Yesu Akamwambia "Lisha Kondoo Zangu" (Yohana 21:17)
Home
Maombi
Ratiba
Shuhuda
Mafundisho
Maswali na Majibu
Barua za Mwezi
Kuchangia Huduma
RIPOTI YA MWAKA 2004


Asante Sana Yesu Kwa Mwaka 2004!

na Christopher na Diana Mwakasege

Tumemwona Mungu akijitukuza tena mwaka 2004 ndani ya mwana wake Yesu Kristo, katika semina na huduma mbalimbali alizotuwezesha kuzifanya. Tumefanya semina za neno la Mungu 17 tukitumia jumla ya siku 100. Hii maana yake kati ya siku 365 za mwaka 2004, tumetumia siku 100 kufundisha neno la Mungu katika semima mbalimbali tulizokuwa nazo.

Tumefanya semina mbili mbili mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Dar es salaam. Lakini pia Mungu ametuwezesha kufanya semina mbili kwa ajili ya watanzania walioko Marekani  semina ya kwanza tuliifanyia mji wa Minneapolis, jimbo la Minnesota mwezi wa tano; na semina ya pili tuliifanya mwezi wa kumi katika mji wa Birmingham, jimbo la Alabama.

Miji mingine hapa nchini tuliyofanya semina moja moja ni Dodoma, Tanga, Shinyanga, Mwanza, Tabora, Kigoma, Mbeya, Iringa, na Ruaha (karibu na viwanda vya sukari vya Kilombero). Kwetu sisi ilikuwa ni mara ya kwanza kufanya semina mjini Tabora, na Mungu alitufungulia mlango mzuri kwa ajili ya ‘shamba jipya’ hili!

Pamoja na kufanya semina sehemu zote hizo; pia tulipata nafasi mara mbili za kukutana na baadhi ya watanzania walioko Uingereza ili kuweka mikakati ya kuanza semina za kila mwaka kwa ajili ya watanzania walioko Ulaya.

Katika miji yote hiyo, na sehemu zote hizo tumetumia siku 100 kufundisha neno, lakini pia tumetumia siku 34 nje ya siku hizo 100 kwa ajili ya kusafiri kwenda na kurudi toka katika semina hizo. Katika hizo siku 34 za kusafiri tumetumia wastani wa masaa 252 barabarani au angani tukisafiri. Ukipiga mahesabu yako vizuri utaona ya kuwa tulikuwa hatupo nyumbani kwa siku zisizopungua 134 katika siku 365 za mwaka 2004.

Shukrani

Tunaamini utaungana nasi kumshukuru Mungu sana kwa ajili ya kutulinda katika safari zote hizo – tumesafiri bila ajali yo yote, na afya zetu Mungu amezitunza!

Lakini kama utakavyokuwa unasoma ripoti hii ambayo tunaandika muhtasari tu wa mambo kadhaa yaliyofanyika mwaka 2004, utaona ya kuwa tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu. Si rahisi kuwa na maneno ya kutosha yanayoweza kuelezea shukrani tulizoanazo mbele za Mungu kwa yale aliyoyafanya katika huduma aliyotupa kwa mwaka 2004. Ndiyo maana sisi na timu nzima tuliyonayo tunasema “Asante Sana Yesu kwa Mwaka 2004!”

Pia, tunamshukuru Mungu sana kwa ajili ya kila mmoja aliyehusika na kutumiwa na Mungu katika kufanikisha semina hizi zote. Si vyepesi kutaja wala kukumbuka majina ya watu wote waliohusika, lakini Mungu anawafahamu wote! Tunachoweza kusema zaidi ya shukrani, ni hiki; “mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya Bwana sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika Bwana” (1 Wakorintho 15:58).

Tunamshukuru Mungu pia kipekee kwa ajili ya familia zetu ambazo zimesimama pamoja nasi katika kazi hii ya Mungu. Muda mwingi tumekuwa hatupo nyumbani,lakini uwepo na upendo na amani ya Mungu vimewafunika, na kuwalinda, na kuwafanikisha.

