Bwana Yesu asifiwe milele!

Unaendeleaje? Je katika mwezi wako huu wa kwanza wa mwaka huu wa 2016, umeweza kumzalia Mungu matunda aliyokuwa anayataka toka kwako?

Je, unajua ya kuwa kuna uhusiano kati ya kiwango cha kujibiwa maombi yako, na kile kiwango chako cha kumzalia Mungu matunda yanayodumu?

Biblia inasema hivi:

“Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lolote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni” (Yohana 15:16)

Unapoyasoma maneno haya ya Bwana Yesu kwa kuyalinganisha na kiwango cha kujibiwa maombi yako – unaona nini ndani yake? Je! unahisi Yesu akisema na wewe binafsi?

Hebu yasome maneno hayo kama vile Yesu anasema na wewe binafsi. Hayo maneno yatasomeka hivi:

“Si wewe uliyenichagua mimi, bali ni mimi niliyekuchagua wewe; nami nikakuweka uende ukazae matunda; na matunda yako yapate kukaa; ili kwamba lo lote umwombalo Baba kwa jina langu akupe”.

Unayaona sasa maneno hayo yanavyosema na wewe?
Sababu mojawapo inayokufanya uwe hai wakati huu ni kwa kuwa Mungu amekuchagua uwepo ili umzalie matunda yanayodumu! Na katika kumzalia matunda huko aweze kupata sababu ya kujibu lolote utakalomwomba katika jina la Yesu.

Si tu suala la kuzaa matunda, bali kuzaa matunda yanayokaa, au matunda yanayoweka ‘alama’ isiyofutika!

Kwa lugha iliyo nyepesi tunaweza kusema ya kuwa Mungu katika kukuwezesha wewe kuishi – siyo kwamba anataka uishi kwa sababu ya kuishi; bali uishi kwa ajili ya kumzalia matunda yanayodumu!

Kujibiwa maombi kunapounganishwa na kuzaa kwako matunda ni motisha kwako kulenga kumzalia Mungu matunda yanayodumu katika maisha yako.

Kwa mantiki hiyo ni vizuri ndani ya moyo wako uyatazame maisha yako hadi sasa kwa jicho la kujitathmini ili uone ikiwa unaridhika na matunda uliyomzalia Mungu. Pia, angalia maisha yako ya baadaye uone ikiwa una mikakati gani au mbinu gani katika kuishi kwako, ili uweze kumzalia Mungu matunda yatakayodumu.

Sisi tumekuwa tukijiuliza swali hili kwa upande wetu; maana nia yetu katika maisha ambayo Mungu ametupa ni kutaka kumzalia Bwana Yesu matunda mengi zaidi kila siku. Na kufuatana na Yohana 15:16 kiwango cha kujibiwa kwa maombi yetu kitakuwa kinaongezeka hatua kwa hatua kwa kadri ya kiwango tunachoongeza kila siku cha kumzalia Mungu matunda yanayodumu.

Katika kuliombea jambo hili na kulitafakari, Roho Mtakatifu ametuongoza katika mambo kadha wa kadha, ambayo baadhi yake tumejisikia huru mioyoni mwetu kukushirikisha. Yamkini ukiyasoma, na kama una nia kama yetu unaweza ukapata mambo kadhaa yatakayokusaidia. Yasome mambo haya ndani ya barua hii na katika biblia; ukijua Roho Mtakatifu anayetuongoza kukuandikia yupo pamoja nawe ili akusaidie upate kuyaelewa!

Je, unayafahamu ni matunda gani hayo ambayo Yesu anayosema kwamba anataka kuyaona kutoka kwa kila aliye wake?

Ukisoma biblia utaona matunda yafuatayo:

Tunda la haki”:

Imeandikwa katika Yakobo 3:18 hivi : “ Na tunda la haki hupandwa katika Amani ya wale wafanyao Amani”.

“Tunda la Midomo”:

Imeandikwa katika Waebrania 13:15 hivi: “ Basi, kwa njia yake yeye, na tumpe Mungu dhabihu ya sifa daima, yaani, tunda la midomo iliungamayo jina lake”

“Tunda la Roho”:

Imeandikwa hivi katika Wagalatia 5:22,23: “ Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, Amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria”.

“Tunda la kazi”:

Imeandikwa hivi katika Wafilipi 1:22: “ Ila ikiwa kuishi katika mwili, kwangu mimi ni matunda ya kazi; basi nitakalolichagua silitambui”.

“Tunda la Toba”:

Imeandikwa hivi katika Mathayo 3:8: “Basi zaeni matunda yapasayo toba”

Semina za Mwezi huu.

Tutakuwa Moshi mjini, kwenye kiwanja cha mpira cha Majengo kwa semina ya siku 6 – tarehe 16 – 21 Februari, 2016. Na tutakuwa Dar es salaam tarehe 28 Februari hadi tarehe 6 Machi 2016, katika kiwanja cha chuo kikuu cha Dar es salaam.

Tuombeane na karibu ikiwa una nafasi ya kufika. Tunakushukuru sana kwa kutuombea wakati tulipokuwa na semina Arusha mjini, kwenye uwanja wa Reli tarehe 24 – 31 Januari 2016.

Ni sisi katika utumishi wa Kristo
Christopher na Diana Mwakasege.