Yesu Akamwambia "Lisha Kondoo Zangu" (Yohana 21:17)
Home
Maombi
Ratiba
Shuhuda
Mafundisho
Maswali na Majibu
Barua za Mwezi
Kuchangia Huduma
RIPOTI SEMINA YA MWANZA SEPTEMBA 2003


SHETANI ANGEJUA ASINGEMSULUBISHA MWANA WA ADAMU!

(Mambo ambayo vyombo vya habari havikutangaza juu ya semina ya Mwanza)

Na Christopher na Diana Mwakasege

           Tarehe 8-15 /9/2003 ‘wingu’ la semina za Neno la Mungu tunazozifanya sehemu mbalimbali nchini lilitua Mwanza mjini. Tunamshukuru Mungu sana kwa kutuwezesha kuifanya semina hii huko Mwanza, maana tulikuwa na hamu nayo kwa muda mrefu, lakini ‘muda wa Bwana’ ulikuwa haujafika. Pia, tunamshukuru Mungu kwa ajili ya kila mtu ambaye alimtumia kutuombea kwa ajili ya semina hiyo, na pia shukrani kwako wewe pia uliyetoa fedha au mali yako au/na muda wako kuifanikisha semina hiyo.

          Mungu wetu akubariki katika maisha yako ya kila siku, ili uuone mkono wa Mungu huyu uliyemtumikia kwa njia hiyo pamoja nasi, akikufanikisha na kukuinua!

Wachawi waalikana ……

….. na mbinu zao zakwama!

Ilikuwa ni patashika kubwa katika ulimwengu wa roho kwa jiji la Mwanza ambayo, tunaambiwa na wenyeji wa hapo ya kuwa ilikuwa haijawahi kutokea. Hata sisi kwetu jambo hili lilikuwa jipya.

          Siku tatu kabla ya kuanza semina hii, tulikuwa ndiyo tunafika Mwanza mjini tukitokea Arusha. Baadhi ya wenzetu walikuwa wamekwisha tangulia kama siku mbili kabla yetu, na wenzetu wengine toka Arusha walikuwa wanafika kesho yake.

          Tulipofika mchana huo wa tarehe 5 Septemba 2003 tulitembelea kiwanja cha Furahisha mahali hema la semina lilipokuwa linajengwa, na pia tukakaribishwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kwenda kumsalimia ofisini kwake.

          Jioni yake tukaambiwa ya kuwa kuna mambo mawili yaliyotokea ya kushangaza. Tuliambiwa ya kuwa kuna mtu aliyekwenda katika kanisa mojawapo hapo mjini na kutoa taarifa ya uongo ya kuwa ‘mgeni aliyepokelewa toka Arusha (yaani Mwakasege) anaumwa, amelazwa hospitalini kwa hiyo semina iliyopangwa haitakuwepo’!

          Hilo jambo halikuwa la kweli maana wakati huo tulikuwa ofisini kwa Mkuu wa Mkoa. Kwa hiyo baadhi ya watu walikwenda hospitalini kumtafuta Mwakasege – lakini hakuwepo huko! Hizo zililikuwa mbinu za wachawi ili kutaka kuleta hofu miongoni mwa watu.

          Siku hiyo hiyo tena lilipitishwa tangazo mjini Mwanza kwa kutumia vipaza sauti likisema hivi: “Kila anayejijua ni mganga wa kienyeji tukutane mahali tunapokutana kwa kuwa tumeingiliwa mjini Mwanza”. Hili lilikuwa jambo jipya lililowashangaza sana wakazi wa Mwanza waliolisikia – kuona ya kwamba ‘wachawi’ wanaitana mchana kweupe ili kupanga mikakati ya kupinga semina yetu isifanyike.

          Lakini mbinu zao zikashindwa! Asubuhi yake baadhi ya waombaji waliowahi kufika katika kiwanja cha Furahisha  (Mahali ambapo tulikuwa tufanyie semina) – walikuta watu wawili walioaminika kuwa wachawi ‘wamenasa’ hapo uwanjani!

