|
MAMBO YA
KUTAFAKARI KABLA YA KUFANYA
UAMUZI WA KUOA AU KUOLEWA
Wiki ya
Nne
Jambo la Nne
Uamuzi wa
kuoa au kuolewa ni muhimu uwe mwangalifu nao,
kwa sababu utakufanya uwajibike zaidi.
Kama
hujawa mtu wa kuwajibika, basi, hujawa tayari kuwajibika, kwa
hiyo usiingie kwenye ndoa! Kuoa au kuolewa kunakufanya uwajibike
zaidi, maana yake ni kutafuta wajibu mkubwa zaidi.
1Timotheo
5:8 anasema, “Lakini mtu ye yote asiyewatunza walio wake,
yaani wale wa nyumbani mwake hasa, ameikana Imani, tena ni mbaya
kuliko mtu asiye amini”, maana yake ni mbaya kuliko mtu
ambaye hajaokoka. Afadhali mtu yule ambaye hajaokoka. Huyo
ambaye ameokoka, lakini hatunzi watu wa nyumbani mwake hasa,
ameikana Imani, maana yake amemkana Yesu; ni mbaya kuliko hata
mtu ambaye hajaokoka.
Hii
inaonyesha ya kuwa unaweza ukaingia kwenye ndoa ukapoteza
wokovu wako, ukakosa kwenda mbinguni, si kwa sababu umefanya
dhambi ya uasherati, lakini kwa sababu umeshindwa kutunza watu
wa nyumbani mwako, na kwa ajili hiyo unahesabika kuwa umeikana
imani.
Ukiangali
kwenye Tito.2:3-5 anasema, “Vivyo hivyo na wazee wa kike
wawe na mwenendo wa utakatifu, wasiwe wasingiziaji, wasiwe wenye
kutumia mvinyo nyingi, bali wafundishao mema, ili wawatie
wanawake vijana akili, wawapende waume zao, na kuwapenda watoto
wao, na kuwa wenye kiasi, na kuwa safi, kufanya kazi nyumbani
mwao, kuwa wema, kuwatii waume zao wenyewe, ili neno la Mungu
lisitukanwe”.
Unaweza
ukaona kabisa ya kwamba Timotheo, anazungumza habari za vijana
wa kiume waliooa na wanafamilia, au umeoa na hujapata mtoto.
Unao watu nyumbani mwako, inawezekana ni msichana umeolewa, huu
mstari pia unakubana. Ukienda kwenye kitabu cha Tito, Tito
anaandika moja kwa moja habari za wanawake wazee, ili wawasaidie
wanawake vijana, maana yake wasichana ambao ndio wameolewa tu.
Anasema, “Wawatie wanawake vijana akili, wawapende waume zao
na kuwapenda watoto wao”.
Usingetegemea
msichana aambiwe awapende watoto wao, hutaona mwanaume anaambiwa
awapende watoto, bali anaambiwa awalee watoto. Mwanamke
anaambiwa awapende watoto, ni kitu ninashangaa kila siku; maana
nisingetegemea mama aliyepata uchungu wa kuzaa aambiwe ampende
mtoto. Watu waliookoka wengi hasa wanapoingia kwenye ndoa,
wanaingia kienyeji - kienyeji tu, hawajali ya kwamba kuna
kuwajibika.
Huwa
ninawaambia vijana siku zote, hata kama mlikuwa mmezoea kutokula
nyumbani mwako, (maana kijana akiwa bado hajaoa, anaweza akakaa
wiki au wiki mbili, jiko lake halijawahi kupika kitu); kijana
akiwa bado hajaoa, hakimsumbui ana hela au hana hela, ataishi.
Chakula kikiisha anaenda kutembelea ndugu na jamaa, kama
hawataki kumpa chakula, atakaa hapo mpaka amekula na ndipo
aondoke. Akikosa kabisa atajitia moyo kwa Bwana kwamba amefunga,
na kumbe ameshinda njaa!
Wakati
mwingine mambo yakimzidia, na hana sabuni ya kufulia nguo
anasema hajali, kwa hiyo anaendelea, hana shida, anabadilisha
nguo sio kwa sababu amefua, lakini anabadilisha ili angalao
jasho liweze kupungua hasa mnuko wake, kwa hiyo anaitundika
mahali ipigwe upepo usiku; na baada ya siku mbili anavaa hiyo
hiyo tena!
Huwa
ninawaambia vijana siku zote kama hauko tayari kuwajibika, usioe.
Kwa sababu kama umeoa, haijalishi ya kwamba unafunga au hufungi,
chakula lazima kiwemo nyumbani mwenu. h haleluya! Na ukishaoa tu,
maana yake umeitangazia dunia nzima ya kuwa umeamua kuwajibika,
na unaweza ukatunza mke. Mambo ya kwenda kuomba -omba msaada
tena inakuwa ni kitu ambacho si wakati wake sasa. Maana
unaposema, mimi nimeamua kuoa, maana yake umekubali kuwajibika –na
hii ni pamoja na kumlisha na kumtunza mke wako.
