Shaloom.

Tunakusalimu katika Jina la Yesu Kristo.

Salamu zetu za mwaka mpya wa 2013 zinatoka katika 1Mambo ya Nyakati 12:32 unaosema

“Na wana wa Isakari, watu wenye akili za kujua nyakati, kuyajua yawapasayo Israeli wayatende… walikuwa watu mia mbili na ndugu zao wote walikuwa chini ya amri yao”

Ni maombi yetu kwa Mungu ya kuwa atakupa ‘akili’ za kuujua mwaka huu wa 2013 ulivyo au umebeba nyakati zipi.

Hii itakusaidia uweze kuzitambua na kuzitambua fursa zilizomo ndani yake – ili ujue cha kufanya sawasawa na Yeremia 29:11

Kwa mfano, ikiwa utaweza kuona fursa moja kwa siku ina maana utakuwa na fursa 365 kwa mwaka 2013 za kutumia!

Na ikiwa utaweza kuona fursa moja tu kwa wiki, ina maana utakuwa na fursa 52 kwa mwaka 2013 za kutumia.

Kumbuka; kuna watu wanaanza mwaka na wanaumaliza mwaka huo, bila ya kuona fursa hata moja ya kuwasaidia watoke katika ngazi ya kimaisha waliyokuwa –nayo, wakati wanaanza mwaka.

Utawatambua kwa kuona maisha yao ya mwanzo wa mwaka hayana tofauti na maisha waliyonayo wanapoumaliza mwaka!
Ndio maana salamu zetu kwako za mwaka mpya – ni maombi kwa ajili yako ili Mungu akupe akili za kujua mwaka 2013 umebeba nyakati zipi, ili uweze kuona fursa zilizopo na uzitumie ipasavyo sawa na Yeremia 29:11.

Kwa mwezi huu Januari 2013 tutahudumu katika semina ya siku moja ya kupanda na kuvuna. Semina hii ambayo imeandaliwa na New Life in Christ mkoani Dar es salaam, itafanyika tarehe 27 January 2013, kuanzia saa 8 mchana hadi saa 12 jioni.

Na itafanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee, katika jiji la Dar es salaam.

Utukumbuke kwenye maombi kwa ajili ya Semina hiyo ya siku moja tu – tena kwa mchana tu. Ukiweza kushiriki  - karibu sana!