|
"Kila
aliye na Mwana anao huo ushuhuda"
kwa hiyo kama una
ushuhuda wowote ambao Mungu amekutendea usisite kututumia ili
tuweze kuuchapisha uwasaidie na kuwajenga wengine kwa ajili ya
utukufu wa Mungu.
Shuhuda
za Matendo
makuu ya Mungu zinaandaliwa kwa ajili ya kuchapishwa mahali hapa
Zifuatazo
ni Shuhuda mbalimbali zilizochpishwa mahali hapa:
|
"Tangazeni
wokovu wake siku kwa siku (kila siku hubirini) habari
za utukufu wake habari za maajabu yake"
(Zaburi 96:2,3)
|
Tunakukaribisha
katika ukurasa huu muhimu ambao tutakuwa tunakuwekea habari za
matendo ambayo Mungu anawatendea watu kupitia huduma mbalimbali
alizotupa.
Kwa wakati huu Mungu ametupa kuwahudumia watu sehemu mbalimbali
kwa njia ya mahubiri/mafundisho; kwa njia ya maombi; kwa njia ya
mtandao; kwa njia ya simu; kwa njia ya majarida na vitabu; na
kwa njia ya barua.
Tumeona na kuelezwa mambo mengi sana ambayo Yesu amekuwa
akiyafanya kupitia huduma alizotupa.
Faida
zake:
Si
watu wengi wanaopenda kuwaeleza wengine mambo ambayo Mungu
amewatendea. Lazima wana sababu zao mbalimbali zinazowafanya
wasiseme habari hizo kwa uwazi. Lakini tunataka kukueleza ya
kuwa kuna faida nyingi zinazopatikana kwa kushuhudia wengine
mambo ambayo unajua Mungu anafanya kwako na kwa wengine. Kwa
mfano tafakari faida zifuatazo za kushuhudia matendo makuu ya
Mungu:
1. Kuthibitisha ya kuwa Yesu Kristo yuko hai na ya kuwa ndiye
Mwana wa Mungu. Soma katika Matendo 3:1-16. Pia angalia Yohana
20:30,31 pale inaposema:
"Na kuna ishara nyingine nyingi alizozifanya Yesu mbele ya
wanafunzi wake zisizoandikwa katika kitabu hiki. Lakini hizi
zimeandikwa; ili mpate kuamini ya kwamba Yesu ndiye Kristo,
Mwana wa Mungu; na kwa kuamini mwe na uzima kwa jina lake"
2. Kuwavuta watu na kuwaweka katika hali ya kuhubiriwa injili.
Yesu Kristo alisema, " Nami nikiinuliwa juu ya nchi,
nitawavuta wote kwangu" ( Yohana 12: 32). Unapotangaza
mambo ambayo Yesu anafanya sasa ni njia mojawapo ya kumwinua.
Ukisoma katika Yohana 6:2 utaona imeandikwa hivi: " Na
mkutano mkuu wakamfuata, kwa sababu waliziona ishara
alizowafanyia wagonjwa"
Kuna wakati mmoja karibu miaka kumi hivi imekwisha kupita
tuliletewa nguo nyumbani kwetu Arusha ya kijana wa kutoka
Likamba aliyekuwa mgonjwa ili tuiombee. Huyo kijana alikuwa na
uvimbe katika paji la uso wake ambalo hata baada ya kulazwa kwa
matibabu hopitalini hakupona.
Tuliombea hiyo nguo, na akapelekewa. Hiyo nguo ilipomgusa tu
usoni, uvimbe ule uliyeyuka na kupotea. Akapokea uponyaji wake
toka kwa Yesu! Jambo hili lilifanya mama yake na ndugu zake
watake kujua zaidi habari za nguvu zinazoponya namna hiyo.
Walipoletwa kwetu tukawaeleza habari za Yesu na wakakubali
kuokoka - tukawaongoza sala ya toba - wakaokoka. Hata sasa miaka
kumi baadaye, bado wanaendelea na Yesu!
Jirani zao wengine ambao walikuwa wameoana lakini bila kujaliwa
mtoto kwa miaka mitano walipata habari za Yesu anayejibu!
Walipoletwa kwetu kuulizia habari hizi tukawaeleza habari za
Yesu, wakakubali kuokoka - tukaomba nao wakaokoka! Tuliomba pia
juu ya hitaji lao la mtoto - na Mungu akajibu na kabla ya mwaka
mmoja kwisha toka wakati huo wakajaliwa kupata mtoto wa kiume!
