Yesu alisema: “Mimi siwezi kufanya neno mwenyewe, kama nisikiavyo ndivyo nihukumuvyo, na hukumu yangu ni ya haki, kwa sababu siyatafuti mapenzi yangu mimi, bali mapenzi yake aliyenipeleka” (Yohana 5;30)

Na kwa kuyatenda mapenzi ya Mungu juu ya maisha yake, na kwa kuzifanya kazi alizopangiwa azifanye, aliacha ushuhuda mkubwa na wa kudumu kwa ajili ya Mungu wake!

Yesu alisema juu ya ushuhuda huo ya kwamba: “Lakini ushuhuda nilio nao mimi ni mkubwa kuliko ule wa Yohana; kwa kuwa zile kazi alizonipa Baba ili nizimalize, kazi hizo zenyewe ninazotenda, zanishuhudia ya kwamba Baba amenituma”. (Yohana 5:36)

Unataka kuweka alama ya ushuhuda gani mwaka huu wa 2016?

Ni swali unalohitaji kujiuliza sasa, katika mwezi huu wa kwanza wa mwaka 2016; na unahitaji kutoa jibu lake katika mwezi huu wa kwanza wa mwaka 2016!

Swali lenyewe ni hili: Je, unataka kuweka na kuacha alama ya ushuhuda gani mwaka huu wa 2016?

Ushauri wetu kwako ni huu: Tenda mapenzi ya Mungu na ukazimalize kazi zake alizokupangia uzifanye kwa mwaka huu wa 2016!”

Kwa kufanya hivyo: utakuwa na uhakika wa kumaliza mwaka 2016 ukiwa umeacha ushuhuda mkubwa unaolitukuza jina la Yesu, na neno lake, na ufalme wake! Na ndiyo maombi yetu kwa jili yako! Nasi tunajiombea, na tunaomba na wewe utuombee pia!

Bwana Yesu asifiwe Milele!

Tunakusalimu katika jina la Yesu Kristo, aliye Bwana na Mwokozi wa maisha yetu! Tunamshukuru Mungu aliyetupa nafasi ya kukusalimu kwa njia ya barua hii, katika mwezi huu wa kwanza wa mwaka huu mpya wa 2016.

Tunayo maombi ambayo Mungu ametupa tukuombee kwa mwaka huu, nayo ni haya yafuatayo:
         “Mapenzi ya Mungu yaliyopangwa yatimizwe mbinguni kwa ajili yako kwa
       
   mwaka huu wa 2016, yatimizwe hapa ulipo duniani katika maisha yako ya
           kila siku, kama yatakavyokuwa yanatimizwa mbinguni”

Maombi haya tunakuombea kwa kusimamia maneno ya Yesu yaliyoandikwa katika Mathayo 6:10 yasemayo hivi: “Mapenzi yako yatimizwe hapa duniani kama huko mbinguni”.

Haya ni baadhi ya maneno yaliyomo ndani ya maombi yanayojulikana zaidi kama ‘sala ya Bwana’. Ni aina ya maombi ambayo Yesu aliwafundisha wanafunzi wake, ili wale walio watoto wa Mungu, wawe wanamwomba Mungu aliye Baba yao pia.

Mtiririko huu wa maneno tuliyopewa na Roho mtakatifu katika kukuombea maombi haya, unaweza na wewe ukautumia katika kujiombea.

Kwa mfano; unaweza ukajiombea kwa kusema hivi: “Ee, Mungu, yale mapenzi yako uliyopanga yatimizwe huko mbinguni kwa ajili yangu katika mwaka huu wa 2016, naomba yatimizwe hapa duniani katika maisha yangu ya kila siku katika mwaka huu wa 2016!”

Baadhi ya faida za kutembea katika mapenzi ya Mungu.

Mapenzi ya Mungu yatakapokuwa yanadhihirishwa kwako mwaka 2016, na wewe ukawa unayatekeleza, utaona yafuatayo yakijitokeza katika maisha yako:

1. Utaanza na utajikuta unaendelea kuwaza moyoni mwako, kama Mungu awazavyo moyoni mwake kwa ajili ya mpango alionao kwa ajili ya kufanikisha maisha yako. Soma   
Yeremia 29:11 na Isaya 55:8 – 11

2. Utaona kiwango cha maombi yako uombayo kwa Mungu na kujibiwa kikiongezeka! Soma 1 Yohana 5:14,15

3. Udhihirisho wa Uwepo wa Mungu katika maisha yako utaongezeka, kwa kuwa utakuwa unayafanya yale yampendezayo Mungu! Soma Yohana 8:29

4. Utajikuta unafaidi matunda ya mfumo wa ufalme wa mbinguni wakati huu ukiwa hai, na hata baada ya kufa kwako! Soma Mathayo 7:21 – 23

Hizi ni baadhi tu ya faida za kujua mapenzi ya Mungu kwa ajili yako, na wewe kutembea ndani ya yake, na kuyatekeleza.

Neno la Mungu kwa Mwaka huu wa 2016.

Neno la Mungu tulilowekewa moyoni kwa mwaka huu wa 2016 ni hili: “Tenda mapenzi ya Mungu na ukazimalize kazi zake alizokupangia uzifanye kwa mwaka huu wa 2016”!

Huu ulikuwa ni msimamo na mtazamo wa Yesu maisha yote, na si tu kwa mwaka mmoja ! Ukiweza kuishi hivi kwa mwaka mmoja, utatamani uendelee kuishi hivi maisha yako yote, na si tu kwa mwaka mmoja huu wa 2016!

Yesu aliwaambia wanafunzi wake hivi: “Chakula changu ndicho hiki, niyatende mapenzi yake aliyenipeleka, nikaimalize kazi yake” (Yohana 4:34)

Ukiyajua mapenzi ya Mungu juu ya maisha yako, utajua na kazi ambazo Mungu amekupangia uzifanye na kuzimaliza!

Ukiyajua na kuyatenda mapenzi ya Mungu juu ya maisha yako, utakuwa unatekeleza kazi alizokupangia, na Mungu atahakikisha unapata “Chakula” chako kwa kupitia kazi hizo unazozifanya! 

Kwa hiyo, tunapokuombea mapenzi ya Mungu aliyoyakusudia na yanayotekelezwa kwa ajili yako huko mbinguni yatatimizwa kwako mwaka huu, ndani yako kujengeke hamu ya wewe kuyatafuta mapenzi yake, ili uyajue na uyatende!

Huduma za Mwezi huu.

  • Tutashiriki kufundisha siku ya kupanda na kuvuna, iliyoandaliwa na New life in Christ ya Mkoa wa Dar es salaam; itakayofanyika tarehe 17 Januari 2016, kwenye ukumbi wa Diamondi Jubilee, kuanzia saa 8 Mchana hadi saa 12 jioni.

  • Tutafanya semina ya neno la Mungu jijini Arusha kwenye uwanja wa Reli tarehe 24 – 31 Januari 2016. Semina hii inayoandaliwa na huduma yetu ya MANA itakuwa inafanyika kila siku katika tarehe hizo kuanzia saa 10 hadi saa 12 jioni.

Tuombee Mapenzi ya Mungu yatimizwe katika huduma hizo. Karibu ushiriki nasi, na usiache kumweleza mwingine ili aweze kuhudhuria.

Ni sisi katika utumishi wa Kristo,
Christopher na Diana Mwakasege.