Shaloom.

Salamu katika jina la Yesu Kristo!

Mungu ni mwema! Tumemaliza semina pale Moshi mjini, tuliyoifanya kwa muda wa siku 6, kuanzia tarehe 28 januari hadi tarehe 2 februari.

Tulimwona na kumshuhudia Mungu kwa mafundisho na matendo, kwa namna ambayo familia nyingi zilipata msaada wa kiroho, kwenye maeneo mengi.

Somo tulilofundishwa lilihusu: “Gharama na Baraka za Sadaka kifamilia”. Malengo tuliyokuwa nayo kwa kufundisha somo hili, yalikuwa ni pamoja na haya:

  1. Kwamba: Kuna gharama zake na baraka zake katika kutoa sadaka zinazogusa familia.
  2. Kwamba: Ndani ya sadaka moja kunaweza kukawa na nguvu ya kugusa mtu zaidi ya mmoja, na pia kugusa kizazi cha familia hiyo zaidi ya kimoja.
  3. Kwamba: Mtu anapotoa sadaka kama kiongozi wa familia, katika nafasi yake kama kiongozi wa familia; ni sawa na mtu kuingia mkataba na benki kwa niaba ya familia. Ikiwa benki ilimpa mkopo – huo mkopo ni wa familia – watadaiwa na wale ambao hawakutia sahihi mkataba huo. Na kiongozi akikimbia familia – hataweza kuukimbia mkopo!
  4. Kwamba: Ni vizuri familia zikaacha kutoa sadaka zinazochanganya Mungu na miungu! Yaani wasije wakajikuta wanatoa kwa Mungu katika Kristo Yesu na pia wakatoa kwa miungu mingine kwa kisingizio cha mila na desturi za kiukoo!