Bwana Yesu asifiwe milele!

Tunakusalimu katika jina la Yesu Kristo! Tunaamini ya kuwa Mungu anaendelea kukutunza vyema.

Huu ni mwezi Julai au mwezi wa 7 katika mwaka huu. Hii ina maana tumekwishamaliza nusu ya mwaka, na mwezi huu tunaanza nusu ya mwisho ya mwaka huu!

Naam! Kwetu miezi sita imepita kwa haraka sana! Utadhani mwezi wa kwanza, yaani mwezi wa januari tulimaliza hivi karibuni!

Tunapoangalia tulichoweza kukifanya katika miezi sita iliyopita, tunawiwa kumshukuru Mungu sana kwa yote aliyotuwezesha kuyafanya.

Tumefanya semina 9 za neno la Mungu, katika maeneo 9 tofauti: Arusha, Moshi, Dar es Salaam, Tanga, Dodoma, Singida, Minneapolis (Marekani), Dallas (Marekani), na Morogoro.

Semina hizo ni bila kuhusisha semina ya siku moja ya kufungua mwaka tuliyoifanyia ukumbi wa Diamond Jubilee, na iliandaliwa na wenzetu wa huduma ya New Life in Christ mkoa wa Dar es Salaam.

Lakini pia, tumefanya semina 4 kwa njia ya simu, ambazo tunaziita “teleseminar”

Hizi ni semina ambazo tunazifanya mara moja kwa mwezi. Ni mwezi wa 5 na ule wa 6 ambao hatukufanya  - kwa kuwa tulikuwa Marekani kwa wiki kadhaa.

Tena, tumeweza kufanya semina 7 za vijana, kila jumamosi asubuhi katika mikoa yote 7 tuliyokwishafanya semina za neno la Mungu katika miezi 6 iliyopita. Hizi ni semina ambazo tunafundisha somo la “Leadership mindset”.

Tusiache kukuambia pia ya kuwa katika kipindi hicho cha miezi 6, tumeweza kwenda Israeli mara moja (mwezi juni kwa siku 10). Tulisafiri na kundi la watu kwa ajili ya kujifunza zaidi mambo ya kiroho, na tulipokuwa tulitembelea maeneo ya kumbukumbu ya kibiblia.

Maelfu kadhaa ya watu waliokoka katika semina 9 tulizokwisha fanya, na wengine kurudisha mahusiano yao na Mungu!

Tunaamini utaungana nasi kumshukuru Mungu kwa kututunza na kutuwezesha kuifanya kazi yake ya kuujenga ufalme wake!