|
MAMBO YA
KUTAFAKARI KABLA YA KUFANYA
UAMUZI WA KUOA AU KUOLEWA
Wiki ya
Tatu
Jambo
la Tatu
Ukiamua kuoa au kuolewa, wakati mwingine
imani yako inaweza ikabadilika.
Wasomaji
wa biblia wanamfahamu mtu mmoja aliyeitwa mfalme Sulemani (unafahamu
ni kwa nini aliandika kitabu cha Mhubiri, maana alipoandika
kitabu cha Mhubiri akasema, mambo yote chini ya jua ni ubatili
mtupu). Biblia inatuambia wazi kabisa ya kuwa Mungu alimpa
hekima ya ajabu, na wasichana wakatoka sehemu mbali mbali
duniani kwenda kufuatilia ile hekima, walipoikuta hawakutaka
kuondoka na wakabaki pale kwake.
Kosa
alilofanya Sulemani ni kwamba wale wasichana walikuwa wanakuja
na miungu yao, na alikuwa anawakaribisha wale wasichana na
miungu yao, anawapa na mahali pa kujengea vibanda vya miungu yao.
Biblia inatuambia wazi kabisa, ilifika mahali wale wakina mama
wakamgeuza moyo wake usiendelee kumpenda Bwana.
Kitabu cha
1 Wafalme 11:4 kinasema hivi: “Maana ikawa, Sulemani
alipokuwa mzee, wake zake wakamgeuza moyo wake, afuate miungu
mingine, wala moyo wake haukuwa mkamilifu kwa BWANA Mungu wake,
kama moyo wa Daudi baba yake.”
Nimeona
vijana wengi sana ambao wanakuwa moto sana kwenye wokovu kabla
hawajaolewa au kuoa, wewe ngoja waingie kwenye ndoa na
wafuatilie baada ya muda, utakuta wengine wamepoa mpaka
wameganda kama barafu! Ukiwauliza ni nini kimewafanya wapoe
kiroho kwa kiwango hicho - wanaweza wakashindwa kusema. Maana
kuna watu wengine wanafikiri ni kuolewa tu na mtu yoyote kwa
sababu tu anasema Bwana asifiwe, ibilisi Pia huwa anaweka na
watu wa kwake huko ndani ya makundi ya watu waliookoka.
Na ukikaa
na vijana utapata baadhi yao wanaosema, ukitaka kupata vijana
waaminifu siku hizi nenda katikati ya waliokoka, kwa hiyo
wanajifanya wameokoka. Akikufuatilia juu ya kuoana na ukimwambia
mbona wewe hujaokoka, na ukamtaka kwanza aokoke ndipo mzungumze,
utakuta baada ya siku chache kupita anajifanya ameokoka, lakini
ni yakubabaisha tu ili akupate. Nimekutana na watu wa namna
hiyo, msichana anaolewa akishafika ndani, ndio kijana anamwambia,
na Yesu wako na wokovu wako nauvua hapa hapa, mimi nilikuwa
nakutafuta wewe, nimekupata basi!
Nimeona!
Sisemi kitu cha hadithi, ninasema kitu ambacho nimeona kwa
macho. Ikiwa umefika katika hali hii basi, ni mpaka kifo
kiwatenganishe, na alikwishawaambia wenzake kwamba Mungu
amenifunulia; kwa hiyo hana ujasiri wa kurudi na kusema kweli
nilikuwa nimekosea, yalikuwa ni mafuniko sio mafunuo! Akitaka
kwenda kwenye maombi anaambiwa hakuna; akitaka kwenda kuhudumu
anaambiwa hakuna; anataka kwenda ‘fellowship’, anaambiwa hakuna;
kaa hapo ndani. Kwa hiyo inabaki kazi moja tu ya kuombea chakula
na chai na kwenda kulala!
Na ni kwa
sababu huyu mtu hakufikiri sawasawa, hakukaa akaona jinsi
ambavyo hili jambo linaweza likambadilishia imani yake kabisa.
Wewe nenda kwenye maandiko, utaona ya kuwa ndoa inaweza
ikakubadilisha. Ndio maana kuna watu wengine wanaolewa, na
wengine wanaoa na wanabadilisha dini, hii sio kitu cha mchezo,
ni maamuzi magumu sana kuyafanya.
Unapobadilisha imani yako unabadilisha msingi wako kabisa wa
maisha yako; kwa hiyo ni lazima uamue jambo ya kuoa au kuolewa
kwa uangalifu sana.
