|
MAMBO YA
KUTAFAKARI KABLA YA KUFANYA
UAMUZI WA KUOA AU KUOLEWA
Wiki ya
Nane
Jambo la Nane
“Je! Uko
tayari kuolewa na nani”
Wengine
hawafikirii namna hiyo, ukiwauliza uko tayari kuolewa na nani,
anasema na mtu aliyeokoka. Bwana anawajua walio wake, hakuna mtu
kwa jinsi ya nje atakayemjua mtu aliyeokoka kisawasawa hasa
alivyo kitabia. Maana watu wengi sana wanasema wameokoka lakini
hawajaokoka, wengine wanasema ‘bwana asifiwe’ lakini ni bwana
mwingine sio Bwana Yesu! Ni mambo ambayo unatakiwa kufikiri,
unataka kuolewa na nani.
Labda
hujawahi kufikiria kitu cha namna hiyo, nataka nikufikirishe
vitu vya kawaida kabisa. Wengine wanasema mimi nataka kuolewa na
mtumishi, hesabu gharama kwanza! Wengine wanaona
tunavyoshirikiana na mke wangu katika huduma wanamtazama
wanasema, wanataka kuolewa na mtumishi; kaamuulize mke wangu,
tulipokutana hata wito haukuweko, na tulikutana wote hatujaokoka.
Tulikuja kuokoka baada ya kuoana!
Mungu
ametuteremshia utumishi tuko kwenye ndoa tayari, kwa hiyo
usitamani ndoa ya kwetu, tamani ya kwako ambayo Mungu
amekupangia. Mke wangu hakunipendea utumishi, sikuwa na tone la
utumishi, wala hata ya kufanania ya kwamba nitaokoka, na yeye alikuwa
hajaokoka pia wakati huo. Lakini kwa saa na kwa makusudi na kwa
utaratibu wa Mungu, tumekuwa jinsi tulivyo. Akatuteremshia
utumishi wakati tumekwishaokoka na tumekwishaoana!
Usijaribu
kufananisha ndoa yako na ndoa ya mtu mwingine, hujui iliko toka,
tamani ya kwako. Sasa unasema wewe unataka mtumishi, lakini
watumishi wako wengi sana, kwa hiyo unataka mtumishi wa namna
gani? Lazima ufikiri juu ya hili pia. Unasema mimi ninataka
mhubiri, hata nabii ni mhubiri, mwinjilisti ni muhubiri, mwalimu
anaweza akahubiri. Kitabia hawafanani, haleluya! Nataka
nikufikirishe ikusaidie, maana nataka nikujengee msingi mzuri wa
maisha ambao ukikanyaga vizuri shetani alie tu, maana hatawezi
kukuvuruga.
Maana watu
wengi wanapata shida sana wanapotaka kuoa au kuolewa, utakuta
wanasema, mimi ninataka kuoa au kuolewa na mtumishi, hayo ni
maombi ya mtu ambaye hajaenda shule ya Roho Mtakatitu, bado yuko
chekechea, unajua lazima uwe ‘very specific’. Mungu anataka
useme naye kile kitu unachokisikia ndani yako. Anajua kabisa
kitu ambacho ni kizuri kwa ajili yako; lakini Mungu hataki
kukulazimishia tu, anataka ushirikiane naye, ili akikupa kitu
ukipokee kwa furaha.
Kwa hiyo
kama unataka mtumishi, ni muhimu useme unataka mtumishi wa aina
gani. Kwa mfano ukisema nataka mwinjilisti, hesabu gharama,
lazima uwe na neema ya kukaa na mwinjilisti. Si unajua
mwinjilisti hakai nyumbani, anazunguka, akikosa watu wa
kuwachapa injili huko nje, anakuja kuchapa injili nyumbani hata
kama mmeokoka wote! Na ujue hawezi kumaliza ibada ya jioni mpaka
awepo mtu wa kutubu, hajatubu ataendelea kufanya maombi. Kama
hauko tayari kuchukuliana na mtu wa namna hiyo usiamue kuoa au
kuolewa naye.
Lazima
useme; au kama unataka kuolewa na nabii jipange, kwa sababu
hajui kuongea na watu, muda wake mwingi yuko kimya, manabii mara
nyingi wanafungwa midomo sio wasemaji ni mtu mkimya. Mara nyingi
amejifungia kuomba peke yake na Mungu. Hata saa nyingine
unatamani uombe pamoja naye, lakini Mungu anataka yeye peke
yake. Wewe nenda kwenye biblia utaona maisha yake yalivyo kila
kitu kinachomzunguka, kila kitu anachovaa, kila kitu
anachokutana nacho, Mungu anaweza akakigeuza ujumbe.
