Tunamshukuru Mungu kwa kuifanikisha semina hii ya Dar es salaam, tunayo kila sababu ya kumshukuru Mungu sana kwa kutulinda toka tunaianza hadi tunamaliza semina hii. Pia katika semina hii Mungu alijidhihirisha kwa kiwango tofauti hivyo kuifanya semina hii kuwa ya kipekee kabisa.

Semina hii ya Dar es salaam tuliifanya kuanzia tarehe 24 february hadi tarehe 3 machi 2013, ndani ya hema tuliyoisimamisha katika viwanja vya Jangwani. Mahudhurio yalikuwa watu 20,000 hadi 30,000 kwa siku za mwanzo ila kwa siku mbili za mwisho walifika 40,000 au zaidi. Pia  mahudhurio ya wasikilizaji kwa njia ya mtandao ilikuwa ni kati ya watu 3000 hadi 4000 kwa siku. Jumla ya watu 2279 waliweza kuokoka katika semina hiyo

Somo lililofundishwa.

Kichwa cha somo kilikuwa “SADAKA INAVYOTUMIKA KUPIMA KIWANGO CHAKO CHA KUMCHA MUNGU”.

Tunaweka msingi katika points Nne.

1. Utoaji sadaka ni njia mojawapo ambayo Mungu anaitumia kupima kiwango chako cha uchaji.
    Mwanzo 22:1 – 2; 12. Mungu alikua anapima uchaji au kiwango cha kumcha Mungu kwa Ibrahimu. Chochote ambacho hakina thamani kwako Mungu hawezi kukitumia kupima Uchaji wako.

2. Shetani nae anapima kiwango chako cha uchaji kwa kuangalia vitu ulivyopewa a Mungu.
     Ayubu 1:8 – 12; Kiwango chako cha uchaji ni sawa sawa na Baraka ulizo nazo, shetani katika mtihani wake anajua kwamba ukinyang’anywa kile ulichopewa na Mungu kiwango chako cha uchaji kinapungua. Mungu akitaka kupinga kiwango chako cha uchaji anaangalia unampa vitu gani, na vinathamani gani kwako?

3. Kuna uhusiano kati ya kiwango cha kumcha Mungu na kiwango cha Mungu kujifunua kwako.
     Mwanzo 28:16 – 17;. Yakobo alipata hofu ya Mungu baada ya Mungu kujidhihirisha kwake. Joshua 4:23 – 24;. Utukufu wa Mungu ni nguvu za Mungu zinazoonekana katika ulimwengu wa kawaida. Uchaji mahali ambapo upo, lazima uwepo wa Mungu upo. Sababu iliyomfanya Mungu afanye muujiza wa kupasua maji ya Yordan ni ili watu wote duniani waujue mkono wa Mungu ili wamhofu(wamche) yeye milele.

4.Uwepo wa Mungu na uwepo wa shetani unapogombania kuheshimika katika eneo moja hilo hilo, watu wa eneo hilo wanajikuta wanapimwa kiwango chao cha kumcha Mungu. Ayubu 1: 8 – 12; Katika mambo ambayo Mungu alijisifia nayo mbele za shetani ni Ayubu kuwa mcha Mungu.

Shetani anatafuta kupima suala la kumcha Mungu kwa wanadamu kwa sababu

Maeneo yaliyoko ndani ya uchaji wa Mungu

1.  Kuna ahadi za Mungu ili upewe katika maisha yako inategemea kiwango chako cha uchaji. Mwanzo 22: 1 -2; Mwanzo 21:5;

2.  Kuna maombi yako ambayo Mungu hawezi kukujibu bila kuangalia kiwango chako cha uchaji

Ebrania 5:7 – 8; Akasikilizwa kwa kuwa alikuwa mcha Mungu. Kila wakati kwenye maandiko tafuta matokeo.

3.  Kuna kiwango cha kumcha Mungu ambacho kinamsaidia mtu aepushwe na hukumu ya Mungu.

Ufunuo14:6 – 7; Ebrania 11:7; Mithali 8:13, Kumbukumbu 14:22 – 23;

4.  Utoaji wa sadaka unaweza kutumika kukufundisha kumcha Mungu daima pia unaweza kutumika kupima kiwango chako cha kumcha Mungu. 

Sababu mojawapo iliyomsukuma Mungu kuachilia masuala ya sadaka ni kumfanya mtoaji ajifunze kumcha Mungu daima.

Mungu anavyotumia sadaka kupima kiwango chako cha Uchaji.

1. Kwa kuangalia kiwango cha hofu ya Mungu ndani yako kinachoonyesha kutii agizo hilo la utoaji kuna dhamani kubwa kwako wewe mtoaji kuliko dhamani ya sadaka hiyo ilivyo kwako.