Mahudhurio yalikuwa
ya kipekee!

Kwetu sisi tuliyaona mahudhurio katika semina tulizozifanya ya kuwa yalikuwa ya kipekee. Tuliyaona ni ya kipekee kwa sababu ya uwingi wa watu waliohudhuria; na aina ya watu mbalimbali waliohuduhuria.

Semina iliyokuwa na mahudhurio makubwa kuliko semina zote tulizofanya mwaka 2004 ilikuwa ni semina ya pili ya Arusha tuliyoifanya mwezi Septemba. Mwandishi mmoja wa gazeti la ‘Nyakati’ la tarehe 26 Septemba 2004 alikadiria mahudhurio ya watu 100,000 kwa siku ya nane ya semina hiyo.

Na kwa sababu si rahisi kupita kila mkoa na kila wilaya zote tunamoalikwa, tumehimiza kamati zinazoandaa semina hizi kukaribisha watu kutoka sehemu zilizo mbali na miji ambayo tunafanyia semina.

Ingawa mialiko hii imeongeza wajibu mkubwa kwa ajili ya kamati za maandalizi, lakini baraka zinazopatikana ni kubwa; na wigo wa semina unapanuka na kuwafikia watu wengi zaidi kwa mara moja.

Kwa mfano, limekuwa jambo la kawaida kwa semina za Arusha, Moshi na Mwanza kuona watu wengi kutoka nchi ya Kenya wakija kuhudhuria semina hizo. Kwa semina ya Mwanza – wengine wanaiita ni semina ya ukanda wa ziwa Victoria. Wanasema hivyo  kwa sababu inahudhuriwa na watu kutoka mikoa ya ziwa Magharibi, Mara, na Shinyanga. Hii ni pamoja na watu kutoka wilaya zote za mkoa wa Mwanza.

Kila semina tuliyokwenda tuliona jambo hili likijirudia. Watu kutoka mikoa ya jirani na ya mbali na mji tunaofanyia semina wanafika katika mafundisho hayo.

Hakuna mahali ambapo pana ukumbi wa kutosha kuwaweka watu wote hao wanaokuja kwenye semina hizo. Hema tunalolitumia kwa semina limekuwa halitoshi ukilinganisha na mahudhurio yanayokuwepo; kwa hiyo tunaendelea kulipanua kila wakati. Kwa semina tunazofanya Dar es Salaam, ukumbi wa “Diamond Jubilee”, ingawa ni mkubwa, lakini kwa sasa umekuwa mdogo!

Mtihani mkubwa kwetu, sisi, na timu nzima na kamati za maandalizi ni kujua namna ya kujipanga katika Mungu kwa namna ambavyo maelfu na maelfu ya watu wanaohudhuria semina hizi “wanapata kile ambacho Mungu amekikusudia wakipate kwenye semina hizi”.

Watu wapya
50,000 waokoka!

Semina tunazozifanya si mikutano ya kiinjilisti, bali ni madarasa ya mafundisho ya neno la Mungu; kwa misingi hii usingetarajia watu wengi ambao hawajaokoka wahudhurie. Lakini Mungu ni Mungu! Na hakuna wa kumfananisha na Yeye!

Sisi tunaungana na Waefeso 3:20,21 tukisema; “Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu; naam, atukuzwe katika kanisa na katika Kristo Yesu hata vizazi vyote vya milele na milele. Amina”

Katika semina zote hizo tulizozifanya mwaka 2004, ni wastani wa watu wapya 50,000 waliokoka! Na watu 24,000 kati ya hao waliokoka katika semina nne tulizozifanya Moshi na Arusha!

Idadi hii ya watu 50,000 haijumlishi wale waliookoka wakisikiliza vipindi vyetu vya neno tulivyovirusha kwa njia ya redio. Na wala haijumlishi wale waliookoka kwa kusoma vitabu tulivyoviandika, wala haijumlishi wale waliokoka kwa kupitia masomo tuliyoweka katika mtandao wa Kompyuta!