Kwa sababu ya miujiza hii mfululizo, tukaitwa kijijini kwao
kuhubiri injili na kuombea wenye shida. Tulikwenda kijijini hapo
tukahubiri habari za Yesu, watu wengi wakaokoka na kupona
magonjwa yao. Kumbuka mambo yote haya yalianza baada ya kijana
mmoja kutangaza habari za uponyaji wake, ambao ndio uliowavuta
wengine kuulizia habari za Yesu aliyemponya!
3. Kuwatia moyo waliokata tamaa na walio na mahitaji wajue ya
kuwa Mungu anaweza kuwasaidia na wao pia katika matatizo yao.
Ni kwa njia hii hata Naamani alipata kupokea uponyaji wa ukoma
uliokuwa unamsumbua. Ukisoma kitabu cha pili cha Wafalme 5:1-14
Naamani alipata habari za Mungu anayeponya kwa njia ya maelekezo
ya watumishi wake kutoka kwa mwanamke kutoka nchi ya Israeli
aliyekuwa anamhudumia mke wake.
Hata leo kuna watu wengi wanaoteseka katika matatizo yao kwa
sababu tu hawajawahi kusikia habari za Yesu anayejibu maombi na
kuponya magonjwa siku hizi.
Kuna wakati tulipigiwa simu kutoka Mbeya na mtu ambaye alikuwa
amesikia habari za Yesu anayejifunua katika maisha yetu. Alisema
ya kuwa anaumwa na anahitaji maombi - tukaomba pamoja naye
kwenye simu, na Mungu akamponya wakati huo huo! Mwingine
akatupigia simu kutoka Tukuyu - Mbeya akisema anaumwa na anaona
hatapona alikuwa anahitaji tumuombee aokoke. Tukaomba naye
kwenye simu - naye akaokoka!
Hawa walitupigia simu kwa kuwa walikuwa wameambiwa habari za
Yesu tuliye naye - na walipowasiliana nasi tukawaelekeza kwa
Yesu naye akawasaidia mahitaji yao.
4. Kuwatia moyo watumishi juu ya neno wanalohubiri na maombi
wanayofanya kwa watu mbalimbali.
Katika Marko 16:20 imeandikwa hivi:
"Nao wale wakatoka, wakahubiri kotekote, Bwana akitenda
kazi pamoja nao, na kulithibitisha lile neno kwa ishara
zilizofuatana nalo"
Watumishi wa Mungu wanaposikia mambo ambayo Yesu anafanya
wanaposema neno lake au wanapoomba kwa Jina lake - wanatiwa moyo
ya kuendelea katika huduma hizo.
Alichosema Mfalme Daudi
Mfalme Daudi katika Zaburi alizoziandika unaona kabisa
anavyosisitiza umuhimu wa kusifu na kutangaza habari za Mungu
wetu na matendo yake katikati yetu.
Katika Zaburi 96:2,3 anasema, " Tangazeni wokovu wake siku
kwa siku, (kila siku hubirini) habari za utukufu wake, (((
habari za maajabu yake". Anaendelea katika mistari ya 4
hadi 6 kutoa sababu anaposema:
"Kwa kuwa Bwana ni mkuu mwenye kusifiwa sana. Na wa
kuhofiwa kuliko miungu yote. Maana miungu yote ya watu si kitu,
lakini Bwana ndiye aliyezifanya mbingu. Heshima na adhama ziko
mbele zake, nguvu na uzuri zimo katika patakatifu pake".
Katika Zaburi ya 44:1, Mfalme Daudi anaeleza jinsi walivyoelezwa
na baba zao habari za matendo makuu ya Mungu wao. Katika Zaburi
za 92 na 98 anahimiza watu kusifu kwa nyimbo matendo makuu ya
Mungu! Katika Zaburi ya 119:95,99 anaeleza jinsi
anavyozitafakari na kuzifikiria shuhuda za Mungu! Lazima ndani
yake alijua wazo linalosema; "There is no God like our God
of Israel!".
Na
sisi Je!
Nasi
tunasema, "There is no Jesus like our Jesus Christ!"
Ndiyo maana tumeona tuwe na ukurasa huu unaoleza mambo ambayo
Mungu anayafanya wakati huu katika huduma alizotupa kwa njia ya
Mwana wake Yesu Kristo. Nia yetu si kujiinua sisi katika haya
utakayokuwa unayosoma, bali kumwinua Yesu Kristo, ambaye peke
yake ndiye anayestahili sifa na heshima zote! Maana ni Yeye
ndiye ayafanyae yote haya kwa uwezo wa Roho wake Mtakatifu!
