Bwana Yesu asifiwe sana!

Tunapokusalimia kwa jina la Yesu Kristo, tunakuomba pia upokee salamu zetu za mwaka mpya huu wa 2015.

Kama vile Mungu alivyokuwa pamoja nasi mwaka 2014, tunaamini ya kuwa pia atakuwa nasi tena mwaka huu wa 2015, tena kwa kiwango kikubwa kuliko cha mwaka jana!

Ni sahihi kabisa kwa Mkristo ye yote, na mtumishi wa Mungu ye yote, anayetumika katika Kristo Yesu, kumwamini Mungu kwa kiwango kikubwa zaidi mwaka huu cha maisha na cha utumishi wake.

Unajua ni kwa nini tunasema hivi, na tunaamini hivi? Ni kwa sababu biblia inasema tunapokuwa ndani ya Kristo tuna nafasi ya kukua – toka utukufu kwenda utukufu (2Wakorintho 3:15) toka imani hata kiwango kikubwa zaidi cha imani (Warumi 1:17); na kutoka nguvu hata kiwango cha juu Zaidi cha nguvu za Mungu (Zaburi 84:7).

Mwaka huu ni mwaka wa 30 kwetu tangu tuanze kumtumikia Mungu. Tunamshukuru Mungu aliyetupa kujua mpango wake aliotupa tuutekeleze – ingawa halikuwa jambo jepesi.

Mwaka 1985 nilipata msukumo ndani yangu mkubwa sana wa kutaka kumtumikia Mungu. Wakati huo nilikuwa nafikiri ukitaka kumtumikia Mungu ni lazima uwe mchungaji. Kwa hiyo nikaamua kutafuta chuo cha Biblia ili nipate kusomea uchungaji.

Nilipata chuo cha Biblia cha kusomea uchungaji, na nikapata pia mtu aliyekuwa tayari kunilipia gharama za kunisomesha mpaka niweze kuhitimu. Lakini siku moja mchana, Roho mtakatifu alisema nami wazi wazi moyoni mwangu ya kuwa, sijaitwa kuwa mchungaji, kwa hiyo nisiende kusomea uchungaji.

Ikabidi niombe radhi kwa wale waliokuwa tayari kunisaidia kusomea uchungaji ya kuwa hapo mwanzoni nilikuwa sijasikia sauti ya Mungu vizuri. Na kwamba sitaweza kwenda tena kusomea uchungaji, maana Roho mtakatifu ameniambia sijaitwa kufanya huduma hiyo.