Bwana Yesu asifiwe sana!

Pamoja na kwamba tumesheherekea kumbukumbu ya siku ya Pasaka mwezi uliopita, tunaamini bado unaweza kupokea salamu zetu za Pasaka, tunazokuletea kwa njia ya barua hii.

Tunakuhimiza utumie mwezii huu, kuimarisha imani yako juu ya msalaba wa Yesu na juu ya Damu ya Yesu! Kila kimoja kina umuhimu wake. Ni muhimu uimarishe Imani yako katika vyote viwili. Kwa mfano: Kuna maeneo 7 ambayo Yesu alimwaga damu yake, kila eneo likiwa na faida kwa mwanadamu!

Eneo la 1: ni akiwa katika bustani ya Getsemane “matone ya damu” yalipomdondoka (Luka 22:44) – Ili kwa damu ya Yesu, tuweze kuwa na ushindi dhidi ya maamuzi ya nafsi, yaliyo kinyume na mapenzi ya Mungu ndani yetu.

Eneo la 2: ni alipovikwa “taji ya miiba” kichwani (Mathayo 27:29) – Ili kutupa ushindi katika damu ya Yesu, dhidi ya laana ya kutofanikiwa kiuchumi ya Mwanzo 3:18.

Eneo la 3: ni wakati alipopigwa “mijeledi” (Mathayo 27:26) – ili katika damu ya Yesu tupate ushindi dhidi ya magonjwa (1Petro 2:24).

Eneo la 4: ni wakati alipopigiliwa misumari katika mikono yake, ili katika damu ya Yesu, tuwe na uhalali wa kutumia mikono yetu kuponya wagonjwa (Marko 16:18), na baraka zipatikane katika kazi tunazozifanya (Kumbukumbu ya Torati 28:8).

Eneo la 5: ni wakati alipopigiliwa misumari kwenye viganja vya miguu yake, ili katika damu ya Yesu,tuweze kuenenda kwa imani (2 Wakorintho 5:7) – huku hatua zetu zikiwa zinaongozwa na Yeye (Zaburi 37: 23,24).

Eneo la 6: ni wakati alipopigwa mkuki ubavuni (Yohana 19:34), ili katika damu ya Yesu, aweze kurudisha tena ndani ya mioyo yetu, au roho zetu, uwezo wa kumzalia Mungu matunda katika maisha yetu; maana “damu na maji” kumwagika kwa pamoja ni ishara ya kuzaliwa kitu!

Eneo la 7: ni wakati alipojeruhiwa na kuchubuliwa katika mwili wake, ili katika damu ya Yesu tupate msamaha na ushindi dhidi ya dhambi na makosa na maovu na madhaifu yetu (Isaya 53:4-6).

Hizo ni baadhi tu ya faida zilizomo kwenye “agano jipya katika damu” yake (Luka 22:20). Kwa hiyo zitafakari ili uimarishe “imani katika damu yake” (Warumi 3:25), “kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, Kristo” (1 Wakorintho 5:7)!

Mwezi wa Machi 2016 tulikuwa na semina Dar tarehe 6 – 13; na pia tulikuwa na Kongamano la maombi la mkoa wa Tanga kwa siku mbili tarehe 16 – 17.

Tunamshukuru Mungu kwa kuwa unaendelea kutuombea juu ya huduma ambayo Mungu ametupa.

Mungu azidi kukubariki
Ni sisi katika utumishi wa Kristo,
Christopher & Diana Mwakasege.