          Siku hiyo hiyo baada ya mbinu hizo za kichawi kushindwa, kukazuka ugomvi kati ya polisi na baadhi wa waislamu uliosambaa sehemu kubwa ya jiji hilo. Ili tusijikute tumeingizwa katika mapambano hayo, tulikubaliana na kamati ya maandalizi ya semina kuhamisha semina yetu ili isifanyike katika kiwanja cha Furahisha na badala yake tukaifanyia katika kiwanja cha Nyakambungo.

          Laiti “shetani angejua asingemsulubisha Mwana wa Adamu”. Haya ni mawazo yaliyotujia mara tu baada ya mambo hayo kutokea. Maana kwa sababu ya vurugu – hizo kutokea, magazeti na radio na vituo vya televisioni yalitutangazia semina yetu bila malipo yo yote! Tena habari ziliposambaa nchi nzima watu wa Mungu wengi sana waliinuka kutuombea ulinzi, mafanikio na ushindi kwa ajili ya semina hiyo!

          Matokeo yake ni kwamba semina ilifanyika na ushindi mkubwa sana ulipatikana, na jina la Yesu Kristo likatukuzwa sana jijini Mwanza katika semina hiyo ya aina yake!

Maelfu ya watu wahudhuria….

….. na maelfu waokoka!

          Hii ilikuwa semina ya kwanza kwetu katika jiji la Mwanza kwa mfumo tunaofanya sasa sehemu mbalimbali nchini. Pamoja na kwamba ilikuwa ya kwanza mahudhurio yalikuwa makubwa. Makisio yaliyofanywa ya watu waliofika kwenye semina ni kati ya watu 7000 (elfu saba) mwanzoni mwa semina hadi kufikia watu 18,000 (elfu kumi na nane) kwenye siku za mwisho za semina.

          Tuliambiwa na kuona watu waliookoka toka kanda ya ziwa Victoria yote wakihudhuria semina hii. Tuliona watu kutoka nchi ya Kenya. Tuliona watu kutoka mikoa ya Kagera, Mara, Kigoma, Shinyanga na Tabora. Kuna watu wachache pia waliotoka Kilimanjaro na Dar es Salaam kwa lengo la kuhudhuria semina hii.

          Zaidi ya yote tunamshukuru Mungu sana kwa watu wengi waliookoka wakati wa semina. Tulioweza kuwaandika majina yao, ni wastani wa watu 4000 (elfu nne), ambao ndiyo waliookoka wakati wa siku za semina. Na wanatoka sehemu mbalimbali za kanda ya ziwa Victoria. Tunachomwomba Mungu katika hili ni awasimamishe waendelee kudumu ndani ya Yesu Kristo – asiwepo wa kurudi nyuma; bali waukulie wokovu siku zote za maisha yao.

Wagonjwa walipona…..

….. Jina la Yesu latukuzwa!

          Ni vigumu sana kuandika shuhuda zote za uponyaji tulizoziona na kuzisikia katika ripoti fupi ya namna hii, lakini tunaona tukushirikishe baadhi yake tu.

          Kuna mama mmoja ambaye alikuja katika siku za karibu na mwisho wa semina, kwa sababu alikuwa amesikia habari za wagonjwa waliokuwa wanapona wakati wa semina. Alipopata nafasi ya kushuhudia alisema alipofika hapo uwanjani alikuwa anaumwa sana kifua, sauti ilikuwa haitoki vizuri na alikuwa anakohoa sana.

          Akieleza yaliyotokea alisema alifika uwanja hapo akiwa anaumwa sana, na wakati wa maombi ya wagonjwa alikohoa sana na kutapika usaha mwingi. Maombi hayo yalipokwisha aliacha kutapika usaha, maumivu ya kifua yalipungua sana ila ilibaki kukohoa, na sauti yake ilikuwa haitoki vizuri.