Ndio maana
ukienda kwenye makabila mengine wanakuambia, ‘kijana unataka
kuoa umejenga nyumba?’ Nimeona makabila mengine wanauliza,
‘kijana wewe utaoaje wakati hata nyumba huna?’ Ndio maana vijana
wanazuiwa kuoa wakiwa shule, kwa nini, kwa sababu katika ndoa
watahitaji kuwajibika. Sio kwa sababu wakiwa shule hawawezi kuoa,
ila ni kwa sababu wanajua suala la kuoa sio kitu cha mchezo,
linahitaji mahali ambapo unahitaji kuwajibika. Ndani yako lazima
uwe umekubali kuubeba wajibu uliomo katika ndoa!
Na kama ni
msichana unataka kuolewa ukubali kuwajibika basi la sivyo
usikubali kuolewa kama hujawa tayari kuwajibika. Tito anawaambia
wazi kabisa, ya kuwa wafanye kazi nyumbani mwao wenyewe. Lakini
sasa unataka hata kama umeolewa, uishi maisha kama msichana, na
hiyo ni hatari sana. Ukiingia kule ndani ya ndoa kuna mabadiliko.
Wakati ule ulikuwa unaosha vyombo vichache maana ni vya kwako
peke yako, sasa na mume wako yuko, na marafiki zake wamekuja –vyombo
vya kuosha vitaongezeka, na kuwajibika kwako kunaongezeka.
Ilikuwa
inakusumbua kupika, unapika mara moja kutwa, na siku hizi
wataalamu wametuletea kitu kinaitwa ‘hot pot’, kwa hiyo hii
mambo ya kupasha pasha moto chakula siku hizi wakati mwingine
hayahitajiki. Mtu ameweka chakula chake anakifunika vizuri,
anakuja jioni anakuta bado cha moto. Lakini ninakuambia labda
umeingia umeolewa na mtu ambaye ni mtumishi, ana wageni nyumbani
kwake kama kituo cha polisi, kila baada ya dakika mbili amekuja
na wageni wengine.
Labda mume
wako ni mkarimu sana, kila mgeni akija anakuambia, “fulani chai
vipi?” Huko jikoni ‘unauma vidole’ maana umeshaingia jikoni
kuanzia asubuhi; labda saa hiyo ni saa tano, na umeshaingia
jikoni kupika mara nyingi, maana wageni wanapishana kila wakati.
Kila saa ‘chai, chai’, unatamani uondoke ili usiendelee kupika,
lakini umebanwa – ndio kuolewa kwenyewe huko. Ukiamua kuolewa
kuwajibika kwako jikoni kutoangezeka zaidi.
Huwezi
ukaamua tu saa yoyote ukasema, mimi nataka kwenda kutengeneza
nywele, huo muda wa uhuru wa jinsi hiyo umekwisha, ukitaka
kwenda kutengeneza nywele lazima uage, huwezi ukaondoka tu saa
yoyote unayotaka, kila kitu kinabadilika. Kuna masuala ambayo
utahitaji kuwajibika nayo pale nyumbani, huwezi kukwepa! Na kuna
mambo mengine hakuna mtu mwingine ambaye atafanya kwa niaba yako;
kama usipotaka kuyafanya wewe.
Ndio maana
watu wanafika mahali, msichana anaolewa lakini wiki ya kwanza
tu anataka msichana wa kazi wakati, hana hata mtoto mdogo.
Unataka msichana wa kazi wa nini, huo ni uvuvi tu. Lazima uwe
mwangalifu, wewe umeolewa tu, unataka msichana wa kazi, wa nini?
Unaweza ukajitetea na kusema ni kukusaidia kazi - kazi zipi?
Unaweza ukajitetea na kusema, aa! Unajua ninachelewa sana kutoka
kazini, angalao nikute mtu wa kupika. Mimi ninakumbia unaanza
vibaya. Kama ndiyo kwanza umeolewa tu, na unataka wakumpikia
chakula mume wako awe ni msichana wa kazi, basi unaanza vibaya.
Wakati huo
ndio saa ya kumtayarishia mume wako mapishi ambayo hajawahi
kuona kwenye nyumba ya baba na mama yake! Akikaa mwenyewe huku
anakula awe anasema, ‘ahsante Yesu kwa kunipa msichana wa namna
hii!’ Kwa sababu hajawahi kuona chakula kizuri cha namna hiyo
ulichompikia - hata hoteli hajawahi kukipata!
Lakini
unaanza tu maisha ya ndoa na kumbandikia mume wako watu wa
kumhudumia, mimi ninakuambia unaanza vibaya, huko unakoelekea na
ndoa yako sio kuzuri. Uamuzi wa kuoa au kuolewa usiucheezee, kaa
chini, fikiri kwanza na kuomba kabla hujaamua.
Mambo ya
Kutafakari Vijana / utang / 1
/
2 / 3 / 4 /
5 / 6 /
7 /
8 /
9 /
10 /
11 /
|