kusikiliza radioni masomo tuliyokuwa tunafundisha. Siku moja wakati wa maombi ya wagonjwa akashindana sana moyoni mwake, kama ashiriki hayo maombi au la. Maana alijiambia mwenyewe ya kuwa; “Nimemfuata Mwakasege kule uwanjani kwenye semina mara mbili zote sikupona, - itakuwaje nipone leo akiwa anaomba kwa njia ya radio tena yuko mbali?” Lakini huyo mama akasema mwishoni akaamua kushiriki maombi hayo. Akasema wakati maombi hayo yalikuwa yanaendelea akaiinua radio yake usawa wa mdomo wake! Tukamuuliza sababu gani zilimfanya ainyanyue radio yake hivyo. Akatujibu ya kuwa; “Ni ili maombi yanapofanyika upako uende moja kwa moja mdomoni, kwenye shida hiyo ya kansa!” Na baada ya maombi hayo alipojikagua mdomoni mwake akakuta nyama iliyokuwa imening’inia ambayo hospitali walisema ni kansa haipo! Na tangu wakati huo (Januari 2003) amepona; na hadi Julai 2003 wakati wa semina hii alikuwa hajapata shida tena!

          Mtu mwingine mwanamke alipona kansa ya ziwa lake la upande wa kulia. Alisema ya kuwa alikuja kwenye semina tuliyoifanya Januari 2003 na baada ya maombi akaamini amepokea uponyaji, ingawa ziwa lake la kulia lilikuwa bado limevimba sana. Akasema alipofika nyumbani, akamweleza mume wake juu ya uponyaji wake huo, lakini hakumwamini kwa kuwa kwa jinsi ya nje uvimbe bado ulikuwa bado na maumivu alikuwa bado anayasikia. Lakini yule mama akasema akaendelea kumshukuru Bwana Yesu kwa uponyaji huo ambao aliamini ya kuwa aliupata kwa njia ya maombi wakati wa semina. Na akasema baada ya siku kadhaa huku akiendelea kumshukuru Mungu wake kila siku, ule uvimbe na maumivu vikaendelea kupungua kidogo kidogo. Na hadi alipokuwa anashuhudia alikuwa amepona kabisa- uvimbe na maumivu vyote vilikuwa vimetoweka; akapona kabisa ile kansa katika ziwa lake la kulia.

          Tukamuuliza mume wake alisema nini alipoona uponyaji huo. Akasema mume wake alishangaa sana na ameishia kusema ya kuwa Mungu yuko kweli!

          Katika shuhuda zote hizi tatu, tuliona kabisa ya kuwa ni ishara kwa wote waliokuwepo pale kwenye semina, na ndani yake kuliwemo na ujumbe. Na ujumbe huu ambao Roho Mtakatifu alitupa, tuliwaeleza watu wote pale pale. Ujumbe wenyewe ni huu: Ni kwamba kwanza watu wasimtazame Mwakasege kwa ajili ya uponyaji wao, bali wamtazame Yesu! Na pili, wanapohitaji uponyaji kwa Bwana Yesu wasikate tamaa. Wakiomba mara ya kwanza na hata mara ya pili, bila kupona bado wasikate tamaa bali waendelee kuomba na kumshukuru Mungu – na hatimaye watapona! Ndiyo yaliyotokea kwa wakina mama hao watatu. Wote walikuwa na magonjwa ya kukatisha tamaa. Wote walikuja semina kuombewa na hawakupona pale pale. Wakiwa majumbani mwao, kila mmoja alipokea uponyaji kwa njia tofauti tofauti kwa kadri Yesu alivyotaka. Jina la Yesu Kristo litukuzwe milele kwa ajili ya uponyaji huo!

          Nasi tunakuambia na wewe unayesoma ripoti hii ya kuwa; Usitazame wanadamu bali mtazame Bwana Yesu kwa ajili ya muujiza unaotaka toka kwa Mungu! Pia, usikate tamaa, endelea kuomba, amini tu, na endelea kushukuru, nawe hatimaye utapokea muujiza wako toka kwa Bwana Yesu! Mungu aliyekupa ahadi ya muujiza wako toka katika neno lake, Yeye ni mwaminifu, naye atafanya na kutekeleza alichoahidi.