Mwanzo 22:1 - 2,12,16,18. Mwanzo 17:15;.

Unawezaje kupima ndani yako kama umepewa maagizo ya kutoa sadaka kama unataka kujua kama huo ni mtihani?

 • Angalia ndani yako kama utoaji huo wa sadaka umekuwa kama jaribu kwako. Jaribu maana yake unawekwa njia panda ya kuhamua utii au usitii kutoa hiyo sadaka.
 • nakuwa na sababu ndani yako kukuzuia usitoe hiyo sadaka kwa Mungu. Mwanzo 22:12,16;  Siku zote Mungu akitaka kukupeleka hatua nyingine chochote ambacho kinaweza kuubana moyo wako usitii cha Mungu, Mungu anakitaka kwenye madhabahu. Heshima yako haiko kwenye kubaki na kile ambacho Mungu anataka ukitoe, bali heshima yako iko kwenye kutii kile Mungu alichokumbia.

Mungu anavyotumia sadaka kupima kiwango chako cha uchaji.

Luka 18:18 – 27; Waebrania 11: 17 – 19; Imani ya utoaji inasema ya kuwa chochote kinachotoka mkononi mwako kama sadaka hakitoki kwenye maisha yako  kamwe.

2. Kwa kuangalia kiwango cha hofu ya Mungu ndani yako kinachoonyesha ya kuwa unampenda Mungu zaidi kuliko sadaka aliyoagiza uitoe.

 • Mwanzo 22:2; Yohana 3:16; Kutoa kunaonyesha upendo lakini hakuonyeshi kiwango cha kupenda lakini thamani ya sadaka unayoitoa inaonyesha kiwango cha upendo kwako.
 • Warumi 5: 6 – 8; Thamani ya sadaka ya Yesu haiko tu ndani ya Yesu ila pia muda ambapo sadaka yenyewe inaachiliwa. Sadaka yako haijalishi ni kubwa kiasi gani lakini ikija kwa muda usiostahili inapoteza dhamani yake.  

3. Kwa kuangalia kiwango cha hofu ya Mungu ndani yako kinachoonyesha unamuhitaji Mungu kwa kiwango kipi katika mazingira uliyonayo.

 • Mwanzo 22:1 – 2, 9; Mwanzo 8:20; 1Wafalme 18:30;
 • Kwa nini wote walihusisha madhabahu na utoaji sadaka wao?

Madhabahu ni Ishara ya nje, inayoonyesha angalau vitu vifuaavyo

 1. Moyo wako umeweka Imani kwa nani?
 2. Moyo wako umehamua kukutana na unayemwamini hapo.
 3. Ya kuwa huyo unayemwamini na unayetaka kukutana naye hapo unamwitaji kwa kiwango kipi katika mazingira ulinayo.
 4. Moyo wako inayoonyesha kiu uliyonayo ya kuwa na kiwango kipya na cha juu zaidi cha Mungu wako cha ushirikiano katika hiyo madhabahu.

Pia madhabahu mahali ilipo ni ishara ya nje ya hao walioweka ya kwamba huyo wanayemwamini na kutaka kukutana naye hapo wanamwitaji kwa kiwango gani. “Thamani halisi ya madhabahu iko moyoni mwa mtu”.

Kutoka 32:1 – 5;

4. Kwa kuangalia kiwango cha hofu ya Mungu ndani yako wakati unatoa sadaka kinachoonyesha msukumo wa moyo wako ya kuwa unataka kiwango kipya cha ushirikiano wako na Mungu.

Mwanzo 22:1 – 2, 9,12.
Mahusiano ya Mungu na wanadamu yanategemea nafasi mwanadamu aliyonayo awapo hapa duniani. Mungu hawezi kukupa maelekezo yoyote kama hauko kwenye nafasi aliyokupangia.

Yohana 15:4. Kama kiwngo cha ushirikiano wako na Mungu cha mwaka juzi hakina tofauti na mwaka huu basi ujue Mungu hawezi kujidhihirisha kwako tofauti na mwaka juzi.

5. Kwa kuangalia kiwango cha hofu ya Mungu ndani ya moyo wa mtu kinachoonyesha kiwango cha utayari wako katika kuachiia hiyo sadaka ili iwe sehemu ya kukukutanisha na kukuunganisha na Mungu wako katika ibada kuliko ikabaki kama sehemu ya maisha yake.

Mwanzo 22:1,2, 5, Yohana 4:23 – 24, Marko 7:6 – 7. Yohana 8:32. Mungu haangalii dini ambayo imekupa kibali cha kuingia kuabudu ila Mungu anaangalia moyo wako.

