|
MAMBO YA
KUTAFAKARI KABLA YA KUFANYA
UAMUZI WA KUOA AU KUOLEWA
Wiki ya
Sita
Jambo la Sita
Uamuzi wa
kuoa au kuolewa unaweza wakati mwingine
kukuletea marafiki au maadui.
Sasa
nakufikirisha hivi vitu vikusaidie, inawezekana kabisa hujafikia
umri wa kuoa au kuolewa, lakini ninakuambia weka maombi yako ya
akiba, (sijui kwa upande wako, lakini mara nyingine huwa
nawaombea watoto wangu maombi ya akiba, kwa ajili ya ndoa zao
kama Yesu atakuwa hajarudi, kwa sababu najua maana yake ni nini).
Ni vizuri
upate maombi ya namna hii mara kwa mara - ujiombee mwenyewe,
ukipata watu wa kukuombea shukuru Mungu, lakini hata kama
hujapata watu wa kukuombea, ninakuambia kazana kujiwekea maombi
ya akiba. Hiyo ni njia panda. Mahali pa kuoa au kuolewa ni njia
panda. Ukichagua njia ambayo haiko sawasawa, maisha yako
yatakuwa magumu sana.
Sasa
ukiangalia kwenye kitabu cha Hesabu.12:1-2 inatuonesha wazi
kabisa ya kwamba, harusi ya Musa ilileta ugomvi katikati yake na
ndugu zake, hasa dada yake na Haruni. Kilichowasumbua ni kwamba
alikwenda kuoa mwanamke Mkushi; au amekwenda kuoa mahali ambako
hawakutarajia, kwa hiyo wakakasirika. Halafu naamini Musa
aliwaambia Mungu amesema naye juu ya kuoa mke huyu, wale watu
wakasema, ‘Mungu anasema na Musa tu peke yake, haiwezekani’ -
ugomvi ukaingia.
Unajua
ugomvi uliingia kiasi ambacho Mungu akasikia yale maneno na
hayakumfurahisha, akawaita kwenye hema. Ikabidi ajieleze wazi
uhusiano wake na Musa.
Kitabu cha
Hesabu 12:6-8 kinasema; “Kisha akawaambia, Sikilizeni basi
maneno basi maneno yangu; Akiwapo nabii kati yenu, Mimi, BWANA,
nitajifunua kwake katika maono, Nitasema naye katika ndoto.
Sivyo ilivyo kwa mtumishi wangu, Musa; Yeye ni mwaminifu katika
nyumba yangu yote; kwake nitanena mdomo kwa mdomo, Maana,
waziwazi wala si kwa mafumbo; Na umbo la BWANA yeye ataliona.
Mbona basi ninyi hamkuogopa kumnenea mtumishi wangu, huyo Musa?”
Alivyomaliza kusema namna hiyo dada yake Musa akapata ukoma!
Ugomvi
umetokea wapi? Musa alipooa! Kwa kuwa ameoa msichana ambaye dada
yake hakumtaka. Mungu alimtaka, lakini dada yake hakumtaka. Dada
mtu akaanza kumsema kaka yake, Mungu akampa adhabu! Dada mtu
alipopewa adhabu ile na kaka mtu akapata shida, Israeli nzima
ikapata shida, hawakusafiri walisimama wote, hawakuendelea na
safari. Ugomvi ulitokea wapi? Ulitokea mtu mmoja alipooa!
Nimeona
ndoa zingine kijana anaoa lakini uhusiano wake na baba yake na
mama yake unakatika wakati huo huo. Vijana wengine wanakuwa
hawako waangalifu hapo, na ndio maana mambo yakiwa magumu, na
wazazi wanawabishia juu ya kuoa au kuolewa kwao hawataki kwenda
kuzungumza na wazazi wao; wanapiga ‘short cut’, wazazi wao
wanakuja kuambiwa tu saa na tarehe ya harusi!
Biblia
inasema, “waheshimu baba na mama yako, hii ni amri ya kwanza
yenye ahadi ili upewe siku nyingi katika nchi upewayo na Mungu
wako” (Waefeso 6:1). Na kwa sababu hiyo vijana wengi sana
wakiishakorofishana wazazi wao hawaendelei katika ndoa muda
mrefu wakiwa na amani.
Sasa
sisemi kwamba wamkubali tu huyo msichana au huyo kijana, ni
zaidi ya hapo unajua. Suala ninalozungumzia hapa ni la wao
kukupa kibali, na wakafurahi. Unaweza ukasema, hawaelewi kitu au
hawajaokoka, kwa hiyo hawahitaji kuelezwa kitu. Hapana!
Ndio maana
unahitaji kuomba. Kwa sababu unajua suala la kutaka kuleta
msichana au kijana ndani, sio la kwako peke yako, linawahusu
wazazi wako na ndugu zako kwa sababu unawaingiza kwenye familia
nyingine. Hata kama unataka kuoa au unataka kuolewa, ni mambo ya
kifamilia maana ni koo mbili zinakutanishwa na kuunganishwa.
Wakati
mwingine unaunganisha kabila mbili au unaunganisha kabila tatu,
(wengine hawaelewi kitu ninachosema, kwa mfano; “Mimi ni
mnyakyusa, mke wangu ni msukuma, watoto wangu ni kabila gani”?
Wanakabila mbili, ni mchanganyiko wa wanyakyusa na wasukuma,
maana ningetaka kujipendelea ningesema ni wanyakyusa.
Lakini
ndani wanaunyakyusa na wanausukuma halafu waolewe na mtu wa
kabila lingine ambalo sio mnyakyusa wala sio msukuma, ni
makabila mangapi yanaungana hapo, matatu! Sasa fikiria na
anayeoa kwangu na yeye awe ametoka kwenye mchanganyiko wa
namna hiyo.
