Bwana Yesu Kristo asifiwe Milele!

Tunakusalimu katika jina la Yesu Kristo, aliye Bwana wa mabwana, na aliye Mfalme wa    wafalme!

Kwa mwaka huu wa 2014, mwezi huu wa nne, umebeba pia sikukuu ijulikanayo kama pasaka. Salamu zetu za pasaka kwako, tunataka tushirikiane na wewe mambo yafuatayo juu ya pasaka.

Jambo la kwanza:

Pasaka ni jina la sadaka kabla halijawa jina la sikukuu!

Yule mwana – kondoo aliyechinjwa, na damu yake ikawekwa na wana wa Israeli, katika miimo na vizingiti vya milango yao, aliitwa “ni pasaka ya Bwana” (Kutoka 12:11).

Jambo hili lilikuwa agizo la Mungu kwao, ili atumie kitendo hicho kuwafungua, toka kwenye utumwa wa miaka 430 wakiwa mikononi mwa wa – Misri.

Ukisoma katika Kutoka 12: 11, 44 anazungumza juu ya kumla pasaka akiwa na maana ya kumla mwana – kondoo aliyetolewa sadaka siku hiyo.

Katika kutoka 12:27, huyo mwana – kondoo anajulikana kama “dhabihu ya pasaka ya Bwana”.

Na Mungu aliwapa agizo la kuwa na kumbukumbu ya jambo hilo kila mwaka katika vizazi vyao vyote.

“Ilikuwa mwisho wa miaka hiyo mia nne na thelathini, ilikuwa siku ile ile, ya kwamba majeshi yote ya Bwana yalitoka nchi ya Misri. Ni usiku wa kuangaliwa sana mbele za Bwana, kwa sababu ya kuwatoa katika nchi ya Misri; huu ndio usiku wa Bwana, ambao wapasa kuangaliwa sana na wana wa Israeli wote katika vizazi vyao”. (Kutoka 12:42).

Inakuwa ni tatizo, na ni rahisi sana kupoteza maana ya pasaka, kama msisitizo wa wakristo utakuwa kwenye sikukuu iitwayo pasaka, badala ya kuweka msisitizo kwenye sadaka iitwayo pasaka.