Ni maombi yetu kwa Mungu ya kuwa atayatunza na kuyakuza mavuno haya. Ungana pamoja nasi kuombea jambo hili. Tunamwamini Mungu ya kuwa kazi aliyoianza ndani ya watu wote hao, ataikamilisha kwa ajili ya utukufu wake mwenyewe!

Tunaamini pia ya kuwa kushiriki rasmi kwa makanisa na huduma mbali mbali za kikristo katika maandalizi ya semina hizi kunasaidia sana utunzwaji wa mavuno yanayotokana na semina hizi. Tumekuwa tukishauri makanisa kila tunapokwenda ya kuwa ikiwa hawajawa nazo kamati za ufuatiliaji ni vizuri ziundwe.

Makanisa mengi yana kamati za uinjilisti, lakini hawana kamati za ufuatiliaji au za malezi ya kiroho. Hizi kamati za ufuatiliaji zikiwepo zitawasaidia sana wachungaji na makanisa yao kuwafuatilia kwa karibu wale wanaookoka wanaotoka ndani au nje ya makanisa yao. Liwe ni jukumu la kamati hizi kuweka mambo ya msingi ndani ya wakristo hao wapya yanayohusu ufuasi na uwanafunzi wa Kristo.

Redio na Kompyuta vyatoa
 msaada mkubwa!

Hadi kufikia mwisho wa mwaka huu tunarusha vipindi vya semina ya neno la Mungu kwa njia ya redio, kwa kupitia redio tano. Kila Jumamosi na Jumapili usiku saa tatu hadi saa nne tunafundisha kupitia redio SAUTI YA INJILI. Hii ni redio inayomilikiwa na kanisa la Kilutheri na inasikika maeneo ya mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Tanga.

Kwa mkoa wa Dar es Salaam tunasikika kupitia redio WAPO kila Jumatano usiku, na kupitia redio ya PRAISE POWER kila Ijumaa usiku. Mkoani Shinyanga tunasikika kupitia redio FARAJA kila Jumamosi na Jumapili usiku. Redio FARAJA inamilikiwa na kanisa la Katoliki – jimbo la Shinyanga.

Pia tunakipindi kila Jumapili jioni katika RADIO FREE AFRICA inayorusha matangazo yake katika masafa ya kati (MW/AM). Kipindi hiki kinarushwa saa kumi na mbili na nusu jioni hadi saa moja na nusu usiku; na kinasikika nchi yote ya Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi na Ruanda. Pia kinasikika mashariki mwa nchi ya Kongo, na kaskazini mwa nchi za Zambia, Malawi na Msumbiji.

Kwa mkoa wa Dodoma tunasikika kupitia redio UZIMA, kila Jumamosi na Jumapili usiku. Redio hii inawafikia asilimia kubwa sana ya wakazi wa mkoa wa Dodoma.

Matokeo ya huduma ya redio hizi ni makubwa sana kuliko tunavyoweza kuelewa au kueleza. Shuhuda nyingi sana tunazipata kutoka kwa wale wanaookoka, na kupona na kujazwa Roho Mtakatifu wakati wakisikiliza vipindi vyetu katika redio hizi.

Tulipokuwa na semina Shinyanga mwaka huu mapema mwezi wa tisa kwa siku mbili; wenzetu wa redio FARAJA walileta mitambo yao mahali tulipokuwa tunafanyia semina na kurusha semina nzima “LIVE” kwa mkoa mzima!

Kwa wale wanaofuatilia takwimu za nchi ya Tanzania watafahamu ya kuwa idadi ya wakristo kwa mkoa wote wa Shinyanga ni wastani wa asilimia tano tu ya wakazi wote wa mkoa huo. Kwa hiyo kwetu sisi kupata nafasi ya kuufikia mkoa mzima kwa siku mbili mfululuzo kupitia redio FARAJA ulikuwa ni muujiza kutoka kwa Mungu uliopanua wigo wa semina ile!

