Bwana Yesu asifiwe sana!

                Tunaamini Bwana Yesu anaendelea kukutunza! Sisi hatujambo. Tunaendelea na kazi ya Mungu, kwa kadri ya neema ya Yesu Kristo, iliyo juu ya maisha yetu. Mungu aendelee kukubariki, kwa ajili ya kusimama pamoja nasi, katika utumishi huu wa Kristo.

                Mwezi huu wa April 2019, tunataka tukuhimize uendelee na juhudi za kuongeza kumjua Mungu. Na kwa kuwa mwezi huu, tunasherehekea kumbukumbu ya sikukuu ya Pasaka, ni vizuri tukatafakari habari za kifo cha Yesu Kristo na kufufuka kwake.

                Lipo jibu moja ambalo Yesu aliwajibu wanafunzi wake – ‘Andrea na Filipo’, walipompelekea ombi la “Wayunani” kadha wa kadha waliotaka kumwona.

                Yesu akajibu akasema: “Amin, amin, nawaambia, chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi (Yohana 12:24).

                Yesu alitaka wajue ya kuwa, kabla ya yeye kufa na kufufuka, isingekuwa rahisi kumjua kwa kiwango kinachotakiwa!

                Yesu alitumia mfano wa mbegu ya ngano, kulielezea jambo hili. Kabla mbegu hujaipanda, na ikafa, na ikaota, si rahisi kujua mbegu hiyo imebeba nini ndani yake.

                Na ndivyo ilivyo kwa Yesu Kristo! Si rahisi ukamjua Yesu ipasavyo, bila ya kufuatilia ni kitu gani kilikuwa ndani ya Yesu, na kilidhihirishwa kwa kufa na kufufuka kwake.

                Ni vizuri, tukakukumbusha ya kuwa; usipomfahamu na kumjua Yesu ipasavyo, haitakuwa rahisi kwako kumfahamu na kumjua Mungu baba, kwa jinsi ipasavyo!

                Yesu aliwahi kusema hivi: “Aliyeniona mimi amemwona Baba” (Yohana 14:9)…halafu akaongeza kusema ya kwamba: “mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu” (Yohana 14:11).

                Ni dhahiri basi ya kwamba, ukitaka kumjua Mungu zaidi, mjue Yesu Kristo zaidi!

                Hebu tafakari pamoja nasi mwezi huu, baadhi ya yaliyodhihirishwa toka kwa Yesu, kwa kufa na kufufuka kwake:

                Kwa mfano:

1. Kwa kufa na kufufuka kwake, Yesu alidhihirisha ya kuwa yeye ndiye: “Mwana – Kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu” (Yohana 1:29). Unapoutafakari mstari huu unganisha na Mwanzo 22:13.
2. Kwa kufa na kufufuka kwake, Yesu alidhihirika ya kuwa yeye ndiye: “Pasaka wetu”, aliyetolewa “kuwa sadaka, yaani Kristo” (1 Wakorintho 5:7). Unapoutafakari mstari huu, unganisha na maneno ya Kutoka 12:1 – 51.
3. Kwa kufa na kufufuka kwake, Yesu alidhihirisha ya kuwa yeye ndiye: “Chakula cha uzima”; na kwamba aendaye kwake na kumwamini “hataona njaa kabisa”, wala “hataona kiu kamwe” (Yohana 6:35). Unapoutafakari mstari huu, unganisha na maneno haya ya Yohana 6:31 – 59.
4. Kwa kufa na kufufuka kwake, Yesu alidhihirika ya kuwa yeye ndiye aliyewekwa na Mungu awe “mrithi wa yote” (Waebrania 1:1 – 4). Na unapotafakari maneno hayo, kumbuka pia Warumi 8:16,17.
5. Kwa kufa na kufufuka kwake, Yesu alidhihirika ya kuwa yeye ni “mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote” (Wakolosai 1:15), tena “ni mzaliwa wa kwanza katika wafu” (Wakolosai 1:18). Soma na kutafakari pia kwa upana mistari hii Wakolosai 1:13 – 20.
6. Je, unajua ya kuwa, bila ya Yesu Kristo kufa na kufufuka, ni vigumu kujua faida kwetu, ya Yesu kufufuka? Yesu kwa kufa na kufufuka kwake, alidhihirika ya kuwa yeye ndiye “ufufuo na uzima” (Yohana 11:25). Tafakari hili kwa kuunganisha na maneno ya 1 Wakorintho 15:12 – 22.

Haya tuliyokushirikisha katika barua hii, ni baadhi ya yale yaliyodhihirika kwa kufa na kufufuka kwa Yesu, Tumekuwekea ili yawe msaada na mtaji wa kutafakari kwako mwezi huu, ili uzidi kufanikiwa katika juhudi na kiu uliyonayo ya kutaka kumjua Mungu zaidi.

Tunakutakia Pasaka njema. Tuzidi kuombeana, usiache kutizama ratiba ya semina zetu. Na pia usiache kutufuatilia kwenye ukurasa wetu wa Facebook kwa ajili ya masomo na taarifa mbalimbali.

                                Ni sisi katika utumishi wa Kristo,

                                Christopher na Diana Mwakasege.