Kwa hiyo
usije ukashangaa kesho akakutazama na akaishia kupata mahubiri
toka kwako, halafu mkirudi nyumbani mnaanza kugombana, na
unamuuliza sasa wewe ulikuwa unanihubirije? Kwani wewe hukujua
ya kwamba ni nabii na anaweza kupata ujumbe unaosema: “kama vile
mke wako alivyovaa, ndivyo na kanisa langu lilivyo asema,
Bwana”!
Wewe
usifanye mchezo! Sasa nyingine mnaishiwa chakula na anaona jinsi
mnavyohangaika, basi utakuta amekwishapata ujumbe kama huu,
“kama vile mke wako alivyokuwa anahangaika kutafuta chakula kwa
ajili ya watoto, ndivyo na mimi ninavyotafuta chakula kwa ajili
ya watoto wangu, asema Bwana”!
Saa
nyingine unavaa nguo zinapasuliwa, mpaka viungo vya ndani
vinaonekana, ujumbe unatoka saa hiyo mara moja, anasema, “Kama
vile mke wako alivyovaa nguo iliyopasuliwa na watu wanaona ndani,
ndivyo na kanisa langu lilivyo vazi lake limepasuliwa na shetani
anaona ndani”!
Lazima
uwe tayari kuwa ujumbe, kama unataka kuolewa na nabii. Uwe
tayari kuwa ujumbe, hujawa tayari usiombe uolewe na nabii!
Unataka kuolewa na mchungaji uwe na moyo mkubwa wa kupokea
wageni. Mwingine anasema mimi ninataka kuolewa na mtumishi
lakini ndani yake anawaza mtu anayezunguka na kuhubiri, kumbe
Mungu ameweka ndani yake mtumishi, lakini ni mfanya biashara.
Mfanya
biashara mwingine anapakwa mafuta kufanya biashara, ndio sehemu
yake kumtumikia Mungu, mwingine ni fundi cherehani, mwingine ni
dereva, wanapakwa mafuta sehemu zao hizo za utumishi, usije
ukafikiri hao wanaoafanya kazi nyingine sio watumishi wa Mungu.
Mungu anawapaka mafuta kwa ajili ya hizo kazi, ili walitumikie
kusudi lake.
Kwa hiyo
unapokwenda katika maombi unasema tu mimi ninaomba mtumishi,
Mungu atakuletea mtumishi yoyote, wako wengi, wengine wanafagia
barabara, ni watumishi wa Mungu, wengine wanasafisha kule kwenye
vyoo vya kulipia ni watumishi wa Mungu, wengine wanasafisha
nyumba za watu, nao ni watumishi wa Mungu,oh haleluya!
Mungu
akikuletea mtumishi yeyote unaishia kusema, mimi sikuomba huyu
niliomba mtumishi. Mungu atakuambia huyu ni mtumishi wangu,
usimnenee kitu cha namna hiyo.
Kama
msichana ni mfupi usitamani kijana mrefu, au kijana ni mrefu
unatamani msichana mfupi. Kwa kweli, sio kwamba Mungu hawezi
kukupa, lakini wewe fikiri tu mwenyewe, haleluya! Maana mwingine
anakuwa mfupi kiasi ambacho anafanana kama vile ni mtoto kwako,
wenzako wanakuuliza tangu lini umepata mtoto na akakua na akawa
mkubwa namna hii, unasema “ninyi msiseme hivyo, ni mume wangu
huyu”.
Ni uamuzi
wako. Sasa, si lazima mfanane urefu, lakini msipishane sana; kwa
kweli ni kwa faida yenu wenyewe, haleluya!
Kama
msichana hupendi mwanaume mwenye ndevu, omba vizuri. Maana
unaweza ukapata mtumishi wa Mungu, lakini ana ndevu na wewe
huzitaki. Ikifika siku umeingia tu kwenye ndoa kitu cha kwanza
unamtafutia wembe ili anyoe ndevu zake – hii ni kumwonea!
Ulimpenda akiwa na ndevu, kumbe wewe ulikuwa unamtegea tu ili
baada ya arusi tu umpe wembe! Wako wasichana wanaopenda wanaume
wenye ndevu, waachie hao!