Maana ya kuabudu kutoka kwa Ibrahimu aliposema naenda kuabudu alikuwa anamaanisha mambo yafuatayo

 1. Naenda mahali pa kukutana na Mungu.
 2. Naenda kukutanisha roho yangu na Roho wa Mungu kufuatana na maelekezo yaliyomuweka huru ndani ya moyo wake.
 3. Alisema Mungu ameagiza sadaka/ Isaka awe sadaka ya kutukutanisha
 4. Aina ya sadaka aliyoagizwa aitoe ilimfanya ndani yake ategemee kiwango cha tofauti.
 5. Ile sadaka ilipofika kwenye madhabahu na Mungu akaipokea iliachilia ujumbe kutoka kwa Ibrahimu unaomwambia Mungu hivi wewe ni Mungu wangu na sina Mungu mwingine ila wewe!

Anapima kiwango cha uchaji kwa kuangalia kiwango cha hofu ya Mungu ndani ya mtu kinachotokana na kiwango cha Imani unachotumia wakati unatoa sadaka yako.

 1. Kuna uhusiano mkubwa kati ya kiwango cha imani katika utoaji sadaka na  kiwango cha uchaji kilichopo ndani ya Yule mtoaji wa sadaka. Ebrania 11:17 – 18, Mwanzo 22:12.
 2. Kuna uhusiano kati ya kiwango cha imani na kumcha Mungu. Ebrania 11:7,
 3. Mungu huwa anatofautisha sadaka inayotolewa kwa imani na ile isiyotolewa kwa imani .Halafu anahakikisha amekujulisha moyoni mwako. Waebrania 11:4,
 4. Jifunze kutofautisha kati ya utoaji sadaka kwa imani na ule utoaji usiokuwa kwa imani ili uweze kuongeza kiwango chako cha uchaji.
 5. Sadaka isiyotolewa kwa imani huwa hairudishwi kwa mtoaji na pia haina faida wala msaada wowote kwa mtoaji wa sadaka.

Mambo yatakayokusaidia ujue kama unatoa sadaka kwa imani au la; 2 Wakorintho 9:7

 1. Toa kama ulivyokusudia moyoni mwako.
 2. Sii kwa lazima ( Unajuaje kuwa unatoa kwa lazima ni pale unapotoa kwa kunung’unika)
 3. Sii kwa huzuni, 2 Wakorintho 7: 9 – 11.
 4. Moyo wa ukunjufu (Utayari wa kuachilia aina na kiwango unachotakiwa kutoa kama sadaka ) 2 Wakorintho 8:12, Warumi 12:3 – 8, Usinie makuu kuliko kiwango cha imani ulicho nacho.

Hali ya hewa
Tunamshukuru Mungu wa Mbinguni kwa kutupa hali ya hewa iliyokuwa njema sana katika siku zote tulizokuwa na semina katika viwanja vya jangwani. Haikunyesha mvua kiasi cha kuharibu mazingira na uchaji wa ibada wakati wa semina ingawa ilinyesha mvua kidogo wakati wa usiku wa kuamkia siku ya nane ya semina. Uwanja wa Jangwani huwa unakuwa na tope linalonata sana kama mvua ikinyesha, sisi tunamshukuru Mungu kwa kuwa mwaminifu kwetu kuzuia mvua wakati wa semina. Mvua ilianza kunyesha siku ya jumatatu mchana baada ya sisi kumaliza semina na kuondoa vifaa vyetu, kwa hili tunamtukuza Mungu wa Mbinguni.

Sehemu ambazo semina hii ilikuwa inasikika.
Tunamshukuru Mungu kuwa semina hii iliweza kurusha na vituo vitatu vya redio, ikiwa ni redio Upendo ya Dar es salaam, Redio Wapo ya Dar es salaam na pia redio Sauti ya Injili ya Moshi mkoa wa Kilimanjaro. Tunamshukuru Mungu kwa watu waliopokea miujiza yao kwa kusikiliza kupitia vituo hivi. Pia tulikuwa live kwenye mtandao wa internet kupitia tovuti ya  www.mwakasege.org na www.kicheko .com.

Semina ya Vijana.
Pia katika semina hiyo tulikuwa na semina ya vijana iliyofanyika siku ya saba tarehe 02 mwezi machi 2013, asubuhi kuanzia saa 3 hadi saa sita mchana katika uwanja huo wa Jangwani. Kulikuwa na mahudhurio makubwa katika semina yaliyoweza kufikia vijana zaidi ya 10,000. Somo lililofundishwa lilikuwa na kichwa kinachosema “JIFUNZE MFUMO WA KUFIKIRI KAMA KIONGOZI”. Baada ya somo vijana wengi waliokoka pamoja na kufanyiwa maombi maalum kuwasaidia kufikiri kama viongozi.