          Tulimuuliza ikiwa aliwahi kwenda hospitalini kupima au kutibiwa. Akasema aliwahi kwenda hospitali na alipopimwa kilionekana kitu ndani ya pafu lake la kushoto kinachofanana na sindano. Haikujulikana hiyo ‘sindano’ iliingiaje! Na madaktari katika hospitali hiyo walishangaa na hawakujua la kufanya, isipokuwa waliimpa dawa za kupunguza maumivu – lakini hali ya mgonjwa iliendelea kuwa mbaya kila siku.

          Kwa hiyo aliposhiriki katika maombi hayo katika siku yake ya kwanza ya kuhudhuria semina hiyo alirudi nyumbani akiwa na nafuu kubwa sana baada ya kutapika ule usaha wakati wa maombi. Na akasema alipofika nyumbani aliendelea kukohoa kwa nguvu, huku akisikia mkwaruzo kwenye koo kila alipokuwa akikohoa.

          Aliendelea kukohoa – na baadaye akakohoa na kutema kitu toka mdomoni na kukwaruza kwenye koo kukakoma, maumivu yakaisha na sauti iliyokuwa imekwama ikaanza kutoka vizuri tu! Alipoangalia kile kitu alichokikohoa alishangaa sana na kushituka maana alikuwa ni mdudu aina ya mende mwenye umbo kubwa! Alimtukuza Mungu kwa uponyaji mkubwa namna hiyo – baada ya kuumwa na kuteseka kwa muda mrefu.

          Ndipo kesho yake baada ya kupona, akaja uwanjani hapo akiwa amepona, na amembeba yule mende aliyemkohoa akiwa amemfunga ndani ya karatasi ili kutuonyesha. Wakati mama huyo akielezea akaja daktari mmoja wa hospitali ya Aga khan aliyekuwepo katika semina siku hiyo na akamtazama yule mdudu na kuthibitisha ya kuwa alikuwa ni mende!

          Maelfu ya watu waliokuwapo kwenye semina siku hiyo – tulimtukuza Mungu sana pamoja na yule mama, kwa ajili ya uponyaji huo mkuu namna hiyo!

          Baba mmoja pia alipona goti lake la kushoto alilokuwa ameumwa kwa miaka mingi sana. Mungu alitupa “neno la maarifa” juu ya ugonjwa huo na tukatangaza juu ya mtu aliyekuwa anaumwa goti la kushoto kwa  miaka mingi bila kupona. Na goti hilo alikuwa ameumia akicheza mpira. Pia, Roho Mtakatifu alituonyesha alipokuwa amekaa. Kwa hiyo tulieleza yote hayo na kumwambia asimame ili apokee uponyaji wake. Aliposimama nguvu za Mungu zilimshukia na maumivu ya goti yakaisha wakati huo huo na akapona kabisa.

          Aliposimama kushuhudia uponyaji huo mbele za watu – alisema ameshangaa sana jinsi tulivyojua tatizo lake bila kuambiwa na mtu, na jinsi alivyopona hapo hapo baada ya kutii neno tulilomwambia la kusimama. Ndipo tulipoeleza kwa kifupi juu ya utendaji wa “karama ya neno la maarifa’ na kwamba sifa na utukufu zimrudie Yesu mwenyewe anayeponya watu apendavyo yeye! Sifa na heshima ni za Yesu Kristo peke yake! Na sisi tunasema Amina! Na wewe itikia – Amina!

Somo lilikuwa tamu….

…. Siku zaonekana chache!

          Wenyeji wa Mwanza walituambia ya kuwa semina hii ilikuwa ya aina yake ambayo haijawahi kutokea kwa ukubwa na jinsi ilivyoandaliwa. Walituambia ya kuwa, Mwanza kumewahi kufanyika mikutano mikubwa ya Neno la  Mungu, lakini ilikuwa ni mikutano ya kiinjilisti na siyo semina za mafundisho.