Lengo letu ni kusema neno la Mungu na watanzania wengi kila wiki kwa kutumia redio mbalimbali kwa kadri Mungu atakavyokuwa anatufungulia mlango na kutupanulia wigo wa usikuvu wa semina za neno la Mungu kwa njia hii.

Redio hizi zimetusaidia sana kufanya mahudhurio ya semina yaongezeke kwa kasi. Kwa kuwa wakazi wa maeneo mengi wanatusikiliza kila wiki kwa njia ya redio, inakuwa rahisi kuhudhuria semina zetu wanaposikia tumefika “live” karibu na maeneo wanayoishi. Mwaka 2005 tunatarajia kurusha vipindi vyetu katika redio zingine mbili hapa nchini. Pia, tunaangalia uwezekano wa kuanza kurusha vipindi vyetu katika vituo vya redio nchini Kenya.

Sifa na heshima zote ni kwa Yesu Kristo. Tunaomba katika vipindi vyako vya maombi usisahau kumshukuru Mungu kwa ajili ya vituo hivi vyote vya redio tunavyovitumia, na waombee baraka na mafanikio zaidi, pamoja na ulinzi.

Kwa mwaka 2005 tuna mpango wa kuweka baadhi ya vipindi vya redio katika mtandao wetu wa kompyuta,ili viweze kusikika ‘online’ kila wiki.

Hii ni kwa sababu watumiaji wa mafundisho tunayotoa kwa njia ya mtandao wetu wa kompyuta wamekuwa wakiongezeka kila siku.

Huduma hii inapatikana katika anwani hetu hii: www.mwakasege.org. Kila wiki tunapata barua nyingi sana za wale wanaohitaji maombi kwa njia hii – na wengi wao wameturudishia majibu yanayomshukuru Mungu kwa kuwa Bwana Yesu amewaponya.

Na barua kadhaa zilitufikia toka kwa watu waliokuwa wanataka kuokoka baada ya kusoma masomo tuliyoyaweka katika mtandao wetu wa kompyuta. Tuliwapa msaada huo na kuwaongoza katika maombi na sasa wameokoka!

Ungana pamoja nasi kumshukuru Mungu kwa ajili ya wenzetu wa KICHEKO.COM kwa huduma wanayoifanya ya kuratibu mtandao wetu wa kompyuta. Ni maombi yetu ya kuwa Mungu ataendelea kuwafanikisha katika kazi zao, na kuwalinda dhidi ya hila za yule mwovu.

Mafundisho tuliyotoa ni
Chakula kwa wakati unaotakiwa!

Neno la Mungu ni chakula. Na biblia inahimiza watumishi kuwapa “watu chakula kwa wakati wake” (Mathayo 24:45). Na sisi tunajitahidi katika Roho Mtakatifu kufanya sehemu yetu katika hili. Tumekuwa tukiyatoa mafundisho kwa kadri tunavyoongozwa na kujaliwa na Roho Mtakatifu yawe chakula kwa wakati unaotakiwa!

Mwaka 2004 tulifundisha masomo yafuatayo katika semina mbalimbali tulizozifanya:

·         Namna ya kulitumia Jina la Yesu (Arusha na Moshi - semina za kwanza)

·         Mambo ya kukumbuka ukitaka maombi yako yajibiwe (Tanga)

·         Kanuni za kufuata ukitaka mapato yako yazidi matumizi yako (Dar – Semina ya Kwanza)

·         Umuhimu wa kusamehe ili maombi yako yajibiwe (Tabora)

·         Sehemu ya Imani na sehemu ya Jina la Yesu katika kujibiwa maombi (Tabora)

·         Faida za kujua tofauti za agano la kale na agano jipya (Kigoma)

·         Unachohitaji kufanya matumizi yako yanapozidi kipato chako (Moshi – semina ya Pili)