Unaunganisha hapo makabila matatu, manne, matano, sasa wewe
unataka wazazi wako wasiifuatilie ndoa hiyo kwa karibu. Kwa nini?
Ukipata shida utarudi kwa wazazi wako, sasa kwa nini wakati wa
maamuzi wasikusaidie!
Na mimi
ninakuambia iko njia ya kutokea, ikiwa utapata tatizo la namna
hii; wewe kukaa kwenye maombi kwa namna ambavyo, kama ni Mungu
kweli aliyekupa huyo msichana au aliyekupa huyo kijana, basi
ataweka kibali hicho hicho ndani ya wazazi wako, ili na wao
wamkubali.
Saa
nyingine unaweza ukapata marafiki wengine wazuri, lakini wakati
mwingine marafiki wengine wanakuwa ni wabaya. Maana ukishaolewa
marafiki wa mume wako ni marafiki zako, ukishaoa marafiki wa
msichana ni marafiki zako. Vijana siku hizi wanaotaka kuoa au
kuolewa wakitaka kujua ukoje, hawakuangalii wewe wanaangalia
marafiki zako. Marafiki ulionao ndio wanaoonyesha picha
uliyonayo ndani yako.
Rafiki wa
kweli hafuati pesa ulizonazo, anafuata tabia uliyo nayo, wale
marafiki wanaokufuata kwa sababu unacho kitu cha kuwapa hao sio
marafiki, wanakufuata kwa sababu unachokitu, siku ukiishiwa
huwaoni. Lakini wale marafiki unakuwa nao wakati wa shida na
wakati wa raha, ni marafiki ambao malengo yenu na tabia zenu,
kufikiri kwenu kusema kwenu zinafanana. Hao ndio marafiki ambao
wanakuwa marafiki zako wa kweli; siku ukiwa na shida ni marafiki
zako, unahela ni marafiki zako, umefilisika ni marafiki zako,
hao ndio marafiki zako!
Sasa kama
mtu anataka kukuangalia ulivyo, anaangalia marafiki zako. Sasa,
akiangalia marafiki zako, hata kama unasema, ‘Bwana asifiwe’,
hata kama unapiga pambio mpaka jasho la damu linatoka, lakini
wanaangalia marafiki zako ulionao, na wakati mwingine ni wabaya
kuliko wale wa kule duniani, wanajua na huyu msichana au huyu
mvulana kuna mahali ‘ana short’.
Kwa
wengine inakuwa vigumu kuliona kwa namna hii, lakini ni lazima
ufahamu ukiwa kama kijana, lazima uwe mwangalifu juu ya marafiki
ulionao. Vijana wengine wanabaki kushangaa kwa nini wasichana
wanahangaika wanasema hatuoni vijana wa kuwaoa, wakati vijana
wapo, lakini nani ataolewa na vijana ambao wameokoka lakini
hawana msimamo? Nani anataka kijana wa namna hiyo ambaye
anashinda vijiweni sawasawa na hao vijana wengine wa duniani?
Mwanaume
akitaka kuoa lazima ajifunze kuwajibika. Hawezi akawa na
marafiki ambao hawawajibiki kimaisha – na akataka aone na
aendelee na urafiki nao. Akiwa karibu na hao marafiki, itakuwa
ni vigumu kuwa na ndoa yenye amani. Angalia tu marafiki alionao,
unashangaa kwamba anaendelea kusema bado ameokoka. Unashangaa
wale marafiki alionao, hawafananii, hawawezi hata kumtia moyo
kuomba, hawawezi kumtia moyo kusoma neno, vitu wanavyozungumza
ni vitu vya ajabu.
Unajua,
hata wakati mmoja hawana maneno ya kutiana moyo ya kuwa na
maendeleo binafsi, lakini ndio anaoshinda nao toka asubuhi mpaka
jioni, halafu anataka kuoa msichana ambaye ameokoka, anayeshinda
kwa Mungu , anayekaa kwenye maombi, anayetaka kuona cha Mungu
kinasimama katika maisha yake, ndiye anataka kwenda kwake ili
amuoe;- hii siyo sawa! Ndoa yao itakuwa na matatizo tu kwa muda
mrefu.
Maana
usije ukapata shida ukiingia kwenye ndoa na kijana wa namna hiyo.
Wewe uliona kabisa marafiki zake walivyo, unaolewa na ndipo
unaposema, ‘mimi sitaki hao marafiki zako’! Imeanza wapi?
Atakuambia vizuri kabisa “ulinikuta nao”, kwa nini hukusema
mapema kabla hatujaoana ya kuwa huwataki?
Msichana
anaolewa na ndipo kijana anamwambia hao marafiki zako nisiwaone
hapa, lakini alikuwa anawakuta chumbani kwako wakati alipokuwa
anakuja kukutembelea na hakusema kitu, na wakati mambo yakiwa
magumu katikati yenu alikuwa anawatumia wao kukubembeleza
ukubali kuolewa naye, sasa umekwishaolewa hawataki. Anaanza
kuwasema ya kuwa tabia zao sio nzuri. Hili jambo si zuri;
alitakiwa aseme mapema juu ya kutoridhika kwake na rafiki zake.
Unapotaka
kuoa au kuolewa, usifikirie tu picha ya yule mtu wakumuoa au
kuolewa naye, ni vizuri kuangalia na aina ya marafiki zake wa
karibu – je unaweza kuchukuliana nao?.
Mambo ya
Kutafakari Vijana / utang / 1
/
2 / 3 / 4 /
5 / 6 /
7 /
8 /
9 /
10 /
11 /
|