          Semina hii iliandaliwa na madhehebu yote ya kikristo yaliyotaka kushiriki na huduma mbalimbali za kikristo zilizotaka kushiriki. Tena pamoja na kwamba watu walikuwa wengi sana – bado walikaa katika hema tunayoitumia kwa semina hizi ambayo ina uwezo wa kukalisha watu 15,000 kwa mara moja. Tunaamini Mwanza na kanda yote ya ziwa Victoria ni maeneo ambayo kwa sasa yamo katika ukurasa mpya wa kiroho kufuatana na ratiba ya Mungu ya watu wa maeneo hayo.

          Somo tulilokuwa tumepewa kwa semina ya Mwanza lilikuwa na kichwa hiki: “Zijue Tabia za Upako wa Roho Mtakatifu Usaidike”. Tulisoma somo hili kwa muda wa siku saba mfululuzo. Kwa kifupi tulijifunza yafuatayo:

          Jambo la Kwanza: Pamoja na kwamba Yesu Kristo alimtambulisha Roho Mtakatifu kama Msaidizi Mwingine kwa ajili yetu. Lakini tuliona ya kuwa:

  • Huwezi kutafuta msaada usiouhitaji
  • Huwezi kutafuta msaada mahali ambapo hujui kama utaupata hapo
  • Unaweza kuletewa msaada na usijue namna ya kuutumia kwa hiyo usisaidike ipasavyo.
  • Unaweza kuletewa msaada kwa njia ambayo wewe huitaki au hujaizoea. Kwa mfano Msaada wa Mungu unaotujia kwa njia ya Roho Mtakatifu.

Jambo la Pili: Tuliweza kuangalia juu ya Tabia 3 zifuatazo za Upako wa Roho Mtakatifu,

  • Tabia ya 1: Upako wa Roho Mtakatifu unagawanyika kwa vipimo, lakini Roho Mtakatifu hapimiki na hagawanyiki.
  • Tabia ya 2: Upako wa Roho Mtakatifu unajidhihirisha kwa wakati maalumu ili kulitimiza kusudi la Mungu katika eneo Fulani.
  • Tabia ya 3: Upako wa Roho Mtakatifu unajidhihirisha kwako unapoamua kupata kile ambacho Neno la Mungu limesema utakipata kwa msaada wa upako huo.

Jambo la Mwisho: Tulikumbushana ya kuwa ukizijua Tabia za Upako wa Roho Mtakatifu itakurahisishia namna ya kuutumia na ukusaidie. Kwa mfano Karibu kila ahadi ya upako iliomo katika Neno la Mungu ina sehemu tatu: (1) Aina ya upako unaoahidiwa kwako (2) Lengo au kazi ya huo upako; na (3) Unachotakiwa kukifanya ili upako ujidhihirishe kwako.

Shukrani

          Ahsante kwa kutuombea, tena ahsante kwa mchango wako uliotusaidia kuifanikisha semina hii ya Mwanza. Mungu wetu akubariki sana, tena sana. Kumbuka tunakuombea pia. Tumemaliza semina nyingine kubwa nzuri Arusha Mjini iliyofanyika tarehe 28 Septemba – 6 Octoba 2003. Ripoti yake inafuata baada ya muda si mrefu. Semina ambazo zinafuata ni Mbeya ( 5 -9 Novemba 2003), Kilombero ( 12 – 16 Novemba 2003) na Dar es Salaam ( 17 – 21 Disemba 2003). Usisahau kutuombea, sisi, na pia kuombea semina hizi na ikiwezekana uhudhurie katika semina hizi.

(Semina ya Mwanza katika picha)

UNATAKA KUOKOKA?
Kama unataka kumpa YESU maisha yako sasa, bonyeza hapa
©2003 Tanzania Social and Economic Trust.  All Rights Reserved.