·         Namna ya kuupata uhuru wa kifedha (Financial Freedom) – kibiblia (Dar – semina ya Pili)

·         Mungu anazo mbinu za kukusaidia uongeze kipato chako ili utoke katika umaskini (Arusha – semina ya pili)

·         Faida za kuomba kwa muda mrefu (Shinyanga)

·         Kuwa tajiri au maskini ni uamuzi wako (Mwanza)

·         Sababu 7 kwa nini hutakiwi uwe maskini ukiwa ndani ya Kristo (Dodoma)

·         Kutajirika ki-Mungu kunategemea mabadiliko katika mawazo yako (Mbeya)

·         Mungu anawaza nini juu ya matatizo ya uchumi yanayotuzunguka? (Iringa)

·         Je! Mungu anaweza kutatua matatizo yako ya kifedha? (Kilombero)

Mafundisho haya yote tumeyaweka kwenye kanda za redio na za video. Ni chakula kimetunzwa! Masomo mengi ya mwaka 2004 yalisisitiza sana maeneo ya uchumi na ya maombi. Kuna sababu yake kwa nini Roho Mtakatifu atupe masomo kwa msisitizo huu, lakini tutakueleza sababu hiyo wakati mwingine. Tunaamini masomo hayo yamelisaidia kanisa na yataendelea kulisaidia kanisa kumjua Mungu zaidi kwa jinsi alivyojifunua katika Kristo Yesu.

Mungu aliyathibitisha mafundisho
kwa ishara na miuujiza!

Katika kitabu cha Marko 16:20 tunasoma habari za wanafunzi wa Yesu ya kuwa: “Nao wale wakatoka, wakahubiri kotekote, Bwana akitenda kazi pamoja nao, na kulithibitisha lile neno kwa ishara zilizofuatana nalo”

Na katika Waebrania 13:8 tunaelezwa ya kuwa: “Yesu Kristo ni yeye yule , jana na leo na hata milele”. Hii ina maana ya kuwa alichofanya Yesu akiwa na wanafunzi wake wakati ule, atafanya na wanafunzi wake wakati huu pia!

Na ndicho tulichokiona sisi na kukisikia katika kila eneo tulilofanya semina za neno la Mungu. Tulishuhudia Mungu akiudhihirisha upako wake kwa nguvu na kwa namna tofauti – tofauti.

Jambo hili lilitutia moyo sana katika utumishi huu tulionao katika mwili wa Kristo. Kwa sababu tulishuhudia Mungu akijidhihirisha kama ishara mojawapo ya kutuonyesha ya kuwa Yeye yupo pamoja nasi kila alikotupeleka!

Watu wengi sana walikuwa wanajitokeza ili kushuhudia hadharani kile walichofanyiwa na Bwana Yesu. Lakini si wote walipata nafasi hizo, kwa sababu ya muda tuliokuwa nao kuwa mchache kulingana na mambo yaliyokuwepo.

Hata hivyo tunataka tukushirikishe baadhi tu ya shuhuda hizo katika ripoti hii. Nia yetu katika kufanya hivi ni ili kumrudishia Mungu utukufu na sifa zote. Tunaamini na wewe utaungana nasi katika kumtukuza Mungu kwa matendo makuu aliyoyafanya katikati ya watu wake.

Tunaweza kuungana kuomba kama Daudi alivyoomba aliposema: “Ee Bwana, kutukuza usitutukuze sisi, bali ulitukuze jina lako, kwa ajili ya fadhili zako, kwa ajili ya uaminifu wako” (Zaburi 115:1)

Tulipofanya semina ya pili mjini Arusha wakina mama wanne walijitokeza kushuhudia jinsi Mungu alivyowajalia kupata uja uzito na kuzaa watoto baada ya maombi tuliyowafanyia katika semina za nyuma tulizozifanya Arusha.

