|
MAMBO YA
KUTAFAKARI KABLA YA KUFANYA
UAMUZI WA KUOA AU KUOLEWA
Utangulizi
Ukifungua
kitabu cha Yoeli.3:14 kinasema, “Makutano makubwa, makutano
makubwa, wamo katika bonde la kukata maneno! Kwa maana siku ya
Bwana i karibu”. Huyu ndugu, mtumishi wa Mungu, aliyekuwa
anaitwa Yoeli, Mungu alimpa nafasi ya kuona mambo ambayo
yamekuwa yanafanyika tangu kuumbwa kwa ulimwengu, mpaka hapo
Yesu atakaporudi tena. Anasema, ameona makutano makubwa,
makutano makubwa, katika bonde la kukata maneno.
Tafsiri
nyingine ya bonde la kukata maneno maana yake ni bonde la
kufanyia maamuzi. Kukata maneno ni kufanya maamuzi. Sasa, bonde
la kukata maneno, kwa tafsiri ya haraka ni dunia hii, wakati huu,
mwanadamu anapoishi duniani.
Kwa sababu
kabla hujazaliwa huna uwezo wa kuamua. Biblia inasema Mungu
alimwambia Yeremia, “Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua,
kabla hujatoka tumboni nalikutakasa” (Yeremia 1:5). Kabla
hajawekwa tumboni mwa mama yake, Mungu alimjua Yeremia, ambayo
inamaanisha Yeremia alikuweko, lakini alifananaje sijui! Lakini
maandiko yananiambia ya kwamba alikuwepo na Mungu alimjua.
Alipokuwa tumboni Mungu alimtakasa, maana yake alimtenga kwa
ajili ya utumishi na wito wake.
Lakini
Yeremia hakuwa na uwezo wa kuamua. Kabla ya kuzaliwa huwezi
kuamua, baada ya kufa huwezi kuamua kitu chochote. Ndio maana
tunatamani kila mtu lazima aokoke, aamue anataka kuishi maisha
ya namna gani baada ya kufa, maamuzi hayo unayafanya kabla
hujafa. Baada ya kufa hakuna mahali pa kufanyia maamuzi hayo
tena!
Kwa hiyo
kipindi hiki, ambacho mwanadamu anaishi ndicho kipindi cha
kukata maneno. Bonde la kukata maneno ni dunia hii. Makutano
makubwa; maana yake aliona watu wengi sana wamekaa katika bonde
ambalo wanatakiwa kufanya maamuzi.
Katika
dunia hii, (Kama ulikuwa hujafahamu afadhali ufahamu), ya kwamba
kati ya jambo muhimu sana ambalo utawajibika nalo mwenyewe ni
kufanya maamuzi. Na yako maamuzi ambayo unahitaji kuwa
mwangalifu sana unapotaka kuyachukua, kwa sababu yatasababisha
mabadiliko ya maisha yako kabisa.
Kwa mfano
maamuzi ya kuokoka, kwa mfano maamuzi ya kumtumikia Mungu,
yanabadilisha kabisa maisha yako, ndio maana Yesu anasema, mtu
kabla hajamfuata, akae chini, ahesabu gharama; kuna gharama
katika kumfuata Yesu, na kuna gharama katika kumtumikia Yesu.
Maisha yako yanabadilika kabisa! Huwa saa nyingine mimi na mke
wangu tunatamani kuishi maisha ya kawaida kama watu wengine,
lakini haiwezekani, (watumishi wa Mungu wataelewa kitu ninacho
elezea hapa), ukiishafanya maamuzi ya kusema unataka kumtumikia
Mungu, maisha yako hayawezi kuwa ya kawaida tena, sio maamuzi
madogo hayo.
Kuna
maamuzi ya masomo, watu wanafanya mchezo wanapotaka kufanya
maamuzi ya masomo, usifanye mchezo, ni maamuzi muhimu. Kuna
maamuzi ya marafiki, unataka kuwa na marafiki wakina nani.
Maamuzi haya yanaweza yakakubadilishia kabisa maisha yako.
Lakini pia kuna maamuzi ya unachotaka kufanya maishani mwako ni
nini. Mwingine atajitetea na atasema, Mungu anajua, - sawa
Mungu anajua, lakini anahitaji maamuzi yako!
Wengine
wanasubiri wakiishamaliza sekondari, au wakiishamaliza chuo
kikuu, ndipo waamue wanataka kufanya nini. Ukiishafika chuo
kikuu ndipo unataka kuamua cha kufanya maishani, utakuwa
umechelewa. Kwa sababu, kama unataka kuamua kufanya kitu ambacho
hukusomea, mambo yanawezayakawa magumu kwako, labda iwe ni Mungu
anakupitisha hapo kwenye eneo hilo jipya.
Lakini pia
kuna masuala ya kuamua kuoa au kuolewa, katika somo hili tutaangalia
somo linalosema, “Mambo ya kutafakari kabla ya kufanya
uamuzi ya kuoa au kuolewa”. Wengine mnaosoma somo hili ni
vijana ambao umri wa kufikia kuolewa bado, lakini huu ni muda
muafaka wa kukufikirisha jambo hili. Wengine wanaosoma somo hili
wana karibia - karibia kuoa au kuolewa; au wameshaingia kwenye
ndoa tayari. Halafu wanajikuta ya kwamba, afadhali wangekuwa
wamejiuliza na kutafakari yaliyomo humu mapema zaidi.
Kwa muda
ambao Mungu ametupa wa kuwahudumia watu mbalimbali katika miaka
ya utumishi ambayo Mungu ametupa, kati ya jambo ambalo
limesababisha maisha ya watu wengi yakawa mabaya au yakawa
mazuri, yakawa magumu au yakawa marahisi, ni suala la kuoa au
kuolewa.
Saa
nyingine huwa ninawaambia vijana, Kama kijana anataka kuoa au
kuolewa na ana haraka sana ya kutaka kuoa au kuolewa, basi asije
kwangu kwa ushauri! Kama unataka kuoa au kuolewa, na una haraka
sana ya kufanya hivyo tafadhali usije. Kwa sababu mambo
niliyoyaona kwenye ndoa mbalimbali yananifanya hata mtu akija
kwa ushauri wa kutaka kuoa au kuolewa, nimpitishe kwenye maswali
magumu sana yatakayomfanya atafakari sana na kuomba kabla ya
kuamua kuoa au kuolewa.
Nia
niliyonayo ni ili nijue kama kweli amefikia mahali ambapo anajua
kitu anachotaka kufanya. Maana wengi wanafikiri ni jambo rahisi.
Mungu wangu aweze kukusaidia kuona ili usilichukuie jambo hili
kwamba ni jambo jepesi, maana linabadilisha kabisa maisha yako.
Mambo ya
Kutafakari Vijana / utang / 1 /
2 / 3 / 4 /
5 / 6 /
7 /
8 /
9 /
10 /
11 /
|