Salamu katika Jina la Yesu Kristo.

Huu ni mwezi wa 4 katika mwaka huu wa 2013. Tunajua Mungu amekupa nafasi ya kuungana nasi katika safari hii ya kumtumikia Yeye, sawasawa na kusudi lake!

Mwezi uliopita wa tatu tuliumaliza kwa semina tuliyoifanya Tanga mjini, kwenye uwanja wa Tangamano kwa siku 6, kuanzia tarehe 12 hadi 17.

Ilikuwa semina nzuri na iliyokuwa na ushindi mkubwa kwa ufalme wa Mungu. Maelfu ya watu waliokoka na kutengeneza maisha yao na Yesu.

Mwezi huu wa April ilikuwa tuwe na safari ya kwenda Israeli. Tumeiahirisha na tumeiunganisha na safari ya kwenda Israeli ya tarehe 12 – 21 Juni 2013.

Semina ya neno la Mungu tuliyonayo mwezi huu wa April ni Dodoma mjini, tarehe 21 – 28. Usisahau kutuombea, na kama unaweza kuhudhuria karibu pia tule pamoja chakula cha neno la Mungu.

Tunachotamani kionekane kwako mwezi huu.

Kujiombea wewe mwenyewe, ili Mungu akupe kuona umuhimu, na akupe nguvu za kuomba, juu ya kuoa au kuolewa kwa mzaliwa wa kwanza, au juu ya ndoa yake.

Wakati fulani nilikutana na mtu mmoja aliyekuwa na umri kama au karibu miaka 60. Mtu huyo alikuwa ananieleza jinsi alivyomshukuru Mungu kwa somo hili la kumwombea mzaliwa wa kwanza ninalofundisha.

Mtu huyo aliniambia ya kuwa toka utoto wake, na hadi wakati huo wa utu uzima, katika ukoo wao walikuwa hawajawahi kuwa na ‘send-off’ wala harusi halali – kwa wasichana wao.

Lakini baada ya kuombea tatizo hilo kwa mtazamo wa wazaliwa wa kwanza kama chanzo cha tatizo hilo, Mungu aliufungua ukoo huo, na kwa mara ya kwanza mwaka huo (2010), walitangaziwa ‘send-off’ na harusi ya msichana katika ukoo wao.

Je, unajua ya kuwa hali ya ndoa, na pia hali ya kuoa au kuolewa, kwa sehemu kubwa inapita kwenye “lango la” na “mkondo wa” mzaliwa wa kwanza katika ukoo au katika familia husika?

Ndoa za wazaliwa wa kwanza hazipigwi vita kwa sababu wamezaliwa kwanza, bali kwa kuwa wao ni lango na mkondo wa Mungu!