|
MAMBO YA
KUTAFAKARI KABLA YA KUFANYA
UAMUZI WA KUOA AU KUOLEWA
Wiki ya
Kumi
Jambo la Kumi
Uko
tayari kuzaa, kutunza na kulea watoto wangapi?
Niliuliza
vijana fulani ambao ndio wametoka tu kuoana, wanafurahia maisha
yao, ghafla nikawauliza swali ambalo hawakutegemea, nikawauliza,
“mna mpango wa nakuzaa watoto wangapi? Walinitazama wakasema,
“Mungu anajua”. Nikawambia; “siyo hivyo! Mungu anajua lakini
ninyi je?” “Wakasema hatujui”, nikawaambia hayo ndio makosa ya
wengi waliomo katika ndoa.
Sasa
ninakueleza hivi kwa sababu ni vitu ambavyo Mungu alisema na
sisi mapema. Hakuna mtoto aliyezaliwa baada ya sisi kuokoka
ambaye sikujua ya kwamba atazaliwa, na hakuna mtoto aliyezaliwa
baada ya sisi kukuokoka ambaye sijajua wito wake. Na Mungu
aliponyamaza na hakutuonyesha mtoto mwingine, hatukuona sababu
ya sisi kutafuta mtoto mwingine. Wengine wanafikiri Mungu hana
mipango ya uzazi (kasome biblia yako vizuri) – Mungu ana
utaratibu wa uzazi kwa kila ndoa anayoisimika.
Ni kitu
ambacho unahitaji kuomba, ili Mungu akujulishe. Nimeona watu
wakishindana ndani ya ndoa, baba anataka watoto wengi, mama
hataki. Nimekuta ndoa nyingine mama anataka watoto wengi
wamzunguke kama timu ya mpira lakini baba hataki. Na ugomvi
mkali unatokea juu ya hili.
Mwingine
anamzalisha mke wake kila mwaka (unaelewa maana ya kila mwaka?)
si unaelewa mimba inakaa miezi tisa tumboni, kwa hiyo anaweza
akazaa kila mwaka! Sasa umewahi kufikiri kila mwaka unazaa, kwa
hiyo ikiwa uko kwenye ndoa miaka kumi basi una watoto kumi. Au
mtu yuko kwenye ndoa miaka mitano, tayari ana watoto wanne na
bado anaendelea kuzaa – hii ni sawa?
Nilikwenda
mahali fulani kwa ajili ya huduma dada mmoja alikuwa anafurahia
muujiza wake wa tumbo, jinsi ambavyo Mungu amemponya, akasema,
“sasa nitakuwa tayari kuzaa mtoto mwingine”. Nikamuuliza, “una
watoto wangapi sasa?” Akasema, “wanne”. Nikamwambia, “Na bado
unahitaji mtoto mwingine”. Akasema, “ndio, ninataka mtoto
mwingine”! Unajua kwa nini ninakueleza vitu vya namna hii, - kwa
sababu kila mtoto ana wajibu wake, ana mzigo wa kwake na
anatunzwa kivyake!
Kadiri
unavyozaa watoto wengi, ndivyo unavyozidi kuwa na wajibu mkubwa
zaidi wa kulea. Watoto hawafanani, huwezi ukawalea kijumla.
Watoto hawalelewi kwa namna hiyo. Kila mtoto ameitwa kivyake,
ana mpango wake, ana njia yake, ana tabia yake na ana namna yake
ya kutunzwa,– hawafanani!
Mtoto
anayezaliwa lazima umlee kwa uangalifu. Hujamfikisha mahali
katika kumlea, tayari ameshakuja mwingine, unafikiri mchezo!
Hao watoto
wawili hujawafikisha mahali katika kuwalea tayari ameshakuja
mwingine, ni kitu kigumu hujawahi kuona! Huyu wa kwanza hapati
tena ule umuhimu wake na nafasi yake, kwa sababu sasa
anakimbiliwa huyu aliye mdogo; akija mwingine anakimbiliwa aliye
mdogo zaidi, hao waliotangulia wanajikuta wanakua kivyao.
Watu wengi
wanabaki kushangaa kwa nini watoto wengi waliozaliwa kwa
kufuatana saa nyingine kwa karibu wanagombana. Ni kwa sababu
huyu mkubwa anaona ameingiliwa na huyu mdogo, na huyu mdogo
anaona kwamba huyu mkubwa ameshakuwa mkubwa, kwa hiyo mimi
niliye mdogo ndiye mwenye haki zaidi. Ni ugomvi unaoweza
ukaendelea mpaka wamekuwa watu wazima.