Mama mmoja alipata mtoto baada ya kushindwa kuzaa kwa miaka sita! Mwingine alipata mtoto wa kiume aliyemuomba baada yakupata watoto wa watatu wote wakiwa wakike mfululuzo! Mwingine mimba zilikuwa zinaharibika mara kwa mara, lakini maombi yalimsaidia na akajaliwa kujifungua mtoto salama. Mama mwingine alikuwa ametaka tumwombee apate watoto mapacha watatu, na Mungu akajibu hayo maombi. Akamjalia kuzaa watoto mapacha watatu  ( - wawili wa kiume na mmoja wa kike)!

Baba mmoja mkaazi wa mkoa wa Tanga alikuja Arusha mahsusi kwa ajili tu ya kushuhudia uponyaji ambao Mungu alimfanyia tulipofanya maombi ya wagonjwa katika semina tuliyoifanya Tanga mwaka 2002.

Akasema mbele ya maelfu ya watu waliohudhuria semina ya Arusha ya kuwa alikuwa ameugua ugonjwa wa TB kwa muda mrefu na kusababisha pafu lake la kushoto kuharibika. Uharibifu huo wa pafu la kushoto ulimfanya apumue kwa shida, na ashindwe kuendesha baiskeli.

Lakini baada ya maombi tuliyomfanyia wakati wa semina ya Tanga mwaka 2002 alipona kabisa; na anapumua vizuri, na anaendesha baiskeli yake bila matatizo yo yote toka wakati huo.

Tulipokuwa Kigoma kwa ajili ya semina mama mmoja alishuhudia jinsi maombi tuliyofanya kwenye semina ya mwaka jana Kigoma yalivyomsaidia kupata mtoto baada ya kushindwa kupata uja uzito kwa miaka nane!

Mama mwingine aliyetokea wilaya ya Uvinza alishuhudia katika semina hiyo ya Kigoma ya kuwa alipona jicho na tatizo la kifua wakati anaangalia mkanda wetu wa video wa semina ya Arusha. Alikuwa anaungalia huo mkanda wetu wa video alipokuwa Uvinza! Bwana Yesu akamponya!

Tukiwa Tabora kwenye semina mtu mmoja alipona jino lake la upande wa kushoto lililokuwa limetoboka kwa  muda mrefu na kushindwa kuutumia upande wake wa kushoto wakati anapotafuna chakula. Maombi yalipofanyika alipona na jino kuzibwa na Bwana Yesu!

Mama mmoja katika semina hiyo hiyo ya Tabora alishuhudia jinsi ambavyo mtoto wake alisimama kwa niaba yake wakati wa maombi tuliyofanya kwa ajili ya wagonjwa tulipofanya semina mjini Moshi mapema mwaka 2004. Alisema mara baada ya maombi hayo ya Moshi yeye alipona akiwa Tabora tatizo la moyo na tatizo la kukosa nguvu mara kwa mara! Ni kweli katika maombi hakuna umbali! Tuliomba tukiwa Moshi na Bwana Yesu akamponya mgonjwa akiwa Tabora!

Tulipokuwa Dodoma kwenye semina vilema kadhaa walitembea baada ya maombi! Sifa kwa Yesu!

Kilema mmoja alikuwa ni mtoto wa miaka 8 ambaye alikuwa hajawahi kusimama wala kutembea tangu azaliwe. Lakini baada ya maombi alisimama mwenyewe na kuanza kutembea!

Mwingine alikuwa ni mtoto wa miaka 3 ambaye pia alikuwa hajawahi kutembea tangu azaliwe. Baada ya maombi katika semina hiyo Bwana Yesu akamponya na aliweza kutembea na kukimbia wakati huo huo!

Mama mwingine aliyepona katika semina hiyo ya Dodoma alikuwa hajaweza kutembea kwa muda wa miaka miwili kwa sababu aliugua ugonjwa uliomfanya apooze maungo yake. Na wakati wa semina alikuwa analetwa na wenzake kwa kubebwa mgongoni wakipokezana. Lakini Mungu alimponya katika semina hiyo. Na hao akina mama wenzake waliokuwa wana-mbeba walifanya hivyo kwa siku tatu mfululuzo bila mwenzao kupona – lakini siku ya nne Bwana Yesu akamponya!