“….Nguvu la Damu ya Yesu ilidhihirika…..!”

          Somo tulilokuwa nalo katika semina hii lilikuwa na kichwa kinachosema “Itumie Damu ya Yesu Ikusaidie”. Roho Mtakatifu alituongoza kupita katika maeneo mazuri sana. Na kila siku tuliona “Bwana akitenda kazi pamoja nasi, huku akilithibitisha hilo somo kwa ishara zilizofuatana nalo!”

          Ukiwa na nafasi tafuta na hakikisha unausikiliza ujumbe huu kwa njia ya kanda za radio au/na za video. Tunaamini utapata cha kukusaidia. (Kama hujui namna ya kuzipata tuandikie au tupigie simu tukuelekeze). Siku moja tulipewa kusema ujumbe kwa ajili ya wakazi wa Mkoa wa Kilimanjaro. Ilikuwa ni juu ya madhara yaliyotokea mkoani humo kwa sababu ya wengi wao kufanya matambiko kwa mizimu ya mababu zao. Tuliwaonyesha kwa neno la Mungu ya kuwa po pote wanapofanya matambiko kwa mizimu namna hii yafuatayo yametokea kwa namna moja au nyingine:

  • roho ya uasherati inaingia kwa nguvu katika familia hizo, na kwa watu wa maeneo hayo (Hosea 4:12,13)
  • mvua ya vuli (siyo ya masika) inazuiliwa – yaani hainyeshi au inanyesha kwa shida. Matokeo yake ni watu kuacha kulima mazao wakati wa mvua za vuli kama walivyokuwa wanafanya zamani (Yeremia 3:1-3)
  • Familia zinatengana. Ndugu na ndugu wanagombana na kutoelewana (Mambo ya Walawi 20:6)
  • Watoto wanapoteza urithi walioachiwa na wazazi wao (1Wafalme 11:9-13).
  • Roho za dini kuongezeka na kuzaa madhehebu yaliyo na misimamo isiyoeleweka; - na yanakuwa na upinzani juu ya wokovu katika Kristo Yesu na nguvu zake za Roho Mtakatifu.

Tuliwaambia ya kuwa dawa ya matatizo haya ni

1. Toba ya kweli kwa Mungu kwa ajili yako kama ulihusika na matambiko/ibada ya mizimu; lakini hata pia kama hukuhusika tubu kwa ajili ya wengine ili mkoa au eneo lenu lipone. 2. Sema neno unalotaka Damu ya Yesu ifanye; na 3. Amini ya kuwa hayo usemayo yametokea nayo yatakuwa yako!

Kama tulivyokuambia hapo mwanzo, watu wengi sana waliokoka  (wastani wa watu 7,000) kwa muda wa siku nane za semina hii. Maelfu pia walijazwa Roho Mtakatifu na kunena kwa lugha mpya! Sifa zote na Heshima na Utukufu  tunamrudishia Mungu wetu katika Kristo Yesu – maana alifanya alichotaka kufanya katika watu wake, - kwa ajili ya utukufu wake!

Shukrani

          Pamoja na kwamba tunamshukuru Mungu sana kwa ajili ya mafanikio tuliyoyaona katika semina hii ya Moshi. Pia, tunashukuru kwa ajili ya kila mtu ambaye Mungu alimtumia kuifanikisha semina hii kabla – wakati – na baada ya semina. Mungu akubariki na kukurudishia mara mia, sawasawa na neno lake.

          Tuzidi kuombeana. Semina zinazofuata ni Mwanza tarehe 8-14/9/2003 katika kiwanja cha Furahisha na Arusha Mjini tarehe 28/09 hadi 5/10/2003. Semina zitakuwa zinafanyika kila siku kuanzia saa 9 mchana katika tarehe zilizotajwa. Tunawaomba radhi wakazi wa Dar es Salaam kwa kutowaarifu mapema ya kuwa semina ambayo ilikuwa tuwe nayo mwezi huu (Agosti) Dar imeahirishwa hadi tarehe nyingine tutakayowatangazia kabla ya mwaka huu kuisha!

UNATAKA KUOKOKA?
Kama unataka kumpa YESU maisha yako sasa, bonyeza hapa
©2003 Tanzania Social and Economic Trust.  All Rights Reserved.