Sasa endelea kusoma shuhuda hizi - zingine ni barua
tulizoandikiwa na zingine ni maelezo tuliyoyachukua moja kwa
moja:
NIMEPONA
TUMBO LA UZAZI
Mpendwa
Mtumishi wa Mungu
Ndugu Christopher Mwakasege.
Nakusalimu katika Jina la Bwana.
Ni matumaini yangu kwamba umzima pamoja na familia yako na Bwana
anakuwezesha katika wito aliokuitia. Bwana asifiwe sana. Mtu wa
Mungu nimeshindwa kunyamaza kwa makuu Mungu alionitendea siku
ile ya tarehe 8/8/1999 siku ambayo ilikuwa ni ya mwisho wa
semina uliyofundisha pale Diamond Jubilee.
Nilikuwa na shida kubwa ya tumbo la uzazi karibu mwaka wa pili
sasa, naumwa lakini navumilia nikijua kwamba ipo siku Mungu
ataniponya tu. Nilijificha sana ili shida hii wengine wasiijue
lakini mume wangu alijua na alinitia moyo sana akaniambia Mungu
atakuponya siku isiyokuwa na jina. Namshangaa Mungu siku ile ya
Jumapili ulivyosema kila mtu ashike mahali panapouma nilishika
tumbo langu sehemu ya uzazi. Ukaomba na mimi nilikuwa naomba
ulivyosema kwamba Mungu amekuponya vidonda na uvimbe kwenye
tumbo la uzazi.
Mtumishi wa Mungu ni kwamba ile hali niliyokuwa nayo ya kutisha
hata kukaa nilikuwa napata shida sana kwa jinsi ambavyo damu
zilikuwa zinatoka lakini muujiza nilioupata ni kwamba damu
zilikauka pale pale na ndipo nilijua na kukumbuka maneno mume
wangu aliyokuwa ananifariji nayo kuwa siku isiyokuwa na jina
Mungu atakuponya; kweli ni ajabu namshukuru sana Mungu kwa tendo
hili kubwa kwangu. Mungu azidi kukubariki katika utumishi huu;
na azidi kukutumia katika nyakati hizi za mwisho. Katika macho
ya kibinadamu hunijui lakini macho ya kiroho unanijua hata na
sura yangu maana Mungu alikuonyesha shida yangu.
(- toka Dar es Salaam)
NIMEPONA
KUPITIA MAJARIDA YA MANA
Wapendwa
katika Kristo Yesu
Baba C. Mwakasege na Mama D. Mwakasege.
Ninayo matumaini makubwa kwa upendo wake Mungu Baba kuwa Mungu
anawatia nguvu, mu ngali bado wazima kimwili na kiroho.
Namshukuru Mungu yeye yule jana, leo na hata milele anayenitia
nguvu kila iitwapo leo. Nilikuwa na jeraha moyoni, Mungu
awabariki kwa kuniponya kupitia majarida ya MANA mliyonitumia.
Na washukuru sana Mungu awasaidie kwani ALICHOANZISHA MUNGU
shetani HAWEZI KUZUIA.
1. Naomba tuzidi kuombeana na Mungu awabariki kujitoa kwenu.
2. Naomba maelezo zaidi juu ya huduma yenu.
3. Nategemea majarida matoleo mengine toka kwenu
(- toka Tukuyu)
SHUKRANI
YA PEKEE
Hii
ni shukrani kwa Mungu kwa mambo makuu ambayo Mungu amenitendea.
1. Amemponya mtoto wangu aliyekuwa katika hali mbaya sana ya
ugonjwa.
2. Terehe 20/02/2000 katika semina ya C. Mwakasege mtoto huyo
aliokoka na kukabidhi maisha yake kwa Bwana Yesu.
Hivyo basi ninaomba shukrani hii itumike kama mchango katika
huduma ya mikutano au semina hizo za Mwakasege ili wengine nao
waje kwa Yesu. Ninamtolea Mungu shs. 20,000/=
(- toka Dar es salaam)
NIMEPONA
KIFUA
Mpendwa
C. Mwakasege, Bwana asifiwe.
Ninakusalimu kwa jina la Bwana Yesu. Mwaka jana (1999)
nilikuandikia barua nikihitaji uniombee. Nilikuwa na maumivu
kifuani ambayo hayakujulikana yanatokana na nini, ingawa
nilipiga x-ray.
* Ninayo furaha kukushukuru kwa maombi yako kwani Bwana Yesu
aliniponya.Roho wa Mungu alinionyesha katika ndoto kuwa
unaniombea. Ninamtukuza na kumbariki Bwana!!
