Shaloom!

Bwana Yesu Kristo Asifiwe milele kwa kutupa nafasi ya kuuona na kuuingia mwaka huu mpya wa 2014.

Mioyo yetu imejaa shukrani sana kwa Mungu, kwa sababu ya neema yake katika Kristo Yesu; inayotupa kuendelea kumtumikia katika kizazi cha nyakati zetu hizi.

Jambo ambalo Roho Mtakatifu ameliweka kwa uzito wa kipekee ndani ya mioyo yetu katika mwanzo huu, wa mwaka huu mpya – ni juu ya uhusiano wa utumishi na uaminifu!

Kuna baraka za kuwa mwaminifu na kuna gharama za kutokuwa mwaminifu katika kumtumikia Mungu kwenye eneo lolote analokupa – hata kama si katika kuhubiri.

Elewa maana ya neno Mwaminifu.

Neno hili “Mwaminifu” linatokana na neno la kiingereza lisemalo “Faithful”. Na ukifuatilia neno hili “uaminifu”, utaona limetokana na neno la Kiingereza la “Faithfulness”.

Kwa tafsiri ilivyo nyepesi, neno “faithful” na neno “faithfulness” – ni maneno mawili mawili lakini yaliyoungwa pamoja.

“Faithful” ni Full of Faith na Faithfulness “Fulness of Faith”. Kwa tafsiri ya Kiswahili maana yake “kujaa Imani”. Kwa hiyo, mtu aliye mwaminifu au aliye “faithful” ni yule aliye – jaa Imani au “full of faith”.

Nasi tunajua ya kuwa kutokana na Warumi 10:17 – “Imani, Chanzo chake ni kusikia, na kusikia huja kwa neno la Kristo”. Hii ina maana ya kuwa mtu aliye mwaminifu ni yule ambaye anatekeleza maelekezo ambayo Mungu amempa. Kwa mantiki hii mtumishi mwaminifu ni yule ambaye anakijua alichoambiwa na Mungu akifanye – na amekifanya alivyotakiwa!