Bwana Yesu asifiwe sana!

Tunakuandikia barua hii tukiwa mjini Singida, ambapo leo tunaanza semina ya Siku tano.

Mwezi huu wa Julai tumeanza semina ya siku 8 mjini Mwanza. Tulikuwa tunajifunza somo linalohusu kujifunza jinsi Mungu anavyoongea na watu ili waweze kufuata vyema maelekezo yake. Semina hiyo ya Mwanza tuliifanya tarehe 3 – 10 Julai 2016.

Na wiki iliyofuata – yaani wiki iliyopita tarehe 14 – 17 Julai 2016 – tulikuwa na semina nyingine mjini Shinyanga. Wakati wa semina hii tulijifunza aina za maombi yanayotengeneza mazingira ya Mungu kutusaidia.

Na wiki hii tutakuwa hapa mjini Singida kwa siku 5 – yaani leo tarehe 20 Julai hadi 24 Julai 2016.

Ndani ya barua hii tunataka tukushirikishe hatua kadhaa za kufanya katika kuombea tatizo la kurithi, linalokwamisha mafanikio yako, ili lipate kuondoka maishani mwako.

Hatua ya 1:

Amua ni tatizo lipi la kurithi unalotaka Mungu akusaidie kuliondoa. Je, ni ugonjwa? Je, ni tabia? Je, ni hali ya maisha? Je, ni tatizo la Ki-imani? Je, ni tatizo la kushindwa kuoa au kuolewa?

Hatua ya 2:

Ikiwa hujui ikiwa tatizo linalokwamisha mafanikio yako ni la kurithi au sivyo – mwombe Mungu akujulishe, na akupe maelekezo ya namna ya kuliombea ili liishe.

Ukisoma yaliyotokea kipindi cha mfalme Daudi katika kitabu cha 2 Samweli 21:1, utaona ya kuwa wakati wa utawala wake, alipata tatizo la ukame kwa mfululizo wa miaka mitatu. Na alipomuuliza Mungu kwa njia ya maombi – aliambiwa ya kuwa tatizo lile la ukame – chanzo chake kilitokana na kosa alilofanya mfalme aliyemtangulia – yaani mfalme Sauli. Na Mungu akampa maelekezo juu ya kipi kifanyike ili ule ukame uishe. Mfalme Daudi alitekeleza maelekezo aliyopewa na Mungu – na tatizo la ukame likaisha.

Hatua ya 3:

Fanya toba juu ya kile kilichosababisha tatizo hilo la kurithi liwepo. Roho Mtakatifu atakuongoza juu ya jambo hili, ili uweze kulifanya kwa usahihi ule unaokubalika mbele za Mungu.

Nehemia alipokuwa anaombea tatizo la kurithi lililosababisha ukuta wa mji wa Yerusalemu kubomolewa, iliwabidi wafanye toba ya aina hii ninayokuelekeza katika hatua hii ya 3. Biblia inasema; “Waliokuwa wa wazao wa Israeli wakajitenga na wageni wote, wakasimama, wakaziungama dhambi zao, na maovu ya baba zao” (Nehemia 9:2).

Hatua ya 4:

Pokea kwa imani msamaha wa toba hiyo uliyoifanya. Hatua hii ya kupokea kwa imani msamaha wa toba yako – itakufanya

Uwe na ujasiri mbele za Mungu wa kuendelea kuomba, ili unufaike na kilichofanyika msalabani na Yesu Kristo kwa ajili yako. Soma kitabu cha 1 Yohana 3:21,22.
Uwe na ujasiri wa kumpinga na kumwondoa shetani anayetumia matatizo ya kurithi ili kukwamisha mafanikio yako. Soma kitabu cha Yakobo 4:7,8.

Utajuaje ya kuwa umesamehewa? Kwanza: Utajua ya kuwa umesamehewa kwa kuliamini moyoni mwako neno la Mungu katika biblia, lihusulo Mungu kusamehe dhambi za watu – kama vile mstari huu wa 1 Yohana 1:9.

Pili: Utajua ya kuwa umesamehewa kwa kuona amani ikijitokeza moyoni mwako, inayokupa ujasiri mbele za Mungu na mbele za shetani, na mbele za watu!

Tatu: Utajua ya kuwa umesamehewa kwa kutokujisikia kushtakiwa wala kujihukumu moyoni mwako – hasa unapokuwa mbele za Mungu na mbele za washitaki wako (shetani au watu wanaowashitaki). Soma kitabu cha 1 Yohana 3:22,23 na Wakolosai 2:13 – 15 na Yohana 8:1 – 11.

Hatua ya 5:

Omba Mungu kwa kutumia damu ya Yesu akutenganishe wewe na vitu vifuatavyo vya kurithi ili vikae mbali na maisha yako. Navyo ni:

  • Dhambi za kurithi
  • Uovu wa kurithi
  • Maagano mabaya ya kurithi
  • Laana za Kurithi
  • Viapo vibaya vya kurithi
  • Kukataliwa na kutengwa na jamii

…nakadhalika – huku ukivunja nguvu ya vitu hivyo juu ya maisha yako.

Hatua ya 6:

Kemea nguvu za giza (mapepo) zilizoambatana na tatizo la kurithi kwenye maeneo yaliyopata shida.

Fahamu hili

Hizi ni baadhi tu ya hatua muhimu tunazozipata ndani ya biblia kwa ajili ya kutusaidia kuondokana na kuepukana na matatizo yanayotokana na sababu za kurithi.

Zidi kutuombea

Mwezi ujao wa nane tuna kongamano la maombi ya kitaifa litakalofanyika Dodoma (2 – 5 Agosti): halafu tutaenda nchini Scotland kwa semina mjini Glasgow (13 – 14 Agosti); na tutafanya semina mjini Kigoma (18 – 21 Agosti); na mjini Tabora (24 – 28 Agosti).

Ni sisi katika utumishi
Christopher na Diana Mwakasege