* Ikiwezekana ninaomba na mimi, nitumiwe gazeti (Jarida) la MANA
ili tushirikiane baraka za Mungu.
(- toka Dar es Salaam)
KITABU
CHA DAMU YA YESU KIMENISAIDIA
Mpendwa
katika Bwana.
Tumsifu Yesu Kristo, Mimi nimeolewa ni mama wa watoto watano pia
ni mkatoliki.
Nimepata mengi sana baada ya kusoma kitabu chako cha "Fahamu
Uwezo wa Damu ya Yesu Kristo". Nimekubali kweli Mungu
alikuwa na mpango nami kuweka hicho kitabu mikononi mwangu.
Kwani mambo yote yaliyoandikwa nimeyaweka katika matendo na
nimeona majibu, ya ukweli kabisa yaani HAI kabisa Jina la Bwana
libarikiwe. Kabla ya kusoma kitabu hicho nilikuwa na shida
nyingi mno kiroho pia kimwili.
Lakini Mungu ni wa ajabu sijui Ndugu nikueleza nini; kwenye
barua siwezi ni mengi mno. Ninachosema tu ninamshukuruni sana
Mungu Baba wa Mbinguni, ninaishukuru pia sana tu Damu ya Yesu
Kristo kwa yote hayo niliyoyapata.
Uzima wa milele nimeuona katika damu ya Yesu, uzima, uponyaji,
amani, upendo, utajiri na kufanikiwa na baraka zingine za Mungu.
Maisha ya ndoa nilikuwa ninayaona magumu sana!! Lakini sasa
sivyo, kwenye ukurasa unapotaka kusafiri ufanye nini? Mungu
amenitendea makuu pamoja na Damu ya Yesu.
Sasa ndugu ninachokuomba, tafadhali unitumie vijitabu vingine au
makaratasi mengine ili niweze kuimarika zaidi katika Neno la
Mungu, kwani mambo yote yatapita lakini Neno litasimama.
Pia katika sala zako uniombee ili nizidi kuimarika zaidi na
zaidi.
Ninasubiri kwa hamu kuliko yule anayesubiri kufunga harusi.
Nikitumaini Bwana atakugusa kwa njia ya pekee uweze kunitumia
hivyo vijitabu vya Neno la Mungu.
(- toka Morogoro)
NIMEPONA
TUMBO LA UZAZI
Mtumishi
wa Mungu.
Bwana asifiwe.
Ninakuandikia, kumrudishia Mungu utukufu kwa matendo makuu
aliyonitendea. Siku ya tarehe 6/8/1999 nilipokea uponyaji.
Nilikuwa ninasumbuliwa na tumbo la uzazi Mwezi Machi/1999
nilipata tatizo la kutoka damu muda mrefu. Nilikwenda hospitali
nikasafishwa - lakini ziliendelea mwezi mzima. Mwezi April na
May nilipata damu kwa matatizo. Mwezi wa sita tatizo
liliongezeka, damu zilikatalia tumboni. Nilipata taabu sana.
Nilikuwa likizo wakati huo. Nikiwa na mama yangu - siku moja
usiku niliona kifo kiko mbele yangu. Mama ameokoka katika huduma
yako pale Iringa.
Alisogea kitandani akaniuliza vipi? Kwa kutaka nisimfadhaishe,
nilimwambia niombee, akaomba, nikalala asubuhi yake nilianza
kupata nafuu tangu tarehe 1 / 7 zilikoma 14/7. Tarehe 2/8 tatizo
lilianza tena. Tarehe 6/8 wakati maombi yanaendelea wakati wa
semina yako, Diamond Jubilee, nikiwa pale mbele, nilipokea
uponyaji, damu ziliacha kububujika palepale. Mpaka dakika hii
naandika - nimepona kabisa. Asante Yesu.
(- toka Dar es Salaam)
NINA
NENA KWA LUGHA
Dhumuni
la barua hii ni kushukuru kwa nakala ya kitabu cha Hongera kwa
Kuokoka nasema ahsante Mungu akubariki. Nilifurahishwa sana na
semina ambayo ilifanyika kanisani ARUSHA mjini kati.
Nilifurahi
kwa sababu nilipata mambo mengi nilijiona nilikua niko nyuma
sana lakini sasa naona Mungu ananisaidia na furaha yangu kubwa
zaidi ni kwamba nilikua sina Roho Mtakatifu lakini semina hiyo
nilifaidi nilikua sijawahi kunena kwa lugha lakini nilifurahi
sana sasa nina Roho Mtakatifu ninanena kwa lugha, nina furaha
isiyokifani.
(- toka Arusha)
|