Mama mwingine wa makamo alikuwa anatembelea magongo kwa miaka miwili baada ya kuanguka na kuvunjika mifupa ambayo hata hivyo haikuunga vizuri. Lakini kwenye semina hiyo ya Dodoma, Bwana Yesu alimponya na akaweza kutembea tena vizuri bila magongo!

Hivi ndivyo ilivyokuwa kila mahali tulipofanya semina. “Bwana Yesu akaitenda kazi pamoja nasi, na kulithibitisha lile neno tulilolifundisha kwa ishara zilizofuatana nalo”!

Ndio maana tunasema “Asante Sana Yesu kwa mwaka 2004”! Zipo shuhuda nyingi sana, lakini si rahisi kuziandika zote katika ripoti hii. Hizi shuhuda chache tulizoziandika zitoshe kukupa changamoto ya kuendelea kumshukuru Mungu pamoja nasi kwa yale aliyotufanyia mwaka 2004.

Lakini hatuoni kama itakuwa sawa tusikueleze habari za mama mmoja kutoka Moshi vijijini alivyoshuhudia katika semina ya Dar jinsi Bwana Yesu alivyomponya mtoto wake ugonjwa wa ukimwi.

Huyu mama alieleza jinsi alivyopelekewa habari akiwa kwake Moshi vijijini ya kuwa mtoto wake aliyekuwa Dar alikuwa amefikia hatua ya kufa kwa ugonjwa wa ukimwi. Akasema ya kuwa alipokuwa anasikiliza maombi tunayotoa kwa njia ya redio aliweka mkono wake juu yake kwa niaba ya mtoto wake aliyekuwa Dar – na nguvu za Mungu zikamshukia yeye na akaamini Mungu amemponya mtoto wake. Na kweli baada ya siku kadhaa hali ya mtoto wake ikaanza kubadilika na akapona kabisa!

Kwa hiyo akaona aje Dar wakati wa semina ashuhudie juu ya muujiza huo akiwa na mtoto wake aliyepona ukimwi kwa njia ya maombi! Jina la Bwana Yesu lihimidiwe milele!

Kazi Inaendelea kwa
huduma ya Maandiko

Mwaka 2004 tulichapa na kutoa vitabu vipya vitatu. Hii inafanya idadi ya vitabu tulivyokwisha kuvitoa kufikia vitabu 15 tangu tuanze huduma ya kufundisha neno la Mungu kwa njia ya vitabu miaka kadhaa iliyopita.

Tunatarajia kutoa vitabu vingine vipya mwaka 2005 vinavyohusu maombi na vingine vinavyohusu mambo ya fedha. Wewe tuombee tu ili tuifanye kazi hii ambayo Mungu ametupa kwa kiwango kile kinachompendeza Yeye, na kuwasaidia watu wake.

Tunapomalizia ripoti hii tunaomba usisahau kuwaombea wafanyakazi wa GAZETI LA NYAKATI kwa kutupa nafasi kila wiki kufundisha neno la Mungu kupitia gazeti hilo. Omba wao wafanikiwe na pia gazeti lao lifanikiwe!

Semina za Marekani
na Uingereza

Mwaka 2004 tumefanya semina mbili kwa watanzania walioko Marekani. Pia, kwa mwaka 2005 tutaanza kufanya semina pia kwa watanzania walioko Uingereza na Ulaya. Usiache kusoma maelezo zaidi juu ya semina hizi katika mtandao wetu wa kompyuta. Ikiwa una mtanzania unayemfahamu aliyeko Marekani au Uingereza au Ulaya – usiache kumweleza juu ya habari za semina hizi.

UNATAKA KUOKOKA?
Kama unataka kumpa YESU maisha yako sasa, bonyeza hapa
©2003 Tanzania Social and Economic Trust.  All Rights Reserved.