Mimi
nimesoma masuala ya uchumi, sijasomea masuala ya kuhubiri. Si
kwa sababu sikupenda kusomea kuhubiri, lakini hakuwa mpango wa
Mungu wa kunilea namna hiyo katika wito. Kuna wengine Mungu
anawapanga na kulea wito wao kwenye vyuo vya biblia; na ni
mpango wa Mungu tu mzuri. Lakini Mungu alikuwa na mpango
mwingine na mimi. Mimi katika chuo nilikwenda kusoma masuala ya
uchumi.
Sasa, siku
moja nchi hii ilitembelewa na wageni, wa kutoka Washington D.C,
wa shirika la fedha ulimwenguni. Wale watu wakatuuliza maswali,
hebu tuambieni mabadiliko ya uchumi yanayoendelea hapa nchini
ninyi mnayaonaje.
Mama mmoja
akanyoosha mkono, akasema, “Tunaelewa umuhimu wa mabadiliko
mengine yanapotokea katika uchumi wa nchi, kwa sababu ya
mazingira tunayoyaona hasa tunapoona vitu vingine havifanyi kazi.
Kwa hiyo kuna umuhimu wa kubadilisha sera zingine ili mambo
yaende sawasawa.
Lakini
tatizo tulilonalo, ni kwamba maandalizi ya kutuandaa sisi kama
watanzania ya kwamba kuna mabadiliko yanakuja, hayo maandalizi
hayajafanyika ya kutosha”. Wakasema, “mama tupe mfano”. Akasema
“kwa mfano, tunatakiwa kuchangia masuala ya afya, tunatakiwa
kuchangia masuala ya elimu, kama tungejua kwa mfano, miaka
mitano au sita kabla, kwamba miaka sita ijayo au miaka kumi
ijayo, ya kuwa pamoja na kwamba sasa elimu ni bure, afya ni bure,
iko siku mtahitaji kutoa pesa zenu mfukoni ili kulipia gharama
hizi – tungekuwa waangalifu tunazaa watoto wangapi.”
Nikagundua
mara moja kwamba huyu mtu wazo lake lilikuwa ni zuri kabisa.Kwa
sababu kwa watanzania wengi inapofika mtoto anazaliwa walijua
anayewajibika kumpeleka huyo mtoto shule ni serikali,
anayewajibika kumlipia gharama za hospitali ni serikali! Wewe
utazaaje ili serikali ikutunzie mtoto? Lazima na wewe uwe na
bajeti yako!
Unajua
biblia haisemi serikali leeni watoto, inaasema enyi wakina baba
leeni watoto. Soma Waefeso 6:4. Sasa pale serikali
itakapokusaidia wacha ikusaidie, lakini usikae unajiambia ya
kuwa mimi nimezaa watoto kumi na tatu, lazima waende shule bure,
lazima waende kwenye hospitali bure. Nani anayegharamia hizo
huduma, unafikiri ni za bure? Hakuna! Wewe unaona huduma hizo ni
bure, lakini yuko mtu ametoa pesa za kugharamia hizo huduma
toka mahali fulani.
Nakumbuka
wakati fulani nlikuwa Zimbabwe, baba mmoja aliyekuwa na cheo
kikubwa tu kwenye makanisa ya kule Zimbabwe, tulikuwa
tunazungumza naye siku moja juu ya masuala ya kusomesha watoto.
Alisema wakati mmoja alikwenda Ujerumani kwenda kutafuta watu wa
kuwasomesha watoto wake.
Yule
mzungu ambaye alikuwa anazungumza naye, akaamuuliza, “ndugu una
watoto wangapi, akasema sita”. Akasema, “unajua mimi nina watoto
wangapi.” Akasema, “sijui”. Akasema watoto wawili”. Akasema,
“unajua ni kwa nini hatutaki kuzaa watoto wengi, usije ukafikiri
tunachukia watoto, hasha ila ni kwa sababu ya gharama, za
kuwatunza zilivyo kubwa”.
Tunataka
angalao kila mtoto atunzwe vizuri na aende shule nzuri,
wakiishakuwa wengi inakuwa si rahisi kuwagharamia wote ipasavyo,
na inabidi ugawe ulichonacho kidogo kidogo. Wanaishia wote
shule ya msingi, kwa sababu huna hela ya kuwapeleka sekondari.
