Jina la Yesu Kristo litukuzwe milele na milele – Amina.

Mungu azidi kukubariki sana kwa kuisoma barua yetu hii, kwa sababu inaonyesha ya kuwa unafuatilia huduma ambayo Mungu ametupa kwa karibu sana!

Mwezi uliopita – yaani mwezi wa saba, tulikuwa na majukumu mawili makubwa kwetu:

Kwanza; Tulikuwa na kongamano la maombi la kitaifa tulilolifanya Dodoma tarehe 9 – 12 Julai

Hilo lilikuwa ni Kongamano la 5 la kitaifa, lenye lengo la kukusanya waombaji wenye mzigo wa kuombea taifa. Karibu watu elfu tatu walihudhuria Kongamano hilo, wakitokea mikoa yote ya Tanzania, na pia walikuwepo waombaji kutoka Unguja na Pemba.

Tulikuwa na kipindi kizuri sana cha kuliombea taifa la Tanzania. Kati ya watu waliohudhuria, tulikuwa na maaskofu saba (7) na wachungaji themanini na saba (87) na viongozi wa huduma wawili (2) toka makanisa na huduma mbalimbali nchini.

Tunatarajia tuwe na kongamano linguine la namna hii mwaka ujao 2014. Tunaamini ya kuwa maombi ya namna hii, – tena ya mara kwa mara kwa ajili ya taifa letu, yanasaidia sana kuifuta mipango ya shetani huku yakifanikisha makusudi ya Mungu wetu aliye hai.

Pili; Tulikuwa na semina ya neno la Mungu katika mkoa wa Mwanza. Semina hii tuliifanya tarehe 21 – 28 Julai katika kiwanja cha Furahisha kilichopo jijini Mwanza.

Semina hiyo ilikuwa na mahudhurio makubwa sana ya watu, kuliko semina zingine tulizowahi kuzifanya katika mkoa wa Mwanza. Tunamtukuza Mungu sana kwa kuifanikisha semina hiyo kwa kiwango kikubwa sana. Sifa na utukufu ni kwake Yesu Kristo, ambaye ndiye atuwezeshae katika kila hatua tunayokwenda nayo katika huduma.

Semina hiyo ilirushwa “live” kupitia www.kicheko.com na www.mwakasege.org. Na pia tulikuwa hewani “live” kupitia redio Sauti ya injili irushayo matangazo yake toka mjini Moshi; na pia kupitia redio ya HHC Alive inayorusha matangazo kutoka mjini Mwanza.

Pia ‘Cable TV’ ya Barmedas ya mjini Mwanza ilikuwa inarusha semina hiyo ‘live’ kwenye ‘TV’ na kupitia kwenye mtandao wa Ustream.

Watu wengi sana waliponywa magonjwa yao, na kuokoka, na kujazwa Roho Mtakatifu. Kumbukumbu tulizonazo zinatuonyesha ya kuwa watu wapatao 3050 waliokoka na kumpa Yesu maisha yao, wakati wa kipindi hicho cha Semina cha siku nane.