|
MAMBO YA
KUTAFAKARI KABLA YA KUFANYA
UAMUZI WA KUOA AU KUOLEWA
Wiki ya
Tano
Jambo la Tano
Uamuzi wa
kuoa au kuolewa, unaweza ukabadilisha
utumishi wako na wito wako kabisa
Ngoja
nikutolee mfano wa kibiblia. Unamkumbuka mtu mmoja aliyeitwa
Samson, alimwoa dada mmoja aliyeitwa Delila, utumishi wake
ulinyongewa huko kwenye maisha yao ya ndoa. Ukisoma kile kitabu
cha Waamuzi.16:21 kinasema hivi, “Wafilisti wakamkamata
wakamng’oa macho, wakateremka naye mpaka Gaza, wakamfunga kwa
vifungo vya shaba naye alikuwa akisaga ngano katika gereza”.
Unajua
huyu alikuwa ni mtumishi wa Mungu mzuri kabisa. Lakini hakujua
ya kwamba yule mwanamke aliyempenda na akamwoa aishi naye
alikuwa ni ‘ajenti’. Hakujua ya kuwa yule dada alikuwa ni
‘ajenti’ wa adui. Yule dada alikuwa ni ‘ajenti’; kabisa
akambembeleza mume wake amweleze siri ya nguvu zake, lakini
Samsoni mwenyewe alikuwa anaficha kusema siri ya nguvu zake iko
wapi. Lakini yule dada alikuwa na ujuzi wa kubembeleza.
Akambembeleza yule baba kiasi ambacho akashindwa kuficha siri
yake, na akaisema.
Unajua
inapofika kwenye masuala ya ndoa inatakiwa muweze kusaidiana,
mtu asitumie udhaifu wako kukuangusha, mtu asitumie udhaifu wako
kukuzamisha, mtu asitumie makosa yako kukupeleka jehanamu,
inatakiwa ukimpata mwenzako ukiwa na udhaifu akusaidie, ukiwa
kwenye dhambi akuombee utoke, unaelekea jehanamu akusaidie
kwenda mbinguni, ndivyo inavyotakiwa iwe kwenye ndoa.
Lakini
ninakuambia ukimpata mtu, na wewe una maisha yanayoelekea
jehanamu, anakuambia nenda salama, hii ni hatari. Yule dada
alikuwa anamfuatilia Samsoni kumnyang’anya kitu kilichokuwa
ndani yake cha utumishi alichokuwa amepewa na Mungu, na Samsoni
hakujua. Alipofika mahali pa kuisema siri yake alifikiri mke
wake ni mwenzake ambaye anaweza akampa siri yake vizuri bila
shida.
Ndio maana
kwenye ndoa ambazo watu hawaaminiani vizuri, siri zao
hawaambiani. Na ikishafika kwenye ndoa, mnasiri mlizozifichana
iko shida, maana yake kuna eneo ambalo usingetaka liingiliwe,
unafunga na ufunguo, kasha unatembea na ufunguo mfukoni. Ni eneo
umeficha, kwenye ndoa mnatakiwa mfahamiane kila siku, na udhaifu
wako, na shida ilioko, na matatizo yaliyoko, kila kitu kiwepo
peupe, ili mwenzako atafute namna ya kukusaidia.
Samsoni
aliona kitu cha tofauti, lakini alikuwa mke wake, maadui wakaja
wakamshika, mke wake anatazama na kushangilia. Badala ya Samsoni
kumtumikia Mungu, akaenda akawa anasaga ngano gerezani. Biblia
inasema wakamtoboa macho. Kwa jinsi ya rohoni ningekuambia,
wanaondoa macho yako ya rohoni, maono ya Kimungu yanapotea,
mtazamo wa Kimungu unapotea, mipango ya Kimungu inapotea.
Ndio maana
unakuta mtu ameolewa ameokoka, au ameoa huku ameokoka, akifika
ndani ya ndoa maono ya Kimungu yanapotea, na utumishi wake
unazama. Anabaki kusema ‘Bwana asifiwe’, kama bado anaweza
akaendelea kusema ‘Bwana asifiwe’, lakini ndani ya moyo
amenyonywa kiroho na hakuna kitu.
Sasa labda
na ninyi ni mashahidi, wewe angalia vijana ambao wameoa na
kuolewa, angalia kama bado wanao moto ule ule wa utumishi, ambao
walikuwa nao kabla hawajaingia kwenye ndoa. Wengine wanabaki
kumsingizia Mungu ya kuwa, ameesbadilishia huduma, wakati sio
Mungu, kumbe ni mume wake amembadilishia huduma, au ni mke wake
tu amembadilishia huduma! Maana hakuhesabu gharama ya ndoa
kwenye wito wake.
Kwa mfano;
Mke wako anakutaka nyumbani, huduma inakutaka kila siku uwepo
barabarani, usije ukafikiri ni kitu kirahisi hicho. Utafika
mahali lazima uamue, unataka kumpendezesha mke wako au unataka
kumpendezesha Mungu.Haya si mambo ambayo ni rahisi kuyaweka
vizuri na kuyaanisha bila msaada wa Mungu. Na kama alikuwa
anajua anaolewa wapi, kusumbuliwa suala la kusafiri kwako kwenye
huduma lisingekuwepo, angekua anakutia moyo na kukuombea, na
kukusindikiza siku nyingine. Lakini inapofika anaanza kupata
shida, maana yake kuoana kwenu kuna kasoro mahali, na kumekuwa
mzigo.
Mambo ya
Kutafakari Vijana / utang / 1
/
2 / 3 / 4 /
5 / 6 /
7 /
8 /
9 /
10 /
11 /
|