Akasema, “sasa ninyi waafrika mambo yenu hayako sawa, wewe
unaona mimi nimezaa kidogo nimejinyima kwa ajili ya watoto wangu
wasome vizuri, sasa unataka fedha ya kwangu nikusomeshee watoto
wa kwako ambao wewe umezaa bila kufikiria jambo la gharama ya
kuwatunza wakiishazaliwa?”
Aliambiwa
kitu cha kweli usoni na mzungu! Unaweza ukafikiri alikuwa
anamtukana, lakini alikuwa anamweleza kitu cha ukweli; watu
wengi sana hawafikiri hiki kitu. Wale wazee wa zamani walikuwa
wakizaa kwa mahesabu huku nyuma. Akizaa watoto wa kike wengi ana
hesabu ng’ombe atakazopata watakapoolewa, usije ukafikiri ana
hesabu gharama, bali ana hesabu ng’ombe atakazopata! Watoto wa
kike kwake ni mradi. Akizaa watoto wa kiume anajua amepata nguvu
kazi ya kulima mashamba, walikuwa wana mahesabu yao.
Lakini
sasa hivi lazima ukae ufikiri kwa namna nyingine,sikuambii ya
kwamba kuwa na watoto wengi ni kitu kibaya, ni uamuzi wako! Kama
unataka kwenda na mstari unaohimiza mkaongezeke mkaijaze nchi (Mwanzo
1:28) hakuna shida! Unaweza ukaendelea na wewe ukawa kwenye
kuijaza nchi, lakini usikazane kuijaza nchi halafu unataka
wengine wakusaidie kulea watoto hao - hiyo sasa sio sawa!
Mimi
sijui kwa upande wako, na sijui kwa upande wa wazazi wako,
lakini ninakueleza ili baadaye uwe mzazi mzuri, ni vitu
unahitaji kufikiri mapema. Niliwaambia watoto wangu siku moja,
nikawaambia sikiliza, tumejiwekea maamuzi ndani ya hii nyumba
mimi na mama yenu, ya kwamba ni wajibu wetu kuwasomesha mpaka
chuo kikuu ili angalau kila mmoja awe na shahada ya kwanza, huo
ni wajibu wetu.
Baada ya
shahada ya kwanza ukitaka kuendelea Mungu akubariki. Mungu
akitupa nafasi ya kukusaidia kuendelea zaidi ya shahada ya
kwanza tutakusaidia. Lakini tumemwomba Mungu atusaidie, kila mtu
lazima afike chuo kikuu. Unajua kama usipoweka malengo ya namna
hii, hata matumizi yako na bajeti yako haviwezi kukaa sawa. Ndio
maana ninakuambia lazima umwombe Mungu akusaidie, usije
ukafikiri kusomesha watoto ni kitu rahisi.
Ninyi
mnajua ambao mko shule, wengine wameshindwa kuendelea na shule
kwa sababu wazazi wameshindwa kutoa karo za shule, na sio kwa
sababu wanafunzi hawataki kuendelea na shule, lakini ni kwa
sababu hakuna fedha za kuwasomesha.
Nilimuuliza msichana mmoja katika mkoa mmoja wakati nilipokuwa
huko kwa huduma, nikamuuliza “umemaliza darasa la ngapi”.
Akasema, “kidato cha sita”. Nikamwambia, “sasa kwa nini hutaki
kuendelea na shule?” Akanitazama usoni, halafu akasema,
“sithubutu hata kumwambia baba anisomeshe zaidi maana
ninawaangalia wadogo zangu huku nyuma walivyo na ninaangalia na
hali ya baba yangu aliyonayo kifedha, amenisaidia nimefika
kidato cha sita, sasa nikifikiria wadogo zangu – ambao bado wako
shule za msingi, naona wacha na wao basi wasogee sogee angalau
wafike sekondari na wao kama mimi. Kwa hiyo mimi nimenyamaza
kimya”.
Huyu
msichana amemaliza kidato cha sita anataka kuendelea na masomo,
lakini hawezi kuendelea kusoma kwa sababu anaangalia hali ya
wazazi wake ilivyo, anajua kabisa angalau na wadogo zake na wao
wasome, lakini sio kwamba anataka kuishia kidato cha sita.
Mambo ya
Kutafakari Vijana / utang / 1
/
2 / 3 / 4 /
5 / 6 /
7 /
8 /
9 /
10 /
11 /
|