BARUA YA MWEZI JUNI 2014.

Bwana Yesu Kristo asifiwe milele.

Tunakusalimu katika jina la Yesu Kristo.

Hatuhitaji kukukumbusha ya kuwa mwezi wa sita au mwezi wa juni, ni mwezi wa mwisho wa kipindi cha kwanza cha mwaka huu wa 2014. Tangu januari hadi mwezi huu wa juni, ni miezi sita. Na mwezi ujao wa julai, tunaanza miezi sita ya kipindi cha pili cha mwaka 2014.

Sisi tunamshukuru Mungu sana sana, kwa jinsi ambavyo tunaona Mungu akituongoza, na kutuchukua hatua kwa hatua, katika utumishi huu aliotuitia.

Hadi sasa, tangu mwezi wa januari, Mungu ametuwezesha kufanya semina 10….ndiyo kumi! Tungewezaje kufanya semina 10 kwa miezi 6 kama si Mungu aliyekuwa pamoja nasi kutuwezesha na kutusaidia!

Nasi tunamshukuru Mungu sana kwa kila mtu ambaye amesimama pamoja nasi, popote pale alipo katika utumishi huu ambao Mungu ametupa katika kizazi hiki.

Pia, tunawashukuru watanzania na wakenya, waliotupokea na kuhudhuria, semina tulizofanya nchini Marekani hivi karibuni.

Tulikuwa nchini Marekani, tulifanya semina Minneapolis, Minnesota tarehe 23 – 25 mei 2014. Halafu tukafanya semina nyingine tarehe 30 mei hadi 1 juni 2014 jijini Dallas, Texas. Na nyingine tukaifanya jijini Washington D.C tarehe 6 – 8 juni 2014.

Tunapoandika barua hii ndiyo tumerudi Arusha, Tanzania, baada ya safari hiyo ya kihuduma nchini Marekani. Tunamshukuru Mungu kwa kutupeleka na kwa kuturudisha salama; na kwa kuifanikisha huduma tuliyoifanya nchini Marekani.

Mungu akipenda, tunatarajia kuwa na semina nyingine nchini Marekani, katika jiji la Birmingham, Alabama, tarehe 10 – 12 Oktoba mwaka huu.

Na kwa wale walioko nchini Uingereza, tutakuwa na semina nchini humo tarehe 26 – 28 Septemba katika jiji la Coventry.