Huyu Bwana
Mungu wetu ni mzuri sana, unajua, saa nyingine huwa ninawaza
jinsi Mungu alivyomuumba mwanadamu na nabaki ninashangaa sana.
Maana kuna wanaume wengine hata ndevu hawana, hata
wakilazimishia kunyoa kidevu kitupu haziji. Sasa mtu mwingine
anajisikia vibaya, akifikiri ya kuwa mtu anaonekana ya kwamba
yeye ni mwanaume kwa sababu tu ana ndevu, si kweli. Kuna wanaume
wengine wametengenezwa namna hiyo ‘special’ kwa ajili ya
wasichana wasiotaka wanaume wenye ndevu, haleluya!
Maana
mwingine anaweza akaachia ndevu zikafunika mpaka karibu na
kwenye pua. Sasa kama ni mtu mweusi sana ‘ni hatari sana’,
giza likiingia tu ndani ya nyumba wewe unamwambia ‘cheka’,
akicheka yale meno yake yanaweza yakamulika kidogo, na utajua
yuko wapi! Hivi vitu ukishaingia kwenye ndoa ni vitu vikubwa
sana, kuliko watu wanapoviangalia kabla hawajaoana.
Wewe
unakuta kijana anaoa msichana ana rangi nyeusi nzuri tu, akifika
ndani unamletea madawa ajikoboe, wewe ulikuwa unamwoa wa nini?
Hiyo sasa ni sawa na kumwambia Mungu kwa kweli nimechukua tu
huyu, lakini sio niliyekuwa namtaka!
Niliyekuwa
namtaka ni mweupe, sasa maandamu umenipa huyu wacha nimkoboe
mpaka afike rangi ninayotaka, - haviendi namna hiyo bwana!
Mungu alipokuwa anamuumba huyo msichana namna hiyo aliona,
alimtazama alivyo na weusi wake huo akaona kila kitu chema,
akajipa sifa, akajipa maksi asilimia mia moja, amefanya kitu
chema!
Sasa
akitaka kupaka rangi hiyo ‘nyumba yake’ na kuinakshi ni kitu
kingine. Unajua kuna nyumba nyingine hazipendezi mpaka uzipake
rangi fulani, haleluya! Mwili ni nyumba, kuna wengine hawawezi
kupendeza mpaka wamepaka rangi fulani kwenye miili yao. Sasa
utapata mtihani mgumu, nimeona, kijana anampenda msichana,
lakini msichana anaweka rangi kwenye midomo yake, kucha zake
anaweka rangi, anachora na kalamu hapa kwenye nyusi kidogo,
ukimtazama vizuri usoni utagundua ya kwamba ameweka kitu kingine
juu ya uso wake.
Umempenda
akiwa namna hiyo. Wakati ulipokuwa unamfuatilia hukumuuliza hayo
maswali, leo ameingia ndani umemuoa, unamwambia sitaki hizo
rangi! Hiyo ni kumwonea, maana ulimkuta akiwa hivyo, kama
ulikuwa humtaki akiwa amejinakshi na rangi hizo, hukutakiwa
kumfuatilia, wako wengine ambao watakuwa radhi na huyo
anayejipaka rangi!
Kuna
kijana alioa msichana, wamefika ndani wakaanza kugombana naye
habari za nywele, mpaka akamrudisha kwao, - nywele tu! Huyu dada
kaenda katengeneza nywele staili fulani, yule kijana haitaki.
Lakini alimkuta yule msichana anatengeneza nywele kwa staili
hiyo, sasa kwa nini hivi vitu hawakutaka kuzungumza kabla ya
kuamua kuoana?
Mimi
ninataka nikusaidie upunguze ugomvi ndani ya ndoa utakayokuwa
nayo; maana vitu ambavyo Mungu atawaletea vya kufanya pamoja
kwenye ndoa ni vikubwa kuliko mnavyofikiri, kiasi ambacho
hamhitaji kutumia muda wenu kushindania vitu vidogo vidogo
ambavyo mlikuwa muwe mmekwisha kuvijadili kabla ya kuoana. Mna
mambo muhimu sana ya kufanya, kiasi ambacho kuanza kushindana na
kubishana juu ya vitu ambavyo mlitakiwa muwe mumeshavizungumza
kabla ya kuoana; huko ni kutokuelewa utaratibu wa Mungu ulivyo
juu ya kumpata mwenzi wa maisha.
Mambo ya
Kutafakari Vijana / utang / 1
/
2 / 3 / 4 /
5 / 6 /
7 /
8 /
9 /
10 /
11 /
|