Bwana Yesu asifiwe

                Tunakusalimu katika jina la Yesu Kristo, aliye Bwana na Mwokozi wetu.

                Jambo mojawapo ambalo tulimwomba Mungu, na tumeendelea kumwomba Mungu atufanyie mwaka 2019, ni kutusaidia, na kutuwezesha, tumjue Yeye zaidi, na pia tumjue zaidi Yesu Kristo aliyetumwa kwa ajili yetu.

                Pamoja na maombi hayo, Roho mtakatifu ametupa mistari ya biblia ya kutusaidia kwenye jambo hili muhimu. Mistari hii ya biblia, tunaitumia kama mwongozo wa kulitafakari jambo hili la kumjua Mungu na Yesu Kristo, huku tukiitumia kama ajenda za kujiombea kila mwezi!

                Tumeona uhuru mioyoni mwetu, kukushirikisha jambo hili, kama mtendakazi pamoja nasi, katika kazi, na huduma ambayo Mungu ametupa kuhusiana na ufalme wa Mbinguni – sasa na hata milele.

                Tunaamini na wewe unaweza ukanufaika na jambo hili, ikiwa utalifuatilia na kulifanya.

                Ngoja tukushirikishe mistari hiyo ya biblia ambayo Roho Mtakatifu ametupa kuona Faida za kumjua Mungu na Kumjua Yesu Kristo:

1. Mwezi wa Januari 2019:

Mstari wa kutafakari na kuutumia kujiombea ni huu:

“Na uzima wa milele ndio huu, wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma” (Yohana 17:3).

Faida ya kumjua Mungu na Yesu Kristo toka kwenye mstahi huu: Ni kuzijua kazi za uzima wa milele ndani yetu, na kunufaika nazo.

2. Mwezi wa Februari 2019:

Mstari wa kuutafakari na kuutumia kujiombea ni huu:

“Mjue sana Mungu, ili uwe na amani, ndivyo mema yatakavyokujia” (Ayubu 22:21).

Faida ya kumjua Mungu na Yesu Kristo kutoka kwenye maneno ya mstari huu ni: Mungu kukupa umiliki wa amani yake kwanza, halafu ndipo aruhusu uyapate mema aliyokupangia kwenye Maisha yako.

3. Mwezi wa Machi 2019:

Mstari wa kuutafakari na kuutumia kujiombea ni huu:

“…lakini watu wamjuao Mungu wao watakuwa Hodari, na kutenda mambo makuu…”(Danieli 11:32).

Faida mojawapo ya kumjua Mungu, na kumjua Yesu Kristo kutoka kwenye maneno ya mstari huu ni: Kubadilisha na kuboresha kwa uwezo na ufanisi wa utendaji wako, ili uwe bora zaidi, kwa utukufu wa Mungu, na kwa faida ya ufalme wa Mungu, na kwa faida yako pia!

                Mungu akubariki, sana na azidi kukubariki, kwa kuwa na kiu ya kutaka kumjua Yeye Zaidi na Yesu Kristo aliyemtuma kwetu! Tuzidi kuombeana

Ni sisi katika utumishi wa Kristo,

Christopher na Diana Mwakasege