Lakini pia
inaweza ikawa ni mkristo kwa mkristo wanataka kuoana, lakini
fahamu kuoa au kuolewa kunaweza kukakubadilisha dhehebu lako la
kikristo, ndio maana lazima mkubaliane juu ya jambo hili kabla
ya kuingia kwenye ndoa. Nilikuta vijana wamekubaliana kuoana,
kijana mmoja mlutheri, kijana mwingine mpentekoste. Mambo yakawa
magumu sana kwao, walipofika masuala ya kujadiliana, juu ya
imani zao. Ilikuwa ngumu sana, mpaka wachungaji wao wakaingilia
kati.
Walipokuja
kuniona, nikawauliza mko tayari kabisa na mnataka kuoana?
Wakasema, ndio. Wakati huo walipokuja kwangu walikuwa tayari
wameshaenda nyumbani kwao, wameshazungumza na wazazi wao, na
kote huko na wakati wote huo hawakufikiria hilo jambo. Sasa
imefika mahali mchungaji wa kanisa hilo la pentekoste hakubali
msichana wake aolewe kwa kijana wa kilutheri. Nikamuuliza
maswali yule msichana akashindwa kujibu.
Unajua
wapentekoste hawabatizi watoto, walutheri wanabatiza watoto.
Mnapooana matokeo yake ni kwamba watoto watazaliwa. Ni lazima
hicho kitu ufikiri kabla hajasema ndio kuolewa, au ndio kuoa.
Sio umekwisha olewa ndipo unasema watoto wangu hawawezi kwenda
huko, - ulikuwa wapi toka mapema ili uliseme hili tatizo? Maana
unaweza ukafikiri ni masuala marahisi, sio masuala marahisi.
Maana
wengine wanalichukulia jambo hili kirahisi, wakati jambo lenyewe
sio rahisi. Masuala ya kwenda kusali kanisa tofauti tofauti huku
mmeoana sio mambo rahisi. Nimeona watu wakisema hakuna tatizo
maana tutaoana, lakini kila mtu wetu atakuwa anakwenda kanisani
kivyake; sawa, ninyi mnaweza mkaenda kivyenu, na watoto je?
Labda kama hamna mpango wa kuzaa!
Maana
niliona kwenye TV, mtu mmoja, - dada mmoja huko ulaya amefuga
mbwa akasema, tuliamua huku ndani tusizae watoto na badala yake
tumefuga mbwa badala ya mtoto, wamempa na jina, wamempa na
chumba wamempa na kitanda, anasahani yake, na bajeti yake, ana
daktari, wameamua wasizae na badala yake, wamefuga mbwa! Labda
kama unataka kuelekea njia hiyo! Lakini kama unaingia kwenye
ndoa na unajua utakwenda kupata mtoto, suala la mahali
mnapokwenda kusali ni muhimu sana kulijadili na kuliamua kabla
ya kuingia kwenye ndoa.
Usiende
kupeleka vita kwenye ndoa yako ambayo haitakiwi kuwepo! Unajua
kuna vita vingine tunavianzisha bila sababu, hata Yesu alijua,
wakati saa yake ya kupigwa mawe ilipokuwa haijafika, alikuwa
anawakwepa wale watu waliokuwa wamepanga kumpiga mawe. Sasa kama
Yesu alikuwa anakwepa majaribu mengine kwa nini wewe
unajitumbukiza? Saa ikifika ya jaribu kuja kwako utalishinda tu,
kwa sababu umetengenezwa na Mungu uwe na uhakika wa ushindi, kwa
sababu ukiwa ndani ya Kristo unashinda na zaidi ya kushinda.
Imeandikwa
hivi katika kitabu cha Warumi 8:37; “Lakini katika mambo
hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye
aliyetupenda”. Lakini majaribu ya kujitafutia, yanaweza
yakayumbisha imani yako.
Maana
watu wengi sana huwa hawajiulizi hili swali mapema lakini
nimeona likiwapa shida. Wengine hata imefika saa ya kufunga ndoa,
ndio kwanza wanaanza kujiuliza, ‘ndoa sasa tunakwenda kufungia
wapi’, hilo sio swali la kujiuliza saa hiyo, utakuwa umechelewa!
Wewe ulikuwa unajua kabisa mwenzako anasali mahali fulani, na
wewe unasali mahali pengine, imefika saa mnataka kufunga ndoa
mnaanza kujiuliza, tukafunge ndoa kwenye kanisa la nani,
ikiishafika hapo mnaanza kushindana na kuvutana; na haifai mambo
kuwa hivyo.
Mambo ya
Kutafakari Vijana / utang / 1
/
2 / 3 / 4 /
5 / 6 /
7 /
8 /
9 /
10 /
11 /
|